Search This Blog

Saturday, March 8, 2014

KWANINI KIWANGO CHA OSCAR KIMESHUKA KATIKA SIKU ZA HIVI KARIBUNI?

Oscar alianza msimu huu akiwa kwenye form nzuri, kiungo mchezeshaji huyo wa kibrazil alifunga mabao 5 katika mechi zake 12 za kwanza premier league na akawa chaguo la kwanza la Jose Mourinho. Mourinho alijenga kikosi chake kumzunguka Oscar, huku Oscar akicheza kama namba 10 anayekaba kuanzia juu, akitafuta kufunga au kutoa assists. Lakini katika miezi ya karibuni kiwango cha Oscar kinaonekana kupungua. 

Kushuka kiwango
Pamoja na kufunga mabao 5 katika michezo 12 ya kwanza ya msimu wa EPL, Oscar ameweza kufunga bao 1 tu katika michezo 14 iliyofuatia na huku kiwango chake katika eneo la kushambulia kikiwa chini. Takwimu zinaonyesha kupiga mipira iliyolenga goli kumeshuka kwa 44%. Mchoro wa hapo unaonyesha takwimu za mchezo wake jinsi zilivyoshuka.


Kama tunavyoona uwezo wake wa kufunga ulivyoshuka kwa kiasi kikubwa. Kutisha kwake kwenye kushambulia kumepungua na amekuwa hatengenezi nafasi nyingi za kufunga pia, amejaribu kutengeneza nafasi 36 katika michezo 26. Willian ambaye amecheza mechi 18 pekee ametengeneza nafasi 39, wakati Eden Hazard ametengeneza nafasi 77. 
Kwa mchezaji anayecheza kwenye nafasi yake tulitegemea makubwa zaidi, hata kama Oscar anafanya kazi kubwa bila na mpira katika pressing.
Oscar hata hivyo anafanya kazi, katika kukaba na kupora mipira. Lakini, Oscar alishindwa kufanya tackling hata moja dhidi ya Fulham na taratibu amekuwa akishindwa kulifanyia kazi hili zoezi, ingawa mpaka sasa ameweza kufanikiwa kwa 59% ya tackling zote alizojaribu. 

Nini tatizo?
Tatizo hili lilianza pale Mourinho alipowaelekeza vijana wake kucheza kwa kukaba zaidi, Hii ilikuja baada ya michezo kadhaa ambayo Chelsea walikuwa wakiruhusu magoli mengi na kisha wakapoteza mechi ya Capital One waliyotolewa na Sunderland. Tangu wakati huo Chelsea wamekuwa wakicheza kwa kukaba zaidi huku watatu wa kushambulia wakilazimika kurudi kukaba zaidi..
Oscar amekuwa akicheza no. 10, Willian kulia pembeni na Hazard kushoto pembeni, wakati kumekuwepo na mabadilishano, Oscar amekuwa akirudi kucheza chinizaidi na hivyo kupelekea mchango wake katika kushambulia uwe mdogo. Dhidi ya Fulham alikuwa akicheza zaidi katika kiungo cha juu, na sio katika eneo ambalo no. 10 hucheza 
oscar4
Oscar alicheza chini sana kuliko kawaida. Katika mchezo huu hakufanikiwa kufanya tackling hata moja, na alijaribu mara tano kufanya hivyo, kitu ambacho hakiridhishi. Huu ulikuwa mchezo mgumu kwa Oscar, alitengeneza nafasi moja tu. Mwishowe alitolewa kwenye dakika 77. 
Tatizo jingine ni uchovu. Oscar ni mchezaji ambaye hufanya kazi sana na mfumo wa Chelsea unamlazimu kucheza kwa namna hiyo. Akirudi nyuma kukaba pamoja kunyang'anya mipira jambo ambalo linamchosha mno kijana huyo mwenye miaka 22. Oscar ameshacheza mechi nyingi sana katika misimu miwili ndani ya Chelsea, mpaka sasa tayari ameshacheza mechi 101, hapo bila kutaja namba ya michezo ya kimataifa anayoichezea Brazil tangu ajiunge na Chelsea. Ndio maana haishangazi kuona akiwa amechoka na Mourinho labda hajampumzisha vya kutosha, hivyo Mourinho anahitaji kumpa mapumziko kiasi ili aweze kupata matunda mazuri kutoka kwa mchezaji huyo kwa mara nyingine tena.  

Hitimisho
Ni vizuri kutambua kwamba Oscar ana umri wa miaka 22 na ataendelea kukua kuimarika kuwa na kiwango kizuri. Amefunga mabao 6 msimu huu, hata kama hivi sasa anakabiriwa na ukame wa mabao. Msimu uliopita aliweza kufunga mabao manne tu kwenye ligi hivyo unaweza kuona amefanya vizuri kuliko msimu uliopita kwenye kufunga. Mfumo wa Mourinho katika kukaba zaidi unamaanisha Oscar anafanya kazi nyingi zaidi kuliko msimu uliopita, jambo ambalo linamkaba mwenyewe katika kufanya vizuri kwenye kushambulia. Anachohitaji sasa ni kufanyiwa rotation na Mourinho na hapo ndipo tutamuona yule Oscar tuliyemzoea. 

TUTAWASHAMBULIA AHLY KUANZIA DAKIKA YA KWANZA ILI TUPATE BAO LA MAPEMA.



Kocha wa Yanga,Hans Van Pluijm amesema hatabadili mfumo uliotumika Dar Es Salaam kwenye mchezo wa kwanza dhidi ya Al Ahly,
‘’Kwenye mchezo wa Dar Ahly waliwatumia  wachezaji tisa nyuma ya mpira na bado tulifanikiwa kutengeneza nafasi nyingi,naamini kwenye mchezo wa marudiano watalazimika kutushambulia nasisi tutatumia mwanya huo huo kuwashambulia.

Napendelea mchezo wa kushambulia,kama unataka kushinda mechi ni lazima ufunge magoli,lakini pia timu yetu ni nzuri sana kwenye idara ya ushambuliaji kuliko idara ya ulinzi,ningependelea mchezo wa kushambulia lakini wachezaji wanahitaji kuwa na nidhamu kubwa ya kufuata maelekezo’’.

Van Pluijm pia amesema kikosi chake kipo vizuri na hakiogopi majina makubwa ya wachezaji wa Ahly, ‘’Majina hayachezi mpira bali timu ndio inacheza, kinachotakiwa ni wachezaji kujiamini na kuamini wanaweza,wakifanikiwa katika hilo naamini tutawashangaza ‘’.



