Search This Blog

Saturday, April 5, 2014

SIMBA YAAMBULIA SARE YA 1-1 KAITABA, RASMI MBEYA CITY WAJIENGUA MBIO ZA UBINGWA, ASHANTI, MGAMBO, PRISONS VITANI KUKWEPA KUSHUKA DARAJA!!

Na Baraka Mpenja, Dar es salaam


MATOKEO ya 0-0 waliyoyapata Mbeya City leo hii kwenye mchezo mgumu wa ligi kuu soka Tanzania bara dhidi ya Ashanti United katika uwanja wa Azam Complex, Chamazi, nje kidogo ya jiji la Dar es salaam yamewagharimu na kuwakosha rasmi ubingwa msimu huu.
Ashanti United waliokuwa na lengo la kupata ushindi leo hii mbele ya Mbeya City wameambulia pointi moja muhimu kuliko kupoteza mchezo huo.
City wamefikisha pointi 46 katika nafasi ya tatu sawa na Yanga waliopo nafasi ya pili kwa pointi 46, lakini kikosi cha Pluijm kina wastani mzuri wa mabao ya kufunga na kufungwa.
Hii ilikuwa mechi ya 24 kwa Mbeya City, hivyo wamebakiza mechi mbili nyumbani  dhidi ya Azam fc na Mgambo JKT.
Kama watashinda mechi zote watafikisha pointi 52 ambazo tayari Azam wameshafikisha kileleni.
Kwa maana hiyo, Mbeya City rasmi wamejitoa kuwania ubingwa na kuwaacha wanaume wawili, Yanga sc na Azam fc kuendelea na vita hiyo.
Kilichobaki kwao ni kuisaka nafasi ya pili, kwani wanaweza kuipata kutegemeana na matokeo watakayopata Yanga SC.
Yanga wamebakiza mechi nne kuanzia ya kesho dhidi ya JKT Ruvu ndani ya dimba la Taifa jijini Dar es salaam.
Kama Mbeya City wanataka  kuchukua nafasi ya pili wanatakiwa kuwaombea Yanga mabaya ili wapoteze mchezo mmoja, washinde mmoja na kutoa sare miwili.
Kama matokeo hayo yatatokea, maana yake Yanga atavuna pointi tano pekee na ukijumlisha na pointi 46 walizonazo sasa watafikisha pointi 5I ambazo Mbeya City atazivuka endapo atashinda mechi zote.
Yanga ataanza kazi kesho dhidi ya JKT Ruvu, baada ya hapo atavaana na Kagera Sugar mechi ya kiporo aprili 9, na hatimaye atasafiri kwenda Arusha aprili 13 kuwavaa JKT Oljoro na kurejea Dar es salaam kufunga msimu dhidi ya Simba uwanja wa Taifa aprili 19 mwaka huu.
Kwa mechi alizosaliwa nazo Yanga si rahisi kutabiri matokeo, lolote linaweza kutokeo, lakini kwa Mbeya City biashara imewakata kwasababu mambo ya kusubiri mwenzako apoteze inaweza kutokea au isitokee.
Hata hivo mtandao huu umezungumza na kocha msaidizi wa Mbeya City, Maka Mwalwisyi ambaye amekiri wazi kuwa mchezo wa leo ulikuwa mgumu sana kwa upande wao.
‘Tunamshukuru Mungu mechi imeisha salama na tumeambulia suluhu. Ni matokeo mabaya kwetu, lakini huwezi jua waliopo juu yetu watapata matokeo ya aina gani huko mbeleni. Kimsingi yametuharibia sana, lakini hatukati tamaa kupambana mpaka dakika ya mwisho”.
“Hata kama itakuwa tofauti na malengo yetu sio mbaya. Huu ni msimu wetu wa kwanza. Tumejitahidi kadri ya uwezo wetu na haya ndio mavuno yetu. Tunarudi kujiandaa na mchezo ujao dhidi ya Azam fc”. Alisema Kocha Maka.
Kocha wa Ashanti United, Abdallah Kibadeni aliwahofia Mbeya City kwasababu ya ubora wao, lakini amemaliza mechi kwa kupata pointi moja muhimu.
Kwa matokeo hayo, Ashanti wanafikisha pointi 22 katika nafasi ya 12 baada ya kushuka dimbani mara 24.
Mchezo ujao watashuka dimbani kukabiliana na Simba uwanja wa Taifa na watahitimisha kibarua chao msimu huu dhidi ya Tanzania Prisons uwanja wa sokoine jijini Mbeya.
Kama Ashanti United watashinda michezo hiyo mitatu watafikisha pointi 31 na pengine kujiweka mazingira mazuri ya kubakia ligi kuu.
Wakati huo huo Mgambo JKT wapo nafasi ya 11kwa pointi 22 kama Ashanti, na wamebakiwa na michezo mitatu.
Kama Mgambo watashinda mechi zijazo dhidi ya Coastal Union, Kagera Sugar na Mbeya City watafikisha pointi 31 kama Ashanti, na hapo timu moja italazimika kushuka kwa kuangalia tofauti ya mabao ya kufunga na kufungwa.
Rhino wapo mkiani kwa pointi 13 na wamebakiza mechi tatu. Kama watashinda zote watafikisha pointi 22 ambazo zimefikiwa na Ashanti, Tanzania Prisons na Mgambo, huku timu hizi zikiwa na mechi tatu mkononi.
Oljoro JKT wapo nafasi ya 13 kwa pointi 15 na wakishinda mechi zao tatu zilizosalia watafikisha pointi 24 ambazo zinaweza kupitwa na Ashanti United, Prisons na Mgambo JKT.
Hivyo kwa mazingira haya, Rhino Rangers na JKT Oljoro zina asilimia kubwa ya kushuka daraja, huku Ashanti, Mgambo na Prisons zikipambana kwa nguvu kukwepa kuungana na timu hizi mbili za mwisho.
Mchezo mwingine umepigwa katika dimba la Kaitaba ambapo wenyeji wa uwanja huo wamewakaribisha wekundu wa Msimbazi Simba sc.
Mechi hiyo imemalizika kwa sare ya bao 1-1.
Simba walikuwa wa kwanza kuandika bao la kuongoza katika dakika ya 45 kipindi cha kwanza  kupitia kwa Zahor Idd Pazzi akipokea krosi kutoka kwa nahodha wao, Nassor Masoud Cholo.
Kagera walisawazisha  bao hilo dakika ya 51 kipindi cha pili kupitia kwa mshambuliaji wao hatari, Them Felix `Mnyama`.
Kwa matokeo hayo, Simba sc wamefikisha pointi 37 katika nafasi ya 4 baada ya kushuka dimbani mara 24.
Kagera Sugar wamefikisha pointi 34 katika nafasi ya 5 baada ya kushuka dimbani mara 23.
Mechi ya Kaitaba haikuwa na ushindani mkubwa kwani timu zote hazikuwa na cha kupoteza, kwa maana ya kutotafuta ubingwa wala nafasi ya pili.
Timu zote zilikuwa zinashambuliana kwa zamu, lakini Kagera Sugar walipata nafasi nyingi zaidi ya Simba.
Hata hivyo ubutu wa safu za ushambuliaji kwa timu zote ,kumeamuru matokeo yawe 1-1 mpaka dakika 90 zinamalizika.
Ligi hiyo itaendelea kesho kwa mechi kadhaa kupigwa katika miji tafouti.
Jijini Dar es salaam, Yanga watakabiliana na JKT Ruvu na ushindi ni muhimu kwa timu zote.
JKT Oljoro watawakaribisha maafande wa Tanzania Prisons katika dimba la Shk. Amri Amri Abeid Kaluta jijini Dar es salaam.
Rhino Rangers watakuwa dimba la Ali Hassan Mwinyi kuumana na Mtibwa Sugar kutoka Morogoro.
Nao wagosi wa Kaya watawakaribisha ndugu zao, Mgambo JKT katika dimba la CCM Mkwakwani, Jijini Tanga.

