Search This Blog

Tuesday, December 31, 2013

CLOUDS MEDIA ILIPOFUNGWA NA MAKIPA WA VODACOM PREMIER LEAGUE MABAO 3-1.

ROBIN VAN PERSIE AKIONYESHA UMAHILI WAKE KWENYE EGESHO LA MAGARI.

Instagram

Monday, December 30, 2013

MZUNGUKO WA PILI LIGI KUU NI VITA YA KUSAKA UBINGWA NA KUKWEPA RUNGU LA KUSHUKA DARAJA!!


Na Baraka Mpenja, Dar es salaam

NGWE ya  lala salama ya  ligi kuu soka Tanzania bara msimu wa 2013/2014 unatarajia kuanza kushika kasi januari  25 mwakani.
Kwasasa timu zote 14 zinazoshiriki ligi hiyo zipo katika maandalizi ya  vikosi vyao ili kufanya vizuri zaidi ya mzunguko wa kwanza.
Wataalamu wengi wa soka wanasema mzunguko wa pili kama ilivyo kawaida timu zinajigawa katika makundi matatu.
Kundi la kwanza linajumuisha timu zinazowania ubingwa, wakati kundi la pili ni lile la timu zinazowania nafasi za katikati ambazo si nzuri sana wala mbaya sana, cha msingi katika nafasi hizi, timu zinakuwa katika mikono salama.
Kundi la tatu ndio balaa, hapo kunakuwepo na timu zinazopigana kushuka daraja, hivyo zinashindana kwa nguvu zote kusaka ushindi wa kuwasogeza mbele.
Ukiangalia msimamo wa ligi kuu mpaka sasa wakati tunasubiri mzunguko wa pili, timu za kundi la kwanza unaweza kusema ni Vinara Yanga, Azam fc, Mbeya City, pamoja na Simba sc.

Simaanishi nyingine haziwezi kuingia katika nafasi hizo. Mpira wa miguu ni mchezo wa hadharani, hivyo baadhi ya timu zikiwemo  Mtibwa Sugar, Kagera Sugar, na Ruvu Shooting zinaweza kuingia katika mbio za kuwania ubingwa endapo zitachanga vyema karata zao.
Msimamo uko hivi; Yanga wapo kileleni kwa pointi 28, nafasi ya pili wapo Azam fc na pointi zao 27, nafasi ya tatu wapo Mbeya City wakijikusanyia pointi 27, huku nafasi ya nne ikishikiliwa na simba SC yenye pointi 24. Timu hizi zinakamilisha  timu nne za juu `Big Four` wakati mzunguko wa pili unasubiriwa.
Nafasi ya tano inakaliwa na Mtibwa sugar wenye pointi 20, sawa na Kagera Sugar katika nafasi ya sita, lakini Mtibwa wana wastani mzuri wa mabao ya kufunga na kufungwa.
Nafasi ya saba wapo Ruvu shooting wakiwa na pointi 17, wakati nafasi ya nne inashikiliwa na wagosi wa kaya, Coastal Union kwa pointi 16, nafasi ya tisa wapo JKT Ruvu na pointi zao 15, huku nafasi ya kumi ikishikiliwa na Rhino Rangers ya Tabora yenye pointi 11.
Kibarua kipo nafasi nne za mwisho ambapo JKT Oljoro wameshikilia nafasi ya 11 kwa pointi 10 sawa na Ashanti United nafasi ya 12, tofauti ni wastani wa mabao ya kufunga na kufungwa.
Nafasi ya 13 wapo Tanzania prisons wakiwa na pointi 9, huku Mgambo JKT waikiburuza mkia kwa pointi 6 tu.
Kwa msimamo huu utagundua kuwa nafasi za juu zinaonekana kung`ang`aniwa na timu za Yanga, Azam fc, Mbeya City pamoja na Simba sc. Lakini Mtibwa Sugar, Kagera Sugar na Ruvu Shooting zinaweza kuingia katika kinyang`anyiro cha ubingwa. Sio hizo tu, hata timu nyingine kama Coastal union, Ruvu Stars zinaweza kupanda juu kutegemeana na matokeo ya timu zilizopo mbele yao.
Mzunguko wa pili utakuwa na ushindani mkubwa sana kwa timu zinazowania ubingwa. Ukiangalia hali zao kiuchumi, morali kubwa, ubora wa wachezaji, mipango yao na makocha waliopo, utagundua kuwa kibarua kitakuwa kizito.
Kwa kifupi tuangalie baadhi ya mabadiliko yaliyopo katika timu nne za juu na maandalizi yao kuelekea mzunguko wa pili.