Friday, March 7, 2014

PICHA YA SIKU: MASHABIKI WA SPURS WAMPELEKEA WILSHARE ZAWADI YA KITI CHA WALEMAVU


RASMI : EMAD MOTEAB KUIKOSA YANGA NA KIUNGO HOSSAM ASHOUR AGOMA KUONGEZA MKATABA.


KIKOSI cha Al Ahly kimeanza kupata pigo kabla ya kuwavaa Yanga baada ya kiungo wake Hossam Ashour kugoma kuongeza mkataba huku mshambuliaji Emad Moteab akiondolewa katika orodha ya nyota 23 walioingia kambini jana kujiandaa na mchezo huo.

Taarifa ambazo zimetolewa jana na klabu hiyo zimeleeza kwamba Ashour ambaye licha ya kugoma kuongeza mkataba atakuwemo katika mechi dhidiya Yanga amegoma kuongeza mkataba mpya wa kuendelea kusalia katika timu hiyo ambapo wachambuzi wanadai hilo limesababishwa na hali mbaya ya kifedha inayoiandama timu hiyo kwasasa.

Kiungo huyo ambaye taarifa zake zimeleta mshtuko mkubwa katika kambi ya Ahly, amewaambia hata saini mkataba kwasasa akiwataka kusubiri mpaka mwisho wa msimu huku taariofa zikienea kwamba ameshasaini mkataba wa awali na klabu ya Gulfs  ambayo haijajulikana mara moja ni timu kutoka Saudi Arabia au Falme za Kiarabu.

Wakati hali ikiwa hivyo kocha mkuu wa Ahly Mohamed Yousef ametangaza nyota 23 waliotangulia Alexandria kuweka kambi ya masaa 48 kabla ya mchezo bila ya mshambuliaji wao Moteab ambaye bado ni majeruhi.

Nyota huyo ambaye pia aliukosa mchezo wa kwanza uliopigwa wiki moja iliyopita jijini Dar ambao Ahly ilichapwa kwa bao 1-0 kikubwa akiwa na maumivu ya mgongo ambayo bado hajaweza kuwa sawa.

Taarifa hizo za kukosekana kwa Moteab ni habari njema kwa kocha wa Yanga Hans Van Pluijm ambaye mara kwa mara amekuwa akimhofia zaidi ambapo mshambuliaji huyo ni hatari kwa kuwahadaa mabeki wa timu pinzani.

Wakati huohuo uongozi wa Ahly umelazimika kuwapoza nyota wao kuwa kupawa posho kabla ya mchezo huo ambapo taarifa kupitia Abdel -Hafiz ambaye ni Mkurugenzi wa Ufundi amesema wamelazimika kuwalipa wachezaji wao kiasi cha Paundi 10000(Sh milioni 2.2) ikiwa ni sehemu ya mishahara yao ya mwezi kutokana na ukata mzito unaowakamili.

ARSENAL WATAKA FIDIA YA PAUNDI 600,000 KWA FA BAADA YA WILSHARE KUUMIA AKIICHEZEA ENGLAND


Katika mkutano wa waandishi wa habari Ijumaa ya leo, meneja wa Arsenal, Arsene Wenger amekiri kwamba Jack Wilshare atakuwa nje ya dimba kwa wiki 8 baada ya kuvunjika mguu.

Kiungo huyo kinda wa Arsenal hivi sasa ana mashaka kama atakuwemo katika kikosi cha ENGLAND kitakachoenda World Cup, huku kukiwa na uwezekano mdogo wa kucheza katika msimu huu wa ligi tena ambao upo mwishoni.

Kwa mujibu wa gazeti la The Sun ni kwamba Arsenal leo wametuma barua rasmi kwenda FA wakidai fidia ya £600,000 baada ya Wilshere kupata majeruhi hayo akiwa anaitumikia England katika mchezo wa ushindi wa 1-0 dhidi ya Denmark.

Arsenal wanasemekana wameudhika kwamba mchezaji huyo ambaye amekuwa akiandamwa na majeruhi aliachwa aendelee kucheza hata baada ya kuumia.

AMISI TAMBWE APIGWA FAINI KWA MATUSI, SIMBA YAPIGWA FAINI KWA UCHAWI NA VURUGU


Bodi ya Ligi Kuu Tanzania (TPLB) imeipiga faini ya jumla ya sh. milioni moja klabu ya Simba kutokana na makosa mbalimbali ikiwemo vitendo vinavyoashiria ushirikina uwanjani.

Simba ilifanya vitendo hivyo katika mechi yake dhidi ya Mbeya City ambapo imepigwa faini ya sh. 500,000. Pia imepigwa faini nyingine ya sh. 500,000 kwa makocha wake Loga, Selemani Matola na Idd Pazi kuingia uwanjani na kumzonga mwamuzi kwenye mechi hiyo.

Naye mshambuliaji wa Simba, Amisi Tambwe amepigwa faini ya sh. 500,000 kwa kushangilia bao alilofunga kwenye mechi hiyo kwa kuonesha ishara ya matusi kwa kidole.

Mbeya City imepigwa faini ya sh. 300,000 kwa washabiki wake kuingia uwanjani na silaha kwenye mechi dhidi ya Kagera Sugar iliyochezwa mjini Bukoba. Klabu za Yanga na Coastal Union zimepigwa faini ya sh. 500,000 kila moja kwa washabiki wao kurusha chupa za maji uwanjani wakati timu hizo zilipopambana jijini Tanga.

Kiungo wa Mtibwa Sugar, Shabani Nditi amepigwa faini ya sh. 500,000 kwa kumpiga mchezaji wa Simba, wakati Salvatory Ntebe pia wa Mtibwa Sugar amepigwa faini ya sh. 500,000 kwa kumtukana refa kwenye mechi dhidi ya Mbeya City.

Pia mshambuliaji wa Mtibwa Sugar, Musa Mgosi amepigwa faini ya sh. 500,000 kwa kosa la kupiga uwanjani kwenye mechi dhidi ya Ashanti United ambapo vilevile atakosa mechi tatu za ligi. Coastal Union imepigwa faini ya sh. 500,000 kwa washabiki wake kumrushia chupa za maji kipa wa Mbeya City.

