Search This Blog

Saturday, April 12, 2014

YANGA KUFA KUPONA KESHO ARUSHA, AZAM FC KUTWAA UBINGWA UWANJA WA SOKOINE?
Na Baraka Mpenja, Dar Es Salaam


Mabingwa watetezi wa ligi kuu soka Tanzania bara, Dar Young Africans kesho katika dimba la Shk. Amri Abeid jijini Arusha watakuwa na kibarua cha kusaka pointi tatu muhimu dhidi ya wenyeji wao, Maafande wa JKT Oljoro.

Hii itakuwa mechi muhimu kwa Yanga na wanahitaji ushindi tu na si matokeo mengine ili kujipa matumaini ya kutetea ubingwa wao msimu hii mbele ya washindani wao Azam fc.

Azam fc kwa muda mrefu wanawanyima usingizi Yanga kwasababu wamekalia kiti cha usukani na wanahitaji pointi 3 tu katika michezo yao miwili iliyosalia ili kuwavua rasmi ubingwa Yanga SC.

Wana Lambalamba mpaka sasa wamejikusanyia  pointi 56 kileleni, huku Yanga wakikalia nafasi ya pili kwa pointi 52, huku timu zote zikibakiza mechi mbili.

Wakati Yanga wakihenyeka Arusha, Azam fc wao watakuwa na kibarua kizito dhidi ya Wagonga nyundo wa Mbeya, klabu ya Mbeya City katika dimba la Sokoine.

Mechi ya Azam fc na Mbeya City pamoja na Yanga dhidi ya JKT Oljoro zimekuwa gumzo na kuvuta hisia za mashabiki wa soka kutokana na uhitaji mkubwa wa ushindi.

Yanga kwa upande wao wamesema wamejiandaa vizuri kuibuka na ushindi hapo kesho, na leo hii asabuhi wamefanya mazoezi katika dimba la Shk. Amri Abeid , uwanja ambao utatumika katika mechi ya kesho.

Kocha mkuu wa Yanga , Mholanzi Hans Van Der Pluijm amesema wachezaji wake wote 23 waliopo jijini Arusha wapo salama na wanaendelea kuwapa maelekezo ya mwisho tayari kwa kusaka ushindi.

Wachezaji waliosafiri na timu kwenda Arusha ni Walinda mlango, Deogratias Munish "Dida" na Ally Mustafa "Barthez"

Walinzi ni Juma Abdul, Mbuyu Twite, Oscar Joshua, Amos Abel, Rajab Zahir, Ibrahim Job, Kelvin Yondani na Nadir Haroub "Cannavaro".

Viungo ni Hamis Thabit, Nizar Khalfani, Frank Domayo, Hassan Dilunga, Salum Telela na Sospter Maiga

Washambuliaji ni Didier Kavumbagu, Hamis Kizza, Jerson Tegete, Mrisho Ngasa, Saimon Msuva, Said Bahanuzi na Hussein Javu

Mechi nyingine ya kesho ni baina ya Simba sc dhidi ya Ashanti United katika dimba la Taifa jijini Dar es salaam kuanzia majira ya saa 10:00 jioni. 

Mtibwa Sugar itacheza na Ruvu Shooting (Uwanja wa Manungu, Morogoro), huku Mgambo Shooting na Kagera Sugar zitaoneshana kazi kwenye Uwanja wa Mkwakwani jijini Tanga .

`BAI BAI` RHINO LIGI KUU, YAPIGWA 4-3 NA PRISONS, RASMI MINZIRO AIOKOA JKT RUVU KUSHUKA DARAJA, YAITANDIKA 1-0 COASTAL MKWAKWANI!

Maafande wa Rhino Rangers kutoka Tabora


Na Baraka Mpenja, Dar es salaam


RASMI Maafande wa jeshi la wananchi Tanzania (JWTZ), Rhino Rangers kutoka mkoani Tabora wamejihakikishia kushuka daraja msimu huu wa ligi kuu soka Tanzania bara.

Hii inatokana na kupokea kipigo cha mabao 4-3 kutoka kwa maafande wa Tanzania Prisons kwenye uwanja wa Sokoine jijini Mbeya jioni hii.

Matokeo haya yanawafanya Rhino waendelee kuwa mkiani kwa pointi 16 tu baada ya kucheza mechi 25. Hata  kama watashinda mchezo wa mwisho haina maana kwao.