YANGA SC
Timu hii ipo katika maandalizi ya mzunguko wa pili wa ligi kuu pamoja na michuano ya ligi ya mabingwa barani Afrika mwakani.
Kwa bahati Mbaya kumetokea mabadiliko ya benchi la ufundi ambapo Uongozi wa klabu ya Young Africans SC umempatia taarifa (Notice) ya siku ya thelathini (30) kocha mkuu mholanzi Ernie Brandts juu ya kusitisha mkataba wake kuanzia  Disemba 22 mwaka huu.
Kwa maana hiyo, Yanga wanahaha kupata kocha mpya kuelekea mzunguko wa pili. Ukipiga hesabu za muda uliobakia kufikia januari 25 na februari ambapo wataanza kampeni za ligi ya mabingwa barani Afrika, utagundua kuwa kocha mpya atakuwa na kazi nzito kuandaa kikosi, na mbaya zaidi akija  na falasafa mpya ya uchezaji.
Lengo sio kuingia kiundani zaidi kuhusu suala hili la kumfukuza kocha ambalo yawezekana ni udhaifu wa viongozi wa Yanga au ni uhalisia wa jinsi kiwango cha timu yao kinavyoshuka siku hadi siku licha ya kusheheni nyota kibao.
Yanga kwasasa wapo chini ya kocha msaidizi, Fredy Felix Minziro na wanajiandaa kwenda kushiriki michuano ya kombe la Mapinduzi inayotarajia kuanza kushika kasi januari mosi mwakani katika uwanja wa Amaan mjini Unguja na Gombani kisiwani Pemba.
Michuano hii itakuwa muhimu sana kwa Yanga, kwani itawapa nafasi ya kupima uwezo wa kikosi chao kabla ya kuanza kutetea ubingwa wake na kushiriki michuano ya kimataifa.
Kuna uongezeka la wachezaji wapya katika kikosi chake, hivyo unaweza kukubaliana na mimi kuwa kutakuwa na mabadiliko ukilinganisha na  mzunguko wa kwanza, lakini endapo atapatikana kocha mwenye ubora wa juu.
Ongezeko la Juma Kaseja, Hassan Dilunga na Emmanuel Anord Okwi, yawezekana kutawapatia nguvu kubwa zaidi na kuendelea kufanya vizuri.
Kaseja ana uzoefu mkubwa sana na ligi kuu pamoja na michuano ya kimataifa. Okwi  naye ni mchezaji bora kwa wakati wote, lakini Dilunga ni chipukizi na anahitaji muda zaidi wa kujiweka sawa katika soka la ushindani.
Kwa usajili wa Okwi, Yanga inafikisha wachezaji watano wa kimataifa,  wengine ni Mbuyu Twite, Didier Kavumbagu, Haruna Niyonzima na Hamis Friday Kiiza. Wachezaji hawa wapo katika kiwango kizuri, ingawa bado wameonekana kutokuwa na makali barabara.
Pia imesheheni wachezaji wazawa wenye kiwango cha juu ambao ni pamoja na Juma Kaseja, David Luhende, Nadir Haroub `Canavaro`, Kelvi Yondan `Vidic`, Athuman Idd `Chuji`, Frank Domayo, Nizar Khalfan, Mrisho Ngassa , kipa Ally Mustapha `Bartez`, Deo Munish `Dida` na wengineo.
Ukiangalia majina ya wachezaji wa Yanga kulinganisha na timu nyingine kama Mbeya City, Ruvu Shooting hata Simba Sc, unaweza kuamini kwa asilimia mia moja kuwa Yanga watashinda mechi zote.
Hakika hakuna ushindani wa majina kabisa, Yanga wanaonekana kuwa na kila aina ya mchezaji, lakini kumbuka mpira wa miguu ni mchezo wa mipango na unachezwa hadharani na ndio maana wakiwa na wachezaji wao bora, walifungwa mabao 3-1 katika mechi ya Nani Mtani Jembe dhidi ya Simba yenye wachezaji wengi vijana.
Kwa kikosi cha Yanga, anahitajika kocha wa kuunganisha timu ili wacheze kitimu. Kama atapatikana mwalimu mzuri, bila shaka Yanga watafanya vizuri ngwe ya pili nap engine kutetea ubingwa wao. Cha msingi tusubiri muda ufike.

SIMBA SC
Simba  wakiwa chini ya kocha Abdallah Kibadeni walianza mzunguko wa kwanza vizuri na kuongoza, japokuwa walikuja kupoteza mwelekeo na kuishia nafasi ya nne.
Waliamua kufanya mabadaliko ya benchi la Ufundi ambapo Kibadeni pamoja na msaidizi wake, Jamhuri Kiwhelo walitimuliwa na mikoba yao kuchukuliwa na Mcroatia Zdravko Logarusic `Loga` akisaidiwa na Seleman Matola `Veron`.
Mbali na kubadili benchi la ufundi, pia wameongeza nguvu katika dirisha dogo ambapo wamewasajili, Ivo Mapunda, Yaw Berko, Donald Mosoti, Awadh Juma Issa, Ali Badru pamoja na kumrejesha Uhuru Seleman Mwambungu aliyekuwa akicheza kwa mkopo Coastal Union ya Tanga.
Mapunda, Awadh, Mosoti, Uhuru,  walicheza mechi ya nani mtani Jembe ambapo waliunganisha nguvu zao na wachezaji wengine wakiwemo, Gerrard Jonas Mkude, Ramadhan Singano `Messi`, Said Ndemla, Betram Mwombeki, Hamis Tambwe, Joseph Owino Gella na wengine.
Katika mechi hiyo, Simba ilicheza vizuri na kuonekana kuimarika. Na sasa inajiwinda na mashindano ya mapinduzi yanayotarajia kuanza kushika kasi januari mosi.
Endapo Simba watatulia na kocha wao na kuongeza nguvu zaidi ya mechi ya Nani Mtani Jembe, basi hapana shaka watarudi mchezoni na kuendelea kutafuta ubingwa wa ligi kuu,  ikizingatiwa wanazidiwa pointi nne tu na Yanga waliopo kileleni.