TAIFA STARS, BURUNDI KUCHEZA APRILI 26 - TIMU YA WATOTO WA MITAANI YANG'ARA BRAZIL

Timu ya Taifa ya Tanzania (Taifa Stars) itacheza mechi ya kirafiki na Burundi (Intamba Mu Rugamba) Aprili 26 mwaka huu ikiwa ni sehemu ya maadhimisho ya miaka 50 ya muungano wa Tanganyika na Zanzibar.

Taifa Stars inayodhaminiwa na Kilimanjaro Premium Lager tayari ipo kambini Tukuyu mkoani Mbeya ikijiandaa kwa ajili ya mechi hiyo ikiwa na wachezaji waliopatikana katika programu maalumu ya kusaka vipaji.

Baadaye wachezaji wengine wa Taifa Stars ambao wapo nje ya programu ya kusaka vipaji wataungana na wenzao kabla ya kutengeneza kikosi cha mwisho kitakachoivaa Burundi.

Mechi hiyo itakayofanyika Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam itachezeshwa na waamuzi wanaotambuliwa na Shirikisho la Kimataifa la Mpira wa Miguu (FIFA) kutoka nchini Kenya.

TIMU YA WATOTO WA MITAANI YACHACHAFYA BRAZIL
Timu ya Watoto wa Mitaani ya Tanzania imefanikiwa kuingia nusu fainali ya mashindano ya Kombe la Dunia yanayofanyika Rio de Janeiro nchini Brazil baada ya jana kuifunga Indonesia kwa jumla ya mabao 5-3.

Hadi muda wa kawaida wa mchezo huo unamalizika timu hizo zilikuwa zimefungana mabao 2-2 ndipo ikatumia mikwaju ya penalti kuamua mshindi. Tanzania ilipata penalti tatu dhidi ya moja ya wapinzani wao.

Kwa matokeo hayo, Tanzania sasa itacheza mechi ya nusu fainali leo dhidi ya Marekani ili kupata timu zitakazocheza mechi za fainali na kutafuta mshindi wa tatu. Mechi za fainali na kutafuta mshindi wa tatu zitachezwa kesho (Aprili 6 mwaka huu).
Timu nyingine zilizoingia nusu fainali na mechi zake zinachezwa leo (Aprili 5 mwaka huu) ni Burundi itakayocheza na Pakistan.


Katika mechi zilizopita, Tanzania ilitoka sare ya mabao 2-2 na Burundi, ikaitandika Argentina mabao 3-0 ikailaza Nicaragua mabao 2-0 na ikafungwa na Philippines mabao 2-0.

KUTUHUMU WACHEZAJI KULA RUSHWA HUWAONDOA MCHEZONI, MASHABIKI YANGA WAWE WATULIVU KUTETEA UBINGWA WAO!!