Nayo JKT Ruvu imepigwa faini ya sh. 300,000 kwa kuchelewa kufika uwanjani kwenye mechi dhidi ya Simba iliyochezwa Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.

Vilevile wamiliki wa Uwanja wa Mkwakwani jijini Tanga wameandikiwa barua ya kufanya marekebisho ya vyumba vya wachezaji, kwa vile havina hewa ya kutosha.

Kwa upande wa Ligi Daraja la Kwanza (FDL) klabu zilizopigwa faini kutokana na makosa mbalimbali ni Friends Rangers (sh. 200,000), Lipuli (sh. 200,000), Majimaji (sh. 400,000), Polisi Morogoro (sh. 400,000) na Transit Camp (sh. 200,000).

Kocha Msaidizi wa Polisi Morogoro, John Tamba atapelekwa kwenye Kamati ya Maadili kutokana na vitendo visivyo vya kimaadili katika mechi dhidi ya Burkina Faso.

Kiongozi wa Lipuli, Hamis Kiemba na wachezaji Boniface Sawaka, George Enock na Green Paul watapelekwa katika Kamati ya Nidhamu kutokana na utovu wa nidhamu waliofanya kwenye mechi dhidi ya Kimondo.


Naye mchezaji Sangalau Nyamoka wa JKT Kanembwa aliyelalamikiwa uhalali wake na Polisi Tabora suala lake linapelekwa Kamati ya Nidhamu.

BARUA YA WAZI YA DAVID MOYES KWENDA MASHABIKI WA MANCHESTER UNITED

Kocha wa Manchester United David Moyes ameandika barua ya wazi kwa mashabiki wa klabu hiyo akielezea kwamba msimu wake wa kwanza ndani ya klabu umekuwa m'bovu zaidi kuliko ilivyotegemewa.

Akiwasifu mashabiki kwa uvumilivu wao, Mscotish ambaye aliteuliwa na Sir Alex Ferguson, amekiri kwamba matokeo yao mabovu yamemshangaza mpaka yeye lakini ana uhakika kila kitu kitakaa sawa mbeleni.

"Wakati nilifahamu hii kazi ingekuwa na changamoto nyingi wakati nilipopewa jukumu hili, lakini msimu mgumu tulionao hakikuwa kitu ambacho nilikifiria, jambo ambalo nina uhakika mashabiki wote hawakudhani hali ingekuwa hivi," aliandika Moyes.

"Wachezaji wangu, na makocha wenzangu wanajaribu kwa kila kuhakikisha timu inarudi katika kufanya vizuri.

"Wote tumezoea kuiona Manchester United inayofanikiwa na sapoti mliyowapa wachezaji na mimi katika kipindi chote cha msimu ni kubwa sana. Tunapocheza ugenini mashabiki wetu waliosafiri wameendelea kuwa bora kabisa katika nchi hii na wakati tunapokuwa Old Trafford imani yenu kwenye timu imekuwa ikionekana wazi.

"Kuisapoti timu yenu wakati inashinda ni rahisi lakini ni ngumu sana wakati mambo yanapokuwa yanaenda vibaya, nyinyi mmekuwa nasi katika kipindi chote."

 "Kila magumu tunayopitia yatatufanya tuwe bora zaidi, timu imara na klabu bora huko mbeleni.

"Kwa miaka mingi sasa mmekuwa mkishuhudia vikosi vya ushindi na kwa muda fulani, nina uhakika kabisa tutaiona Manchester United tuliizoea."

VIDEO: HUYU NDIO MRITHI WA VICTOR VALDES FC BARCELONA

VIDEO: ANGALIA WACHEZAJI WA CHELSEA WAKICHEZA WIMBO WA TUPOGO WA OMMY DIMPOZ


Mtanzania anayekipiga timu ya Chelsea Adam Nditi amewarekodi wachezaji wenzie wa Chelsea wakiwa wanacheza wimbo wa mwanamuziki wa kitanzania Ommy Dimpoz uitwao 'TUPOGO'

YANGA VS AL AHLY SASA KUPIGWA ALEXANDRIA - OKWI NA KIIZA WAWASILI


Baada ya utata juu ya ni sehemu gani utakaofanyika mchezo wa marudiano kati ya wenyeji Al Ahly dhidi ya wawakilishi pekee wa Tanzania kwenye mashindano ya Kimataifa Young Africans huku ikiwa iebakia siku tatu kabla ya mchezo, maamuzi ya shirikisho la soka nchini Misri yameamulu mchezo huo utafanyika mjini Alexandria katika Uwanja wa Border Guard stadium (Haras el Hadod)

Taarifa ya Chama cha Soka nchini Misri imesema mchezo huo ambao awali ulikua ufanyike katika jiji la Cairo sasa utafanyika katika mji wa Alexandria takribani kilometa zaidi ya 200 kutoka Cairo ambapo kikosi cha Young Africans kimeweka kambi kujiandaa na mchezo huo.

Mara baada ya kupata taarifa hizo kupitia Ubalozi wa Tanzania nchini Misri, uongozi wa Young Africans uliopo jijini Cairo ukiongozwa na makamu mwenyekiti Clement Sanga ambaye pia ndio mkuu wa msafara, tayari umeanza maandalizi ya kuhakikisha timu inakwenda mjini Alexandria kucheza mchezo huo wa jumapili na kufanya vizuri.

Ni jambo la kushangaza taarifa za Uwanja zinatolewa siku tatu kabla ya mchezo huku fika wahusika wakitambua kuwa Young Africans ilifahamu mchezo huo utafanyika Cairo takribani wiki mbili zilizopita viongozi wa Al Ahly waliopokuwa nchini Tanzania walidhibitisha hilo.

Pamoja na mabadiliko hayo ya ghafla ya sehemu utakapofanyika mchezo siku ya jumapili, benchi la ufundi pamoja na wachezaji na viongozi waliopo jijini Cairo bado wana imani ya kufanya vizuri na kusonga mbele katika hatua ya 16 bora.

Wakati huo huo washambuliaji wawili wa timu ya Taifa ya Uganda Hamisi Kizza na Emmanuel Okwi tayari wameshawasili jijini Cairo majira ya saa 7 usiku kwa shirika la ndege la Egypt Air wakitokea nchini Zambia walipokuwa wakiiwakilisha timu yao ya Taifa kwenye mchezo wa kirafiki jana siku ya jumatano.

