Search This Blog

Saturday, June 1, 2013

BREAKING NEWS: SIMBA NA YANGA HATARINI KUSHIKI KOMBE LA KAGAME DARFUR

Siku kadhaa baada ya Baraza la Vyama vya soka Afrika Mashariki na Kati - CECAFA kuidhinisha michuano ya kombe la Kagame kuchezwa mjini Darfur -Sudan, serikali ya Tanzania imetoa tamko kuhusu timu za Simba na Yanga kwenda kushiriki michuano hiyo huko Sudan kwenye eneo ambalo limekuwa likiandamwa na vurugu kwa miaka kadhaa sasa.
 Kwa mujibu wa msemaji wa klabu ya Simba Ezekiel Kamwaga ni kwamba serikali haidhani ni busara kwa vilabu vya Simba na Yanga kwenda kwenye eneo hilo kushiriki Kagame Cup kutokana hali mbaya ya usalama iliyopo Darfur.
HIVI NDIVYO ALIVYOANDIKA KAMWAGA KWENYE UKURASA WAKE WA FACEBOOK.
Ezekiel Kamwaga
Breaking News...... Serikali imesema haioni busara ya Kagame Cup kupigwa Darfur.... Hakuna hoteli ya maana na watu wanashauriwa kutembea na fulana zinazozuia risasi kupenya... Nadhani hii ndiyo stori kubwa ya kimichezo kwa leo.... Je, mnadhani itakuwa busara kwa Simba na Yanga kushiriki?

MANCHESTER UNITED INAVYOZIZIDI BARCELONA NA REAL MADRID KWENYE KUINGIZA FEDHA NYINGI KWENYE UDHAMINI WA JEZI


Real Madrid, klabu inayoongoza kuwa thamani kubwa zaidi duniani ($3.3 billion), imesaini dili la udhamini wa jezi na kampuni ya Emirates ambao utaiingizia klabu hiyo $39 million kwa mwaka kwa kipindi cha miaka 5.
 
Dili hilo na kampuni ya ndege ya Dubai limeshindwa kuipa Madrid fedha nyingi kama ilivyo kwa vilabu vingine vya juu barani ulaya.
 
Ndio, Los Blancos watapata asilimia 30 zaidi ya walichokuwa wakipewa na mdhamini wa sasa Bwin. Lakini kiasi hicho wanacholipwa na Emirates ni kidogo ukifananisha na wanacholipwa Manchester United(yenye thamani ya $3.2 billion) na Barcelona($2.6 billion) kwenye mikataba yao ya udhamini wa jezi. Mashetani wekundu wameingia mkataba na Chevrolet utakaowaingizia kiasi cha $80 million kwa mwaka kuanzia msimu wa 2014-15 - kwa miaka 5, wakati Barcelona wana mkataba wa miaka mitano Qatar Foundation wenye thamani ya $44 million kwa mwaka - dili linaloanza mwezi ujao.
 
Real Madrid walitakiwa kupewa angalau dili lenye thamani ya kuzidi lile la Barcelona - ikitajwa kuwa klabu yenye mafanikio zaidi kwenye karne hii, imeshinda mataji mengi zaidi ya La Liga na Champions League, pia kwa sasa ina mchezaji mkubwa na maarufu zaidi kwenye ulimwengu wa mitandao ya kijamii Cristiano Ronaldo.

 LISTI YA TIMU ZINAONGOZA KWA KUINGIZA FEDHA NYINGI KUPITIA UDHAMINI WA JEZIKATUNI YA LEO: REST IN PEACE ALBERT MANGWEA


Friday, May 31, 2013

TAIFA STARS WATAKIWA KUJITUMA KUHAKIKISHIA WANARUDI NA USHINDI NA KUFUZU KOMBE LA DUNIA

Balozi wa Tanzania nchini Ethiopia, Joram Biswaro amewataka wachezaji wa Taifa Stars kuhakikisha wanaipeleka timu hiyo kwenye fainali za Kombe la Dunia zitakazofanyika mwakani nchini Brazil.

Ametoa changamoto hiyo wakati alipotembelea mazoezi ya timu hiyo jana (Mei 29 mwaka huu).

Taifa Stars inayodhaminiwa na Kilimanjaro Premium Lager imepiga kambi nchini Ethiopia na inafanya mazoezi kwenye Uwanja wa Addis Ababa.

“Watanzania tunafurahi kutokana na uwezo mnaouonyesha, hasa baada ya kuifunga Morocco mabao 3-1. Kama mliwafunga nyumbani hata kwao mnaweza kuwafunga. Tunataka kuwaona Maracana (Brazil) mwakani, mimi tayari ninayo tiketi mtanikuta kule,” amesema Balozi Biswaro ambaye enzi zake aliwahi kuichezea timu ya Yanga.

Taifa Stars ambayo iko Addis Ababa tangu Jumatatu (Mei 27 mwaka huu) imeweka kambi katika hoteli ya Hilton ambapo Jumapili (Juni 2 mwaka huu) itacheza mechi ya kirafiki na Sudan (Nile Crocodile) kwenye Uwanja wa Addis Ababa.

Balozi Biswaro ameikaribisha Taifa Stars ubalozini Addis Ababa mara baada ya mechi dhidi ya Sudan ambapo itakutana na baadhi ya Watanzania wanaoishi Ethiopia kabla ya kuondoka alfajiri kwenda Marrakech, Morocco kwa kupitia Cairo, Misri.

Kocha Kim Poulsen amesema kikosi chake kinaendelea na mazoezi vizuri na kitaimarika zaidi baada ya wachezaji Mbwana Samata na Thomas Ulimwengu wanaochezea timu ya TP Mazembe ya Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo (DRC) kujiunga nacho Juni 3 mwaka huu jijini Marrakech kwa ajili ya mechi dhidi ya Morocco itakayochezwa Juni 8 mwaka huu.

Naye Meneja wa Bia ya Kilimanjaro Premium Lager, George Kavishe, akizungumza kutoka Dar es Salaam, alisema wao kama wadhamini wamefarajika kuona timu inaendelea vizuri Mjini Addis na  inaleta matumaini kuwa watacheza vizuri katika mechi dhidi ya Morocco Juni 8.
 “Tuna imani sana na Taifa Stars kwani wameshatuonesha yote yanawezekana…watanzania waiombee timu yetu ili na sisi tupate nafasi ya kucheza Brazil mwakani,” alisema.

Wachezaji walioko katika kikosi cha Stars jijini Addis Ababa ni Juma Kaseja, Aggrey Morris, Mwadini Ally, Ally Mustafa, Shomari Kapombe, Kevin Yondani, Erasto Nyoni, Haroub Nadir, Mwinyi Kazimoto, Frank Domayo, Mrisho Ngasa, Khamis Mchana, Amri Kiemba, Salum Abubakar, Simon Msuva, John Bocco, Vicent Barnabas, Mudathiri Yahya, Athuman Idd, Haruni Chanongo na Zahoro Pazi.