Mchezo wa leo  ulikuwa mgumu zaidi kwa Prisons kwasababu walikuwa wanasaka pointi tatu ili angalau kujinusuru kushuka daraja.

Kwa upande wa Rhino walishakata tamaa siku nyingi, lakini leo hii walikuwa wanajidhatiti angalau kushinda mechi mbili walizosaliwa nazo.

Baada ya kupoteza mechi hii, rasmi jahazi la Rhino limeshazama  na kinachofuata ni kujiandaa kukamilisha ratiba na kuungana na timu za daraja la kwanza ili maisha mengine yaendelee.

Katibu mkuu wa Tanzania Prisons, Insepekta Sadick Jumbe ameueleza mtandao huu kuwa mchezo wa leo ulikuwa mgumu kwao, lakini vijana waliingia kwa nguvu zote kuhakikisha wanaibuka na pointi tatu.

“Unajua huu ulikuwa mchezo wa kuwashusha rasmi Rhino, walipambana na kuufanya mchezo uwe na mvutoi”.

“Lakini wasingekwepa kipigo kwasababu hatukuwa na sababu ya kupoteza mechi ya tatu mfululizo wakati tunajua tuko katika wakati mgumu”. Alisema Jumbe.

Katibu huyo aliongeza kuwa baada ya mechi ya leo wanasubiri matokeo ya mechi ya kesho baina ya wekundu wa Msimbazi Simba na Ashanti United katika dimba la Taifa jijini Dar es salaam.

“Kama Ashanti United watafungwa mechi ya kesho, basi tukikutana Morogoro aprili 19 watalazimika kutufanga mabao 10 kama wanataka kubaki ligi kuu”.

 Imani yetu ni kubwa na tunawaambia mashabiki wetu kuwa wasiwe na wasiwasi”. Aliongeza Jumbe.

Kwa matokeo hayo, Prisons wamefikisha pointi 25 kwa kucheza mechi 25 na kupanda nafasi ya 10 , huku wakiwashusha Mgambo JKT waliokuwa nafasi hiyo kwa pointi 25.

Mgambo wanashuka mpaka nafasi ya 11 wakiwa na pointi 25 kama Prisons, lakini wastani wa mabao ya kufunga na kufungwa unawafanya maafande hawa wa Tanga kuwa chini ya Wajelajela.

Mechi nyingine imechezwa katika dimba CCM Mkwakwani jijini Tanga ambapo Coastal Union waliwakaribisha maafande wa JKT Ruvu.

Mechi hiyo imemalizika kwa JKT Ruvu ya kocha Fredy Felix Minziro kuibuka na ushindi wa bao 1-0.

Kwa matokeo hayo, JKT Ruvu wamefikisha pointi 31 na kupanda nafasi mbili kutoka ya 9 waliyokuwepo kabla ya mechi ya leo mpaka nafasi ya 7.

JKT Ruvu wamewashuka Mtibwa Sugar waliokuwa nafasi ya 7 mpaka ya 8 kwa pointi zao 30, huku Coastal Union wao wakiendelea kukalia nafasi ya 9 kwa pointi 29.

Mpaka hapo Minziro amefanikisha malengo yake kwasababu alipatiwa timu kwa matarajio ya kuinusuru isishuke daraja msimu huu.

Baada ya mechi hiyo, Kocha Minziro amefurahishwa na matokeo hayo huku akiwapongeza vijana wake kwa kupambana na kupata bao moja muhimu.

“Mechi ilikuwa ngumu, lakini nawashukuru sana wachezaji wangu kwa kujituma”.

“ Malengo yangu ilikuwa ni kuinusuru timu isishuke daraja. Nadhani sasa nimefanikiwa na nitajipanga kwa msimu ujao”. Alisema Minziro.

Kwa upande wa Coastal Union, afisa habari wa klabu hiyo, Hafidh Kido amesema kuwa timu yao imecheza vibaya na kupoteza mchezo, lakini ndio matokeo ya soka.

“Hakika vijana wametuangusha leo.Wamecheza chini ya kiwango”.