Wachezaji hao mara baada ya kuwasili Uwanja wa ndege moja kwa moja wameungana kambini na wachezaji wengine katika Hoteli ya Nile Paradise Inn kuendelea na maandalizi ya mchezo huo wa jumamosi.

Mchezo huo wa siku ya jumapili ambao unafanyika mjini Alexandria katika Uwanja wa Border Guard Stadium (Haras El Hadod) hautakua na watazamaji kutokana na mamalaka ya ulinzi na usalama kuzuia mashabiki kuingia katika mchezo wowote wa mpira wa miguu nchini Misri.

OKWI NA KIIZA TAYARI WAMETUA NCHINI MISRI!

 Washambuliaji wa Yanga, Emmanuel Okwi na Hamis Kiiza wamewasili jijini Cairo usiku wa manane wakitokea nchini Zambia walikokuwa na timu ya Taifa ya Uganda tayari kuwakabili Al Ahly hapo siku ya jumapili mjini Alexandria.
Wachezaji hao walipokelewa uwanja wa ndege wa Cairo na afisa habari wa timu hiyo Baraka Kizuguto pamoja na maafisa wawili kutoka ubalozi wa Tanzania nchini Misri.
         Kiiza,Okwi na Shaffih mara baada ya kufika uwanja wa ndege wa Cairo.

Mara baada ya kuwasili wachezaji hao walielekea moja kwa moja kwenye kambi ya timu iliyopo nje kidogo ya mji wa Cairo.


KUTOKA KWENYE FB! YANGA YAWASILI SALAMA NCHINI MISRI.








Thursday, March 6, 2014

MOURINHO: WACHEZAJI WA MADRID WANAJALI ZAIDI MUONEKANO WAO KULIKO KUSHINDA VIKOMBE


Kocha wa Chelsea Jose Mourinho amesema kwamba wachezaji wa klab yake ya zamani ya Real Madrid wanajali zaidi kuhusu muonekano wao hadharani kuliko hata kushinda makombe.

Kocha huyo mreno ambaye aliondoka Madrid na kurudi Chelsea baada ya kukaa Santiago Bernabeu kwa misimu mitatu amesema hakuwa anapendezewa na tabia hiyo wakati yupo kwenye klabu hiyo.

"Mara nyingi pale Real Madrid, wachezaji utawakuta kwenye vioo kabla ya mchezo ya mchezo wakati refa anawasubiri kuelekea uwanjani," Mourinho aliliambia gazeti Esquire.

"Lakini hivi ndivyo ilivyo jamii ya vijana wa siku hizi. Vijana wanajali sana kuhusu muonekano wao, wapo katika miaka ya 20 na mie 51 na ikia unataka kufanya kazi na watoto inabidi uielewe dunia yao.

WIKI MOJA KABLA YA MECHI YAO - MASHABIKI WA LIVERPOOL WAMUITA MOYES "GENIUS WA SOKA"


Mechi yao inaweza kuwa wiki kadhaa mbele kutoka sasa, lakini mashabiki wa Liverpool tayari wameshaanza maandalizi ya mchezo dhidi ya Manchester United utakaopigwa Old Trafford March 16th.

Kwa mara ya kwanza katika kipindi cha muda mrefu, Liverpool wapo juu ya Manchester United katika msimamo wa ligi mpaka kufikia mwezi huu. Wakishika nafasi ya pili wakati kikosi cha David Moyes kikiwa nafasi ya 7.

Huku wakiwa na matumaini ya kubeba ubingwa mbele ya Chelsea, City - mashabiki wa Liverpool wapo katika hali ya kuwakejeli wenzano wa United, na sasa tayari wameshatengeneza bango kubwa la kumkejeli kocha wa mahasimu wao David Moyes.

Hili ndio bango linalosomeka 'David Moyes ni Genius wa Soka'



MATOKEO YA MECHI ZOTE KIRAFIKI: URENO, BRAZIL ZAUA, UFARANSA YAINYOOSHA UHOLANZI, SPAIN YAENDELEA KUMUONEA ITALY


FT Japan 4 – 2 New Zealand
FT India 2 – 2 Bangladesh
FT Malawi 1 – 4 Zimbabwe
FT Burundi 1 – 1 Rwanda
FT Georgia 2 – 0 Liechtenstein
FT Iran 1 – 2 Guinea
FT Kosovo 0 – 0 Haiti
FT Russia 2 – 0 Armenia
FT Zambia 2 – 1 Uganda
FT Azerbaijan 1 – 0 Philippines
FT Lithuania 1 – 1 Kazakhstan
FT Bulgaria 2 – 1 Belarus
FT Burkina Faso 1 – 1 Comoros
FT Mozambique 1 – 1 Angola
FT Albania 2 – 0 Malta
FT Algeria 2 – 0 Slovenia
FT Greece 0 – 2 South Korea
FT Hungary 1 – 2 Finland
FT Mauritania 1 – 1 Niger
FT Montenegro 1 – 0 Ghana
FT South Africa 0 – 5 Brazil
Postp. Sudan ? – ? Kenya
FT Czech Republic 2 – 2 Norway
FT Israel 1 – 3 Slovakia
FT Bosnia-Herzegovina 0 – 2 Egypt
FT Andorra 0 – 3 Moldova
FT Botswana 3 – 0 South Sudan
FT Colombia 1 – 1 Tunisia
FT Cyprus 0 – 0 N.Ireland
FT FYR Macedonia 2 – 1 Latvia
FT Namibia 1 – 1 Tanzania
FT Senegal 1 – 1 Mali
FT Luxembourg 0 – 0 Cape Verde
FT Turkey 2 – 1 Sweden
FT Gibraltar 1 – 1 Estonia
FT Morocco 1 – 0 Gabon
FT Romania 0 – 0 Argentina
FT Ukraine 2 – 0 USA
FT Austria 1 – 1 Uruguay
FT Switzerland 2 – 2 Croatia
FT Belgium 2 – 2 Ivory Coast
FT Germany 1 – 0 Chile
FT Ireland 1 – 2 Serbia
FT Poland 0 – 1 Scotland
FT Wales 3 – 1 Iceland
FT Australia 3 – 4 Ecuador
FT England 1 – 0 Denmark
FT France 2 – 0 Netherlands
FT Portugal 5 – 1 Cameroon
FT Spain 1 – 0 Italy