OFFICIAL: RADAMEL FALCAO MCHEZAJI MPYA WA MONACO

SHAFFIH DAUDA ATEMBELEA OFISI ZA SERENGETI FREIGH UK

MZEE WA KAZI CHRIS LUKOSI AKIMSHUKURU MDAU SHAFII

Jana mdau Shaffih Dauda wa clouds FM akiongozana na Ismail Sota walitembelea ofisi za SERENGETI FREIGH UK kujionea jinsi boxi linavyopigwa

Pamoja na kujionea wazee wa kazi wakipiga boxi mdau Shafii ambaye pia ni mmiliki wa blog ya sports iitwayo Shaffihdauda.com aliingia mkataba wa kuwarusha hewani wazee wa kazi bila malipo kwa mwaka mzima baada ya kufurahishwa na jinsi wazee wa kazi walivyoweza kulirusha jina la Tanzania/Serengeti UK na kuwa mfano bora kwa vijana wengine wennye nia ya kujiajiri.

UJASIRIAMALI
WAKIANGALIA BOXI LINAVYOPIGWA

HIVI NDIVYO MANCHESTER UNITED WANAVYOTENGENEZA MAMILIONI KWA SIKU KUPITIA WATALII WANAOKWENDA OLD TRAFFORD


Uwanja wa klabu ya Manchester United Old Trafford ndio kivutio cha kimichezo cha utalii maarufu kuliko vyote nchini Uingereza.

Karibia watalii millioni moja kutoka duniani kote walitembelea na kuangalia mechi kadhaa nchini Uingereza mwaka uliopita.

   
Johnstone Malunda

Kwa mujibu wa kitengo cha utalii hapa UK, watalii zaidi ya 900,000 kutoka nje ya UK walitumia kiasi cha £706 million, kwa wastani wa £785 kwa kila shabiki.

Old Trafford ndio iliongoza kwa kutembelewa ikifuatiwa na dimba la Liverpool - Anfield.
Uwanja wa Manchester City Etihad Stadium ulishika nafasi ya saba.

NAMNA OLD TRAFFORD INAVYOIINGIZIA MAMILIONI MANCHESTER UNITED 

Gharama za kufanya ziara ya saa moja ndani ya Old Trafford kwa kichwa ni paundi 16. Na kwa mujibu wa tour guide wa Old Trafford - watalii wapatao 1500 hutembelea uwanja wao kwa siku moja.

Kimahesabu uwanja huo unaitengenezea United paundi 24,000 kwa siku, ambazo ni sawa na paundi 168,000 kwa wiki na paundi millioni 8.6 kwa mwaka ambazo kwa pesa za madafu za kitanzania ni zaidi ya billioni 23. Hii ni pesa inayopatikana kupitia utalii tu wa Old Trafford.


Sota


Shabiki wa Man United Ismail Sota nilikuwa nae kwenye tour ndani ya Old Trafford.
KALI YA LEO: SHABIKI WA MAN CITY ATEMBELEA MAKUMBUSHO YA OLD TRAFFORD AKIWA AMEVAA JEZI YA CITYSmith akiwa mwanae ndani ya Old Trafford
Siku ya leo wakati nikiwa kwenye ziara yangu ndani ya Theatre of Dreams - Old Trafford nilikutana na kali ya mwaka baada ya kumshuhudia shabiki wa klabu ya Manchester City akiwa miongoni mwa mamia ya wapenzi wa soka waliokuja kutalii ndani ya Old Trafford.

Kitendo hicho ambacho ni kigumu kuweza kutokea kwa timu zenye upinzani mkali kama wa City na United kilionekana kutowashangaza watu wengi waliokuja kwenye ziara ndani ya Old Trafford, lakini kwangu mie niliyezoea vurugu na uhasama usiokuwa na dira wa Simba na Yanga nilishangazwa sana. Hivyo nikajaribu kumuuliza Bwana Peter Smith imekuwaje amekuja kutembelea sehemu ya makumbusho wa klabu ambayo ndio mpinzani wake? Smith alinijibu kwamba hilo ni jambo la kawaida tu kwao ingawa yeye hakuwa anataka kwenda kutembelea vivutio vya Old Trafford ila alilazimishwa na mwanae mpenzi ambaye ni shabiki wa mkubwa wa Manchester United na mchezaji Wayne Rooney.

Kwa wakati wote tuliokuwa kwenye ziara hiyo mamia ya mashabiki wa United hawakuwa na habari kidogo na shabiki huyo aliyevaliwa jezi ya Manchester City ndani ya makumbusho ya OT - waliendelea na shughuli zao bila kumbugudhi mpaka ziara ilipomalizika.

Je itawezekana shabiki wa Simba aende makao makuu ya Yanga pale mtaa wa jangwani akiwa kavaa jezi nyekundu na kutoka salama bila bugudha?? Tuige mfano mzuri wa wenzetu waliotutangulia na kuwa wastaarabu.

TOUR YANGU NDANI YA OLD TRAFFORD: HATIMAYE MANCHESTER UNITED KUBADILI NYASI MBOVU ZA OLD TRAFFORD BAADA YA MIAKA 10

Shaffih Dauda, Ismail Sota, tour guide wa Old Trafford, na Jonstone Mulunda
Siku ya leo nikiwa bado hapa nchini Uingereza nilifanikiwa kufanya ziara kwenye uwanja wa pili kwa ukubwa hapa UK - uwanja wa Manchester United - Old Trafford.

Katika ziara yangu ya leo kwenye makao makuu ya klabu ya Manchester United nimefanikiwa kujifunza vitu vingi sana, na kwa utaratibu nitaanza kuwajuza wapenzi wasomaji wa mtandao huu.

UWANJA WA OLD TRAFFORD - SEHEMU YA KUCHEZEA
Nikiziaga nyasi za Old Trafford ambazo zinatarajiwa kuondolewa

Katika kipindi cha hivi karibuni sehemu ya kuchezea ya uwanja Manchester United imekuwa ikalalamikiwa kwamba haina ubora mzuri. Kufuatiwa malalamiko hayo uongozi wa Manchester United umeamua kubadilisha nyasi za sehemu ya kuichezea za uwanja zilizodumu kwa takribani miaka 10 sasa. 

Uwanja huo ambao United walianza kuutumia mnamo mwaka 1910 ndio uwanja wa tisa wa ukubwa barani ulaya wenye uwezo wa kuingiza watu 75,765, katika miaka ya hivi karibuni umekuwa ukichezewa mechi za mchezo wa Rugby tangu mwaka 1998, mechi ambazo zimepelekea uharibifu mkubwa wa sehemu ya kuchezea ya Old Trafford.
Timu ya watoto wa Manchester United

Uwanja huo kwa sasa unachezewa na timu ya watoto ya Manchester United baada ya msimu wa ligi kumalizika, na sasa unatarajiwa kuanza kufanyiwa marekebisho baada ya mechi ya magwiji wa klabu ya Manchester United dhidi ya wale wa Real Madrid itakayofanyika siku ya jumapili wiki hii.

