Maafande wa Rhino Rangers kutoka Tabora |
Na Baraka Mpenja, Dar es salaam
RASMI Maafande wa jeshi la wananchi Tanzania
(JWTZ), Rhino Rangers kutoka mkoani Tabora wamejihakikishia kushuka daraja
msimu huu wa ligi kuu soka Tanzania bara.
Hii inatokana na kupokea kipigo cha mabao 4-3
kutoka kwa maafande wa Tanzania Prisons kwenye uwanja wa Sokoine jijini Mbeya
jioni hii.
Matokeo haya yanawafanya Rhino waendelee kuwa
mkiani kwa pointi 16 tu baada ya kucheza mechi 25. Hata kama watashinda mchezo wa mwisho haina maana
kwao.
Mchezo wa leo ulikuwa mgumu zaidi kwa Prisons kwasababu
walikuwa wanasaka pointi tatu ili angalau kujinusuru kushuka daraja.
Kwa upande wa Rhino walishakata tamaa siku nyingi,
lakini leo hii walikuwa wanajidhatiti angalau kushinda mechi mbili walizosaliwa
nazo.
Baada ya kupoteza mechi hii, rasmi jahazi la Rhino
limeshazama na kinachofuata ni kujiandaa
kukamilisha ratiba na kuungana na timu za daraja la kwanza ili maisha mengine
yaendelee.
Katibu mkuu wa Tanzania Prisons, Insepekta Sadick
Jumbe ameueleza mtandao huu kuwa mchezo wa leo ulikuwa mgumu kwao, lakini
vijana waliingia kwa nguvu zote kuhakikisha wanaibuka na pointi tatu.
“Unajua huu ulikuwa mchezo wa kuwashusha rasmi
Rhino, walipambana na kuufanya mchezo uwe na mvutoi”.
“Lakini wasingekwepa kipigo kwasababu hatukuwa na
sababu ya kupoteza mechi ya tatu mfululizo wakati tunajua tuko katika wakati
mgumu”. Alisema Jumbe.
Katibu huyo aliongeza kuwa baada ya mechi ya leo
wanasubiri matokeo ya mechi ya kesho baina ya wekundu wa Msimbazi Simba na
Ashanti United katika dimba la Taifa jijini Dar es salaam.
“Kama Ashanti United watafungwa mechi ya kesho,
basi tukikutana Morogoro aprili 19 watalazimika kutufanga mabao 10 kama
wanataka kubaki ligi kuu”.
Imani yetu
ni kubwa na tunawaambia mashabiki wetu kuwa wasiwe na wasiwasi”. Aliongeza
Jumbe.
Kwa matokeo hayo, Prisons wamefikisha pointi 25 kwa
kucheza mechi 25 na kupanda nafasi ya 10 , huku wakiwashusha Mgambo JKT
waliokuwa nafasi hiyo kwa pointi 25.
Mgambo wanashuka mpaka nafasi ya 11 wakiwa na
pointi 25 kama Prisons, lakini wastani wa mabao ya kufunga na kufungwa
unawafanya maafande hawa wa Tanga kuwa chini ya Wajelajela.
Mechi nyingine imechezwa katika dimba CCM
Mkwakwani jijini Tanga ambapo Coastal Union waliwakaribisha maafande wa JKT
Ruvu.
Mechi hiyo imemalizika kwa JKT Ruvu ya kocha Fredy
Felix Minziro kuibuka na ushindi wa bao 1-0.
Kwa matokeo hayo, JKT Ruvu wamefikisha pointi 31 na
kupanda nafasi mbili kutoka ya 9 waliyokuwepo kabla ya mechi ya leo mpaka
nafasi ya 7.
JKT Ruvu wamewashuka Mtibwa Sugar waliokuwa nafasi
ya 7 mpaka ya 8 kwa pointi zao 30, huku Coastal Union wao wakiendelea kukalia
nafasi ya 9 kwa pointi 29.
Mpaka hapo Minziro amefanikisha malengo yake
kwasababu alipatiwa timu kwa matarajio ya kuinusuru isishuke daraja msimu huu.
Baada ya mechi hiyo, Kocha Minziro amefurahishwa
na matokeo hayo huku akiwapongeza vijana wake kwa kupambana na kupata bao moja
muhimu.
“Mechi ilikuwa ngumu, lakini nawashukuru sana
wachezaji wangu kwa kujituma”.
“ Malengo yangu ilikuwa ni kuinusuru timu isishuke
daraja. Nadhani sasa nimefanikiwa na nitajipanga kwa msimu ujao”. Alisema
Minziro.
Kwa upande wa Coastal Union, afisa habari wa klabu
hiyo, Hafidh Kido amesema kuwa timu yao imecheza vibaya na kupoteza mchezo,
lakini ndio matokeo ya soka.
“Hakika vijana wametuangusha leo.Wamecheza chini
ya kiwango”.
“ Yote kwa yote JKT Ruvu walikuwa katika nafasi ya hatari na ndio maana walichezwa
kwa nguvu na kutufunga. Tunajiandaa kwa mechi ya mwisho dhidi ya Kagera Sugar
hapa Mkwakwani”. Alisema Kido.
No comments:
Post a Comment