AZAM FC
Klabu hii imeachana na kocha wake , Mwingereza  Sterwart John Hall na kuanza maisha mapya na kocha raia wa Cameroon,  Joseph Marius Omog.
Wanakwenda Zanzibar kutetea ubingwa wao wa kombe la Mapinduzi. Pia watatumia michuano hiyo kujiandaa na mzunguko wa pili wa ligi kuu bara pamoja na michuano ya kombe la shirikisho mwakani.
Katika dirisha dogo la usajili, Azam fc wamemuongeza mshambuliaji mmoja kutoka Ivory Coast, Mouhamed Kone.
Bila shaka baada ya kumalizika kwa mzunguko wa kwanza, benchi la ufundi lilijiridhisha na uwezo wa wachezaji wake kikosini.
Klabu hii yenye makazi yake Mbande, Chamazi, nje kidogo ya jiji la Dar es salaam, imekuwa ikishindana kwa misimu mitatu mfululizo.
Msimu wa 2011/2012 walikuwa wanashindana na Simba katika mbio za ubingwa na kujikuta wakiambulia nafasi ya pili. Msimu wa 2012/2013, Simba wakajitoa, kibarua kikabaki kwa Azam fc na Yanga na wakaishia nafasi ya pili.
Msimu huu wapo katika mbio za ubingwa, Simba wapo nyuma yao, wanapambana na Yanga pamoja na Mbeya City.
Ukiangalia mfululizo wa kufanya vizuri kwa Azam, japokuwa hawajafanikiwa kutwaa ubingwa, utajiridhisha kuwa wamekuwa wapambanaji wa kweli na bila shaka wataendelea na kasi yao chini ya kocha mpya, Omog.
Yanapotokea mabadiliko ya kocha, kuna mambo mawili; Moja, timu inaweza kuongeza kiwango na pili inaweza kupoteana endapo wachezaji watashindwa kuenda sambamba na falsafa ya mwalimu.
Kwasasa ni mapema kuwatabiria lolote, tunaamini wanatambua nini cha kufanya na ndio maana wapo katika maandalizi kabambe.
Mzunguko wa pili, Azam fc wanaweza kuendana na kasi ya ushindani.

MBEYA CITY
Hii ni timu ngeni ligi kuu. Msimu huu ni wa kwanza kushiriki michuano hii mikubwa, lakini wameonesha ukomavu mkubwa na kuleta changamoto kali mzunguko wa kwanza.
Hakuna timu yoyote iliyoweza kupata pointi tatu mbele ya Mbeya City chini ya kocha wake Mzalendo, Juma Mwambusi akisaidiwa na Maka Mwalwisyi.
Waliungana kwa dhati na mashabiki wao waliokuwa wanawafuata popote pale wanapoenda. Wachezaji walikuwa na morali kubwa na kuucheza mpira kwa kasi kubwa, umakini na malengo ya ushindi.
Walifanikiwa kushinda nyumbani na ugenini na hivyo kuamsha ari kwa wapenzi wengi wa soka hususani jijini Mbeya.
Kwasasa wapo katika maandalizi ya mzunguko wa pili na bahati nzuri wamepata nafasi ya kucheza mapinduzi Cup kwa mara ya kwanza.
Hii itawajenga zaidi kwani watakutana na mazingira tofauti na bara. Watacheza na timu za Zanzibar pamoja na timu za Kenya na Uganda.
Itakuwa nafasi nzuri kwao kujipima uwezo wao kuelekea mzunguko wa pili ligi kuu bara.
Cha kufurahisha hakuna mabadiliko ya kikosi chao, lakini wamemuongeza  mchezaji mmoja tu ambaye ni Saad Kipanga.
Ni ngumu kusema Mbeya City wataendeleza makali yao, lakini inawezekana kutegemeana na maandalizi yao, motisha kwa wachezaji na mipango ya ndani na nje ya uwanja.
Lakini bado nawatabiria kufanya vizuri kutokana na kusheheni wachezaji wenye kasi kama Deus Kaseke, Mwagane Yeya, Paul Nonga, Peter Richard, Jeremiah John, Alex Seth na wengine wengi.
Ni suala la kusubiri muda ufike ili tuone maujanja yao. Pia mapinduzi itaonesha wazi kama wana mwelekeo japokuwa itakuwa sehemu ya kujaribu kikosi chao.
Kukutana na timu za Tusker, AFC Leopard, KCC na URA itakuwa changamoto nzuri sana achilia mbali Simba, Yanga na Azam  ambazo tayari wameshakutana nazo ligi kuu.
Baada ya kuangalia timu nne za juu, kwa nafasi za katikati huwa hazina ushindani sana kwani timu hzi huwa zinakuwa na uhakika wa kubakika ligi kuu kwa msimu unaofuata.
Timu nyingine kama ilivyo kwa timu za juu, zimefanya usajili katika dirisha dogo kama ifuatavyo;

ASHANTI UNITED
 Ndiyo inayoongoza kwa wachezaji 15 ambao ni Kassim Kilungo, Mohamed Banka, Bright Obinna, Victor Costa, Juma Mpongo, Juma Jabu, Ally Kondo, Shafii Rajab, Mohamed Faki, Abubakar Mtiro, Patrick Mhagama, Ally Kabunda, Hassan Kabuda, Idd Ally na Rahim Abdallah.