Gharama za marekebisho ya nyasi mpya zinazotarajiwa kuwekwa kwenye uwanja huo wa Old Trafford zina gharama ya £250,000, na ukarabati wa huo utaanza rasmi siku ya jumatano.


Thursday, May 30, 2013

PICHA YA LEO: HUU NDIO UZI MPYA WA REAL MADRIDHATIMAYE MARK HUGHES ATAMBULISHWA RASMI KUWA KOCHA MPYA WA STOKE CITYUSAJILI WA KISHABIKI/KUKOMOANA WA SIMBA NA YANGA UNAIDHOOFISHA TAIFA STARSSIMBA na Yanga zote za Dar es Salaam zimeanza kuchuana kuwania saini za wachezaji nyota, lakini tayari hisia za ushindani, kukomoana na kuonyeshana jeuri ya fedha zimeanza.

Yanga imeingia Msimbazi na kumnyakua kiungo mshambuliaji, Mrisho Ngassa ambaye alikuwa akiichezea timu hiyo kwa mkopo akitokea Azam FC. Simba iliwahi kutangaza kumsajili mchezaji huyo lakini imepigwa bao.

Muda mfupi tu baada ya dakika 90 kumalizika katika mchezo kati ya Yanga na Simba 18 Mei mwaka huu kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam, huku Yanga ikiwa imeibuka na ushindi wa mabao 2-0, mashabiki wa klabu hiyo ya mtaa wa Jangwani walimbeba Ngassa juu juu kama vile ndiye shujaa katika mchezo ule huku wakiwa wamemvalisha jezi ya rangi ya njano na kijani inayoyotumiwa na timu hiyo.

Hizo zilikuwa dalili za wazi za Yanga kumsajili Ngassa kwa mkataba wa miaka miwili. Saa 48 baadaye, Ngassa alitambulishwa mbele ya waandishi wa habari kwamba amejiunga na Yanga.

Baada ya pigo hilo, Simba nayo ikawa inafuatilia saini ya kiungo wa Yanga aliyemaliza mkataba na klabu hiyo, Haruna Niyonzima ili aweze kutua Msimbazi. Mengi yalisemwa lakini mwisho Niyonzima alionekana mbele ya waandishi wa habari akitangaza kuwa ameongeza mkataba Yanga.

Yanga imemsajili Ngassa, je, anakwenda kucheza wapi? Nani ataathirika na ujio wa mchezaji huyo?

Nafasi anayokwenda kucheza Ngassa ndiyo pia anacheza Simon Msuva kwa sasa. Hii ina maana ili Ngassa acheze, inabidi ama Msuva awekwe benchi au kiungo Frank Domayo apumzishwe. Ikitokea hivyo itabidi Niyonzima arudi kucheza kama kiungo wa kati halafu Ngassa na Msuva wagawane winga kila upande.

Kwa hali hiyo, ni wazi nafasi ya Domayo inaweza kuathiriwa siyo katika klabu yake tu, bali hata timu ya taifa kwani atakuwa akicheza kwa muda mfupi mno katika kikosi cha Yanga.

 
Hivi ndivyo alivyopotezwa Nizar Khalfan katika Taifa Stars; alipokosa nafasi ya uhakika katika kikosi cha Yanga, akakosa fursa ya kuonekana na akakosa kuitwa Taifa Stars.

Yanga inaendelea na usajili ambao kwa hakika umejaa zaidi ushabiki na ushindani na timu nyingine bila kuzingatia mahitaji ya timu. Hivi sasa Yanga inafanya kila linalowezekana kumsajili Kabange Twite aweze kuichezea timu hiyo msimu ujao wa Ligi Kuu ya Bara, baada ya kushindwa kuitumikia timu hiyo msimu uliopita.

Ilipomsajili awali, Kabange kutoka FC Lupopo ikashindwa kumtumia kutokana na hitilafu katika uhamisho wake. Yanga ikikamilisha usajili wake, Kabange ataungana na viungo wengine kibao waliojazana kikosini hivyo kuendeleza kujaza wachezaji wa aina moja kikosini.

Kabange ataungana na Nizar, Nurdin Bakari, Niyonzima, Athuman Idd ‘Chuji’, Domayo, Ngassa, Msuva, Omega Seme, Hamis Kiiza (kama atabaki kikosini kwani mkataba wake umeisha) na wengineo ambao hadi sasa wangali wanawania nafasi ya kucheza.

Atakayekosa nafasi ya kwanza atakosa pia uwezekano wa kuitwa Taifa Stars.

  

Simba nayo imeshaanza harakati za usajili na tayari imeshamsajili kipa wa Kagera Sugar, Andrew Ntala, kiungo mshambuliaji wa Coastal Union, Ibrahim Twaha, Zahor Pazi na beki Issa Rashid wa Mtibwa Sugar.

Kwa usajili huu, Simba imefanya kitu kizuri lakini inaweza kuwa imechemsha kwa kipa Ntala ambaye hadi ligi inaisha, alikuwa kipa namba moja katika kikosi chake. Sasa ni wazi hatakuwa na nafasi mbele ya makipa Juma Kaseja na Abel Dhaira anaowakuta kikosini.

Kipaji cha Ntala sasa kinaelekea ukingoni, vinginevyo Kaseja aondoke sasa kikosini huku Dhaira naye akiachana na timu hiyo, nje ya hapo Ntala atakuwa mchezaji wa akiba msimu mzima. Uwezekano wa Ntala kuwa kipa nambari wani uko kwenye mikono ya aliyekuwa kocha mkuu wa Kagera Stars, Abdallah Kibadeni ambaye pia anahamia Msimbazi.

Kiungo Pazi anaweza kucheza kwani kwa nafasi yake na uzoefu alionao vinaweza kumfanya kuwa miongoni mwa wachezaji nyota watakaokuwa hawakosi nafasi kikosi cha kwanza kama itakavyokuwa kwa beki wa pembeni, Issa Rashid.

Tunaweza kuipongeza Azam FC kwa kutangaza mapema kwamba haitafanya usajili wowote mkubwa zaidi ya kuwaongezea mikataba wachezaji wake ambao inao sasa huku mikataba yao ikiwa imeisha.

Kocha wa Azam, Stewart Hall na uongozi mzima wa timu hiyo, ni watu wanaoheshimu uamuzi wa kila upande kulingana na hali halisi tofauti na Simba na Yanga, ambazo hata shabiki anaweza kusajili.