Na Baraka Mpenja, Dar es salaam


KIPIGO walichokipata Yanga sc kutoka kwa Mgambo JKT machi 30 mwaka huu kwenye uwanja wa CCM Mkwakwani, jijini Tanga kimezidi kuwavuruga zaidi viongozi, makocha, na mashabiki wa klabu hiyo.
Imeonekana kuwa ajabu kwa Mgambo JKT kuwafunga Yanga, wakati mpira wa miguu huwa una matokeo ya aina hiyo.
Katika mechi, wachezaji 22 wanapambana kwa maana ya wachezaji 11 kwa kila timu.
Kama wachezaji wanakuwa sawa kwa timu zote kwa mujibu wa sheria, basi kushinda ni haki kwa timu yoyote.
Lakini kuna wakati timu moja inaweza kujipa matumaini zaidi ya kushinda mechi na kusahau kuwa inaenda kucheza na watu waliojiandaa kama wao.
Hakuna ubishi, kupata matokeo kunatokana na mipango mizuri ya uwanjani na nje ya uwanja.
Viongozi wa timu wana wajibu mkubwa kwa nafasi yao kuhakikisha kila kitu kinaenda sawa, mfano; kuhudumia kambi ya wachezaji.
Inapofika muda wa uwanjani, makocha pekee na wachezaji ndio wenye wajibu wa kulipa fadhili za viongozi wao na mashabiki waliopo nyuma yao.
Kutokana na ubora wa Yanga katika kikosi chao, mashabiki wake waliamini Mgambo lazima wale kipigo kikali jijini Tanga.
Ikimbukwe kabla ya mechi hiyo, Yanga walitoka kushinda mabao 5-0 dhidi ya Tanzania Prisons.
Kwa tafsiri hiyo, safu ya ushambuliaji ya Yanga ilionekana kuwa na uchu mkubwa wa kufumania nyavu, hivyo watu wengi walitegema kuona karamu nyingine ya mabao dhidi ya timu ya Mgambo inayoonekana kuwa dhaifu msimu huu.
Kwa watu wanaojua mpira, kama hawakuthubutu kusema Yanga wana asilimia zote kushinda mechi ile, bali waliwapa asilimia nyingi ya kupata matokeo mazuri zaidi ya Mgambo.
Kuipa timu asilimia kubwa ya ushindi kwasababu ya ubora wa kikosi, ni suala la kawaida sana hata huko duniani.
Ndio maana Manchester United walitaniwa kuwa wanaenda kupambana na Bayern Munich yenye kazi nyepesi ya kuvuna ushindi.
Wengine walisema ni vita ya Daudi na Goliathi, lakini wakasahau kuwa mpira wa miguu una matokeo ya aina yake.
Man United walikuwa na haki ya kupata matokeo yale, hata kama Bayern ni bora zaidi yao kwa sasa.
Haimaanishi timu fulani kuwa na kikosi dhaifu, basi haina haki ya kushinda. Soka la uwanjani linahitaji mipango. Ukipata nafasi tumia.
Mgambo JKT walikuwa na haki ya kushinda licha ya kucheza pungufu kwa dakika 60 baada ya mchezaji wao Mohamed  Hussein Neto kuoneshwa kadi nyekundu.
Walionekana kukomaa zaidi na kuwa na mipango mizuri na ndio maana waliweza kuwafunga Yanga.
Kinachoonekana kwa baadhi ya mashabiki wa Yanga ni kuamini timu yao ina haki ya kushinda katika kila mechi kwasababu ya  ubora wa kikosi chao.
Lakini mpira huwa hauendi hivyo, kufungwa kupo hata kama una ubora mkubwa.
Mara ngapi timu ndogo zinapata matokeo mbele ya timu kubwa?. Mpira huwa hauna fomula ya kushinda mechi zote.
Kipigo cha Mgambo kimezidi kuibua mengi. Mojawapo ni tuhuma za baadhi ya wachezaji kula rushwa kupoteza mchezo.
Si rahisi kubaini kama kweli wanaotuhumiwa walikuwa rushwa,  kwasabau jambo hili hufanyika kwa siri na ushahidi unahitajika unapolisema.
Kuna wakati Azam fc walijiingiza mkenge wa kuwatuhumu kula rushwa Erasto Nyoni,  Said Morad na Aggrey Morris na kusababisha timu kufungwa.
Watu wa mpira wanakumbuka  kesi hii ilifikishwa mpaka taasisi ya kuzuia na kupambana na rushwa (TAKUKURU), lakini baadaye ushahidi ulikosekana na kuwaachia huru.
Azam fc walijikuta wakipoteza muda mwingi na kuigharimu timu bila sababu yoyote ya msingi.
Kuwatuhumu wachezaji kula rushwa imekuwa tamaduni ya Simba na Yanga, lakini msimu huu viongozi wa Yanga wameonekana kuwa makini na kukanusha kila inapotokea taarifa kama hizi.
Wengine wamekuwa wakiandika na kusema mitaani kuwa baadhi wa wachezaji wa Yanga ambao ni Athumani Idd `Chuji` , Kelvin Yondani na Juma Kaseja wamesimamishwa kwasababu ya tuhuma za kuhujumu timu kwenye mechi dhidi ya Mgambo.
Duru za habari kutoka Yanga zimesema kuwa uongozi wa klabu hiyo unasikitishwa na taarifa zinazotolewa na baadhi ya vyombo vya Habari tangu siku ya jumatano kwamba wachezaji  Kaseja, Yondani,  na "Chuji" wamefukuzwa kwenye timu na Emmanuel Okwi ameondoka kurejea kwao nchini Uganda.
Yanga wamesema taarifa hizi ni uongo mtupu, na zina lengo la kuwagawa wachezaji.
“Hakuna mchezaji yoyote aliyefukuzwa kwenye timu baada ya kupoteza mchezo dhidi ya Mgambo Shooting mwishoni mwa wiki, taarifa hizo zinasambazwa kwa Propaganda ili kuweza kuvunja umoja uliopo ndani ya timu kwa wachezaji na walimu,  pia kwa Viongozi na wanachama”. Ilisema taarifa ya Yanga.
Taarifa hiyo ilizidi kufafanua kuwa Kelvin Yondani hakuungana na wenzake kambini baada ya kuomba kupumzika na kutatua matatizo yake ya kifamilia.
Benchi la Ufundi lilimpa ruhusa hiyo kwa kuzingatia mchezaji mwenyewe asingeweza kutumika kwa mchezo wa jumapili dhidi ya JKT Ruvu kufuatia kuwa na kadi tatu za njano, lakini ataungana na wenzake mara baada tu ya mchezo huo.
Pia Athumani Idd "Chuji", David Luhende pamoja na kiungo Haruna Niyonzima ni wagonjwa, wanaendelea na matibabu kuhakikisha wanakua `fiti` na kuungana na wachezaji wao mara baada ya mchezo wa siku ya jumapili.
Aidha taarifa hiyo ilisema kuwa Juma Kaseja yupo kambini pamoja na mlinda mlango Deo Munish "Dida" aliyekua majeruhi kwa takribani wiki tatu kufuatia kupata jeraha katika mkono wakati timu ikijiandaa na mchezo dhidi ya Mtibwa Sugar.
Pia Emmauel Okwi yupo jijini Dar es salaam akiendelea na matibabu kufuatia kutonesha goti katika mchezo dhidi ya Mgambo mwishoni mwa wiki, awali Okwi aliiumia katika mchezo dhidi ya Prisons na kutolewa nje na machela.
Kimsingi viongozi wa Yanga wanapokanusha taarifa hizi, unaweza kugundua kuwa wanaelewa kuwa soka huwa lina matokeo kama waliyopata kule Tanga.
Kuwatuhumu wachezaji kunawafanya wawe na msongo wa mawazo na kubeba mzigo mzito kichwani.
Ufanisi wao unapungua wanapokuwa uwanjani, kwasababu wanacheza kuogopa kukosea.
Kama ni mshambuliaji anaweza kuogopa kujaribu kupiga mashuti kwa hofu ya kukosa bao na kutuhumiwa kula rushwa.
Kama ni mlinda mlango anashindwa kujiamini akiwa langoni, na ikitokea akafungwa bao, basi anajivuruga zaidi.
Si wakati muafaka kwa wanayanga kuanza kutuhumiana kwa mambo ya rushwa ikizingatiwa wana kibarua kizito kuteteta ubingwa wao.
Wanapolumbana muda huu na kuwasema vibaya wachezaji wao, wanaingiza balaa katika kikosi chao.
Mbele yao wapo Azam fc waliopo katika hali tulivu zaidi. Kuwang`oa kileleni umakini mkubwa na jitihada  vinahitajika.
Yanga wakubali matokeo ya uwanjani na wajiandae kufungwa kwani mpira ndivyo ulivyo.
Hawana haki ya kushinda tu, hata kupoteza pia.  Hivyo lazima wajifunze kuwa watulivu wanapoharibu ili kujipanga kwa mchezo mwingine.
Kutuhumiana kwa mambo ya rushwa si wakati wake kwasasa.