“ Yote kwa yote JKT Ruvu walikuwa  katika nafasi ya hatari na ndio maana walichezwa kwa nguvu na kutufunga. Tunajiandaa kwa mechi ya mwisho dhidi ya Kagera Sugar hapa Mkwakwani”. Alisema Kido.

AZAM FC YAKWEA PIPA KUWAFUATA WAGONGA NYUNDO WA MBEYA!!KIKOSI cha vinara wa ligi kuu soka Tanzania bara, Azam FC, kinaondoka asubuhi ya leo Dar es Salaam kwa ndege kwenda jijini Mbeya kwa ajili ya mechi ya Ligi Kuu sokaTanzania Bara dhidi ya wenyeji Mbeya City  kwenye Uwanja wa Sokoine mjini humo.

Azam fc wanakwenda Mbeya kuhitaji pointi tatu ambazo zitawapa ubingwa  rasmi na kuwavua mabingwa watetezi, Dar Young Africans.

Kocha Mcameroon wa Azam FC, Joseph Marius Omog alikuwa mwenye furaha baada ya ushindi wa 3-0 juzi Uwanja wa Mabatini, Mlandizi mkoani Pwani dhidi ya wenyeji Ruvu Shooting, lakini akasema shughuli haijaisha. 

“Ni furaha. Ni ushindi mzuri, tumevuka kikwazo kimoja, vijana waliuanza mchezo vizuri wakizingatia nilichowaambia. Karibu kila mmoja alitekeleza majukumu yake vizuri. Wapinzani walikuwa wagumu, lakini tumechukua pointi tatu,”alisema.

Omog alisema anajivunia wachezaji wake na hana cha kuwaambia zaidi ya asante pamoja kama timu na akawataka kuendeleza mshikamano huo daima.
 Hata hivyo, Omog amewaambia wachezaji wake kwamba wanahitaji kushinda pia mechi mbili za mwisho ili wamalize ligi vizuri.

Ushindi huo umeifanya Azam FC ifikishe pointi 56 baada ya kucheza mechi 24 na kujivuta karibu kabisa na chumba kinachohifadhi Kombe la ubingwa wa Ligi Kuu, ikiwaacha kwa pointi nne mabingwa watetezi, Yanga SC wenye pointi 52 za mechi 24 pia.

Timu hiyo ya Alhaj Sheikh Said Salim Awadh Bakhresa na familia yake, baada ya mechi ya kesho itacheza mechi ya mwisho dhidi ya JKT Ruvu Aprili 19, Uwanja wake wa Azam Complex, Chamazi, Dar es Salaam.

CHANZO: TOVUTI YA AZAM

UFALME WA RAGE SIMBA WAFIKA KIKOMO, SWALI NANI KURITHI MIKOBA YAKE?, KAZI KWA WANACHAMA!!
Na Baraka Mpenja , Dar es salaam