MAKALA HII IMETOLEWA KATIKA GAZETI LA MAWIO, IMEANDIKWA NA ELIUS KAMBILI

YANGA WAKABIDHIWA SHILINGI MILLIONI 25 ZA ZAWADI YA UBINGWA WA VODACOM NA KILIMANJARO

Meneja wa Bia ya Kilimanjaro George Kavishe kushoto akimkabidhi mfano wa hundi Katibu Mkuu wa Young Africans Lawrence Mwalusako leo katika hafla iliyofanyika katika kiwanda cha bia TBL iIlala
 
 
 
 
 
 
 
 
 
 
 
 
 
 
 
Kilimanjaro Premium Lager – wadhamini wakuu wa timu ya Yanga  imetoa kiasi cha shilingi milioni 25 kama zawadi kwa timu hiyo kwa kushinda Ligi Kuu ya Vodacom 2012/2013. 
 
Akikabidhi hundi ya Sh milioni 25 kwa Yanga SC, Meneja wa bia ya Kilimanjaro Premium Lager, George Kavishe alisema Kilimanjaro Premium Lager imefurahishwa sana na ushindi wa timu ya Yanga na kusema imejizatiti kikamilifu kuisaidia timu ambayo imeibuka bingwa katika ligi yenye ushindani mkubwa kutokana na kuibuka kwa timu mpya zenye nguvu.
    
“Yanga imekuwa ikicheza mpira mzuri kipindi chote cha msimu wa ligi kuu, na sio ajabu wao kuibuka washindi wa Ligi hii. Napenda kuwapongeza wachezaji wa Yanga, kocha na Uongozi mzima wa Yanga kwa  matokeo mazuri ya kushinda Ligi kuu kwa mara ya 24 sasa.”
 
Kavishe aliongeza kuwa zawadi hiyo ni sehemu ya sh bilioni 1.5 ya udhamini wa Kilimanjaro Premium Lager kwa Yanga   na imetolewa kwa lengo la kuhamasisha klabu kujitahidi kwa ushindi zaidi na kusaidia klabu katika maandalizi yake kwa ajili ya mashindano ya kimataifa ambayo tayari Yanga ina sifa za kushiriki kutokana na ubingwa waliojipatia.
 
Akipokea hundi hiyo, Katibu mkuu wa Yanga , Bwana Lawrence Mwalusako alisema Yanga inaishukuru sana Kilimanjaro Premium Lager kwa mchango wao. Aliongeza kuwa Yanga ni timu nzuri na yenye nguvu kutokana na uongozi imara pamoja na udhamini mkubwa kwa bia ya Kilimanjaro Premium Lager.  
 
‘‘Mafanikio yetu ya uwanjani ni kielelezo cha mafanikio ya kampuni na pia (TBL) na bia ya Kilimanjaro Premium Lager kwa ujumla ambayo imekuwa ikitusaidia sana. Kilimanjaro  Premium Lager imetoa mchango mkubwa sana katika kuipa timu msukumo uliopelekea mafanikio haya,’’ alisema Mwalusako.
 
Mwalusako aliongeza “Yanga sasa ina nafasi ya kuonekana kwenye jukwaa la kimataifa la soka kutokana na mafanikio haya’’.  “Tunaamini kuwa kutokana na udhamini wa Kilimanjaro Premium Lager tutaendelea kukua na kufanikiwa.’’
 
Yanga itawakilisha Tanzania katika michuano ya Klabu Bingwa Afrika na Kombe la Kagame.
 
 

HATIMAYE JOSE MOURINHO ASAINI MKATABA WA MIAKA MINNE KUJIUNGA TENA NA CHELSEA

JOSE MOURINHO ni boss mpya wa Chelsea — na hiyo ni rasmi kwa mujibu wa gazeti la The Sun!

The Special One ameripotiwa kusaini mkataba mpya wa miaka minne wenye thamani ya £40million jana usiku.
Kwa mujibu wa ofisa mmoja wa juu wa Chelsea: “Ni rasmi Jose ni kocha wetu tena! Kila mtu anafurahia ujio wake - klabu, wachezaji na mashabiki.
“Tayari tunajiaandaa na msimu ujao - tuna uhakika utakuwa msimu mzuri sana.”
 
Mechi ya kwanza ya Mourinho inatarajiwa kuwa kwenye mechi ya mataarisho nchini Thailand dhidi ya  Singha All Stars XI, katika ziara ya huko Malaysia na Indonesia.
Baada ya hapo The Blues wataenda Marekani kwenye michuano ya  International Champions Cup itakayohusisha timu za Real Madrid na Inter Milan, pia Everton, Juventus, AC Milan, Valencia na LA Galaxy.

Wednesday, May 29, 2013

MAREHEMU NGWAIR ALIKUWA SHABIKI MKUBWA WA KLABU YA MANCHESTER UNITED

Katika kumfahamu marehemu Albert Mangwea nje ya muziki wake niligundua ni mpenzi mkubwa wa soka na alikuwa mmoja ya mashabiki wakubwa wa Klabu bingwa ya England Manchester United.

Ngwair ambaye alikuwa mmoja ya wanamuziki wakubwa wa Bongo Flava amefariki dunia nchini Afrika ya Kusini jana kwa sababu ambazo bado hazijafahamika.
Mwenyezi mungu ailaze mahala pema peponi roho ya marehemu.

MAMBO MATATU MUHIMU DAVID MOYES ANAPASWA KUWA AMEFANYA KABLA YA AUGUST NDANI YA MANCHESTER UNITED


Mpaka kufikia mwezi wa nane katikati David Moyes atakumbana na presha kubwa kuliko watu wengi kwenye ulimwengu wa soka. Nani ataweza kumlaumu kwa hili?
Kuvaa viatu vikubwa vya kocha aliye na mafanikio zaidi kwenye soka la Uingereza sio jambo rahisi hata kidogo na kwa bahati mbaya pamoja na Sir Alex Ferguson kuwaomba mashabiki kumpa muda na sapoti Moyes wakati akiwaaga - ukweli ni kwamba ikiwa matokeo hayatokuwa yakiwafurahisha mashabiki mpaka kufikia November, maswali yataanza kuzuka kama mscotland huyo ni mtu sahihi kurithi mikoba ya Fergie?
Pamoja na hilo pia Moyes ana changamoto nyingine kubwa 3 na muhimu za kukabilina nazo kabla ya msimu haujaanza. 

1 - KUHAKIKISHA WACHEZAJI WAKONGWE WOTE WANAMUUNGA MKONO. 

Kama ilivyo kwa vilabu vingi vikubwa basi Manchester United nayo ina wachezaji ambao wanasikilizwa sana ndani ya timu (mafaza); Ryan Giggs, Nemanja Vidic, Rio Ferdinand na Patrice Evra. Baada ya kumalizika kwa siku ya kwanza mazoezini itampasa kuwa na mikutano tofauti na wachezaji hawa, hasa Ryan Gigg. Kujadili mipango yake kwenye timu na wachezaji hawa husika. Chumba cha kubadilishia nguo cha United kina umuhimu mkubwa katika mafanikio katika soka la kisasa kama ambavyo tumeshuhudia Manchester City, Mancini alipoteza sapoti kutoka kwenye 'dressing room' jambo ambalo lilipelekea au kuchangia kufeli kwa City na hivyo kupelekea kutimuliwa kwake. Moyes akifanikiwa kuwaweka mafaza wa United upande wake basi timu itakuwa na umoja mkubwa na hivyo kujirahisishia kazi yake ndani ya Old Trafford.