YANGA YA PLUIJM NA DAKIKA 360 ZA UTUMWA MBELE YA AZAM FC!!


Na Baraka Mpenja, Dar es salaam


MABINGWA watetezi wa ligi kuu soka Tanzania bara, Dar Young Africans wapo katika msongo wa mawazo baada  ya kuweka rehani ubingwa wao msimu huu mbele ya wana Lambalamba Azam fc wanaotesa kileleni kwa pointi 53.
Ligi ikiwa katika hatua za mwisho, Yanga wanaonolewa na kocha mkuu, Mholanzi, Hans Van Der Pluijm wamebakiza mechi 4 tu ambazo sawa sawa na dakika 360.
Katika msimamo, Yanga wapo nafasi ya pili baada ya kushuka dimbani mara 22 na kujisanyia pointi 46, pointi 7 nyuma ya Azam fc.
Dakika 360 zilizosalia kwa Yanga zitawafanya wawe watumwa kwasababu ya kasi ya Azam fc waliopo kileleni.
Wana Lambalamba wameshuka dimbani mara 23 na hawajawahi kupoteza mchezo hata wowote.
Kwa matokeo hayo, Azam fc wanasalia kuwa timu bora zaidi msimu huu kwa maana ya matokeo ya uwanjani.
Wakati mwingine, mpira wa miguu una matokeo yasiyotabirika, hasa ushindi unapokuwa muhimu kwa klabu yoyote ili kuamua hali fulani, mfano kutwaa ubingwa au kukwepa kushuka daraja.
Kwa kawaida, timu moja inapotangulia kufunga bao katika mchezo, inamfanya mwenzake kuwa mtumwa.
Utumwa huu unatokana na ukweli kuwa, klabu iliyofungwa  inahangaika kutafuta bao la kusawazisha.
Kwa fomula nyepesi, huwezi kuandika mbili bila moja. Unapofungwa bao 1-0 dakika ya 1, utakuwa mtumwa wa dakika 89 kutafuta njia ya kusawazisha na hatimaye kuandika bao la pili na la ushindi.
Ukiangalia msimamo wa ligi kuu mpaka sasa, Yanga wamebaki kuwa watumwa wa uwanjani zaidi ya klabu yoyote.
Utumwa wao upo katika mazingira mawili ambayo yanaonekana kufanana, lakini yana utofauti.
Mosi; ni watumwa wa kuhitaji kutetea ubingwa wao katika ligi yenye ushindani mkubwa zaidi.
Ili kuendeleza heshima yao, wanalazimika kujituma kwa ngvu zote katika michezo minne iliyosalia, ili kufanikisha malengo yao.
Kupata ubingwa ni jambo zuri, lakini unapotetea msimu unaofuata, inakuwa nzuri zaidi na unadhihirisha kuwa hukubahatisha kutwaa taji.
Pili; Yanga ni watumwa wa kuhitaji kusawazisha pointi 7 walizopo nyuma ya Azam fc ili kuweza kutetea ubingwa wao.
 Wakati wakiwa katika mazingira hayo magumu, Azam fc nao wanajitahidi kuziba njia za kukamatwa na Yanga.
Njia inayotumika na Azam fc ni kuhakikisha wanashinda mechi zote tatu zilizosalia.
Tayari Azam fc wapo mbele dhidi ya Yanga, kwa maana nyingine unaweza kusema Yanga ni watumwa wa vinara hao wa ligi kuu.
Hawana namna ya kutetea ubingwa bila kusawazisha pengo la pointi saba na kuwaombea Azam fc wafanye vibaya.
Kama Yanga watashinda mechi zote nne zilizosalia, wataweza kufikisha pointi 58, wakati Azam nao wana uwezo wa kuzifikia na zaidi.
Azam wamebakiza mechi tatu, kama watashinda zote watafikisha pointi 62. Kwa pointi hizo, hata Yanga wakishinda michezo yote kwa mabao 100, bado ubingwa utatua Chamazi.
Kwa matokeo yanayopatikana mechi hizi za mwisho, huwezi kutegemea Yanga na Azam fc kushinda mechi zao zilizosalia.
Kumbuka jumapili Yanga wanakabiliana na JKT Ruvu uwanja wa Taifa jijini Dar es salaam.
Huu utakuwa mtihani mwingine wa Pluijm kuanza  rasmi utumwa wa kuwafukuzia Azam fc kileleni.
JKT Ruvu wapo nafasi ya 9 kwa pointi 28. Kiukweli wapo mazingira tata ya kushuka daraja, kwa maana hiyo wanatakiwa kupambana kwa nguvu zote kupata pointi tatu mbele ya Yanga .
Kuwafahamu wapinzani wako kunakufanya uongeze maarifa ya kuwakabili.
Kocha wa JKT Ruvu, Fredy Felix Minziro anawafahamu wachezaji wote wa Yanga kwasababu alikuwa nao mzunguko wa kwanza.