CRISTIANO RONALDO SASA NDIO MFUNGAJI BORA WA MUDA WOTE WA URENO

Mwanasoka bora wa dunia na nahodha wa timu ya taifa ya Ureno Cristiano Ronaldo ameandika historia mpya katika soka jana usiku kwenye mchezo wa kirafiki dhidi ya Cameroon ambapo Ureno walishinda mabao matano kwa moja.
Ronaldo ambaye alifunga mabao mawili kwenye mchezo huo yaliyomfanya kuweka rekodi ya kuwa mchezaji wa timu ya taifa ya Ureno aliyefunga mabao mengi zaidi katika historia ya timu hiyo ya taifa.
Winga huyo wa Real Madrid sasa amefikisha jumla ya mabao 49, mawili zaidi ya Pauleta ambaye alikuwa anashikilia rekodi ya kufunga mabao huko nyuma.
Listi ya wafungaji bora wa muda wote wa Ureno
1. Cristiano Ronaldo (109 caps) - 49 goals
2. Pauleta (88 caps) - 47 goals
3. Eusebio (64 caps) - 41 goals

4. Luis Figo (127 caps) - 32 goals
5. Nuno Gomes (79 caps) - 29 goals

Wednesday, March 5, 2014

HIKI NDICHO KIKOSI CHA TIMU YANGU KWENYE BBALL KITAA



POINT GUARDS;
1.ASHRAF HAROUN
2.ROMA
3.EVANCE

SHOOTING GUARD;
4.STEPHANO MSHANA
5.SARINGO HAROUN
6.GODY MLAGILA

POWER FORWARD;
7.ACHIM JOACHIM
8. STEVE MACHO
9.JOAS

FORWARD:
10. DAUDI
11. FRANK MWEMEZI
12.CHACHA TUBERT

COACH;
MOHAMMED MBWANA

ASST COACH;
SHAFII DAUDA

FRED CHIMELLA AACHWA KATIKA SAFARI YA TAIFA STARS BAADA YA KIPINDI CHA MIAKA 8.....


   Fred Chimella ( kulia ) akiwa na Shaffih Dauda.


Mtunza wa vifaa wa timu ya taifa ya Tanzania Fred Chimella ameachwa katika safari ya timu hiyo iliyoenda kuivaa Namibia katika mchezo wa kirafiki uliopo kwenye kalenda ya FIFA.
Hapo awali  alibaki aweze kuondoka na wachezaji Hassani Mwasapili na Edward Charles ambao walikuwa hawana hati ya kusafiria,lakini baada ya hati za wachezaji hao kuchelewa kutoka ilibidi safari hiyo isiwepo tena. 

Chimella ambaye safari yake ya kwanza nje ya nchi ilikuwa wakati Tanzania inaenda kupambana na Msumbiji mwaka 2006 - wakati ikiwa chini ya kocha mbrazil Marcio Maximo.

Taifa Stars ilikodisha ndege ya serikali kwenda nchini Msumbiji, lakini katika hali isiyoeleweka jina la Chimella halikuwekwa kwenye orodha ya wanaosafiri na timu. Hivyo timu ilipotoka kambini Msasani kuelekea Airport, Chimella alibaki hotelini.

Timu ilipofika uwanja wa ndege wachezaji wote na viongozi  waliingia kwenye ndege tayari kwa safari, lakini kocha Marcio Maximo alipoingia kwenye ndege hakumuona kit manager wake bwana Chimella, alipomuulizia mahala alipo,wachezaji wakamjibu kabaki hotelini kwa sababu jina lake halikuwemo kwenye listi ya wanaosafiri kwa sababu alikosa nafasi.
Maximo akachukua listi akaliona jina la Afisa Habari wa TFF wakati huo bwana Florian Kaijage na akawaambia viongozi wa msafara Mohamed Dewji na Crescentus Magori kwamba wamuondoe Kaijage kwa sababu hakuwa na msaada kwake na badala yake asafiri Fred Chimela. 


Hivyo iliwabidi Magori na Dewji wamfuate Chimela Msasani wakiongozwa na Polisi Escort ili wasikae kwenye foleni, hatimaye walifanikisha kumfuata Chimella na akasafiri na timu.Tangu wakati huo Chimella mwenye cheti cha utunzaji vifaa vya michezo alichokipata nchini Brazil hajawahi kuikosa safari ya Taifa Stars.

NIONAVYO MIMI: KUNA MUDA TUNAMUONEA BURE JAMAL MALINZI


Na Oscar Oscar Jr.
0789-784858

Utani wa mashabiki wa Simba na Yanga kwenye mechi za wao kwa wao au mmoja dhidi ya timu nyingine kutoka nje ya nchi kuna muda naupenda na naona faida yake ingawa,kuna muda unakosa maana. Ukiona mashabiki wa Simba wanaiponda Yanga,maana yake ni kwamba,wanawafanya Yanga waendelee kufanya vizuri kwa kukwepa kuzongwa na mashabiki hao wa Msimbazi na kinyume chake, ushabiki wa namna hii, binafsi naupenda. Sina tatizo kabisa siku nitakapokutana na habari kuwa mwenyekiti Ismail Aden Rage ameamua kuwauzia Yanga mshambuliaji wake Amis Tambwe huku, Yussuph Manji naye akiwauzia watani zake hao kiungo, Haruna Niyonzima. 

Kitendo cha kung'oa viti kilichotokea uwanja wa Taifa kwenye mchezo wa timu ya Yanga dhidi ya mabingwa watetezi wa kombe la klabu bingwa Afrika timu ya National Al Ahly toka nchini Misri si cha kiungwana na wala si cha kistaarabu kabisa. Tukio hilo sio mara ya kwanza kutokea, iliwahi pia kutokea kwenye mchezo wa ligi kuu kati ya timu ya simba dhidi ya Kagera Sugar mzunguko wa kwanza msimu huu baada ya mashabiki wa simba kuonekana kutoridhika na maamuzi ya mwamuzi wa mchezo huo. Mashabiki hao walionyesha hasira zao kwa kung'oa viti na kuvitupa chini! Nadhani kuna haja ya kulitazama swala hili upya huku kipaumbele kikiwa ni kupeana elimu na kuepuka kunyoosheana vidole.