RUVU SHOOTING; Ally Khan na Jumanne Khamis,
RHINO RANGERS; David Siame, John Kauzeni, Salum Mamlo, Jingo Seleman, Darlington Enyinna, Rajab Twaha, Godfrey Mobi na Mussa Digubike.

TANZANIA PRISONS; Dennis Liwanda, Godfrey Pastory, Henry Mwalugala, Jamal Salum na Brayton Mponzi.

OLJORO JKT; Jacob Masawe, Mansour Ali, Juma Mohamed, Amour Mohamed, Mohamed Ali, Mussa Nahoda, Benedict Ngasa, Seleman Makame, Shija Mkina, Ali Omar na Shaweji

MGAMBO SHOOTING; Suleiman Khatib, Bolly Ajali, Amri Sambinga na Issa Ali.

JKT RUVU; Chacha Marwa, Sino Augustino, Idd Mbaga na Cecil Luambano.

Coastal Union, Mtibwa Sugar na Kagera Sugar hazijafanya usajili kutokana na kuviamini vikosi vyao.
Timu zote zimeshaanza mipango ya mazoezi, kinachosubiriwa ni muda muafaka kufika.
Kulingana na usajili wa timu hizi, labda tunaweza kupata kitu kipya kutoka kwao, lakini timu zinazoshika nafasi za mwishoni zitakuwa na kibarua kizito zaidi.

Mgambo Jkt, Tanzania Prisons, Ashanti United na JKT Oljoro zinatakiwa kujipanga zaidi ili kuepuka mkasi wa kushuka daraja.
Baadhi ya timu za mkiani, zimeanza  harakari za kujinasua na mtego wa kuporomoka daraja, hivyo kwa kuanzia, zimebadili makocha wao.
Prisons imepata kocha mpya David Mwamwaja, Ashanti United, Abdallah Kibadeni,  na JKT Oljoro imnasa  Hemed Morroco.
Mabadiliko haya yamelenga kuzinusuru timu hizi na tayari zote zimeshaanza mazoezi na kambi kujiwinda na mzunguko wa pili ambao utakuwa wa mapambano ya kufa na kupona.
Tusubiri kuona matunda ya mabadiliko haya, na inawezekana zikaja na sura mpya au zikazidi kwenda shimoni.

TFF KUWENI MAKINI NA MAAMUZI YA BODI YA LIGI, KAMA KWELI TUNATAKA MAENDELEO YA SOKA TUACHANE NA SIASA....


KANUNI YA 24
KUVURUGA MCHEZO
1.     Wachezaji na viongozi wa timu itakayosababisha mchezo kuvurugika na hatimaye kuvunjwa, itapoteza mchezo huo hata kama ilikuwa inaongoza kwa magoli na timu pinzani itapewa ushindi wa pointi tatu na magoli matatu, iwapo timu pinzani inaongoza kwa magoli zaidi ya matatu, itabakia na idadi ya magoli hayo iliyokwishafunga.

2.     Magoli yaliyofungwa na wachezaji wa timu iliyosababisha mchezo kuvunjika yatafutwa lakini magoli yaliyofungwa na timu pinzani hayatofutwa na yataendelea kuonekana katika idadi ya magoli yaliyofungwa na wachezaji wa timu hiyo wakati wa kutafuta mfungaji bora.

3.     Endapo itatokea vurugu ya aina yoyote ile na kusababisha mchezo kusimama, mwamuzi atasubiri kwa dakika zisizozidi kumi na tano, na endapo hali ya vurugu bado inaendelea mwamuzi atavunja mchezo na kuwasilisha taarifa ya mchezo kwa kamati ya Usimamizi ya ngazi husika.

4.     Timu iliyosababisha vurugu itapoteza mapato yote ya mchezo.

5.     Timu iliyosababisha kuvurugika kwa mchezo italipa faini ya shilingi 300,000/=.

3.           Faini hiyo italipwa kabla ya mchezo unaofuatia.

4.           Mchezaji/wachezaji na kiongozi/viongozi watakao bainika kusababisha vurugu zilizopelekea mchezo huo kuvunjika watafungiwa kujihusiha namasuala yote ya mpira kwa kipindi cha miaka mitano.

5.           Endapo uvunjikaji wa mchezo utakuwa nje ya kanuni ya 22(3), mchezo huo utarudiwa kama inavyoainishwa katika kanuni ya 9(e) na utachezeshwa na waamuzi wengine katika siku itakayo pangwa na chombo husika. 


2013 - ULIKUWA NI MWAKA WA ATHUMAN IDD ' CHUJI'


