Na Baraka Mpenja , Dar es salaam
0712461976
KWA MUDA mrefu mashabiki na wanachama wa Simba sc wamekuwa wakiamini
kuwa klabu yao imefika hapo ilipo kwasababu ya mwenyekiti wao Ismail Aden Rage
kuongoza vibaya.
Rage amekuwa akisuguana na wanachama wake kwa muda
mrefu, lakini sasa ameshatangaza kutogombea tena nafasi hiyo katika uchaguzi Mkuu
unaotarajia kufanyika mei 4 mwaka huu.
Rage alitangaza maamuzi hayo machi 16 mwaka huu katika mkutano mkuu wa wanachama ulioitishwa maalumu kwa ajili ya kufanya
marekebisho wa katiba.
Kauli ya aina yake katika mkutano
huo ilikuwa ile ya Rage kuwaita wanachama wa Simba ni ‘mbumbumbu’
Kufuatia kauli hiyo, Rage,
alilazimika kuwaomba radhi wanachama hao zaidi ya 571 waliohudhuria mkutano
huyo uliofanyika kwenye Ukumbi wa Bwalo la Polisi, Oysterbay jijini Dar es
Salaam.
“Napenda kuwaomba radhi wanachama
wenzangu kutokana na nilivyosema tuache umbumbumbu, lakini sikuwa namaanisha
kama wengi wenu mlivyoelewa,” alisema Rage.
Licha ya kusema hatagombea tena
uongozi, Rage, alisema ataendelea kuwa mwanachama mwaminifu wa Simba na atatoa
mchango wake ili kufanikisha maendeleo.
Ikumbukwe kuwa kabla ya kauli hiyo,
Rage alishawahi kusema kauli za aina yake.
Mwezi machi mwaka jana aliwahi kuuita
mkutano wa wanachama walioaminika kuwa
zaidi ya 600 ambao ulitangaza kumpindua madarakani kuwa ni kama `kikao cha harusi`.
Pia
novemba mwaka jana kamati ya utendaji ya Simba ilitangaza kumuondoa madarakani
mwenyekiti wake, Ismail Aden Rage.Kamati hiyo ilifikia uamuzi wa kumsimamisha Rage akiwa nje ya nchi na kumtangaza aliyekuwa Kaimu Makamu Mwenyekiti, Joseph Itang’are ‘Mzee Kinesi’ kushika nafasi hiyo ya juu zaidi katika klabu hiyo.
Mzee Kinesi alisema walifikia maamuzi hayo kutokana na mwenyekiti huyo kwenda kinyume na makubaliano na Kamati ya Utendaji ya Simba.
Lakini baadaye ya mwanaume huyo kurudi alitamba
kuwa yeye ni mwenyekiti halali wa Simba na kikao hicho kilikuwa kikao cha
harusi.
Wakati anawasili uwanja wa ndege wa kimataifa wa
Mwalimu Nyerere kulikuwa na kundi kubwa la watu walioaminika kuwa wanachama wa Simba
waliojitokeza kumlaki na kumshangilia kwa nguvu.
Kweli jamaa alirudi na baadaye TFF walitangaza
kumtambua kuwa ndiye mwenyeki halali wa Simba, lakini wakamtaka aitishe mkutano
wa dharura na kumpangia ajenda.
Rage aligoma na kusema yeye ndiye mwenye mamlaka
ya kupanga ajenda za mkutano kwa mujibu wa katiba.
Yapo mengi ya kuyasema kuhusu Rage, lakini sasa
ameshatangaza kung`atuka baada ya muda mrefu wa mvutano na viongozi wenzake pamoja
na wanachama wa Simba.
Baadhi ya wananachama wa Simba wanafikiria kuwa
Rage ndiye mchawi wa klabu yao, hivyo kuondoka kwake ni jambo la heri.
Tarehe ya uchaguzi ilishatangazwa na tayari kamati
ya uchaguzi ilishaundwa chini ya mwenyekiti wake, Dr. Damas Ndumabro ambaye ni
mwanasheria kitaaluma.
Hata hivyo, Kamati ya uchaguzi ya klabu ya
Simba imetangaza kuwa mchakato wa
uchaguzi wa klabu hiyo utaweza kuendelea baada
ya msajili wa vyama vya michezo
kuipitisha rasimu ya katiba ya Simba iliyopelekwa hivi karibuni.
Mwenyekiti wa kamati hiyo Damas Ndumbaro alisema
jana kuwa kamati yake ilikaa Alhamisi wiki hii na kujadili masuala mbalimbali
kuhusiana na mchakato wa uchaguzi ambao awali ulipangwa kufanyika mapema mwezi
ujao.
Mwenyekiti wa kamati ya uchaguzi ya Simba Damas
Ndumbaro amewataka
wanachama wa klabu ya Simba kuvuta subira hadi
hapo msajili wa vyama
vya michezo atakaposaini rasimu ya katiba ndipo
watakapo tangaza kuanza rasmi kwa harakati za kuwania nafasi mbalimbali ndani
ya klabu
hiyo.
Haya sasa mambo yameshaiva ingawa bado rasimu ya
katiba ikisubiriwa kusajiliwa.