Tutakuwa tunamuonea bure Rais wa TFF Jamal Malinzi kama hadi suala la ulinzi wa viti uwanjani tunahitaji yeye ndiye asimamie. Ni muda muafaka sasa kwa viongozi wa klabu zetu zote nchini kukaa chini na mashabiki na wanachama wao na kuwaelimisha juu ya umuhimu wa kutunza miundombinu ya viwanja vyetu hasa, ule wa taifa uliopo jijini Dar es salaam. Tukiendelea kunyoosheana vidole huku hawa wakisema wanaong'oa viti ni mashabiki wa Simba na wale, wakisema ni mashabiki wa Yanga, tutajikuta uwanja wote hauna kiti hata kimoja na hakuna wakumuuliza!

Lakini pia, mashabiki wa Simba na Yanga ni lazima watambue kwamba pamoja na kuwa uwanja huo wa Taifa umejengwa jijini Dar es salaam haina maana kuwa wananchi wanaoishi katika jiji hilo ndiyo wamiliki wa uwanja huo. Mashabiki wachache wanaoharibu miundombinu ya uwanja huo ni lazima watambue kuwa hawawatendei haki wananchi waishio Mwanza, Tabora, Singida, Kigoma, Songea na sehemu mbalimbali za Jamhuri ya muungano wa Tanzania kwa sababu na wao wamechangia kupatikana kwa uwanja huo kupitia kodi mbalimbali wanazolipa serikalini.

Kwenda kuangalia mpira uwanjani ni mtoko kama wanavyotoka watu na familia zao kwenda kwenye majumba ya sinema,kwenda Bar, kuna watu wanakwenda kutembelea mbuga za wanyama na kwenye vivutio mbalimbali. Mashabiki wa klabu ya Arsenal wa jijini London Uingereza huwa wanafurika kuanzia asubuhi maeneo ya starehe yanayozunguka uwanja wao wa Emirates kila siku timu hiyo inapokuwa na mechi hata kama mchezo huo utafanyika saa 1 jioni, wanashinda nje ya uwanja huo wakistarehe na familia zao mpaka muda wa mechi unapofika.

Uwanja wa Ali Hassan Mwinyi-Tabora, Kumbukumbu ya Sokoine-Mbeya na Jamhuri-Dodoma ni baadhi ya viwanja ambavyo nimewahi kuvitembelea na kuangalia mechi mbalimbali lakini kwa utafiti wangu mdogo, nimegundua wanaume ndiyo wengi wanaokwenda kutazama mpira uwanjani. Ukijiuliza kwa nini wanawake,watoto na wazee hawaendi viwanjani,jibu ni rahisi tu. Hivi ni nani atakwenda na mwanae uwanjani wakati timu moja ikifungwa, mashabiki wa timu pinzani wanarusha mawe na makopo ya haja ndogo? Ni nani atakwenda uwanjani na bibi yake wakati kuna muda mabomu ya machozi yanatumika kuwatuliza mashabiki wang'oa viti?

Moja kati ya sababu zinazotajwa kusababisha vurugu viwanjani ni pamoja na watu kutumia pombe hasa aina ya Viroba ambapo mashabiki wa timu kama Mbeya City wa jijini Mbeya wamegueza kama ndiyo utamaduni wao. Lakini najiuliza tena,mbona watu wengi wanakwenda na familia zao Bar kila mwisho wa wiki sehemu ambayo Viroba na vileo vingine viko "Full charge" na wanarudi nyumbani salama? au Viroba vya uwanjani ndiyo vikali zaidi? au kuna kaushamba fulani? au hatujui maana halisi ya mchezo wa soka? au tunamuhitaji Jamal Malinzi atuelekeze na hili?

Mechi ya Senegal dhidi ya Ivory Coast ambayo ilichezwa mwaka 2012 mjini Dakar kuwania kufuzu fainali za AFCON 2013 ililazimika kusitishwa kipindi cha pili baada ya mashabiki wa Senegal kuanza kung'oa viti na kutupa mawe uwanjani kufuatia Ivory Coast kuwa mbele kwa mbao 2-0.Matukio kama haya yaliyowahi kutokea kwa wenzetu ni lazima tujifunze na kuchukuwa hatua mapema za kuyadhibiti.Kazi ya kuwadhibiti hawa "mashabiki maandazi" sio ya Jamal Malinzi,ni jukumu la kila mdau wa soka bila kujali timu unayoshabikia.

Tukiamua,hatumuhitaji Malinzi wala askari polisi kutusaidia kuwadhibiti watu wachache wanaotaka kutufanya watanzania wote tuonekane hatuna maana.Kila mmoja akiwa mlinzi wa mwenzake ninaamini,huo utakuwa ulinzi wenye tija kuliko kitu chochote kile.Kama walevi wanaweza kuwadhibiti watu wachache ambao huwa wanawaletea vurugu wakati wao wakistarehe na wanafanikiwa,iweje sisi tunawachekea hawa wasio litakia mema soka la nchi yetu?

Ushabiki sugu kuna muda unakuwa kama ujinga.Mara kadhaa tumekuwa tukisikia kwenye vyombo vya habari mashabiki wameuwawa au wamejiuwa baada ya timu wanazoshabikia kutopata matokeo mazuri,huu ni upuuzi.Wakati wewe umejidhuru au kutuharibia miundombinu ya uwanja wetu,wachezaji walioshiriki kwenye mchezo huo baada ya dakika 90,wanabadilishana jezi na kukumbatiana! Hivi unadhani Yussuph Manji na Ismail Aden Rage hawasemeshani? hahahaa...utakuwa bado unaishi zama za mawe!

Rais wa TFF bado anakazi kubwa sana ya kuufikisha mpira wa Tanzania mahali ambapo watu wengi wanatamani tufikie.Watanzania wanatamani kuona klabu zetu zikifika mbali na kupata mafanikio kwenye michuano ya CECAFA na ile ya CAF ili tuweze kutengeneza timu bora ya taifa na yenye ushindani kwenye michuano mbalimbali kama vile ile ya kufuzu CHAN,AFCON na ikiwezekana,hata kombe la dunia pia tunalitaka lakini,kama hadi ulinzi wa viti uwanjani tunamtaka Jamal Malinzi asimamie,atamaliza muda wake hajafanya lolote na tusimlaumu kabisa.

MWAPEWA MTUMWA , FLORA KAYANDA POMBE YA NINI TWIGA STARS?, MNAWAKERA WAPENDA SOKA!!