0712461976

KWA MUDA mrefu mashabiki  na wanachama wa Simba sc wamekuwa wakiamini kuwa klabu yao imefika hapo ilipo kwasababu ya mwenyekiti wao Ismail Aden Rage kuongoza vibaya.
Rage amekuwa akisuguana na wanachama wake kwa muda mrefu, lakini sasa ameshatangaza kutogombea tena nafasi hiyo katika uchaguzi Mkuu unaotarajia kufanyika mei 4 mwaka huu.
Rage alitangaza maamuzi hayo machi 16 mwaka huu katika mkutano mkuu wa wanachama  ulioitishwa maalumu kwa ajili ya kufanya marekebisho wa katiba.
Kauli ya aina yake katika mkutano huo ilikuwa ile ya Rage kuwaita wanachama wa Simba ni  ‘mbumbumbu’
Kufuatia kauli hiyo, Rage, alilazimika kuwaomba radhi wanachama hao zaidi ya 571 waliohudhuria mkutano huyo uliofanyika kwenye Ukumbi wa Bwalo la Polisi, Oysterbay jijini Dar es Salaam.
“Napenda kuwaomba radhi wanachama wenzangu kutokana na nilivyosema tuache umbumbumbu, lakini sikuwa namaanisha kama wengi wenu mlivyoelewa,” alisema Rage.
Licha ya kusema hatagombea tena uongozi, Rage, alisema ataendelea kuwa mwanachama mwaminifu wa Simba na atatoa mchango wake ili kufanikisha maendeleo.
Ikumbukwe kuwa kabla ya kauli hiyo, Rage alishawahi kusema kauli za aina yake.
Mwezi machi mwaka jana aliwahi kuuita  mkutano wa wanachama walioaminika kuwa zaidi ya 600 ambao ulitangaza kumpindua madarakani  kuwa ni kama `kikao cha harusi`.
Pia novemba mwaka jana kamati ya utendaji ya Simba ilitangaza kumuondoa madarakani mwenyekiti wake, Ismail Aden Rage.
Kamati hiyo ilifikia uamuzi wa kumsimamisha Rage akiwa nje ya nchi  na kumtangaza aliyekuwa Kaimu Makamu Mwenyekiti, Joseph Itang’are ‘Mzee Kinesi’ kushika nafasi hiyo ya juu zaidi katika klabu hiyo.
Mzee Kinesi alisema walifikia maamuzi hayo kutokana na mwenyekiti huyo kwenda kinyume na makubaliano na Kamati ya Utendaji ya Simba.
Lakini baadaye ya mwanaume huyo kurudi alitamba kuwa yeye ni mwenyekiti halali wa Simba na kikao hicho kilikuwa kikao cha harusi.
Wakati anawasili uwanja wa ndege wa kimataifa wa Mwalimu Nyerere kulikuwa na kundi kubwa la watu walioaminika kuwa wanachama wa Simba waliojitokeza kumlaki na kumshangilia kwa nguvu.
Kweli jamaa alirudi na baadaye TFF walitangaza kumtambua kuwa ndiye mwenyeki halali wa Simba, lakini wakamtaka aitishe mkutano wa dharura na kumpangia ajenda.
Rage aligoma na kusema yeye ndiye mwenye mamlaka ya kupanga ajenda za mkutano kwa mujibu wa katiba.
Yapo mengi ya kuyasema kuhusu Rage, lakini sasa ameshatangaza kung`atuka baada ya muda mrefu wa mvutano na viongozi wenzake pamoja na wanachama wa Simba.
 Baadhi ya wananachama wa Simba wanafikiria kuwa Rage ndiye mchawi wa klabu yao, hivyo kuondoka kwake ni jambo la heri.
Tarehe ya uchaguzi ilishatangazwa na tayari kamati ya uchaguzi ilishaundwa chini ya mwenyekiti wake, Dr. Damas Ndumabro ambaye ni mwanasheria kitaaluma.
Hata hivyo, Kamati ya uchaguzi ya klabu ya Simba imetangaza kuwa mchakato wa uchaguzi wa klabu hiyo utaweza kuendelea baada ya msajili wa vyama vya michezo kuipitisha rasimu ya katiba ya Simba iliyopelekwa hivi karibuni.

Mwenyekiti wa kamati hiyo Damas Ndumbaro alisema jana kuwa kamati yake ilikaa Alhamisi wiki hii na kujadili masuala mbalimbali kuhusiana na mchakato wa uchaguzi ambao awali ulipangwa kufanyika mapema mwezi ujao.