Iliwafundisha akiwa kocha msaidizi, na kuna wakati aliwafundisha bila uwepo wa kocha mkuu, Ernies Brandts.
Mchezo wa jumapili utakuwa mgumu kwa timu zote mbili. Yatahitajika maarifa makubwa kwa makocha wote wawilli kupata ushindi.
Yanga wataingia wakiwa na kumbukumbu ya kufungwa mabao 2-1 na Mgambo JKT , wakati JKT Ruvu walishinda mechi yao ya mwisho dhidi ya Rhino Rangers kwa mabao 3-1.
Utumwa wa pili wa Pluijm utakuwa  aprili 9 mwaka huu uwanja wa Taifa jijini Dar es salaam dhidi ya Kagera Sugar.
Wakata miwa hawa wa Kaitaba, hawahitaji ubingwa wala nafasi ya pili. Malengo yao ni nafasi ya tatu na nne.
Kama wana malengo hayo, basi wamejipanga na wanaendelea kujipanga ili kufanya vizuri katika michezo yao minne iliyosalia kuanzia wa leo dhidi ya Simba sc.
Bila shaka mechi hii ya Yanga na Kagera itakuwa na upinzani mkubwa kwa timu zote.
Haitakuwa rahisi kwa Pluijm kuchomoka katika mechi hii, lakini akiwa na mipango safi ataweza kuvuna pointi tatu muhimu.
Baada ya mechi hiyo, Yanga sc watasafiri kwenda mkoani Arusha kuwakabili JKT Oljoro aprili 13 mwaka huu kwenye uwanja wa Shk. Amri Kaluta Abeid.
Endapo kwa wakati huo JKT Oljoro watakuwa kwenye nafasi nzuri ya kubakia  ligi kuu, basi itakuwa mechi ngumu kwa Yanga.
Kwakuwa Oljoro mpaka sasa wapo nafasi ya 13 kwa kushuka dimbani mara 23 na kujikusanyia pointi 15 pekee, wanahitaji kujidhatiti kushinda mechi zote tatu walizosalia nazo, japokuwa inaonekana haitawasaidia kubakia.
Oljoro wapo katika hatari zaidi ya kushuka daraja, lakini haimaanisha Yanga watakuwa na kazi rahisi kuibuka na ushindi. Mipango mzuri ya uwanjani itahitajika.
Mechi ya mwisho ya Yanga itakuwa aprili 19 dhidi ya mahasimu wao wakubwa, Simba Sc.
Mechi ya watani haitabiriki kirahisi, bali matokeo yanaamriwa ndani ya dakika 90.
Mechi hizi nne zilizosalia, zimewaweka Yanga katika mazingira ya utumwa zaidi ili kutetea ubingwa wao.
Azam fc wao wamebakiza mechi dhidi ya Ruvu shooting, Mbeya City na JKT Ruvu.
Ruvu Shooting hawapo nafasi ya hatari katika msimamo, lakini wataingia kwa lengo la kulinda heshima na pengine kuhitaji kuwa timu pekee kuanza kuvuruga rekodi ya Azam ya kutofungwa msimu huu.
Timu ya kuharibu rekodi ya Azam fc haijapatikana, na kinachosubiriwa ni klabu hizi tatu zilizobakiza mechi nao.
Kocha wa Azam fc, Joseph Marius Omog anahitaji kujiandaa vyema  kwenda kuvuna pointi tatu kwa Ruvu Shooting kule Mabatini, Mlandizi mkoani Pwani.
Atahitaji kuwa na tahadhari kubwa kama kweli anataka  kutwaa ubingwa.
Pia mechi ya Azam fc na  Mbeya City itakuwa na kimuhemuhe zaidi kwasababu City nao wanauwinda ubingwa msimu huu.
Mpaka sasa City wameshashuka dimbani mara 23 na kujikusanyia pointi 45 pointi moja nyuma ya Yanga.
Katika uwanja wa sokoine, Wagonga nyundo hawa wa Mbeya, hawajawahi kufungwa, hivyo Azam fc watahitaji kujipanga kuvunja rekodi yao.
Mechi ya mwisho kwa Azam fc itakuwa dhidi ya JKT Ruvu ,na  uzito wa mechi hiyo utategemeana na matokeo ya timu zote katika michezo miwili ijayo.
Kama JKT Ruvu watakuwa wamefikia hatua nzuri kabla ya mechi ya mwisho, basi inaweza kuwa msaada kwa Azam fc.
 Lakini kama bado watakuwa kwenye mstari mwekundu wa kushuka daraja, basi itakuwa kibarua kizito zaidi.
Hakika utumwa wa Yanga katika dakika 360 za michezo minne iliyosalia ni mkubwa sana na wanahitaji kufuta pengo la pointi 7 dhidi ya Azam fc.
Hakuna jinsi, Yanga lazima washinde mechi zote zilizosalia, huku wakiomba dua mbaya kwa Azam fc  wapoteze angalau michezo miwili.
Azam fc wametangulia mbele kwa pointi, Yanga ni watumwa wa kusawazisha hali hiyo, hivyo wanatakiwa kuwa na mipango mizito zaidi.