2 - KUSHUGHULIKIA SUALA LA ROONEY. 

Kitu kimoja ambacho kilimfanya Ferguson awe tofauti na makocha wengine kilikuwa ni kuuza wachezaji kwenye muda sahihi. Sasa hivi kuna suala la mmoja wa wachezaji wa United Wayne Rooney ambaye ameonekana kutaka kuondoka kwenye klabu hiyo kwa mujibu wa Ferguson. Mashabiki wa Manchester United wamegawanyika wengine wakitaka auzwe na wengine wakitaka abaki, mchezaji mwenye ubora wa aina yake inabidi abaki kwa gharama yoyote ni mawazo ya baadhi huku wengine wakidhani kwamba dau la 30+ million kwa Rooney ni biashara nzuri na inaweza ikatoa nafasi kwa wachezaji wachanga kuonekana, wachezaji wenye njaa ya mafanikio wenye kucheza nafasi ya Rooney.
Imeanza kuwa hali kama iliyojitokeza wakati wa David Beckham, Rooney ameanza kuhisi amekuwa mkubwa kuizidi klabu ya Manchester United, kukasirishwa na kutopata muda mwingi wa kucheza katika mechi alizokuwa fiti, akiwa tayari ameshaomba kuuzwa inaonekana uhusiano baina ya Rooney na Manchester United upo kwenye hali mbaya. Moyes anahitaji kumuuliza Rooney kama anahitaji kuendelea kuichezea Manchester United, kama hahitaji itabidi amuuze kwa dili zuri na kumbadili na mchezaji sahihi, kama Bale. Ikiwa bado anahitaji kubaki United, basi inabidi amkumbushe kwamba yeye (Moyes) ndio boss na ikiwa atahitaji kupata nafasi basi atahitaji ni kujituma pekee ndio kutamfanya acheze mechi zote.

3 - KUJENGA TIMU YAKE MWENYEWE.
Ni muhimu kwa Moyes kujua kwamba hii timu sasa ni ya kwake, na japokuwa United walishinda ligi kwa urahisi kiasi na wachezaji ambao Fergie alikuwa akiwahusudu, lakini kwa Moyes inaweza ikawa tofauti. Pamoja Wascotland hawa kufanana kwa kiasi fulani - lakini ni watu wawili tofauti kabisa. Kwa kawaida lazima Mashabiki wa United watakuwa wameandamwa na kumbukumbu za Manchester United kwenye zama za Fergie, hili ni jambo la kawaida. Moyes haihtaji hii hali, kwa mara ya kwanza kwenye masiaha yake ya ukocha atakuwa na fedha nyingi za usajili. Ikiwa atazitumia vizuri na kwa umakini kwenye maeneo sahihi basi ataweza kutengeneza utawala mpya wa Manchester United katika zama zake na kutowapa watu sababu za kuangalia nyuma kwenye kwenye 'siku za ushindi'.

TAIFA STARS WAENDELEA KUINOLEA MAKALI MOROCCO ADDIS ABABA

TAIFA STARS YAANZA KUJINOA ADDIS ABABA
Taifa Stars imetua jijini Addis Ababa, Ethiopia leo (Mei 28 mwaka huu) alfajiri kwa ndege ya EgyptAir ambapo itaweka kambi ya wiki moja kujiandaa kwa mechi ya mchujo ya Kombe la Dunia dhidi ya Morocco (Lions of the Atlas) itakayochezwa Juni 8 mwaka huu jijini Marrakech.

Stars iliyotua na kikosi cha wachezaji 21 imefikia hoteli ya Hilton, na imeanza mazoezi leo (Mei 28 mwaka huu) saa 12 jioni kwenye Uwanja wa Addis.

Kwa mujibu wa Kocha Kim Poulsen, Stars inayodhaminiwa na Kilimanjaro Premium Lager itakuwa na vipindi (sessions) vinne vya mazoezi kabla ya kucheza mechi ya kirafiki na Sudan (Nile Crocodile). Mechi dhidi yan Sudan itachezwa Jumapili kuanzia saa 11 jioni kwenye Uwanja wa Addis.

Sudan ambayo pia imeweka kambi yake Addis Ababa kujiandaa kwa mechi ya mchujo ya Kombe la Dunia ilicheza mechi yake ya kwanza jana (Mei 27 mwaka huu) dhidi ya wenyeji Ethiopia na kulala mabao 2-0.

Wachezaji wanaounda Stars ni nahodha Juma Kaseja, nahodha msaidizi Aggrey Morris, Mwadini Ally, Ally Mustafa, Shomari Kapombe, Kevin Yondani, Erasto Nyoni, Haroub Nadir, Mwinyi Kazimoto, Frank Domayo, Mrisho Ngasa, Khamis Mchana, Amri Kiemba, Salum Abubakar, Simon Msuva, John Bocco, Vicent Barnabas, Mudathiri Yahya, Athuman Idd, Haruni Chanongo na Zahoro Pazi.

Kikosi hicho kinatarajiwa kuondoka Addis Ababa kwenda Marrakech alfajiri ya Juni 3 mwaka huu kwa ndege ya EgyptAir. Stars itatua siku hiyo hiyo Casabalanca na kuunganisha moja kwa moja kwenda Marrakech.

Tuesday, May 28, 2013

KUTOKA KWA ROMARIO MPAKA RONALDINHO - JE NEYMAR ATAFUATA NYAYO ZA WABRAZIL WENZIE NA KUTAMBA CAMP NOU

Romário (1993), Ronaldo (1996), Rivaldo (1997), Ronaldinho (2003) na Neymar (2013). Neymar anajiunga ma urithi mzuri wa washambuliaji wa Brazil unaoundwa na wanaume wanne waliopata mafanikio makubwa katika miongo kadhaa iliyopita na kupata mafanikio makubwa ndani ya Nou Camp - sasa ni zamu  Neymar da Silva.

Romário na Ronaldo
Romário aliigusa mioyo ya mashabiki wa Barca kwenye msimu wa 1993-4, wakati alipopewa jina la “cartoon footballer” kutokana na kuwa uwezo mkubwa mno wa kucheza soka. Aliposajiliwa alihaidi kufunga mabao 30 ya ligi na akatimiza ahadi yake huku kikosi cha Cruyff kikishinda ubingwa msimu huo, Romario alirudi Brazil baada ya nusu ya msimu uliofuatia.

Mara baada ya Romario kuondoka kinda la miaka 19 - Ronaldo De Lima aliwasili Camp Nou. Alikuwa na nguvu, mwenye ujuzi na mwenye uchu wa mabao - kwenye msimu wake wa kwanza alifunga mabao 47 kwenye mechi 51.