Mwenyekiti wa kamati ya uchaguzi ya Simba Damas Ndumbaro amewataka
wanachama wa klabu ya Simba kuvuta subira hadi hapo msajili wa vyama
vya michezo atakaposaini rasimu ya katiba ndipo watakapo tangaza kuanza rasmi kwa harakati za kuwania nafasi mbalimbali ndani ya klabu
hiyo.
Haya sasa mambo yameshaiva ingawa bado rasimu ya katiba ikisubiriwa kusajiliwa.
Lakini cha msingi wakati unaoamini kuwa wa ufalme wa Rage kuiongoza Simba unaelekea ukingoni.
Wanachama wa Simba ndio wenye mamlaka kikatiba ya kuchagua kiongozi wao mkuu.
Ni wanachama hawa hawa waliomchagua Rage kwa kura nyingi, lakini walimkana baadaye na kuona hana maana kwa klabu.
Sasa swali la msingi kwa wanachama wa Simba, Rage anaondoka, nani wanadhani atakuwa mbadala wake?.
Nadhani wapo wengi watakaojitokeza kugombea nafasi ya mwenyekiti pamoja na wajumbe wa kamati ya utendaji.
Kuna watu wataomba kwa lengo la kuleta mabadiliko na kuifufua Simba ya miaka ya nyuma, lakini hata wachumia matumbo watakuwepo tu.
Unajua kila mtu anataka kazi fulani kwa sababu zake.
Simba ni chama kubwa, pesa zipo na ukitaka kula utakula sana kwasababu kumekosekana watu makini wa kufuatilia mahesabau ya klabu yao.
Si Simba tu, hata klabu nyingine kama Yanga kuna matatizo kama haya.
Wapo watu wanaoneemeka kuwepo katika klabu hizi na wanajulikana.
Walikuwa wa kawaida, lakini kupitia nafasi za uongozi wazipatazo, wanazidi kuwa watu maarufu kwa mkwanja.
Ukichunguza vyonza vya pesa zao utagundua ni pesa za mpira wazivunazo katika  klabu wanazozitawala.
Niliwahi kuongea na kiongozi mmoja wa chama cha juu cha soka, alinipa siri kuwa hakuna pesa nyepesi na za bure kama kwenye mpira.
Mazungumzo yetu yalikuwa ya kawaida tu na alisema kamwe nisiseme. Ni miaka mingi imepita na sasa si kiongozi tena.
Kama mtu anaingia kwa maslahi binafsi basi hana maana yoyote kwa Simba.
Ikumbukwe kuwa viongozi wetu wanakuwa na mtandao mkubwa sana.
Anapotoka huyu anataka amrithishe mtu ambaye wana mahusiano ya karibu ili waendele kuvuna mapato yasiyo halali.
Ni wakati wa wanachama wa Simba kuwapima watu watakaoomba kugombea nafasi za juu katika klabu hiyo.
Najua ni ngumu kuwajua kwa macho, lakini angalau wawatafiti wanaotarajia kuomba.
Ndani ya klabu yao, wapo walioonesha nia ingawa kwasasa hatuwezi kuwataja kwasababu mchakato bado.
Lakini wanajulikana na wanachama wanawajua vizuri tu. Na bahati nzuri walishaanza kuwapigia debe chini kwa chini.
Nawatahadhirisha Simba kutochagua kwa hasira za muda mrefu walizokuwa nazo juu ya Rage.
Najua lipo kundi kubwa lisilomuunga mkono Rage, hivyo kuondoka kwake kunawapa raha.
Lakini wasije wakachagua mtu kwa kufikiria raha ya kuondoka kwa Rage.
Kinachotakiwa ni kupima uwezo wa watu wanaoweza kuwafikisha mbali.
Najua Simba ina uchu wa mafanikio makubwa wakianza na kurejesha hadhi yao iliyopotea kuanzia uongozi na mambo ya uwanjani.
Wanahitaji mtu mwenye malengo makubwa, nia ya dhati ya kuikoa klabu hii hapa ilipo.
Watu wa aina ni wachache sana, hivyo lazima wanachama watumie muda wao kuwapima watu wanaotarajia kuomba nafasi ili mwisho wa siku wajue nani anafaa.
Wakati wa mabadiliko ndio huu, nafasi ya kubadii timu umefika.
Nafasi ndio hii, kama watakosea kufanya hivyo, watasubiri mpaka wakati mwingine uchaguzi utakapofika.
La sivyo wataendelea na sinema zao za kumpindua kiongozi, lakini mwisho wa siku wanaonekana hawana maana na vikao vyao kuitwa vikao vya harusi.
Ili kuirudisha Simba kwenye hadhi yake, wanachama fikirieni mara mbilimbili ili kupata watu sahihi.
Kwa msimu wa pili sasa, Simba sc inakosa mashindano ya kimataifa, kwasababu msimu huu wataishia nafasi ya nne au ya tano kama wakikosea hesabu zao  katika mechi mbili za mwisho.
Msimu huu wamevuna matokeo mabaya mno, na tatizo linaloonekana ni kwenye uongozi ambao kuna maamuzi ya msingi huamuriwa bila kuona mbali.
Pia kuna lawama za uongozi wa Rage kutowalipa wachezaji maslahi yao. Makocha nao hufukuzwa mara kwa mara.
Sasa mwisho wa haya ni mei 4, lakini wakikosea tu, majanga kama kawaida yataendelea.
Kila la kheri wanachama wa Simba sc katika harakati zenu za kuleta mapinduzi klabuni kwenu.