Search This Blog

Saturday, April 12, 2014

YANGA KUFA KUPONA KESHO ARUSHA, AZAM FC KUTWAA UBINGWA UWANJA WA SOKOINE?




Na Baraka Mpenja, Dar Es Salaam


Mabingwa watetezi wa ligi kuu soka Tanzania bara, Dar Young Africans kesho katika dimba la Shk. Amri Abeid jijini Arusha watakuwa na kibarua cha kusaka pointi tatu muhimu dhidi ya wenyeji wao, Maafande wa JKT Oljoro.

Hii itakuwa mechi muhimu kwa Yanga na wanahitaji ushindi tu na si matokeo mengine ili kujipa matumaini ya kutetea ubingwa wao msimu hii mbele ya washindani wao Azam fc.

Azam fc kwa muda mrefu wanawanyima usingizi Yanga kwasababu wamekalia kiti cha usukani na wanahitaji pointi 3 tu katika michezo yao miwili iliyosalia ili kuwavua rasmi ubingwa Yanga SC.

Wana Lambalamba mpaka sasa wamejikusanyia  pointi 56 kileleni, huku Yanga wakikalia nafasi ya pili kwa pointi 52, huku timu zote zikibakiza mechi mbili.

Wakati Yanga wakihenyeka Arusha, Azam fc wao watakuwa na kibarua kizito dhidi ya Wagonga nyundo wa Mbeya, klabu ya Mbeya City katika dimba la Sokoine.

Mechi ya Azam fc na Mbeya City pamoja na Yanga dhidi ya JKT Oljoro zimekuwa gumzo na kuvuta hisia za mashabiki wa soka kutokana na uhitaji mkubwa wa ushindi.

Yanga kwa upande wao wamesema wamejiandaa vizuri kuibuka na ushindi hapo kesho, na leo hii asabuhi wamefanya mazoezi katika dimba la Shk. Amri Abeid , uwanja ambao utatumika katika mechi ya kesho.

Kocha mkuu wa Yanga , Mholanzi Hans Van Der Pluijm amesema wachezaji wake wote 23 waliopo jijini Arusha wapo salama na wanaendelea kuwapa maelekezo ya mwisho tayari kwa kusaka ushindi.

Wachezaji waliosafiri na timu kwenda Arusha ni Walinda mlango, Deogratias Munish "Dida" na Ally Mustafa "Barthez"

Walinzi ni Juma Abdul, Mbuyu Twite, Oscar Joshua, Amos Abel, Rajab Zahir, Ibrahim Job, Kelvin Yondani na Nadir Haroub "Cannavaro".

Viungo ni Hamis Thabit, Nizar Khalfani, Frank Domayo, Hassan Dilunga, Salum Telela na Sospter Maiga

Washambuliaji ni Didier Kavumbagu, Hamis Kizza, Jerson Tegete, Mrisho Ngasa, Saimon Msuva, Said Bahanuzi na Hussein Javu

Mechi nyingine ya kesho ni baina ya Simba sc dhidi ya Ashanti United katika dimba la Taifa jijini Dar es salaam kuanzia majira ya saa 10:00 jioni. 

Mtibwa Sugar itacheza na Ruvu Shooting (Uwanja wa Manungu, Morogoro), huku Mgambo Shooting na Kagera Sugar zitaoneshana kazi kwenye Uwanja wa Mkwakwani jijini Tanga .

No comments:

Post a Comment