Search This Blog

Friday, April 4, 2014

VPL: ASHANTI VS MBEYA CITY, YANGA VS JKT RUVU NI MITANANGE MIZITO ZAIDI WIKIENDI HII, MECHI YA SIMBA, KAGERA HAINA `PRESHA`!!Na Baraka Mpenja, Dar es salaam


LIGI kuu soka Tanzania bara inatarajia kuendelea kesho na keshokutwa, huku mechi kubwa yenye uzito wa hali ya juu ni kati ya Yanga dhidi ya JKT Ruvu na ile ya Ashanti United na Mbeya City.
Kesho jumamosi zitapigwa mechi mbili ambapo wauza mitumba wa Ilala watawakaribisha Mbeya City katika dimba la Azam Complex, Chamazi, nje kidogo ya jiji la Dar es salaam.
Mechi hii itakuwa na mvuto wake kutokana na mazingira ya timu zote mbili katika msimamo wa ligi hiyo.
Mbeya City wapo nafasi ya tatu wakiwa wameshuka dimbani mara 23 na kujikusanyia pointi 45, pointi moja nyuma ya mabingwa watetezi Yanga waliopo nafasi ya pili kwa pointi 46 baada ya kucheza mechi 22.
Kocha Juma Mwambusi ataingia kesho kwa lengo la kutafuta ushindi ili kujiongezea pointi katika harakati zake za kuwania ubingwa wake wa kwanza msimu huu.
Mbeya City ni timu pekee iliyofanya vizuri na kuwashangaza wapenzi wa soka kati ya klabu tatu zilizopanda ligi kuu msimu huu unaoelekea mwishoni.
Wenzao, Ashanti United na Rhino Rangers wapo katika hatari ya kushuka daraja, lakini maafande wa Tabora wanaonekana kwa asilimia kubwa wameshashuka daraja.
Ashanti wameshuka dimbani mara 23 na kujikusanyia pointi 21 katika nafasi ya 12, wakati Rhino Ranger ndio wanaoburuza mkia kwa kuwa na pointi 13 katika nafasi ya 14 baada ya kucheza mechi 23.
Katika mchezo wa kesho, kocha mkuu wa Ashanti United, Abdallah Kibadeni hahitaji matokeo mengine yoyote zaidi ya ushindi kwasababu akipoteza mchezo atazidi kujiweka mazingira magumu zaidi ya kubakia ligi kuu.
Lakini atahitaji kuwa na mipango mizuri zaidi mbele ya Wagonga nyundo, kwasababu umoja walio nao na uwezo wa kikosi chao, wanaweza kuibuka na ushindi.
Kule Kaitaba kutakuwa na mchezo mmoja kesho jumamosi ambapo wenyeji Kagera Sugar watakuwa wanachuana na Simba sc ya jijini Dar es salaam.
Simba sc wanaingia katika mchezo wa kesho wakiwa hawana cha kupoteza, kwasababu hawahitaji ubingwa wala nafasi ya pili.
Hata hivyo ushindi ni muhimu kwao ili kulinda heshima yao inayozidi kupotea siku za karibuni.
Wataingia uwanjani wakiwa wamepoteza mechi mbili zilizopita dhidi ya Coastal Union na Azam fc, hivyo kupoteza mechi ya kesho ni kuwatonesha zaidi kidonda mashabiki wao.
Simba mpaka sasa wapo nafasi ya 4 katika msimamo baada ya kucheza mechi 23 na kujikusanyia pointi 36.
Kagera Sugar wao wanahitaji nafasi ya tatu au nne msimu huu, hivyo kesho wataingia kutafuta pointin tatu  muhimu.
Kagera kwasasa wapo nafasi ya 5 wakiwa na pointi 33 baada ya kucheza mechi 22.
Ligi hiyo itandelea tena jumapili  (aprili 6) ambapo mechi kali ni baina ya mabingwa watetezi, Yanga  dhidi ya JKT Ruvu uwanja wa Taifa.
Umuhimu wa ushindi kwa timu zote mbili ndio sababu ya mchezo huo kuwa na mvuto kwa mashabiki wa soka.
Yanga wanahitaji matokeo kwa njia zote ili kupunguza pengo la pointi na vinara Azam fc wenye pointi 53 kileleni.
Wanajangwani hao wameshuka dimbani mara 22 na kujikusanyia pointi 46 katika nafasi ya pili, na nyuma yao wapo Mbeya City wenye pointi 45.
Yanga wanahitaji kutetea ubingwa wao walioweka rehani mbele ya Azam fc, hivyo kushinda kesho ni muhimu zaidi kwasababu mechi iliyopita walifungwa mabao 2-1 na Mgambo JKT Kule Tanga.
Nao JKT Ruvu chini ya kocha mkuu Fredy Ferlix Minziro wanahitaji pointi tatu muhimu ili kuendelea kujiimarisha katika mazingira mazuri ya kubakia ligi kuu.
Kwasasa wapo nafasi ya 9 kwa pointi 28 baada ya kucheza mechi 23, hivyo ushindi katika mechi hiyo utakuwa na maana kubwa kwao.
Matokeo yamekuwa magumu kuyatabiri kwa sasa, timu yoyote inaweza kushinda bila kujali ubora na majina ya wachezaji kutofautiana.
Mechi nyingine za jumapili ni kati ya Coastal Union dhidi ya Mgambo uwanja wa Mkwakwani jijini Tanga.
Vibonde JKT Oljoro watakuwa na kibarua muhimu na maafande wa jeshi la Magereza kutoka jijini Mbeya, Tanzania Prisons `Wajelajela` katika dimba la Shk. Amri Kaluta Abeid jijini Arusha.
Rhino Ranger waliopoteza matumaini ya kubakia ligi kuu watawakaribisha, Mtibwa Sugar kutoka Marogoro kwenye uwanja wa Ali Hassan Mwinyi mjini Tabora.
Mechi ya Ruvu Shooting na Azam iliyotakiwa kupigwa jumapili imesogezwa mbele mpaka aprili 9 mwaka huu kwasababu wachezaji wengi wa Azam fc wameondoka na kikosi cha timu ya Taifa ya vijana chini ya miaka 20, Ngorongoro Heroes.

No comments:

Post a Comment