Rivaldo na Ronaldinho
Wakati Ronaldo alipohamia Inter, Rivaldo akaja Camp Nou akitokea Deportivo. Rivaldo akawa nyota wa kikosi cha Van Gaal kilichoshinda ligi mara mbili. Alifanikiwa kushinda mchezaji wa dunia mwaka 1999.

Kuwasili kwa Ronaldinho mwaka 2003 kukaleta mageuzi makubwa kwa klabu ya Catalunya na kuleta tabasamu lilopotea na mashabiki wa Barca. Baada ya ukame wa miaka mitano bila kombe, aliiongoza Barca kushinda ubingwa wao wa pili wa ulaya jijini Paris na kushinda uchezaji bora wa ulaya na dunia kwa mara kadhaa. 

Evaristo, Giovanni and Anderson
Romário, Ronaldo, Ronaldinho na Rivaldo wanaweza kuwa ndio washambuliaji wa kibrazil waliopata mafanikio makubwa zaidi, lakini hawakuwa wabrazil pekee walioleta sura za furaha Camp Nou. Kwa mfano miaka ya1950s, Evaristo de Macedo alifunga mabao 173 kwenye 219. Miongo kadhaa baadae mwishoni mwa miaka ya 90, Giovanni Silva na Sony Anderson pia walileta sura za furaha Catalunya kwa viwango vyao.

Sasa ni zamu ya Neymar - je atafuata nyayo za magwiji ya Brazil waliomtangulia kucheza Camp Nou na kuwafunika kabisa kimafanikio? Muda utaongea.

EXCLUSIVE: ADAM NDITI - NIPO TAYARI KUICHEZEA TAIFA STARS MWALIMU AKINIHITAJI KWENYE TIMU YAKE


Wakati nikiwa hapa jijini London leo hii nimepata nafasi ya kukutana na kijana Adam Nditi ambaye mtanzania anayeichezea klabu ya Chelsea ya umri chini ya miaka 21.

Nditi ambaye alizaliwa Zanzibar mwaka 1994 kabla ya kujiunga na timu ya Chelsea U13 miaka kadhaa iliyopita baada ya kuhamia England na familia yake, katika siku za hivi karibuni ameibuka kuwa mjadala mkubwa suala lake la kuichezea timu ya taifa ya Tanzania. 

Siku za nyuma shirikisho la soka nchini TFF liliwahi kutoa ripoti kwamba walijaribu bila mafanikio kuweza kumpata Adam kupitia ubalozi wa Tanzania nchini Uingereza lakini hawakufanikiwa - ingawa Adam Nditi mwenyewe anakanusha hakuwahi kupokea taarifa yoyote kutoka kwa TFF wala ubalozi wa Tanzania UK kuhusu suala la kuja kuichezea Tanzania.
 
"Sijawahi kutafutwa wala kutumiwa mwaliko na TFF, ingawa siku zote nimekuwa tayari kwenda kuitumikia timu yangu ya Taifa kwa sababu mie bado ni mtanzania halisi kabisa."


Mzee Eric Nditi akitukaribisha chakula cha mchana mie na Ismail Sota - baada ya Interview

Kwa upande wa baba yake ya Nditi, aitwaye Eric Nditi amesema yeye kama mzazi wa mchezaji huyo hayupo tayari kumruhusu mtoto wake kuja kuitumikia Taifa stars mpaka pale taratibu zote zitakapofuatwa. "Kiukweli kabisa kama taratibu zote hazitofuatwa Adam hatokwenda Tanzania kuichezea timu ya taifa. Sitokubali mwanangu aende Tanzania kwa taarifa za magazetini, kiutaratibu ili mchezaji aitwe kwenye timu taifa inabidi benchi la ufundi la timu husika lijilidhishe na kiwango cha mchezaji na sio kumuita tu bila kumfanyia scouting, pia inabidi mchezaji atumiwe taarifa rasmi," anasema Nditi.
Nikiwa na Adam Nditi, Ismail Sota na Johnstone Malunde

Pia Eric Nditi amesikitishwa sana na taarifa kwamba mwanae hataki kuichezea timu ya taifa ya Tanzania. "Tatizo la nchi yetu siasa zipo kila mahala, bora wewe Shaffih umekuja mpaka huku kujua ukweli. Adam ni mtanzania wa kuzaliwa na kukulia kwenye nchi hiyo na yupo tayari kuichezea nchi yake  ikiwa atatakiwa na mwalimu. Napenda kuona anaisadia nchi yake lakini kwa utaratibu unaoeleweka."

Monday, May 27, 2013

MAKALA: KWANINI RADAMEL FALCAO ANAKWENDA MONACO? MKATABA ALIOSAINI AKIWA KINDA UNAMFANYA AWE MTUMWA

Kwa umeshasikia kwamba Radamel Falcao anaelekea Monaco. Kulikuwa na tetesi nyingi  Manchester United, Chelsea, Real Madrid na timu nyingine - sasa kwanini ameishia kwenda Monaco?

Jibu ni kwa sababu ya kitu kinachoitwa "third-party ownership" (umiliki wa sehemu tatu) unaomhusisha Radamel Falcao. Kulikuwa na hali kama hii kwenye sajili wa Hulk alipohamia Zenit.

Third-party ownership ni nini?
 Ni umiliki wa haki za kiuchumi za mchezaji zinazomilikiwa na wakala/kampuni/taasisi.

Kuelezea hili inabidi kuangalia mifano ya nyuma na kuona ni namna gani "third party ownership" inavyofanya kazi. Ambao wanafuatilia ligi ya England tayari watakuwa wameshakutana na kitu hiki huko nyuma wakati Carlos Tevez na Javier Mascherano walipojiunga na West Ham United. Hapa ilikuwa mastaa wawili wa kutoka Argentina wakijiunga na klabu ya London ambao walikuwa wanahangaika kubaki kwenye ligi kuu. Utata wa usajili wachezaji hawa wawili ulipelekea West Ham kuwalipa fidia ya £18M  Sheffield United, na hatimaye FA kupiga marufuku third party ownership.

Lakini third party ownership bado ipo na inaendelea kufanyika kwenye bara la ulaya. Inatumika zaidi wachezaji wa Amerika ya Kusini kuhajihakikishia kwenda kucheza Ulaya. Jinsi inavyofanya kazi ni pale wakala/kampuni/taasisi inaponunua haki usajili za mchezaji anayechipukia. Hili linafanyika muda mwingine wakati mchezaji akiwa kwenye klabu, au muda mwingine wakati wa usajili.

Kwa mfano: Kuna mchezaji mmoja mwenye miaka 16 huko Amerika ya kusini atafuatwa na wakala na kuambiwa kama kama nahitaji msaada kwenye masuala ya masoko na kuweza kupenya kwenda kucheza ulaya. Dili za namna hii kawaida huwa zinahusisha suala la kumlipa mshahara mzuri mchezaji, kumtafutia wakala mzuri, management nzuri, mikataba ya matangazo n.k. Ikiwa mchezaji anapokubali, mmiliki wa 3 (third party owner) ataenda kwenye klabu iliyomsajili na kufanya makubaliano ya kununua haki za mchezaji za usajili - aidha zote au nusu.