Lakini cha msingi wakati unaoamini kuwa wa ufalme
wa Rage kuiongoza Simba unaelekea ukingoni.
Wanachama wa Simba ndio wenye mamlaka kikatiba ya
kuchagua kiongozi wao mkuu.
Ni wanachama hawa hawa waliomchagua Rage kwa kura
nyingi, lakini walimkana baadaye na kuona hana maana kwa klabu.
Sasa swali la msingi kwa wanachama wa Simba, Rage anaondoka,
nani wanadhani atakuwa mbadala wake?.
Nadhani wapo wengi watakaojitokeza kugombea nafasi
ya mwenyekiti pamoja na wajumbe wa kamati ya utendaji.
Kuna watu wataomba kwa lengo la kuleta mabadiliko
na kuifufua Simba ya miaka ya nyuma, lakini hata wachumia matumbo watakuwepo
tu.
Unajua kila mtu anataka kazi fulani kwa sababu
zake.
Simba ni chama kubwa, pesa zipo na ukitaka kula
utakula sana kwasababu kumekosekana watu makini wa kufuatilia mahesabau ya
klabu yao.
Si Simba tu, hata klabu nyingine kama Yanga kuna
matatizo kama haya.
Wapo watu wanaoneemeka kuwepo katika klabu hizi na
wanajulikana.
Walikuwa wa kawaida, lakini kupitia nafasi za
uongozi wazipatazo, wanazidi kuwa watu maarufu kwa mkwanja.
Ukichunguza vyonza vya pesa zao utagundua ni pesa
za mpira wazivunazo katika klabu
wanazozitawala.
Niliwahi kuongea na kiongozi mmoja wa chama cha
juu cha soka, alinipa siri kuwa hakuna pesa nyepesi na za bure kama kwenye
mpira.
Mazungumzo yetu yalikuwa ya kawaida tu na alisema
kamwe nisiseme. Ni miaka mingi imepita na sasa si kiongozi tena.
Kama mtu anaingia kwa maslahi binafsi basi hana
maana yoyote kwa Simba.
Ikumbukwe kuwa viongozi wetu wanakuwa na mtandao
mkubwa sana.
Anapotoka huyu anataka amrithishe mtu ambaye wana
mahusiano ya karibu ili waendele kuvuna mapato yasiyo halali.
Ni wakati wa wanachama wa Simba kuwapima watu
watakaoomba kugombea nafasi za juu katika klabu hiyo.
Najua ni ngumu kuwajua kwa macho, lakini angalau
wawatafiti wanaotarajia kuomba.
Ndani ya klabu yao, wapo walioonesha nia ingawa
kwasasa hatuwezi kuwataja kwasababu mchakato bado.
Lakini wanajulikana na wanachama wanawajua vizuri
tu. Na bahati nzuri walishaanza kuwapigia debe chini kwa chini.
Nawatahadhirisha Simba kutochagua kwa hasira za
muda mrefu walizokuwa nazo juu ya Rage.
Najua lipo kundi kubwa lisilomuunga mkono Rage,
hivyo kuondoka kwake kunawapa raha.
Lakini wasije wakachagua mtu kwa kufikiria raha ya
kuondoka kwa Rage.
Kinachotakiwa ni kupima uwezo wa watu wanaoweza
kuwafikisha mbali.
Najua Simba ina uchu wa mafanikio makubwa wakianza
na kurejesha hadhi yao iliyopotea kuanzia uongozi na mambo ya uwanjani.
Wanahitaji mtu mwenye malengo makubwa, nia ya
dhati ya kuikoa klabu hii hapa ilipo.
Watu wa aina ni wachache sana, hivyo lazima
wanachama watumie muda wao kuwapima watu wanaotarajia kuomba nafasi ili mwisho
wa siku wajue nani anafaa.
Wakati wa mabadiliko ndio huu, nafasi ya kubadii
timu umefika.
Nafasi ndio hii, kama watakosea kufanya hivyo,
watasubiri mpaka wakati mwingine uchaguzi utakapofika.
La sivyo wataendelea na sinema zao za kumpindua
kiongozi, lakini mwisho wa siku wanaonekana hawana maana na vikao vyao kuitwa
vikao vya harusi.
Ili kuirudisha Simba kwenye hadhi yake, wanachama
fikirieni mara mbilimbili ili kupata watu sahihi.
Kwa msimu wa pili sasa, Simba sc inakosa mashindano
ya kimataifa, kwasababu msimu huu wataishia nafasi ya nne au ya tano kama wakikosea
hesabu zao katika mechi mbili za mwisho.
Msimu huu wamevuna matokeo mabaya mno, na tatizo
linaloonekana ni kwenye uongozi ambao kuna maamuzi ya msingi huamuriwa bila
kuona mbali.
Pia kuna lawama za uongozi wa Rage kutowalipa
wachezaji maslahi yao. Makocha nao hufukuzwa mara kwa mara.
Sasa mwisho wa haya ni mei 4, lakini wakikosea tu,
majanga kama kawaida yataendelea.
Kila la kheri wanachama wa Simba sc katika
harakati zenu za kuleta mapinduzi klabuni kwenu.
No comments:
Post a Comment