Search This Blog

Saturday, April 28, 2012

COUNTDOWN YA MNYAMA VS YANGA: TUJIKUMBUSHE - ZAMOYONI MOGELA ALIIFUNGA YANGA MARA MOJA TU KATIKA MAISHA YAKE YA SOKA

Zamoyoni Mogella
ZAMOYONI Mogella amewahi, hajawahi kuifunga Yanga?
Mpachika mabao mashuhuri wa zamani nchini, Mogella aliyezaliwa miaka 58 iliyopita mjini Morogoro, amekuwa gumzo kubwa hata baada ya kustaafu kwake soka.
Kumekuwa na ubishi kuhusu nyota huyo kwamba aliwahi au hajawahi kuifunga Yanga. Ukweli ni kwamba, Mogella aliifunga Yanga, tena lilikuwa bao ambalo lilielekea kuipa ushindi wa jumla wa mchezo huo Simba.
Ilikuwa ni Julai 14, mwaka 1984 kwenye Uwanja wa Taifa, sasa Uhuru mjini Dar es Salaam, wakati Golden Boy alipotangulia kuifungia Simba kwenye mchezo wa Ligi Daraja la Kwanza Tanzania Bara, sasa Ligi Kuu katika dakika ya 17.
Hata hivyo, mchawi wa vichwa enzi hizo, Abeid Mziba aliisawazishia Yanga bao hilo katika dakika ya 39.
Kabla ya kujiunga na Simba, Mogella alichezea timu za Jogoo, Reli, Tumbaku zote za Morogoro tangu mwaka 1974, hadi mwaka 1981, alipotua Mtaa wa Msimbazi.
Alijiunga na Simba baada ya soka yake kuwavutia viongozi wa Simba alipokuwa akichezea timu ya taifa ya vijana chini ya umri wa miaka 20. Mogella aling'ara zaidi alipokwenda na timu hiyo kwenye michuano maalumu ya vijana iliyofanyika nchini Norway.
Alitua Simba kwa dau la Sh 50,000 tu, ambayo tena alilipwa kwa awamu, kwanza 25,000 na nyingine akamaliziwa baadaye.
Tangu anajiunga na Simba, Mogella pia alianza kuichezea timu ya taifa ya Tanzania, Taifa Stars. 
Mwaka 1986, Mogella alikwenda kucheza soka ya kulipwa nchini Kenya katika klabu ya Volcano na baada ya miezi sita alikwenda Oman ambako alicheza hadi mwaka 1989.
Alirejea Simba mwaka 1990 na aliichezea hadi mwaka 1992, alipohamia Yanga ambako alicheza kwa msimu mmoja tu.
Ingawa wengi wanajua Athumani Juma Chama 'Jogoo' ndiye pekee aliyekuwa akimpa wakati mgumu Mogella uwanjani, lakini mwenyewe anawataja pia Yussuf Ismail Bana, Allan Shomari na Isihaka Hassan kwamba nao walikuwa wakimuumiza kichwa
Hivi sasa Mogella ni baba wa watoto wanne, akiwemo Farshed, anayefuata nyayo za baba yake kwenye soka.
Farshed, aliyezaliwa miaka 17 iliyopita, mbali na kucheza soka shuleni kwao, pia anachezea timu ya mtaani, Buibui nafasi ya ushambuliaji kama baba yake. Farshed ana pacha wake, Fuhal, aliyehitimu kidato cha Nne mwaka jana katika Shule ya Sekondari Green Acres.

JERRY SANTO: SIMBA NI NYUMBANI NIPO TAYARI KURUDI


Miezi kadhaa iliyopita niliripoti kwamba mchezaji wa zamani wa klabu ya Simba kutoka Kenya Jerry Santo amepata timu ya kuichezea nchini Albania ya KF Tirana - kabla ya hivi karibuni kutoka kwa taarifa kwamba hatoweza kuichezea tena timu hiyo tena.

Sasa nikiwa hapa Kenya Jerry Santo amenieleza kiundani kilichosabaisha asiweze kuichezea  KF Tirana ambayo tayari ilishatangaza kumsajili mapema mwaka huu.

"Kiukweli nilishasajiliwa na kupewa mkataba wa miaka 2 na ile timu, lakini nikiwa katika maandalizi ya kujiunga nayo yakafanyika mabadiliko makubwa katika uongozi wa klabu ile ambayo yaliutoa uongozi ulionisajili ndani ya timu ile. Uongozi mpya ulipoingia madarakani nao ukafanya baadhi ya changes ndani ya timu hiyo - kwanza baadhi ya wachezaji wapya tuliosajiliwa na uongozi wa zamani mikataba yetu wote ikavunjwa. Hivyo hicho ndicho kilichotokea mpaka nikashindwa kucheza soka kule."