Mchezaji huyu sasa atakuwa kwenye mikono ya utawala wa timu na umiliki wa third party ownership group, ambao watakuwa wanamuongoza kwenye kila jambo linalohusiana na kazi yake ya soka kutokea hapo. Hilo kawaida huhusisha kumlipa mshahara mkubwa juu ya ule anauolipwa na klabu yake, kumtafutia masoko kwenye vilabu vingine ili kujulikana zaidi, nk.

Namna nyingine ambayo third-party ownership inavyofanya kazi ni pale wakala/kampuni/taasisi inapolipa ada ya uhamisho ya mchezaji. Kwa mfano Porto wanataka kumsaini mchezaji kutoka Brazil lakini hawana fedha za kufanikisha jambo hilo, basi watawafuata wakala/kampuni/taasisi kwa ajili ya kuwezeshwa kifedha kwa dili ya kugawana 50-60% za haki za usajili wa mchezaji husika.
   
Wakala/kampuni/taasisi itawekeza kwa kila kitu kwa mchezaji ikiwa na tumaini kwamba mchezaji kwa muda fulani huko mbele atakuja kuimarika kiuchezaji, kuwa star, na watamuuza kwa gharama kubwa .

Baadhi ya mifano: Tevez na Mascherano waliwekwa kwenye klabu ya West Ham na wawekezaji kwa kuweza kuwapa utambulisho mkubwa kwenye soka la ulaya. Hilo lilifanya kazi kwa wachezaji wote wawili - Liverpool walimsaini Mascherano( kwa kununua haki zote za mchezaji kutoka kwa wewekezaji) na Manchester City hatimaye wakaweza kununua haki zote za Tevez - Manchester United hawakuwa wamenunua haki za usajili za Tevez.Turudi kwa Falcao. Alinunuliwa na third-party ownership group kwenye usajili wake wa kwenda Porto. Wawekezaji walinunua zaidi ya 55% ya haki zake za usajili, walilipa mshahara alipokuwa Porto na baadae wakamuhamishia Atletico kwa dhumuni la mwishowe wamuuze Real Madrid. Wakati Falcao akiwa Atletico, wawekezaji walikuwa wanalipa karibia mshahara wake wote na huku wakifanya kazi ya kumtafutia matangazo ya biashara na pia kutafuta timu tajiri yenye uwezo wa kumnunua ili warudishe fedha zao na faida kubwa juu.

Takwimu za kifedha za Porto zinaonyesha yafuatayo kuhusu uhamisho wa Falcao::
Kuuzwa kwa 60% ya haki za kiuchumi za mchezaji kwa kampuni ya  Natland Financieringsmaatschappij B.V., mwezi July 2009, kwa kiasi cha fedha kinachokadiriwa kufikia 1,500,000 Euro, (manunuzi yamefanyika chini ya mchakato wa umiliki wa 40% za haki za usajili wa Falcao)
Pia kuna kipengele kingine kinachosema kwamba Porto waliwauzia 5% nyingine za Falcao, pia kuna kipengele kingine kinachosema kwamba third party wana ruhusa ya kununua asilimia nyingine 10.

Kitu kama hichi kilitokea kwamba Porto walikuwa wanamiliki 45% ya haki za Hulk.
Falcao akiwa Jorge Mendes pamoja Maradona
Kitu kingine cha kuvutia kuhusu umiliki wa Falcao. Kundi la kibiashara Doyen Sports ambayo ipo chini ya umiliki wa Jorge Mendes (maarufu kama wakala wa Cristiano Ronaldo, ambaye ndiye wakala anayeongoza kwa dili za third party.) pamoja na Peter Kenyon (CEO wa zamani wa Man United na mwenyekiti wa zamani wa Chelsea).
Katika mtandao wao wana ukurasa maalum wa Falcao pia unaweza ukaona wachezaji wengine walio chini yao. Falcao, kama ilivyokuwa kwa Hulk,akaishia kwenye hali ambayo fedha nyingi ziliwekezwa kwenye jina lake kiasi kwamba itahitaji fedha nyingi sana kwa wewekezaji kupata faida ya uwekezaji wao. Walikuwa wanalipa mshahara wake kwa misimu kadhaa, waliwapa Atletico fedha fulani ili kuwawezesha kujiendesha na wakapata udhamini wa jezi kama marejesho ya uwekezaji wao.
Falcao aliishia kujiunga na Atletico kwa ada ya uhamisho wa 40M  - japokuwa Atletico walisema msimu wa nyuma kwamba itabidi wauze wachezaji ili kuweza kupata  220M euro za deni la kodi wanalodaiwa na serikali ya Spain. Ikaja kugundulika kwamba lilikuwa dili la 20 + 20M kwa pande zote mbili klabu na akina Mendes. Mwanzoni Atletico walikubali kulipa kwa vipande 20m yao kwa Porto - wakachelewa kulipa sehemu ya kwanza ya deni na wakaishia kutoa 2.5m na kupelekea Porto kutishia kuwashtaki na kuwapeleka FIFA. Mwishowe 18M za upande wa Atletico zikalipwa na kampuni ya Doylen na hatimaye asilimia 60 za Falcao zikawa mikononi mwa kampuni hiyo. Pia imekuja kuonekana wakati Falcao akiwa na Atletico, Doylen walichukua asilimia nyingine za Falcao baada ya kuwalipia deni lao kwa Porto, kitu ambacho kilipelekea Doylen kuchukua mkataba wa udhamini wa jezi. Namna yoyote, wakawa na shea nyingi kwenye haki za Falcao na Atletico wakawa hawana msemo wowote juu ya mchezaji. Mwishowe inaonekana kama tu ilikuwa suala la mkopo kwa Atletico kutokana na kuwa na hisa chache katika haki za usajili za mchezaji.

Raisi wa Atletico Madrid alikuwa akisistiza mara kwa mara kwamba wanammiliki Falcao kwa asilimia zote, lakini jambo hilo halikuwa ukweli.

Falcao yupo kwenye mkataba wa kulipwa 10M euro kwa mwaka, na kutokana na kulipa mshahara huo wawekezaji wakataka kupata 60M euro katika ada ya uhamisho. Bei hii ikaviondoa vilabu vingi vilivokuwa vikimtaka mchezaji huyo. Atletico hawakuwa na mamlaka ya kuamua ni wapi Falcao aende.

Vilabu vya PSG, Monaco, Real Madrid, Chelsea na City vilikuwa vikimtaka. City kwa sasa hawafanyi uwekezaji mkubwa kwenye usajili. PSG tayari wana washambualiaji wa kutosha. Real Madrid hawakuwa tayari kulipa 60M za usajili + 50M za mshahara wa miaka 5. Chelsea walikuwa tayari kulipa  60M lakini mshahara wa 10M baada ya kodi ulikuwa ni mgumu kuutimiza. Pia Chelsea walikuwa wanashindwa kumnunua mchezaji huyo moja kwa moja kutoka kwa third-party owner - kitu ambacho kiliwaondoa Man United pia kwenye mbio za kusaka saini ya Falcao. Hivyo walihitaji uwepo wa hali ya kama ilivyokuwa wakati wakimsajili David Luiz.

