Na Baraka Mpenja, Dar es salaam
0712461976
HAKUNA jambo baya kama kujijengea mazingira ya kutoaminiwa
kwa maamuzi yako hasa unapokuwa kiongozi mwenye dhamana ya kuongoza taasisi,
chama, idara na sehemu nyingine za kazi.
Ukiwa kiongozi
inaweza kufika wakati ukakaa na viongozi wenzako na kufikia maamuzi fulani
baada ya kujadiliana, lakini unapowasilisha kwa watu wanaohusika na maamuzi
hayo akajikuta unawaumiza na kushindwa kukuamini.
Niliwahi kufunndishwa kuwa moja ya sababu ya
migogoro mingi katika jamii ni kukosekana kwa mawasiliano baina ya pande mbili
zinazohusika katika jambo fulani.
Mawasiliano na watu unaowaongoza ni muhimu sana
ili kuepukana na lawama zisizo za msingi.
Kila kitu hutokea kwasababu fulani, lakini
unaposhindwa kubainisha sababu ya kufikia maamuzi yako, husababisha jamii inayokuzungukoa
kushindwa kukuamini.
Kwasasa ligi kuu soka Tanzania bara imefikia hatua
ya mwisho ambapo kama kawaida imejigawa katika makundi matatu.
Mosi; kuna timu ambazo zinachuana katika
kinyang`anyiro cha ubingwa.
Hapa unawazungumzia wanaume wawili, vinara Azam fc
na mabingwa watetezi, Dar Young Africans.
Azam fc wapo kileleni kwa pointi 56 baada ya
kucheza mechi 24, wakati Yanga wapo nafasi ya pili kwa pointi 52 kufuatia
kushuka dimbani mara 24.
Ubora wa Azam fc umewafanya wasifungwe katika
mechi 24 walizocheza mpaka sasa.
Mchuano huu mkali unaweza kufika tamati hapo kesho
majira ya saa 12 jioni.
Timu zote mbili zitashuka dimbani ambapo Yanga
watakuwa wageni wa maafande wa JKT Oljoro katika uwanja wa Shk. Amri Abeid, mjini Arusha.
Azam fc watakuwa na kibarua dhidi ya Mbeya City
katika dimba la Sokoine ,jijini Mbeya.
Kwanini nasema biashara ya kusaka ubingwa inaweza
kumalizika kesho? Sababu si nyingine bali ni kama Azam fc watashinda mechi yao,
rasmi watakuwa wamewavua ubingwa Yanga msimu huu.
Wana Lambalamba hao wakishinda watafikisha pointi
59 kileleni ambazo Yanga hata wakishinda mchezo wao wa kesho na wa mwisho dhidi
ya Simba hawataweza kufikisha pointi 59.
Kwa maana hiyo kesho ni siku nzuri ya kufuatilia
hatima ya Azam fc katika harakati zake za kuchukua taji kwa mara ya kwanza,
wakati Yanga wakiwa katika presha ya kutetea mwari wao.
Mbeya City wao wanaisaka nafasi ya tatu katika
msimu wao wa kwanza tangu wapande ligi kuu, hata hivyo wameshaichukua kwasababu
hakuna timu yoyote ya chini inayoweza kufikisha pointi 47 walizonazo mpaka sasa.
Kuelekea katika mechi za kesho, tayari mengi
yameshasemwa sana ikiwemo Azam fc kuaminika kuwahonga Mbeya City ili wawape
ushindi wa chee.
Jana niliandika kuhusiana na jambo hili, hivyo
unaweza kurejea katika habari zetu kwenye mtandao huu.
Pili; zipo timu zinazosaka nafasi nzuri katika
msimamo. Hapa unakutana na Simba sc, Kagera Sugar, Mtibwa sugar, Ruvu Shooting,
na Coastal Union . Hizi hazina presha kubwa kwasababu zina uhakika wa kubakia
ligi kuu.
Tatu; kuna kundi la kifo, hakika hizi timu
zinachuana vikali kukwepa kushuka daraja.
Angalau JKT Ruvu na Mgambo wanaonekana kujitahidi
kujikwamua kwasababu wamevuka pointi 24.
Mgambo wapo nafasi ya 10 kwa poiniti 25 baada ya
kucheza mechi 24, wakati JKT Ruvu wapo nafasi ya 9 kwa pointi 28 kufuatia
kucheza mechi 24.
Lakini unapozungumzia Prisons na Ashanti zenye
poiniti 22 kila moja katika nafasi za 11 na 12 unazungumza jambo muhimu sana.
Timu hizi zinachuana vikali ili kupata klabu moja
itakayoungana na Rhino Rangers na JKT Oljoro kushuka daraja msimu huu.
Taarifa ya shirikisho la soka Tanzania iliyotumwa
kwa vyombo vya habari jana ilieleza kuwa leo kutakuwa na mechi tatu za ligi kuu
soka Tanzania bara ambapo Simba wataumana na Ashanti United uwanja wa Taifa,
Prisons dhidi ya Rhino Rangers uwanja wa Sokoine, halafu Coastal Union na JKT
Ruvu uwanja wa Mkwakwani.
Lakini muda mfupi baadaye ilitumwa taarifa ya
marekebisho ya ratiba ambapo mechi ya Simba na Ashanti United ilisogezwa mpaka
kesho jumapili.
Kwa bahati mbaya sana haikuelezwa sababu za
kusogeza mechi hiyo kutoka leo hii
kwenda kesho.