Vipi je upo tayari kurudi Simba ikiwa watakuhitaji?
"Nipo tayari kurudi Simba, ni timu ambayo naipenda na kuitahmini. Nina marafiki wengi pale na nina maelewano mazuri na uongozi wa klabu ile. Pale sasa ni kama nyumbani ikiwa watanihitaji nitarudi kuitumikia Simba." - amesema Santo ambaye bado ana ndoto za kwenda kucheza soka nje ya Afrika.

JOSEPH SHIKOKOTI - DIET MBOVU CHANZO CHA WAGENI WENGI KUTOKUFANYA VIZURI KATIKA LIGI YA TANZANIA

Unamkumbuka Joseph Shikokoti?
Beki wa kati Ngongoti kimataifa wa Kenya aliyewahi kuja Tanzania kuitumikia klabu bingwa ya Afrika mashariki na kati Dar Young African na akaichezea mechi takribani 6 kabla ya kuondoka na kwenda kucheza Tusker ya Kenya kwa mkopo mpaka mkataba wake ulipoisha.

Nikiwa hapa Kenya nimekutana nae na kupata nafasi ya kuongea nae juu ya kwanini alicheza kwa muda mfupi sana katika ligi kuu ya Tanzania huku akiwa kiwango cha chini.

"Kiukweli nilikuwa napenda sana kucheza soka Tanzania lakini kuna vitu kadhaa vilipelekea uwepo wangu Bongo uwe mfupi. Kwanza nilipata uzito mkubwa nilipokuwa Yanga ndani ya muda mfupi niliokuwepo pale, kitu ambacho kilichangia kushuka kwa kiwango changu. Uzito huu ulichangiwa na mlo ambao nilikuwa nalishwa pale Yanga - yaani diet haikuwa katika mpangilio kabisa. Utakuta asubuhi mnakula manyama na vyakula vyenye wanga mwingi, mchana labda wali nyama na usiku wali kuku. Yaani haikuwa diet iliyopangiliwa kabisa mwisho wa siku nilijikuta naongezeka kilo katika hali isiyokuwa ya kawaida na kiwango kushuka kwa kasi sana."

Hili ni tatizo ambalo limewakumba wachezaji wenzangu kama Mike Baraza, Jerry Santo, Ambani na baadhi ya wachezaji wengine ambao wanatoka nje kwenda kucheza soka Tanzania." - Alisema Shikokoti ambaye hivi karibuni alienda kujaribu kutafuta timu ya kucheza nje ya nchi lakini akakwama na kurudi Tusker.

SALUM KINJE: MTANZANIA AMBAYE NI KIUNGO BORA KATIKA LIGI KUU YA KENYAIdadi ya wachezaji raia wa Tanzania wanaocheza nje ya nchi inazidi kuongezeka kila siku. Wengine waliondoka bongo wakiwa wadogo na wakaanza kucheza soka nje na wengine waliondoka ukubwani baada ya kukosa nafasi katika ulimwengu wa soka hapa nchini.

Katika ligi kuu ya Kenya kuna mchezaji mmoja anayeichezea klabu ya AFC Leopard Salum Kinje - ambaye kwa sasa anatajwa kwamba ndio kiungo bora kabisa katika ligi kuu ya soka ya KPL.

"Kiukweli huyu jamaa anajua sana mpira namkubali na kumuheshimu sana - nimecheza Tanzania lakini ni bado sijabahatika kuona mchezaji mwenye kiwango cha kumfikia huyu Salum" - Haya ni maneno ya mchezaji wa zamani wa Simba ya Tanzania Jerry Santo akizungumzia kijana Salum Kinje - mtanzania ambaye aliondoka Bongo miaka kadhaa iliyopita kuja Kenya kucheza soka.

Kinje anasema aliondoka Tanzania baada ya kuhangaika sana kuweza kupata mafanikio awakati akiichezea Manyema na baadae Palsons ya Arusha - kabla hajachukuliwa na mkurugenzi wa sasa wa ufundi wa TFF bwana Sunday Kayuni ambaye wakati huo alikuwa kocha wa Coastar Star ya Kenya.