Na Baraka Mbolembole 

Athumani Idd ' Chuji' , sahau kuhusu umri wake, kiungo huyu wa ulinzi na mashambulizi wa klabu ya soka ya Yanga, amepitia vipindi vingi vigumu katika maisha yake ya soka. Akianzia soka lake katika timu ya Polisi Dodoma, 2005, Chuji alitokea kuwa mlinzi bora wa kati katika soka la Tanzania, alikuwa akipata nafasi ya kucheza mara kwa mara katika timu ya taifa ya vijana ' Serengeti Boys' mwaka huo, akitokea timu za nje ya Dar es Salaam. Kupata nafasi ya moja kwa moja katika timu ya taifa ukitokea mkoani, bila shaka wewe utakuwa mchezaji ' asiyegusika' popote pale.
Namba tano mwenye sifa za utulivu, mpangaji mzuri wa ngome na kiongozi mwenye kujiamini, ni sifa ambazi zilimfanya Chuji kusajiliwa na Simba, kwa ajili ya msimu wa mwaka 2006. Chuji, 25 kwa sasa ( umri huu ndiyo unaotambulika' aliingia Simba na kukuta wachezaji wengine wazuri kama yeye. Katika nafasi ya ulinzi wa kati ambayo alikuwa akicheza katika timu ya Polisi Dodoma, ndani ya Simba, nafasi hiyo ilikuwa chini ya Victor Costa, na beki Mrundi, Said Koko'o hivyo ilimfanya kukutana na upinzani mkali wa kuwania nafasi.
TUMIA NAFASI YAKO VIZURI...
Chuji, alitumia mwanya wa matatizo ya kinidhamu yaliyopelekea baadhi ya wachezaji muhimu kuwa kando ya timu. Costa, hakuwa na maelewano mazuri na kocha Neidor dos Santos, na ni hapo ndipo ikapatika nafasi ya Chuji, kuonesha kandanda lake la uhakika. Dos Santos, alipendezwa na viwango vya wachezaji vijana wakati huo, Chuji, Henrry Joseph na Kelvin Yondan na akaamua kuwapata nafasi ya wachezaji watovu wa nidhamu.
YANGA WALIMUONEA SIMBA....
Soka la uhakika akicheza katika idara ya kiungo kwa dakika 120 lilimtambulisha kiungo, mwenye mapafu ya ' mbwa' katika soka la Tanzania. Japo alikuja kukosa mkwaju wake wa penati baada ya mchezo huo wa nusu fainali ya michuano ya Tusker dhidi ya mahasimu wao Yanga, kumalizika kwa sare ya bao 1-1.
ATUA RASMI YANGA, AONESHA TABIA MBAYA KWA SIMBA...
Baada ya kumalizika kwa msimu wa mwaka 2006, Chuji alijiunga na Yanga katika kile alichokiita usajili wa maslai zaidi na si mapenzi. Ni wakati huo alikuwa akisema kuwa kurudi Simba ni bora akauze ndimu. Simba walipigania sana haki zao lakini wakaishia kupigwa chenga na kiungo huyo kila walipomuomba wakae naye meza moja kumaliza utata uliokuwa umegubika usajili wake, na kama kwenda Yanga aende kwa amani. Wazee wa Yanga wakamng'ata masikio na kumwambia akifanya hivyo tu amekwisha kisoka. Mifano mingi ikatolewa huku akiambiwa kuwa Mwinyi Rajab ni mfano mzuri kuhusu wasemayo. Baadae akaruhusiwa kuichezea Yanga na shirikisho la soka nchini, TFF. Baadae akafungiwa kwa kosa la kuonesha kidole cha kati katika moja ya michezo yake ya kwanza akiwa mchezaji wa Yanga. Alifungiwa kwa muda wa miezi sita.
CHUJI WA KADI ZA MARA KWA MARA....
Hata aliporudi uwanjani baada ya kumalizika kwa adhabu yake, Chuji alikuwa ni mchezaji wa kiwango kilekile, akizima kila kitu kuhusu tabia yake kucheza soka la ukosefu wa nidhamu kwa kiwango chake na mchezo uliochangamka. Moja kati ya majuto makubwa ya aliyekuwa kocha wa timu ya taifa ya Tanzania, Taifa Stars, Marcio Maximo ni adhabu ya mchezaji huyo. Akiwa mfuasi ya nidhamu ni wazi Maximo alikuwa akitambua mchango wa Chuji katika kati yake. Tabia yake mbaya ilimfanya kuingia katika vifungo vya mara kwa mara, na hivyo kukosa nafasi ya kuichezea timu ya taifa mara kwa mara.
SAHAU YOTE, ALITUPELEKA  CHAN
Kiwango kizuri cha Chuji, kilionesha ni kwa nini kocha Maximo alipinga adhabu yake wakati ule, 2007. Chuji alikuwa sehemu muhimu ya wachezaji wa timu ya taifa waliozisukuma nje, Kenya, Uganda na Sudan kisha kutinga kwa michuano ya CHAN, 2009, nchini Ivory Coast. Alifunga moja ya mabao bora wakati Stars ikiifunga, Sudan katika mchezo wa mwisho wa kufuzu, jijini Dar, kabla ya kwenda kusaidia ushindi wa kukumbukwa ugenini, jijini Khartoun.
CHUJI APOTEZA DIRA....
Wakati kiwango chake kiliposhuka zaidi, 2009. Chuji aliishia kugombana na kocha Maximo katika timu ya taifa. Makocha wa klabu yake, Dusan Kondic, na baadaye, Kostadin Papic bado walikuwa wakisema kuwa hakuna kiungo kama Chuji katika nyakati za sasa nchini. Baadae kiwango kilizidi kuporomoka huku mambo ya nje ya uwanja yakimuathiri kimchezo, akashuka thamani hata kwa mashabiki wake mwenyewe. Alitumia misimu miwili kuanzia 2009- 10, na 2010 - 11 akicheza soka huku akiitwa ' mzee'. Kisha baada ya kumalizika kwa mkataba wake na Yanga, klabu haikumuongeza tena mkataba. Akarudi Simba, na kusajili katika michuano ya Kagame, 2011. Akaishia kucheza dakika zisizozidi kumi wakati timu yake ikicheza michezo sita hadi fainali.
NITAENDELEA KUMUHUSUDU PAPIC KWA HIKI...
   