David Luiz alikuwa mchezaji ambaye alikuwa na mkataba na third-party owner hivyo wakati Chelsea wanataka kumnunua iliwalazimu Benfica kununua haki zote za David Luiz kwa asilimia 100 ili kuwauzia Chelsea na kuepeuka sheria ya kukataza biashara ya kununua mchezaji kutoka third-party owner iliyopo nchini England.

Kwa sababu zote zilizotajwa ikabakia klabu moja tu: Monaco. Wana 60M za kuwalipa wawekezaji pia wanazo za 10M mshahara wa mwaka baada ya kodi.

Mwishowe Falcao anazungushwa kwenye vilabu tofauti barani ulaya na wawekezaji wake kwa lengo la kutafuta faida. Yeye mwenyewe hana kauli kwenye kuamua ni wapi anataka kwenda kucheza kwa sababu ya mkataba aliosaini wakati akiwa kidan unamfunga.
IMEANDALIWA NA AIDAN SEIF CHARLIE 

HIZI NDIO SILAHA ZILIZOPATIKANA KWENYE FAINALI YA COPPA ITALIA KATI YA LAZIO VS AS ROMA

Fainali ya mwaka huu ya Coppa Italia kwa mara ya kwanza imezikutanisha timu kutoka Rome, Lazio vs AS Roma hivyo timu zote zikacheza kwenye uwanja wake wa nyumbani (Stadio Olimpico ambao unatumiwa na timu hizo zote). Kutokana na mechi hiyo kuhusisha timu zenye upinzani mkali tena zikigombania kombe mamalaka za usalama walihisi kungeweza kutokea vurugu kubwa hivyo wakaimarisha ulinzi mkubwa kwenye mji huo na viunga vyote vya uwanja wa Stdio Olimpico.

Kufuatiwa ulinzi huo Polisi jijini Roma walikamata silaha nyingi ambazo zingeweza kutoa uhai wa mashabiki ambao wenye upinzani mkali kutokana na mapenzi yao kwa vilabu hivyo viwili vya mji huo - ilipatikana mishale na visu ambazo vingeweza kuharibu mchezo huo wa kihistoria.

Mchezo huo ulifanyika kwa amani na mwishowe Lazio walifanikiwa kubeba kombe la Coppa Italia kwa kuwafunga Roma 1-0, likiwa kombe la 7 la Coppa na la kwanza tangu mwaka 2009.

KALI YA LEO: RIBERY ALALA KITANDA KIMOJA NA KOMBE LA ULAYA PAMOJA NA MKEWE

Winga wa Bayern Munich Franck Ribery amefichua kwamba alilichukua kombe la ubingwa wa ulaya na kwenda kulala kufuatiwa ushindi wa 2-1 dhidi ya Borrusia Dortmund.

Mabingwa wa Bundesliga wamefika kwenye fainali ya Champions League mara tatu katika mika minne lakini wameshinda ubingwa wa ulaya kwa mara ya kwanza tangu mwaka 2001.


Na Ribery akazungumzia namna alivyosherehekea ubingwa huo mara baada ya mchezo: "Nilikuwa macho mpaka saa 11 au 12 asubuhi,"  Sky Sports News.

"Nilienda kulala kabla ya saa 12 na nikachukua kombe la ulaya nikaenda nalo kulala kwenye kitanda kimoja pamoja na mke wangu."

Sunday, May 26, 2013

TAIFA STARS NDANI YA SUTI MPYA ZILIZOANDALIWA KWA AJILI YAO NA MBUNIFU SHERIA NGOWI

Wachezaji wa Taifa Stars na benchi la ufundi katika picha ya pamoja wakionesha suti zao.

Wachezaji wa Taifa Stars, benchi la ufundi na maofisa wakuu wa TBL katika picha ya pamoja wakati wa kuonesha suti mpya

Wachezaji wakifurahia huku wakishangiliwa baada ya kuonesha suti zao mpya.

John Bocco na Erasto Nyoni

Wageni waalikwa wakifuatilia matukio wakati wa hafla ya Kilimanjaro Premium Lager kukabidhi suti mpya kwa Taifa Stars.

TAIFA STARS WAONDOKA KWENDA KUIWEKEA KAMBI MOROCCO ADDIS ABABA

Timu ya Taifa ya Tanzania (Taifa Stars) inatarajia kuondoka leo (Mei 26 mwaka huu) usiku kwenda Addis Ababa, Ethiopia ambapo itaweka kambi na kucheza mechi moja ya kirafiki kabla ya kwenda Morocco.

Stars inayodhaminiwa na Kilimanjaro Premium Lager itaondoka saa 5 usiku kwa ndege ya EgyptAir ikiwa na kikosi cha wachezaji 21 chini ya nahodha wake kipa Juma Kaseja.

Timu hiyo ikiwa Ethiopia, Juni 2 mwaka huu itacheza mechi ya kirafiki dhidi ya Sudan ambapo siku inayofuata itaondoka kwenda Marrakech, Morocco kwa kupitia Cairo, Misri. Mechi hiyo ya mchujo ya Kombe la Dunia dhidi ya wenyeji Morocco itachezwa Juni 8 mwaka huu jijini Marrakech.

Mbali ya nahodha Kaseja, wachezaji wengine wanaoondoka katika kikosi hicho ambacho kina wiki sasa tangu kingie kambini jijini Dar es Salaam ni Mwadini Ally na Ally Mustafa ambao wote ni makipa.

Wengine ni Shomari Kapombe, Kevin Yondani, Aggrey Morris, Haroub Nadir, Mwinyi Kazimoto, Frank Domayo, Mrisho Ngasa, Khamis Mchana, Amri Kiemba, Salum Abubakar, Simon Msuva, John Bocco, Vicent Barnabas, Mudathiri Yahya, Athuman Idd na Haruni Chanongo.

Wachezaji Mbwana Samata na Thomas Ulimwengu ambao wako na timu yao ya TP Mazembe ya Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo watajiunga moja kwa moja na Stars jijini Marrakech, Juni 4 mwaka huu wakitokea Maputo, Msumbiji mara baada ya mechi yao ya Kombe la Shirikisho dhidi ya Liga Muculumana ya huko.

Katika msafara huo wa Ethiopia benchi la ufundi la Stars linaundwa na Kim Poulsen (Kocha Mkuu), Sylvester Marsh (Kocha Msaidizi),Juma Pondamali (Kocha wa makipa), Leopold Tasso (Meneja wa timu), Dk. Mwanandi Mwankemwa (Daktari), Frank Mhonda (Mtaalamu wa tibamaungo) na Alfred Chimela (Mtunza vifaa).