"Nilicheza Costal Star na baadae nikahamia Bandari ambapo nilionekana na timu ya Sofapaka kabla ya kuhamia AFC Leopard ambayo nipo nayo mpaka sasa." - Salum Kinje

Baada ya kuonyesha uwezo mkubwa katika ligi kuu ya Kenya aliitwa katika timu ya taifa ya Harembee Stars lakini baadae walikuja kujua kwamba  sio Mkenya hivyo akaondolewa huku akifanyiwa mipango ya kupewa uraia lakini akagoma hivyo mpango wa kuichezea timu ya Harembee ukafa.

"Naamini nina kiwango kizuri na ninaweza kutoa mchango mkubwa kama nikiitwa katika timu ya taifa. Nipo tayari kuitumikia nchi yangu na kuweza kuisadia katika harakati za kupata nafasi ya kufanya vizuri katika mechi za kimataifa."

KUELEKEA PAMBANO LA WATANI WA JADI - EBU TUMKUMBUKE SAID MWAMBA KIZOTANI orodha ndefu ya wachezaji waliohama kutoka Simba kwenda Yanga na kutoka Yanga kwenda Simba, tangu enzi za akina Emanuel Mbele 'Dubu', lakini ni wachache waliong'ara kote kote.
Athumani Mambosasa (sasa marehemu), Zamoyoni Mogella, Method Mogella (sasa marehemu), Hamisi Gaga (sasa marehemu), Deo Njohole, Akida Makunda, Alphonce Modest, Monja Liseki, Shaaban Ramadhan, Eustace Bajwala, Joseph Katuba (sasa marehemu) wote hao ni baadhi ya wachezaji waliotoka Simba na kwenda kucheza Yanga.
Maulid Dilunga 'Mexico', Ezekiel Greyson 'Jujuman', Justin Mtekere (wote marehemu), Ally Yussuf 'Tigana', Yussuf Macho, Godwin Aswile, Ismail Suma, Steven Nemes, Nico Bambaga, Bakari Malima, Willy Martin, Edibily Lunyamila, Mtwa Kihwelo, Omar Hussein 'Keegan', Athumani China, Mohamed Hussein 'Mmachinga', Mohamed Banka na Amri Kiemba wote pia ni baadhi ya wachezaji waliotoka Yanga na kucheza Simba. Banka na Kiemba wamo kwenye kikosi cha msimu huu (2009/10) pia.
Athumani China akiwa Yanga, aliifunga Simba bao la mapema, dakika ya tatu, Oktoba 9, mwaka 1991 kwenye Ligi ya Muungano, wakati watoto wa Jangwani wakiibuka na ushindi wa 2-0. Bao la pili la Yanga lilifungwa na Abubakar Salum 'Sure Boy' dakika ya 54.
China tena aliifunga Yanga akiwa Simba, lilikuwa bao la pili katika ushindi wa 4-1 kwa Wekundu wa Msimbazi, Julai 2, mwaka 1994. Ally Yussuf Suleiman 'Tigana', pia alifunga mabao kote kote, Thomas Kipese kadhalika naye aliwafunga Simba na baadaye Yanga.
Akida Makunda aliihama Simba kuingia Yanga akiwa hana kumbukumbu ya kufunga bao kwenye mechi ya watani, lakini mara baada ya kutua kwa wana Jangwani aliingia kwenye orodha ya nyota waliofunga mabao kwenye mechi baina ya wababe hao wa soka ya Tanzania.
Ilikuwa Februari 21, mwaka 1998 katika mchezo wa kwanza wa Ligi Kuu Tanzania Bara, wakati huo ikidhaminiwa na Kampuni ya Bia Tanzania (TBL) kupitia bia yake ya Safari Lager, wakati Makunda alipofunga bao lililoelekea kuwatoa Yanga kifua mbele kwenye mchezo huo, dakika ya 46.
Lakini Athumani Macheppe alizima shangwe za wana Yanga zikiwa zimesalia dakika mbili mchezo huo kumalizika kwa bao lake safi.
Sahau kuhusu Akida, kama yupo mchezaji ambaye aliyewapa raha mashabiki wa timu zote hizo, basi ni Said Nassor Yussuf Mwamba (pichani), maarufu kama Kizota enzi zake, aliyefariki dunia Februari 11, mwaka 2007. Kizota ni mchezaji aliyewasisimua kwa namna yake mashabiki wa Yanga na Simba kutokana na mabao yake.
Kizota alifariki dunia baada ya kugongwa na gari eneo la Veterinary, akiwa anatoka kushuhudia mchezo wa marudiano, Kombe la Shirikisho la Soka Afrika, Raundi ya Awali kati ya wenyeji Simba dhidi ya Textil de Pungue ya Msumbiji. Alitoka kwa huzuni uwanjani siku hiyo baada ya kushuhudia timu yake ya zamani, Simba ikitolewa na wageni kwa mikwaju ya penalti 3-1, kufuatia sare ya jumla ya 2-2.