Friday, April 4, 2014

TAARIFA RASMI YA YANGA KUHUSU SAKATA LA OKWI, KASEJA NA CHUJI

Hakuna mchezaji yoyote aliyefukuzwa kwenye timu baada ya kupoteza mchezo dhidi ya Mgambo Shooting mwishoni mwa wiki, taarifa hizo zinasambazwa kwa Propaganda ili kuweza kuvunja umoja uliopo ndani ya timu kwa wachezaji na walimu pia kwa Viongozi na wanachama.Uongozi wa klabu ya Young Africans unasikitishwa na taarifa zinazotolewa na baadhi ya Vyombo Vya Habari tangu siku ya jumatano kwamba wachezaji Juma Kaseja, Kelvin Yondani, Athuman Idd "Chuji" wamefukuzwa kwenye timu na Emmanuel Okwi ameondoka kurejea kwao nchini Uganda ni za uongo mtupu.

Kelvin Yondani hakuungana na wenzake kambini baada ya kuomba kupumzika na kutatua matatizo yake ya kifamilia, Benchi la Ufundi walimpa ruhusa hiyo kwa kuzingatia mchezaji mwenyewe asingeweza kutumika kwa mchezo wa jumapili dhidi ya JKT Ruvu kufuatia kuwa na kadi tatu za njano, ataungana na wenzake mara baada ya tu ya mchezo huuo.

Athumani Idd "Chuji", David Luhende pamoja na kiungo Haruna Niyonzima ni wagonjwa, wanaendelea na matibabu kuhakikisha wanakua fit na kuungana na wachezaji wao mara baada ya mchezo wa siku ya jumapili.

Juma Kaseja yupo kambini pamoja na mlinda mlango Deo Munish "Dida" aliyekua majeruhi kwa takribani wiki tatu kufuatia kupata jeraha katika mkono wakati timu ikijiandaa na mchezo dhidi ya Mtibwa Sugar.

Emmauel Okwi yupo jijini Dar es salaam akiendelea na matibabu kufuatia kutonesha goti katika mchezo dhidi ya Mgambo mwishoni mwa wiki, awali Okwi aliiumia katika mchezo dhidi ya Prisons na kutolewa nje na machela.

Okwi akiongea na katibu mkuu wa Yanga Beno Njovu leo ofisini makao makuu ya Klabu ya Ynaga, amesema anaendelea vizuri na ataaungana na wenzake mara baada ya mchezo wa jumapili, lakini akisikitishwa na habari zilizotolewa juu yake amabazo hazina ukweli wowote.

Kufuatia wachezaji hao kushindwa kuungana na timu siku ya jumanne katika mazoezi ya jioni, kocha mkuu Hans Van der Pluijm alichagua wachezaji 20 ambao wap kambini kujiandaa na mchezo huo:

Magolikipa: Juma Kaseja, Deo Munish "Dida" na Ally Mustafa "Barhez"

Walinzi: Juma Abdul, Mbuyu Twite, Ibrahim Job, Raja Zahir ,Oscar Joshua na Nadir Haroub "Cannavaro" 

Viungo: Frank Domayo, Said Dilunga, Nizar Khalfani , Salum Telela na Hamis Thabit

Washambuliaji: Hussein Javu, Hamisi Kizza, Mrisho Ngasa, Saimon Msuva, Jerson Tegete na Didier Kavumbagu.

Waati huo huo klabu ya Yanga imewasilisha barua ya malalamiko kwa TFF juu ya mchezaji Mohamed Hussein Neto kuchezea timu ya Mgambo JKT pasipokuwa na uhamisho wa kimataifa ITC,  kibali cha kuishi na kufanya kazi nchini, mchezaji huyo ni raia wa Kongo na jina lake halisi ni Noel Melondoo.

 


SIMBA WATUA SALAMA BUKOBA, WAFANYA MAZOEZI YAO YA MWISHO KAITABA LEO BILA KOCHA WAO LOGA!!, KESHO NI PATASHIKA KAGERA SUGAR v SIMBA SC

Baadhi ya Viongozi wa Simba wakiteta jambo kwenye Uwanja wa Kaitaba leo hii jioni, Bila shaka ni swala zima la mtanange wao kesho na Kagera Sugar huku wakijiuliza maswali kadhaa na kuucheki uwanja wa Kaitaba jinsi ulivyo katika kipindi hiki. Kocha wa Simba Zdravko Logarusic hakuwepo kabisa kwenye Mazoezi Hapa Kaitaba na inaoneka hakuja na Wachezaji wake. Taarifa zaidi inasemekana atakuja kesho jumamosi siku ya Mtanange.
Wachezaji wa Simba wakishuka kwenye basi lao kuingia kwenye uwanja wa Kaitaba, Tayari kufanya mazoezi kujiweka fiti na mtanange wa kesho na Wenyeji Kagera Sugar.
Baadhi ya Wachezaji wa Simba wakiingia tayari kwenye nyasi za Kaitaba hapa Bukoba
Safi sana...siku nyingi!!!
Tayari kwa mazoezi....
Wachezaji wa Simba wakiomba dakika chache kabla ya mazoezi yao kwenye Uwanja wa Kaitaba jioniWachezaji wa Simba wakiteta jambo kabla ya mazoezi, Kipa Ivo Mapunda (katikati) akiwacheki kwa karibu.Viongozi wa Simba wakiwacheki vijana wao wakijifua!Kesho tucheka na nyavu tuu....
Simba sc wanaingia katika mchezo wa kesho wakiwa hawana cha kupoteza, kwasababu hawahitaji ubingwa wala nafasi ya pili.