Hata wakati, Chuji akiitwa 'mzee' katika utawala wake Yanga, kocha Papic bado aliendelea kusema kauli yake ile ile kuwa Chuji ni kiungo wa aina yake. Baada ya kumalizika kwa michuano ya Kagame, Simba iliamua kumtema Chuji, na hivyo akajikuta nje ya soka kwa muda wa miezi sita. Kila mtu alikuwa akisema lake, wapo waliokuwa wakisema kuwa mwisho wake umefika na kuna wakati akakanusha taarifa za yeye kutumia madawa ya kulevya ndiyo sababu ya kutemwa kwake Simba. Baada ya Sam Timbe kufukuzwa kazi ya ukocha, Yanga ilimrejesha Papic na kocha huyo akaamua kumpatia mkataba wa miezi sita ndani ya Yanga.
Akafanya vizuri na kupewa mkataba wa miaka miwili zaidi, na mapema mwezi uliopita alirefusha kwa miaka miwili zaidi ya kuendelea kuichezea Yanga. Kwa sasa, amepevuka zaidi na amekomaa kimaamuzi. Si mkorofi akiwa uwanjani, ana jiheshimu na kuheshimu mchezo wenyewe. Amekuwa kiongozi, na mchapakazi mzuri kwa timu. Kama ni safari, Chuji amepitia safari ndefu, ila kwangu nampa tuzo ya mchezaji mwenye nidhamu kwa kipindi cha mwaka mzima, 2013. Amefanya kazi yake vizuri. Ningemrudisha Chuji katika nafasi ya ulinzi wa kati ili anisaidie katika timu yangu. Nafasi hii inahitaji busara zaidi, na pengine hata Dos Santos angemrudisha katika nafasi aliyomtoa. Beki tano.

CAMEROON KWENDA BARANI ULAYA KUWASHAWISHI WACHEZAJI KURUDI KUITUMIKIA NCHI YAO


Ujumbe wa kutoka nchini Cameroon wanatarajiwa kwenye nchi Ulaya kuwashawishi wachezajiwa wa nchi hiyo wanachezea katika nchi za ulaya kujiunga na timu ya taifa ya nchi hiyo "Indomitable Lions".

Mpango huo wa kusaka vipaji vipya umekuja wakati Cameroon ikiwa inajiandaa kushiriki fainali za kombe la dunia mwaka kesho nchini Brazil.

Chama cha soka cha Cameroon - Fecafoot kimesema mpango wao kwa sasa ni kushawishi wachezaji wanne wanaocheza soka ya kulipwa nchini Ufaransa.

Wachezaji hao Axel Ngando anachezea klabu ya Auxerre ya ligi daraja la pili nchini Ufaransa, Samuel Umtiti anachezea Lyon na Jean- Christophe Behebeck anachezea Valenciennes.

Mchezaji mwinginie anayewindwa ili kuuongeza nguvu kwenye timu ya taifa ya Cameroon ni Paul Geoges Ntep de Madiba ambaye pia naye anayechezea Auxerre ya Ufaransa.

Tunataka kuwashawishi hao wachezaji wachezee timu ya taifa ya Cameroon, na hasa kwenye fainali za Kombe la Dunia na pia wachezee Cameroon kwa hapo baadae Shirikisho la soka la Cameroon limesema kwenye taarifa yake.

Sunday, December 29, 2013

FARES MAGESA NA MICHAEL MALUWE CHALI,JOHN BANDIE,SALEH ZONGA,MICHAEL MWITA,MANASSEH ZABLON NA AMINA AHMED WAIBUKA KIDEDEA UCHAGUZI WA TBF.



MAGOLIKIPA WA LIGI KUU YA VODACOM WAIFUNGA CLOUDS MEDIA MABAO 3-1.

 Wachezaji wa timu ya Clouds Media Group wakifanya mazoezi mepesi kabla ya kuanza kwa mtanange wa kufunga mwaka dhidi ya timu ya magorikipa wanaocheza Ligi Kuu ya soka tanzania Bara.
Mbwiga akijifua.
 Kocha mchezaji wa timu ya Clouds Media Group, Mbwiga Mbwiguke (kulia) akiwaongoza wachezaji wenzake katika mazoezi.
 Wachezaji wa timu ya Makipa wanaocheza Ligi Kuu wakifanya mazoezi kwenye Uwanja wa Makurumla jijini Dar es Salaam.
 Mchezajki swa timu ya Makipa, Ivo Mapunda akisalimiana na Shaffih Dauda.
 Kikosi cha Clouds Media Group
 Timu ya Makipa wa Ligi Kuu wakiwa katika picha ya pamoja.
 Wachezaji wa tizmu ziote mbili wakisimama kwa dakika moja kuomboleza kifo cha kocha wa makipa wa timu ya Simba, Marehemu James Kisaka.
 Mchezaji wa timu ya Makipa Shaban Kado akimiliki mpira huku Bakari Masuli (kulia) akijaribu kumzuia.
Said Saleh 'Mbwiga Mbwiguke' (katikati) akitafuta mbinu za kumpokonya mpira Ivo Mapunda. 