Haikuelezwa kama uwanja wa Taifa utakuwa na
shughuli nyingine au kuna sababu zozote za kiusalama kwa timu zote.
Kila mtu alisema lakwake, wengine wakasema ni
kuhofia mvua zinazoendelea kunyesha kuanzia jana.
Lakini wakahoji kama ni hivyo, nani anayeweza kujua
kama leo kutakuwa na mvua uwanja wa Taifa?.
Kimsingi kila mtu anasema ya kwake. Sikuona haja
ya kuwatafuta TFF kwanini wameahirisha mechi hiyo hata bila wao wenyewe kutoa
sababu ya moja kwa moja.
Lengo langu si kutaka kuandika juu ya sababu ya
kuahirisha mechi hiyo, bali ni udhaifu walionao katika suala la mawasiliano na
kuwafanya waonekane wanaleta `figisufigisu`.
Labda watasema sababu wakishinikizwa na vyombo vya
habari au wakuu wa juu ndani ya TFF, lakini najua ilikuwa ni muhimu kwao
kuwasiliana na umma kuueleza kwanini mechi hiyo inasogozwa mbele, kwa lugha
nzuri kwanini inaahirishwa.
Hapa ndipo dhana ya mawasiliano inapokuja. Kama
TFF wangesema mapema, au kueleza sababu za kuahirishwa kwa mechi hiyo wangeeleweka
mapema kuliko kukumbatia sababu yao na kuonesha kama wana ubabe au mamlaka ya
kuamua watakavyo na si kuwafikiria waathirika.
Ona sasa wanavyojijengea mazingira ya kutoaminiwa
na jamii yao.
Kwa anayefuatilia vyombo vya habari, jana Tanzania Prisons wamekerwa mno na
mabadiliko haya ya ratiba.
Hoja ya Prisons ilikuwa kama yangu tu, kwanini
mechi imeahirishwa ghafla na nani mwenye mamlaka ya kuahirisha mechi
iliyopangwa.
Inspekta Sadick Jumbe, katibu mkuu wa Prisons
alisema wameshangazwa sana na maamuzi hayo ya Bodi ya ligi kwasababu wanataka
kupanga matokeo.
Sheria zipo wazi hasa ile ya kuahirisha mechi
ambao kuna kipengele kinahusu majanga ya asili ambayo si mpango wa binadamu.
Mfano kama kuna mvua kubwa kama ili ye Mabatini
jumatano, mwamuzi anayo mamlaka ya kuahirisha mechi mpaka siku nyingine
itakayopangwa.
Kwa hii ya Prisons haikufikia hatua hiyo, kibaya
zaidi walioahirisha hawajasema kwanini.
Prisons wanaona kama TFF wanapanga matokeo
kwasababu wanajua wazi kuwa Ashanti ni wapambanaji wenzao wa kukwepa daraja.
Ilikuwa jambo nzuri kwa mechi za klabu hizi
kuchezwa kwa wakati mmoja ili kuepuka kumpa nafasi mwenzake kujua matokeo ya
mapema.
Kama Prisons anacheza leo, manake Ashanti watakuwa
wanawasikilizia wanafanya nini na wao waingiaje kesho uwanjani dhidi ya Simba
sc.
Kwa sababu za Prisons, nadhani jamaa wana pointi
ndani yake.
TFF lazima wabadilike sana hasa katika kuchukua
maamuzi muhimu yanayogusa maslahi ya kundi fulani.
Hakuna sababu ya kuendelea kutoa taarifa bila
sababu. Kama kuna sababu kubwa ya kuahirishwa kwa mechi hiyo, kulikuwa na ubaya
gani kuisema mapema ili hata Prisons wajiridhishe.
Hivi kweli waliwasiliana na Prisons mapema juu ya
mabadiliko hayo?, au ndio watu wachache walikaa na kuamua tu.
Kukosekana kwa mawasiliano ni kujijengea mazingira
mabaya ya kuwa una ajenda za siri.
Wakati huu ambao ligi inafikia tamati, kashfa ya
kupanga matokeo huwa inajitokeza, hivyo TFF kuweni makini na mechi
zinazohusisha timu zinazotafuta ubingwa na kushuka daraja.
Jambo nzuri ni kujenga utataribu kwa kujibu swali
la kwanini?
Kama mechi inasogezwa mbele au inaahirishwa, eleza
kwanini?.
Kama unachukua maamuzi fulani unayodhani yana
maslahi, weka wazi kwanini?
TFF kama wataendelea kutokuwa makini watalaumiwa
sana kama hili la Prisons ambalo hawakubainisha kwanini wamesogeza mechi.
Kama watatoa sababu, basi ni baada ya kushituliwa, lakini toka
awali hawakueleza katika taarifa yao zaidi ya kusema mechi itachezwa kesho
jumapili.
Prisons wana pointi, TFF fikirieni sana ili siku
zijazo mjiepushe na maamuzi kama haya bila kuwasilina na wahusika na inafika muda hawajui kwanini jambo
fulani limetokea.
Rais Jamal Malinzi, jamii ya watu wa mpira bado
ina imani kubwa na wewe. Jaribu kurekebisha kasoro kama hizi ili kujiepusha na
kashfa ndogo ndogo kama hizi.
Kuna watu wachache watakaokuharibia taswira yako
bila sababu ya msingi.
No comments:
Post a Comment