Hata hivyo ushindi ni muhimu kwao ili kulinda heshima yao inayozidi kupotea siku za karibuni.
Wataingia uwanjani wakiwa wamepoteza mechi mbili zilizopita dhidi ya Coastal Union na Azam fc, hivyo kupoteza mechi ya kesho ni kuwatonesha zaidi kidonda mashabiki wao. 
Simba mpaka sasa wapo nafasi ya 4 katika msimamo baada ya kucheza mechi 23 na kujikusanyia pointi 36.
Kagera Sugar wao wanahitaji nafasi ya tatu au nne msimu huu, hivyo kesho wataingia kutafuta pointin tatu muhimu.
Kagera kwasasa wapo nafasi ya 5 wakiwa na pointi 33 baada ya kucheza mechi 22.
Ligi hiyo itandelea tena jumapili (aprili 6) ambapo mechi kali ni baina ya mabingwa watetezi, Yanga dhidi ya JKT Ruvu uwanja wa Taifa.
Umuhimu wa ushindi kwa timu zote mbili ndio sababu ya mchezo huo kuwa na mvuto kwa mashabiki wa soka.Moja ya Kipa wa Simba, Ivo Mapunda mlinda mlango wa zamani wa Yanga na Klabu ya Gor Mahia ya Kenya akiwa kwenye nyasi za Uwanja wa Kaitaba hii leoMakipa wote wa Tatu wa Simba wakijifua!Ivo MapundaIvo Mpunda ajikiuliza kama kesho wanatoka au la!!Nani kesho ataanza langoni mwa Simba?Kipa ni Mchezaji muhimu sana kwenye Klabu yoyote ile, na Hapa Ivo Mapunda na mwenzake wanataka ushindi kwani wao ni wazoefu kwenye swala zima la kulinda milango.Baadhi ya Viongozi wa wekundu wa Msimbazi ya Jijini Dar es SalaamKesho tunataka timu yetu iibuke na pointi tatu muhimu!Kipa mwingine wa Simba
 
 Picha zote na Na Faustine Ruta wa www.bukobasports.com

CHAMPIONS LEAGUE ROBO FAINALI KWENYE NAMBA: MAN UNITED, BAYERN, RONALDO WAWEKA REKODI MPYA KATIKA MICHUANO HIYO• Wachezaji Cristiano Ronaldo na Frank Lampard walitimiza mechi zao 100 za UEFA Champions League appearances katika mechi za kwanza za robo fainali na hivyo kuwa mchezaji wa 20 na 21 kufikia namba ya mechi hizo. Wachezaji pia walianza kucheza katika michuano ya ulaya siku moja,  16 September 2003.


• Lampard amekuwa mchezaji wa 12 kufanikiwa kutimiza mechi 100 akiwa na klabu moja na ndio mchezaji wa kwanza wa Chelsea kutimiza idadi ya mechi hizo.

• Idadi ya mechi 100 za Ronaldo imegawanyika katika sehemu mbili - ameitumikia Manchester United FC (mechi 52 ) na Madrid (48). Yupo karibuni kuweka rekodi ya kuwa mchezaji wa kwanza duniani kucheza 50 katika klabu mbili tofauti. 

• Hakuna mchezaji mwingine atakayeweza kufikisha idadi ya mechi 100 msimu huu katika wachezaji waliobakia kwenye mashindano - zimebakia mechi 4 - Mchezaji Andres Iniesta, John Tery wote wamecheza jumla ya mechi 95. Rio Ferdinand na Xabi Alonso wamecheza mechi 93 na 91. 
• Frank Ribery alitimiza mechi 50 za UEFA Champions League - zote amecheza akiwa na FC Bayern M√ľnchen.
• Mechi ya sare ya Manchester United dhidi ya Bayern imewafanya watimize jumla ya mechi 199 za  UEFA Champions League; mechi ijayo itawafanya watimize mechi 200 katika michuano hiyo. Wao ndio wanaongoza kwa kucheza mechi za UCL - ikiwa Real Madrid watafanikiwa kucheza mpaka fainali basi wataungana na United katika listi ya vilabu vilivyotimiza mechi 200.
• Mechi hiyo iliyofanyika Old Trafford ilikuwa mechi ya 99 ya michuano hiyo kufanyika katika dimba hilo - ni uwanja mmoja tu unaoizidi OT kwa kuchezewa mechi nyingi za UCL - San Siro, ambao unatumiwa na vilabu vya AC milan na  FC Internazionale Milano, uwanja huo umetumika kufanyika mechi zaidi ya (131).
• United na Bayern zote mbili zilitimiza jumla ya mechi 25 za hatua ya robo fainali ya UCL - hii ni rekodi ya mashindano. Barcelona na Real Madrid wote wamecheza mechi 17 za hatua hiyo.