 Mbwiga Mbwiguke (kushoto), akichuana na golikipa wa Mtibwa Sugar Hussein Sharif ''Cassilas''.
 Mbwiga Mbwiguke (kushoto), akichuana na Hussein Sharif.
 Mbwiga akimtoka kipa wa Yanga Deogratius Munishi 'Dida'.
 Mshambuliaji wa Clouds Media Group, Maulid Kikucha akimiliki mpira mbele ya golikipa wa JKT Ruvu Said Mohammed.
 Beki wa Clouds Media Group, Said Tully akimiliki mpira huku akizongwa na Hussein Sharif.
 Hekaheka......
 Mbwiga akifanya mahojiano na Juma Pondamali na Abdulhalim Humud.
 Huniwezi......

Said Mohamed akimtoka mchezaji wa Clouds Media.

AZAM FC YALISAKA KOMBE LA MAPINDUZI KWA MARA YA TATU, KUTUA ZANZIBAR JANUARI 1 KAMILI GADO!!


Na Baraka Mpenja,  Dar es salaam

MABINGWA watetezi wa kombe la Mapinduzi, klabu ya Azam fc imetamba kwenda kutetea taji hilo kwa mara ya tatu mfululizo katika michuano inayoanza kutimua vumbi januari mosi mwakani.

Jafar Idd Maganga, Afisa habari wa klabu hiyo amesema panapo majaaliwa timu hiyo inatarajia kung`oa nanga jijini Dar e salaam januari 1 mwaka huu kuelekea visiwani Zanzibar tayari kuanza harakati za kutafuta kombe hilo.

“Michuano hii ni muhimu sana kwetu. Kocha mkuu Mcameroon, Joseph Marius Omog atakuwa na nafasi nyingine ya kupima kikosi chake na kuelewa wapi kuna matatizo ili kuiandaa timu kwa ajili ya mzunguko wa pili wa ligi kuu soka Tanzania bara na michuano ya kimataifa”. Alisema Jafar.

Jafar aliongeza kuwa tangu timu ipate kocha mpya, wachezaji wamekuwa wakipambana kutafuta nafasi   katika  kikosi cha kwanza.

“Mapinduzi Cup itawajenga wachezaji wetu. Kila mchezaji anataka kuonekana mbele ya kocha, ushindani umeongezeka zaidi, bila shaka baada ya kumalizika kwa michuano hii muhimu, Kocha Omog atakuwa amepata kikosi chake”.

“Kikosi kipo safi, wachezaji wanaonesha juhudi kubwa. Cha msingi wote wanaelewa nini cha kufanya, dira ya Azam fc ipo wazi kabisa kuwa inataka kupata mafanikio makubwa zaidi anga za kitaifa na kimataifa”. Alisema Jafar.

Mashaindano ya mapinduzi yatakuwa ya kwanza kwa kocha Omog,  achilia mbali ile mechi ya kirafiki iliyocheza Alhamisi  ya kujaribu mfumo wa Tiketi za electroniki ndani ya uwanja wa Chamazi dhidi ya Ruvu shooting.

Katika mchezo huo, Omog aliiongoza Azam fc kupata ushindi wake wa kwanza wa mabao 3-0 , ambapo mshambuliaji mpya  kutoka Ivory Coast, Mouhamed Kone  alifunga bao mojawapo, huku mengine yakifungwa na Jonh Raphael Bocco `Adebayor` na Kipre Herman Tchetche kwa mkwaju wa penati.

Kombe la Mapinduzi mwaka huu litajumuisha timu 12 kutoka ndani na nje ya nchi ambazo zimegawanywa katika makundi matatu yenye timu nne.

Kundi A: kuna timu za Pemba Combine, Chuoni, URA kutoka Uganda na Mbeya City, huku kundi B likiwa na klabu za Simba, KMKM, AFC Leopard ya Kenya pamoja na KCC kutoka Uganda.

Wana Lambalamba, Azam fc ambao ndio mabingwa watetezi wapo kundi C na timu za Tusker fc ambao ni makamu bingwa, Dar Young Africans na Unguja Combine.

Pazia la michuano hiyo litafunguliwa rasmi januari mosi ambao mechi ya kwanza itakuwa saa 10:00 jioni baina ya KMKM dhidi ya KCC, kwenye uwanja wa Amaan, mjini Unguja.
Mechi ya ufunguzi itapigwa saa 2:00 usiku ambapo wekundu wa Msimbazi, Simba Sc watakuwa na kibarua kizito dhidi ya AFC Leopard kutoka nchini Kenya na mgeni rasmi atakuwa kocha mkuu wa timu ya Taifa ya Italia, Cesare Prandelli.

Shughuli itaendelea januari 2 ambapo katika uwanja wa Amaan, Azam fc watashuka dimbani saa 10:00 jioni  kukipiga na Unguja Combine, na usiku saa 2:00, Dar Young Africans watakuwa kibaruani dhidi ya Tusker fc.

Katika uwanja wa Gombani Pemba, URA watakabiliana na Chuoni (kundi C) majira ya saa 8:00 mchana, huku Mbeya City ikishuka dimbani dhidi ya Pemba Combine, saa 10:00 jioni katika mchezo wa kundi A.

Fainali ya michuano hii itapigwa siku ya sherehe za Miaka 50 ya Mapinduzi ya Zanzibar, januari 12 na mechi ya fainali itapigwa saa 2:00 usiku katika uwanja wa Amaan mjini Unguja.