Mchezo wa kwanza Msumbiji, Simba ililazimisha sare ya 1-1 na marudiano nayo pia walibanwa kwa sare aina hiyo hiyo, hivyo kufanya mshindi aamuliwe kwa mikwaju ya penalti. Ntota ya timu ya kiwanda cha nguo Msumbiji ndiyo iliyong'ara jioni hiyo.
Kama kuna miaka ambayo Kizota alifanya vitu vya 'babu kubwa' kwenye soka ya Tanzania, basi ni 1993, kwani mapema tu mwaka huo aliibuka mfungaji bora kwenye michuano ya Klabu Bingwa Afrika Mashariki na Kati mjini Kampala, Uganda, akiiwezesha Yanga pia kutwaa ubingwa wa michuano hiyo kwa kuwafunga wenyeji, SC Villa.
Lakini pia, alikuwa mfungaji bora wa Ligi ya Tanzania. Yote tisa, kumi ni pale Kizota alipofunga mabao mawili peke yake, wakati Yanga inaibuka na ushindi wa 2-1 dhidi ya Simba kwenye mchezo wa kwanza wa Ligi ya Tanzania Bara, Uwanja wa Taifa, (sasa Uhuru) mjini Dar es Salaam.
Ilikuwa ni Machi 27, mwaka huo 1993, wakati Kizota alipomchambua kipa hodari nchini enzi hizo, Mwameja Mohamed katika dakika za 47 na 57.
Simba ikielekea kulala 2-0, shukrani kwake Edward Chumila (naye marehemu pia) aliyewafungia Wekundu wa Msimbazi bao la kufutia machozi, dakika ya 75.
Baada ya kipigo kikali cha mabao 4-1, Julai 2, mwaka 1994, Yanga ilivunja kikosi ikiwafukuza karibu nyota wake wote wa kikosi cha kwanza kwa tuhuma za kuhusika kuihujumu timu katika kipigo hicho kilichotokana na mabao ya George Masatu, Athumani China, Madaraka Selemani na Dua Saidi, bao la kufutia machozi la Yanga likifungwa na beki imara, Constantine Kimanda.
Kati ya nyota waliotupiwa virago Yanga ni Kizota, ambaye kutokana na makali yake wakati huo, akiwa tegemeo la timu ya taifa ya Tanzania na miongoni mwa nyota waliotoa mchango mkubwa kwenye kikosi kilichochukua Kombe la Challenge nchini Kenya, Simba wakamwambia: "Usipate tabu Said, njoo upumzike huku".
Kizota alitaka kuwaonyesha Yanga kwamba, walifanya kosa kumwacha na katika mchezo wa marudiano baina ya watani hao wa jadi wa Ligi Kuu ya Bara, Oktoba 4, 1995, Yanga ikiwa inaelekea kabisa kushinda mchezo huo 1-0, Said Mwamba alitibua furaha ya wana Jangwani dakika ya 70 kwa kufunga bao safi la kusawazisha.
Yanga ilitangulia kupata bao kupitia kwa mpachika mabao wake mahiri enzi hizo, Mohamed Hussein 'Mmachinga' dakika ya 40. Bao la Kizota liliwachanganya Yanga na dakika tisa baadaye, wakapachikwa bao la pili. Safari hiyo alikuwa ni Mchunga Bakari 'Mandela' aliyewaambia wana Jangwani; kutangulia si kufika.
Baada ya msimu huo, Yanga walikiri kosa lao na wakaenda kumpigia magoti Kizota arejee nyumbani. Kwa sababu Kizota alikuwa anaishi nyumba ya pili kutoka klabu ya Yanga, akiishi na mkewe Tosha, Mtaa wa Jangwani, hivyo ilikuwa rahisi kumrubuni na kurejea nyumbani.
Na aliporejea Yanga, Kizota aliifunga tena Simba. Ilikuwa Novemba 9, mwaka 1996, katika sare ya ajabu ya watani, ya mabao 4-4 mjini Arusha.
Kizota aliifungia Yanga bao la kusawazisha lililofanya sare ya 3-3 katika dakika 70, baada ya awali Kipese kuifungia Simba, dakika ya saba, Edibily Lunyamila kuisawazishia Yanga kwa penalti dakika ya 28, Ahmed Mwinyimkuu kuifungia Simba la pili dakika ya 43, kabla ya Dua Said kufunga la tatu dakika ya 60 na Mustafa Hoza kuisawazishia Yanga kwa kujifunga dakika ya 64.