VPL: ASHANTI VS MBEYA CITY, YANGA VS JKT RUVU NI MITANANGE MIZITO ZAIDI WIKIENDI HII, MECHI YA SIMBA, KAGERA HAINA `PRESHA`!!Na Baraka Mpenja, Dar es salaam


LIGI kuu soka Tanzania bara inatarajia kuendelea kesho na keshokutwa, huku mechi kubwa yenye uzito wa hali ya juu ni kati ya Yanga dhidi ya JKT Ruvu na ile ya Ashanti United na Mbeya City.
Kesho jumamosi zitapigwa mechi mbili ambapo wauza mitumba wa Ilala watawakaribisha Mbeya City katika dimba la Azam Complex, Chamazi, nje kidogo ya jiji la Dar es salaam.
Mechi hii itakuwa na mvuto wake kutokana na mazingira ya timu zote mbili katika msimamo wa ligi hiyo.
Mbeya City wapo nafasi ya tatu wakiwa wameshuka dimbani mara 23 na kujikusanyia pointi 45, pointi moja nyuma ya mabingwa watetezi Yanga waliopo nafasi ya pili kwa pointi 46 baada ya kucheza mechi 22.
Kocha Juma Mwambusi ataingia kesho kwa lengo la kutafuta ushindi ili kujiongezea pointi katika harakati zake za kuwania ubingwa wake wa kwanza msimu huu.
Mbeya City ni timu pekee iliyofanya vizuri na kuwashangaza wapenzi wa soka kati ya klabu tatu zilizopanda ligi kuu msimu huu unaoelekea mwishoni.
Wenzao, Ashanti United na Rhino Rangers wapo katika hatari ya kushuka daraja, lakini maafande wa Tabora wanaonekana kwa asilimia kubwa wameshashuka daraja.
Ashanti wameshuka dimbani mara 23 na kujikusanyia pointi 21 katika nafasi ya 12, wakati Rhino Ranger ndio wanaoburuza mkia kwa kuwa na pointi 13 katika nafasi ya 14 baada ya kucheza mechi 23.
Katika mchezo wa kesho, kocha mkuu wa Ashanti United, Abdallah Kibadeni hahitaji matokeo mengine yoyote zaidi ya ushindi kwasababu akipoteza mchezo atazidi kujiweka mazingira magumu zaidi ya kubakia ligi kuu.
Lakini atahitaji kuwa na mipango mizuri zaidi mbele ya Wagonga nyundo, kwasababu umoja walio nao na uwezo wa kikosi chao, wanaweza kuibuka na ushindi.
Kule Kaitaba kutakuwa na mchezo mmoja kesho jumamosi ambapo wenyeji Kagera Sugar watakuwa wanachuana na Simba sc ya jijini Dar es salaam.
Simba sc wanaingia katika mchezo wa kesho wakiwa hawana cha kupoteza, kwasababu hawahitaji ubingwa wala nafasi ya pili.
Hata hivyo ushindi ni muhimu kwao ili kulinda heshima yao inayozidi kupotea siku za karibuni.
Wataingia uwanjani wakiwa wamepoteza mechi mbili zilizopita dhidi ya Coastal Union na Azam fc, hivyo kupoteza mechi ya kesho ni kuwatonesha zaidi kidonda mashabiki wao.
Simba mpaka sasa wapo nafasi ya 4 katika msimamo baada ya kucheza mechi 23 na kujikusanyia pointi 36.
Kagera Sugar wao wanahitaji nafasi ya tatu au nne msimu huu, hivyo kesho wataingia kutafuta pointin tatu  muhimu.
Kagera kwasasa wapo nafasi ya 5 wakiwa na pointi 33 baada ya kucheza mechi 22.
Ligi hiyo itandelea tena jumapili  (aprili 6) ambapo mechi kali ni baina ya mabingwa watetezi, Yanga  dhidi ya JKT Ruvu uwanja wa Taifa.
Umuhimu wa ushindi kwa timu zote mbili ndio sababu ya mchezo huo kuwa na mvuto kwa mashabiki wa soka.
Yanga wanahitaji matokeo kwa njia zote ili kupunguza pengo la pointi na vinara Azam fc wenye pointi 53 kileleni.
Wanajangwani hao wameshuka dimbani mara 22 na kujikusanyia pointi 46 katika nafasi ya pili, na nyuma yao wapo Mbeya City wenye pointi 45.
Yanga wanahitaji kutetea ubingwa wao walioweka rehani mbele ya Azam fc, hivyo kushinda kesho ni muhimu zaidi kwasababu mechi iliyopita walifungwa mabao 2-1 na Mgambo JKT Kule Tanga.
Nao JKT Ruvu chini ya kocha mkuu Fredy Ferlix Minziro wanahitaji pointi tatu muhimu ili kuendelea kujiimarisha katika mazingira mazuri ya kubakia ligi kuu.
Kwasasa wapo nafasi ya 9 kwa pointi 28 baada ya kucheza mechi 23, hivyo ushindi katika mechi hiyo utakuwa na maana kubwa kwao.
Matokeo yamekuwa magumu kuyatabiri kwa sasa, timu yoyote inaweza kushinda bila kujali ubora na majina ya wachezaji kutofautiana.
Mechi nyingine za jumapili ni kati ya Coastal Union dhidi ya Mgambo uwanja wa Mkwakwani jijini Tanga.
Vibonde JKT Oljoro watakuwa na kibarua muhimu na maafande wa jeshi la Magereza kutoka jijini Mbeya, Tanzania Prisons `Wajelajela` katika dimba la Shk. Amri Kaluta Abeid jijini Arusha.
Rhino Ranger waliopoteza matumaini ya kubakia ligi kuu watawakaribisha, Mtibwa Sugar kutoka Marogoro kwenye uwanja wa Ali Hassan Mwinyi mjini Tabora.
Mechi ya Ruvu Shooting na Azam iliyotakiwa kupigwa jumapili imesogezwa mbele mpaka aprili 9 mwaka huu kwasababu wachezaji wengi wa Azam fc wameondoka na kikosi cha timu ya Taifa ya vijana chini ya miaka 20, Ngorongoro Heroes.