MWAMBUSI: YANGA, SIMBA , AZAM AFADHALI NIMEKUTANA NAZO, TIMU ZA KENYA, UGANDA SIJUI MUZIKI WAKE KOMBE LA MAPINDUZI!!


Na Baraka Mpenja, Dar es salaam

KLABU ya Mbeya City Kwa mara ya kwanza inakutana na timu kutoka nje ya Tanzania ambazo zitashiriki michuano ya Mapinduzi inayotarajia kuanza kushika kasi januari mosi mwakani katika Uwanja wa Amaan mjini Unguja na Gombani kisiwani Pemba.

Klabu hii imepanda ligi kuu msimu huu na tayari imeshaonesha kiwango cha juu kwa kuziwekea ngumu timu kubwa za Simba, Yanga na Azam fc , na kumaliza ngwe ya kwanza  ligi kuu ikijikusanyia pointi 27 katika nafasi ya tatu bila kupoteza mchezo wowote.

Mbeya City wanakwenda Zanzibar huku wakijua wazi kuwa wanakwenda kukabiliana na changamoto kubwa tatu.

Moja; wanashiriki kwa mara ya kwanza michuano hii mikubwa tangu kuanzishwa kwao.
Pili; wanakwenda kukutana kwa mara ya kwanza  na timu za Kenya , Uganda zenye wachezaji wanaocheza mazingira tofauti na ligi kuu Tanzania bara.

Tatu; wanakwenda kukutana na timu za visiwani Zanzibar kwa mara ya kwanza.
Ukiangalia mambo haya matatu, utagundua kuwa Mbeya City ni wageni wa kila kitu kuelekea mashindano haya.

Lakini ni nafasi yao kuoenesha ubora wao kama walivyofanya ligi kuu. Pia itasaidia kupima uwezo wa wachezaji wao mbele ya timu ngeni kabisa machoni kwao.
Itakuwa changamoto mpya kwa wachezaji wa Mbeya City,  ambapo wengi wao ni vijana wanaochipukia katika soka la ushindani.

Ukitazamana timu zenye majina makubwa mfano URA, Tusker,  AFC Leopard , KCC, Simba, Yanga, na Azam fc, Mbeya City imekutana na timu tatu tu yaani Simba, Yanga na Azam fc kwenye michuano ya ligi kuu soka Tanzania bara.

Na ndipo kocha mkuu wa klabu hiyo, Juma Mwambusi anakiri wazi kuwa michuano hii ni migumu kwake, hivyo ameichukulia uzito wa hali ya juu.

Ili kukabiliana na changamoto mpya, Mwambusi alisema atatumia kikosi cha kwanza  kupima uwezo wa wachezaji wake mbele ya wachezaji wa kimataifa kwa lengo la kujiridhisha kabla ya kuanza mzunguko wa pili ligi kuu.

“Tunaenda kushiriki kwa mara ya kwanza. Vitu vingi sisi ni wageni, lakini naamini maandalizi yetu yatatupatia mafanikio. Mwenyezi Mungu akitupa uzima, tutawasili Zanzibar desemba 31”. Alisema Mwambusi.

Mwambusi alisema uwepo wa Simba sc, Yanga na Azam fc sio tatizo kwao kwani afadhali wameshakutana ligi kuu, lakini changamoto kubwa ni timu ngeni kutoka Kenya na Uganda .

Hata hivyo, Mwambusi aliongeza kuwa timu za Tanzania bara zimeongeza wachezaji wapya , hivyo wataongeza kasi  tofauti na mzunguko wa kwanza wa ligi kuu.
Yanga wameongeza nguvu kwa kumsajili Kipa, Juma Kaseja, Kiungo, Hassan Dilunga , na mshambuliaji , Mganda Emmanuel Okwi

Michuano iliyopita, Yanga haikushiriki kwani kwa wakati ule ilikuwa na ziara nchini Uturuki (Barani Ulaya) kujiandaa na mzunguko wa pili wa ligi kuu ambao waliishia kutwaa ubingwa na kuivua Simba sc.
Kwa upande wa Simba,  nao wameongeza wachezaji wapya katika dirisha dogo ambao ni Uhuru Selemani, Ivo Mapunda, Ali Badru, Awadh Juma, Donald Mosoti na Yaw Berko.
Azam fc wao hawakuona haja ya kuongeza wachezaji wengi, lakini wamemsajili mshambuliaji mmoja kutoka nchini Ivory Coast, Mouhamed Kone, hivyo kuongeza kasi  zaidi katika safu ya ushambuliaji inayoongozwa na Kipre Tchetche pamoja  na nahodha John Bocco, `Adebayor`.

Mabadiliko hayo katika vikosi vya timu hizi za Bara yanampa shida kocha Juma Mwambusi kwani ni wachezaji mahiri, lakini ametamba kuonesha kandanda bora kama kawaida yao.
Timu za Azam fc, Simba sc na Yanga zimeshatangaza kushuka na vikosi vyao vya kwanza  “full nondo”  kwa lengo la kupima uwezo wa wanandinga wao.

Tofauti na Simba, Mbeya City ambazo malengo yao ya kushiriki mashindano hayo ni kuandaa vikosi kwa ajili ya ligi kuu, klabu za Yanga , KMKM na Azam fc zitayatumia mashindano haya kuandaa vikosi vyao kwa ajili ya michuano ya ligi kuu na  kimataifa barani Afrika.