Na Baraka Mpenja 

NDOTO kubwa ya wanandinga wa Tanzania na Afrika nzima ni kucheza soka la kulipwa katika ligi kubwa duniani kama vile ligi kuu nchini England, Hispania, Ujerumani, Ufaransa, na Italia.
Hakuna mwanasoka mwenye malengo asiwaze kucheza katika ligi hizo zilizosheheni klabu zenye mvuto mkubwa zaidi duniani na wanasoka bora wa Dunia.
Hakika ni sifa kubwa sana kwa mchezaji wa Kiafrika kuonekana katika runinga akisakata kabumbu anga za kimataifa. Simaanishi anaishia kupata sifa tu, bali hata `mkwanja` unaopatikana katika soka hilo ni mkubwa.
Nani asiyefahamu utajiri wa Samuel Eto`o, Didier Drogba, Yaya Toure na wengine wengi kutoka nchi za magharibi mwa Afrika.
Hapa Tanzania bado hatujafanikiwa kupata wanasoka mahiri wa kwenda kucheza ligi za wenzetu zaidi ya kuwaona wachezaji wetu wakienda kucheza ligi za kawaida kabisa huko Uarabuni na mataifa ya kiwango cha chini kisoka barani Ulaya.
Wengine kama Mbwana Ally Samatta na Thomas Emmanuel Ulimwengu wamejaribu na wamethubutu na ndio maana unawasikia na kuwaona TP Mazembe ya Jamhuri ya kidemokrasia ya Kongo.
TP Mazembe ni moja ya klabu kubwa yenye utajiri mkubwa barani Afrika. Kwa wachezaji wa Kitanzania ni moja ya klabu inayowafaa na ndio maana Samatta alitajwa kuwa miongoni mwa wachezaji wanaowania tuzo ya mwanasoka bora wa Afrika kwa wachezaji wanaocheza ligi za ndani.
Ukiwauliza wachezaji wengi wa Tanzania, nini malengo yao? Jibu huwa ni jepesi sananataka kucheza soka la kulipwa. Sio tatizo kwa jibu hili, lakini bado ipo haja ya kujiuliza tena, huyu anayetaka kucheza soka hilo anaweza kutimiza ndoto hizo?.
Swali hili huwa linanikosesha majibu ya haraka kila nikitafakari hali halisi ya wachezaji wa Kitanzania ambapo wengi wao wana malengo makubwa, lakini utekelezaji wake ni mdogo sana, nidhamu mbovu na kulewa sifa wakati bado hajafanikiwa malengo yake.
Achana na hayo, kwasasa Dunia  inajadili sana soka la wanawake.
Hakika Mpira wa miguu kwa wanawake ni moja ya michezo inayokuwa kwa kasi katika bara la Afrika na hata hapa nyumbani.
Idadi ya wasichana wanaoshiriki katika mpira wa miguu imekuwa ikiongezeka mwaka hadi mwaka.
Ukiwasikia TFF /TWFA pamoja na wadau wa soka,  wanaamini kuwa ili kuwa na kiwango kizuri na maendeleo katika mpira wa miguu wa wanawake  ni lazima kuanza na vijana wadogo.
Wakati mawazo haya yakitawala vichwani mwa viongozi wa soka, tayari Wapenda michezo nchini wameshaanza kushabikia soka la wanawake.
Leo hii mashabiki wanaenda kuishangilia timu ya Taifa ya wanawake, Twiga Stars na wengine kuiombea dua njema ili ifanikiwe katika harakati zake za kulitangaza soka la wanawake.
Sina wasiwasi na vijana wa Twiga stars, nimefanya mahojiano nao mara kwa mara.
Kiukweli ukiwasikia, wana nia ya kucheza soka la kulipwa kama ilivyotokea kwa dada yao na nahodha, Sophia Mwasikili ambaye alibahatika kupata timu nchini Uturuki, ingawa kwasasa amerudini nchini.
Hivi karibuni, Twiga Stars ilikuwa katika mchezo mgumu wa kuwania kufuzu fainali za mataifa ya Afrika kwa wanawake (AWC) dhidi ya Zambia (Shepolopolo).
Twiga Walifungwa mabao 2-1 mjini Lusaka na waliporudi nyumbani walitoka sare ya bao 1-1 uwanja wa Azam Chamazi na kutolewa kwa wastani wa mabao 3-2.
Matokeo sio ishu ya kujadili kwa sasa, stori kubwa ni taarifa ya jana ya TFF kuwa kuna wachezaji wawili wa Twiga Stars walitimuliwa kambini na kocha mkuu wa timu hiyo, Rogasian Kaijage kwa sababu za utovu wa nidhamu.
Afisa habari wa TFF, Boniface Wambura Mgoyo aliwaambia waandishi wa habari jana kuwa Kocha Kaijage aliwatimua kambini wachezaji Mwapewa Mtumwa na Flora Kayanda kutokana na vitendo vya utovu wa nidhamu wakati Twiga Stars ikijiandaa kwa mechi ya marudiano ya michuano ya Afrika kwa Wanawake (AWC) dhidi ya Zambia.
Akaongeza kuwa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) linatafakari hatua zaidi za kinidhamu dhidi ya wachezaji hao wawili wa kikosi cha Twiga Stars walioondolewa kwenye timu hiyo na Kocha Kaijage.
Hoja ya msingi kujadili ni utovu upi wa nidhamu walioufanya hawa wachezaji.
Ilielezwa na Wambura kuwa kuna siku kocha Kaijage aliwapa mapumziko ya siku moja wachezaji wake ili wakasalimie ndugu na jamaa, huku akiwataka kurejea saa 12 jioni  siku hiyo.
Wachezaji hao waliporudi kambini jioni walibainika kuwa wamelewa pombe.
Kwa maana hiyo hawakwenda kusalimia kama walivyoambiwa, bali wao walikwenda kutafuta pombe ili kujiburudisha. Kama walikwenda kusalimia, labda walipata pombe huko.
Sisemi mtu hatakiwa kunywa pombe kama anadhani ina faida kwake. Huo ni uhuru wa mtu. Lakini hoja yangu ni mazingira ambayo wachezaji hawa walikuwa nayo kwa wakati huo.
Walikuwa wanakabiliwa na mechi ngumu ya mashindano, huku watanzania wanaopenda soka, usiku na mchana wakiwatia moyo na kuwaombea dua ili wawafunge Zambia na kusonga mbele.
Najiridhisha kuwa ilikuwa ni wakati wa wachezaji wote wa Twiga kutafakari mchezo huo na kuweka akili yao yote.