Sanifu Lazaro aliifungia Yanga bao lililoelekea kuwa la ushindi dakika ya 75, lakini walishindwa kulinda lango lao na kuruhusu bao la dakika za lala salama, lililofungwa na Duwa Said dakika ya 90, hivyo kuwa sare ya 4-4.  
Kizota alijiunga na Yanga mwaka mwaka 1988, akitokea timu ya Shirika la Posta la Tabora, enzi hizo likijulikana kama Posta na Simu, wakati akicheza kama kiungo.
Baada ya kung'ara akiwa na Yanga, msimu wa 1988 ulipomalizika alichukuliwa na Al-Jazira ya Abu Dhabi, Falme za Kiarabu. Akiwa Abu Dhabi katika timu yake mpya, Kizota alikutana na aliyekuwa nyota wa timu ya Taifa ya Malawi, Lawrence Waya, ambaye alikuwa winga machachari sana enzi zake. Kwa pamoja Kizota na Waya waliifanya timu yao kuwika mno katika soka ya Uarabuni.
Kutokana na vitu vyake vya uhakika, Kizota alikubalika mno na mashabiki wa soka Abu Dhabi, jambo ambalo lilifanya Waarabu waanze kumrubuni abadili uraia na kuwa raia wa huko. Ghiliba hizo hakupewa Kizota peke yake, bali hata Waya.
Kizota aliingiwa na ghiliba hizo na kuanza kufanyiwa taratibu za kupewa uraia, lakini wakati taratibu zikifanywa, mwanasoka huyo aliomba likizo ya kurejea nyumbani Tanzania kuoanana na familia yake na ndipo alipobadili mawazo ya Uarabu. Hiyo ilikuwa ni mwaka 1989.
"Hakuna kingine ni Yanga tu, nilipofika tu viongozi wakasema wananihitaji sana, hivyo nikaamua kubaki Yanga," aliniambia Kizota nilipozungumza naye mwaka 1999. Kizota aliingia kwa makeke, safari hiyo hakuwa kiungo, bali alihamia kwenye nafasi ya ushambuliaji na kufanikiwa kuipeleka Yanga kileleni kwa mabao yake.
Hata hivyo, viongozi wa timu yake baada ya kuona kimya kimezidi, walimtaka haraka sana kurejea. Alitumiwa ujumbe wa simu ya maandishi (Fax) ambao aliupuuza, lakini baadaye alifuatwa na viongozi hao walioondoka naye kurejea Abu Dhabi.
Kizota aliondoka nchini akiwa anaongoza kufunga mabao na Ligi imefikia ukingoni, huku Yanga ikihitaji pointi chache tu kutangaza ubingwa, jambo ambalo liliwezekana, licha ya yeye kuondoka na vijana wa Jangwani kurejesha taji walilopokonywa na Coastal Union ya Tanga mwaka 1988.
Kizota aliishi Uarabuni hadi mwaka 1991, aliporejea kupumzika na kuikuta Yanga ikiwa katika hali mbaya, soka ya Tanzania inatawaliwa na watani wao wa jadi, Simba, ambayo mwaka huo wakati anarejea (Simba) ilikuwa imetangaza ufalme wa soka kwa nchi za Afrika Mashariki na Kati, sasa Kombe la Kagame.
"Kama nilivyokwambia naipenda sana Yanga, nikaamua kubaki, lakini jamaa (Al-Jazira) walikuwa wakinitaka nirejee haraka sana, nikawadanganya naumwa, wakati wananitumia fedha za matibabu, kumbe mie niko safi kabisa," aliniambia Kizota, aliyehitumu elimu yake ya msingi mwaka 1981 katika shule ya Mabatini, Tabora alikozaliwa.
Kizota aling'ara Yanga tangu mwaka huo, akiiwezesha kutwaa Kombe la Kagame mwaka 1993, kufika fainali ya michuano hiyo mwaka 1992, Nusu Fainali nchini Sudan mwaka 1994, kabla ya 1994 kuhamia Simba.
Aliporejea Yanga 1996, alicheza kwa misimu miwili zaidi kabla ya mwaka 1998 kutimkia Al-Nasar ya Oman. Alikaa huko msimu mmoja tu, kabla ya kurejea nchini katikati ya msimu wa Ligi Kuu na kujiunga na timu iliyokuwa Daraja la Kwanza, Kariakoo United ya Lindi, ambako akiwa na wakongwe wenzake kama Mustafa Hoza waliipandisha Ligi Kuu.
Baada ya kuipandisha timu hiyo, Kizota alirejea Yanga ambako aliiwezesha timu hiyo kutwaa Kombe la Kagame tena Uganda mwaka 1999, ingawa kutokana na umri wakati huo, alirejea kucheza nafasi ya ulinzi. Hadi anafariki dunia, Kizota alikuwa mume wa Tosha na baba wa watoto wawili, Hamim na Rabii. 

imeandikwa na Mahmoud Zubeiry - http://bongostaz.blogspot.com/

Friday, April 27, 2012

TITO VILANOVA KOCHA MPYA WA BARCA: RAFIKI WA GUARDIOLA TANGU UTOTO - ADUI WA MOURINHO UKUBWANI

Pamoja na Barcelona kuvunja rekodi ya mafanikio chini ya Pep Guardiola katika miaka minne iliyopita - akiiongoza timu hiyo kubeba jumala ya makombe 13 - msaidizi wake mkuu Tito Vilanova amekuwa mara nyingi hazungumziwi.
Mpaka leo, pindi kocha huyu mwenye miaka 42 alipoushangaza ulimwengu wa soka baada ya kuthibitishwa kwamba ndiye kocha atakayemrithi Guardiola na kuliongoza benchi la ufundi la Barcelona katika msimu ujao wa 2012-13.

Alizaliwa katika ukanda wa Catalan eneo la Bellcaire d'Emporda mwaka 1969, Vilanova amekuwa mtu wa karibu sana na kocha huyu wa sasa Blaugrana kwa wakati wote. Wawili hawa wamekuwa pamoja katika kituo cha La Masia katika miaka 1980s. Lakini wakati Guardiola alipoenda na kuwa star katika kikosi cha Johan Cruyff -Dream Team - wakishinda makombe sita ya La Liga na moja la Ulaya katika miaka 11 - Vilanova alishindwa kuhitimu, na miaka miwili baada ya kukaa na kikosi cha Barcelona aliamua kuondoka na kwenda kucheza katika timu za Figueres, Celta Vigo, Badajoz, Mollorca, Lleida, Elche na Gramenet - ambapo aliamua kustaafu mwaka 2002, miaka 14 baada ya kuanza kucheza katika evel ya juu.

Vilanova baadae akaamua kuhamia katika ukocha. Experience kubwa zaidi ni pale alipokuwa mjurugenzi mkuu wa klabu ya daraja la 3 kuanzia mwaka 2006-07. Baadae akaamua kurudi Barcelona wakati kiangazi cha 2007 kama kocha msaidizi wa kikosicha Barca B chini ya Pep Guardiola.
Wakati Guardiola alipomrithi Frank Rijkaard mwaka 2008, Vilanova alijiunga na Guardiola katika kikosi cha kwanza na kuwa kocha msaidizi katika kikosi cha kwanza cha Barcelona.
Mourinho na Vilanova wakizinguana

Tukio kubwa ambalo lilimuhusisha msaidizi wa Guardiola lilitokea mwezi wa nane tarehe 18 mwaka 2011 katika muda wa nyingeza wa mechi ya Supercopa mechi ya pili kati ya Barcelona na Real Madrid pale Nou Camp. Rafu ya kijinga ya Marcelo dhidi ya Cesc Fabregas ilizusha ugomvi mkubwa katika timu zote mbili, na mwishowe Jose Mourinho akamtia kidole cha jicho Vilanova - kitendo ambacho kiliripotiwa sana na vyombo vya habari vya Hispania.
 Kwa mujibu wa mkurugenzi wa ufundi wa Barcelona Andoni Zubizarreta, uteuzi wa Vilanova kama mrithi wa Guardiola ni sahihi kabisa kwa sababu ni watu wanaoshea mawazo na mbinu za kimchezo pamoja na staili ya kucheza yenye filosofi moja.

Lakini baada ya makombe 13 - au 14 ikiwa Barca watashinda Copa del Rey mwezi ujao - ndani ya miaka 4, Vilanova ana kazi ngumu sana ya kufuata nyayo za rafiki yake kipenzi.