Haikuwa wakati sahihi wa kuwaza kunywa pombe endapo watapewa siku ya mapumziko na kurejea kambini jioni.
Hapa ndipo suala la kukosa malengo linapoibuka kwa wanandinga wa Tanzania.
 Najaribu kuwaza kinadharia endapo Twiga Stars wangeishinda Zambia na kufanikisha kusogea mbele, hatimaye kufuzu fainali hizo, bila shaka ingekuwa nafasi yao kujitangaza na kuonekana kimataifa.
Huwezi jua, labda ndio ingekuwa bahati ya vijana hao kwenda ulaya kucheza soka.
Hakuna namna ya kufika mbali katika soka kama hujaonekana. TP Mazembe walimuona Samatta ligi ya mabingwa ndio maana walimsajili. CAF walimuona kijana huyo ligi ya mabingwa ndio maana wakamtaja kuwania Tuzo.
Upo umuhimu mkubwa wa kuisaidia timu kufuzu mashindano ya kimataifa kwani itaweza kuwa mlango wa kutokea.
Kwa wachezaji Mwapewa Mtumwa na Flora Kayanda  imekuwa  tofauti kwao, wakati kila mtu anawategemea, wao wanawaza pombe endapo wakipewa mapumziko. Tutafika? Malengo ya wachezaji wetu kufika mbali yatatimia kama wanavyojieleza mara zote?.
Nimeguswa sana na kitendo hiki. Nimepata nafasi ya kuzungumza na watu wengi kujiridhisha kama nipo sahihi kuchukizwa na tabia hii mbaya. Matokeo yake, wadau wengi wanasema wachezaji hawa wa Twiga wamelitia aibu Taifa na kuwaangusha watanzania wakati huu muhimu kwao.
Nikiwa njiani kurudi nyumbani baada ya tafakuri hiyo ya siku kwangu, nikabahatika kuonana na mchezaji wa zamani wa Yanga na sasa kocha wa mpira wa miguu, Seklojo Johnson Chambua na kumshirikisha jambo hili kwani kwa wakati huo alikuwa hajapata taarifa hiyo.
Baada ya kumsimulia ishu hiyo, Chambua aliuliza mara mbili akisema hajanielewa. Nikadhani labda Kiswahili kimekuwa kigumu kwake. Kumbe alikuwa anahakikisha anachokisikia kutoka kwangu.
Hapo sasa!, Chambua kama nyati aliyejeruhiwa, alianza kueleza kwa masikitiko makubwa sana juu ya kitendo hicho.
Ninaunga mkono hatua ya kocha Kaijage kuwatimua vijana hawa. Pili nawaomba TFF wachukue hatua kali ili iwe fundisho kwa wengine. Alisema Chambua.
Mwanasoka huyo wa zamani aliongeza kuwa tatizo la vijana wetu ni kwamba hawaandaliwi vizuri kutambua wakati waliopo kwani Twiga ilikuwa inahitaji ushindi kwa nguvu zote.
Kwa mchezaji aliyeandaliwa vizuri hawezi kuwaza pombe wakati muhimu kwa timu. Akili yake inatafakari mechi tu. Sasa linapotokea suala kama hili, ni rahisi kujua kuwa wachezaji wengi wa Tanzania hawana malengo na kazi yao. Alisema Chambua.
Aidha akashauri kuwa walimu wa soka wawe wepesi wa kuwajenga vijana wao katika misingi bora ya kujitambua na kutambua mchango wao kwa Taifa.
Hayo ni baadhi ya maneno ya Chambua kati ya mengi aliyosema. Hakika mawazo yake yalikuwa sahihi na alionekana kuguswa na utovu huu wa nidhamu.
Lakini wakati huo nikapokea simu nyingi kutoka kwa watu wa mpira wakieleza machungu yao.  
Wote walilaani vikali tabia mbovu ya wachezaji wa Tanzania na kusema wanalitia aibu taifa.
Kitendo cha kulewa pombe kiliwakera sana na wamewataka wachezaji hawa kuliomba radhi taifa kwa tabia yao mbaya.
Kutokana na mchango wa watu wengi nilioongea nao, nikagundua kuwa mashabiki wengi wa soka wana hamu ya kuona timu zao zinafanikiwa, lakini wanandinga wao wanaowaangusha vibaya mno.
Wanashindwa kukata kiu kwasababu wanaathiriwa na sababu nyingi za nje ya uwanja. Wanalewa Sifa na kujiona wamefika.
Kwa ujumla, Mwapewa na Flora mmewaudhi Watanzania. Kaeni chini na kutafakari upya. Kama mtagundua kuwa mmekosea, ombeni radhi kwa Taifa.
Kujituma kwenu ndio siri ya Taifa. Kuondolewa kikosini yawezekana mlivuruga mipango ya kocha kaijage kutokana na ukongwe wenu.
Wapo vijana wengi nyuma yenu wanaohitaji kujifunza kutoka kwenu. Tabia hii mliyoionesha inakera kwa mtu yeyote anayependa mpira.
Hatuingilii uhuru wenu, starehe ni haki yenu. Lakini suala la wakati lazima mzingatie.
Sidhani kama tungeyazungumza haya endapo mngeyafanya baada ya mechi na Zambia Chamazi. Hapana.
Lakini kwakuwa mmeyafanya wakati ambao timu inajiandaa kukabiliana na mechi ngumu, lazima tuseme ukweli kuwa mmewakosea Watanzania wanaopenda soka.
Cha msingi wachezaji wote wa Twiga Stars na Taifa stars mnatakiwa kutambua suala la wakati.
Fanyeni kazi kwanza, baaya ya kufanikiwa nendeni mkalewe wakati mnajiweka sawa kwa mambo mengine ya uwanjani.
Sisemi kulewa kuna faida kwenu, lakini najaribu kusema, ni vyema mkaangalia kama pombe inawafaa wakati huu mnaotafuta mafanikio.
Kama mtagundua jibu ni ndiyo, Nendeni, lakini mkiona sio, msiende. Au ulizeni waliotangulia wawaeleze uhusiano uliopo kati ya pombe na mpira.
Lakini kwa busara zangu, nawashaurini msiendekeze starehe wakati huu mgumu kwenu mkihitaji mafanikio.
Twiga Stars itacheza mechi za mchujo za michezo ya 11 ya Afrika (All Africa Games) ambayo itafanyika mwakani nchini Congo Brazzaville.
Mungu Ibariki Tanzania, Mungu Ibariki Twiga Stars, Taifa Stars.
Naomba kuwasilisha…………………