Search This Blog

Saturday, April 5, 2014

YANGA YA PLUIJM NA DAKIKA 360 ZA UTUMWA MBELE YA AZAM FC!!


Na Baraka Mpenja, Dar es salaam


MABINGWA watetezi wa ligi kuu soka Tanzania bara, Dar Young Africans wapo katika msongo wa mawazo baada  ya kuweka rehani ubingwa wao msimu huu mbele ya wana Lambalamba Azam fc wanaotesa kileleni kwa pointi 53.
Ligi ikiwa katika hatua za mwisho, Yanga wanaonolewa na kocha mkuu, Mholanzi, Hans Van Der Pluijm wamebakiza mechi 4 tu ambazo sawa sawa na dakika 360.
Katika msimamo, Yanga wapo nafasi ya pili baada ya kushuka dimbani mara 22 na kujisanyia pointi 46, pointi 7 nyuma ya Azam fc.
Dakika 360 zilizosalia kwa Yanga zitawafanya wawe watumwa kwasababu ya kasi ya Azam fc waliopo kileleni.
Wana Lambalamba wameshuka dimbani mara 23 na hawajawahi kupoteza mchezo hata wowote.
Kwa matokeo hayo, Azam fc wanasalia kuwa timu bora zaidi msimu huu kwa maana ya matokeo ya uwanjani.
Wakati mwingine, mpira wa miguu una matokeo yasiyotabirika, hasa ushindi unapokuwa muhimu kwa klabu yoyote ili kuamua hali fulani, mfano kutwaa ubingwa au kukwepa kushuka daraja.
Kwa kawaida, timu moja inapotangulia kufunga bao katika mchezo, inamfanya mwenzake kuwa mtumwa.
Utumwa huu unatokana na ukweli kuwa, klabu iliyofungwa  inahangaika kutafuta bao la kusawazisha.
Kwa fomula nyepesi, huwezi kuandika mbili bila moja. Unapofungwa bao 1-0 dakika ya 1, utakuwa mtumwa wa dakika 89 kutafuta njia ya kusawazisha na hatimaye kuandika bao la pili na la ushindi.
Ukiangalia msimamo wa ligi kuu mpaka sasa, Yanga wamebaki kuwa watumwa wa uwanjani zaidi ya klabu yoyote.
Utumwa wao upo katika mazingira mawili ambayo yanaonekana kufanana, lakini yana utofauti.
Mosi; ni watumwa wa kuhitaji kutetea ubingwa wao katika ligi yenye ushindani mkubwa zaidi.
Ili kuendeleza heshima yao, wanalazimika kujituma kwa ngvu zote katika michezo minne iliyosalia, ili kufanikisha malengo yao.
Kupata ubingwa ni jambo zuri, lakini unapotetea msimu unaofuata, inakuwa nzuri zaidi na unadhihirisha kuwa hukubahatisha kutwaa taji.
Pili; Yanga ni watumwa wa kuhitaji kusawazisha pointi 7 walizopo nyuma ya Azam fc ili kuweza kutetea ubingwa wao.
 Wakati wakiwa katika mazingira hayo magumu, Azam fc nao wanajitahidi kuziba njia za kukamatwa na Yanga.
Njia inayotumika na Azam fc ni kuhakikisha wanashinda mechi zote tatu zilizosalia.
Tayari Azam fc wapo mbele dhidi ya Yanga, kwa maana nyingine unaweza kusema Yanga ni watumwa wa vinara hao wa ligi kuu.
Hawana namna ya kutetea ubingwa bila kusawazisha pengo la pointi saba na kuwaombea Azam fc wafanye vibaya.
Kama Yanga watashinda mechi zote nne zilizosalia, wataweza kufikisha pointi 58, wakati Azam nao wana uwezo wa kuzifikia na zaidi.
Azam wamebakiza mechi tatu, kama watashinda zote watafikisha pointi 62. Kwa pointi hizo, hata Yanga wakishinda michezo yote kwa mabao 100, bado ubingwa utatua Chamazi.
Kwa matokeo yanayopatikana mechi hizi za mwisho, huwezi kutegemea Yanga na Azam fc kushinda mechi zao zilizosalia.
Kumbuka jumapili Yanga wanakabiliana na JKT Ruvu uwanja wa Taifa jijini Dar es salaam.
Huu utakuwa mtihani mwingine wa Pluijm kuanza  rasmi utumwa wa kuwafukuzia Azam fc kileleni.
JKT Ruvu wapo nafasi ya 9 kwa pointi 28. Kiukweli wapo mazingira tata ya kushuka daraja, kwa maana hiyo wanatakiwa kupambana kwa nguvu zote kupata pointi tatu mbele ya Yanga .
Kuwafahamu wapinzani wako kunakufanya uongeze maarifa ya kuwakabili.
Kocha wa JKT Ruvu, Fredy Felix Minziro anawafahamu wachezaji wote wa Yanga kwasababu alikuwa nao mzunguko wa kwanza.
Iliwafundisha akiwa kocha msaidizi, na kuna wakati aliwafundisha bila uwepo wa kocha mkuu, Ernies Brandts.
Mchezo wa jumapili utakuwa mgumu kwa timu zote mbili. Yatahitajika maarifa makubwa kwa makocha wote wawilli kupata ushindi.
Yanga wataingia wakiwa na kumbukumbu ya kufungwa mabao 2-1 na Mgambo JKT , wakati JKT Ruvu walishinda mechi yao ya mwisho dhidi ya Rhino Rangers kwa mabao 3-1.
Utumwa wa pili wa Pluijm utakuwa  aprili 9 mwaka huu uwanja wa Taifa jijini Dar es salaam dhidi ya Kagera Sugar.
Wakata miwa hawa wa Kaitaba, hawahitaji ubingwa wala nafasi ya pili. Malengo yao ni nafasi ya tatu na nne.
Kama wana malengo hayo, basi wamejipanga na wanaendelea kujipanga ili kufanya vizuri katika michezo yao minne iliyosalia kuanzia wa leo dhidi ya Simba sc.
Bila shaka mechi hii ya Yanga na Kagera itakuwa na upinzani mkubwa kwa timu zote.
Haitakuwa rahisi kwa Pluijm kuchomoka katika mechi hii, lakini akiwa na mipango safi ataweza kuvuna pointi tatu muhimu.
Baada ya mechi hiyo, Yanga sc watasafiri kwenda mkoani Arusha kuwakabili JKT Oljoro aprili 13 mwaka huu kwenye uwanja wa Shk. Amri Kaluta Abeid.
Endapo kwa wakati huo JKT Oljoro watakuwa kwenye nafasi nzuri ya kubakia  ligi kuu, basi itakuwa mechi ngumu kwa Yanga.
Kwakuwa Oljoro mpaka sasa wapo nafasi ya 13 kwa kushuka dimbani mara 23 na kujikusanyia pointi 15 pekee, wanahitaji kujidhatiti kushinda mechi zote tatu walizosalia nazo, japokuwa inaonekana haitawasaidia kubakia.
Oljoro wapo katika hatari zaidi ya kushuka daraja, lakini haimaanisha Yanga watakuwa na kazi rahisi kuibuka na ushindi. Mipango mzuri ya uwanjani itahitajika.
Mechi ya mwisho ya Yanga itakuwa aprili 19 dhidi ya mahasimu wao wakubwa, Simba Sc.
Mechi ya watani haitabiriki kirahisi, bali matokeo yanaamriwa ndani ya dakika 90.
Mechi hizi nne zilizosalia, zimewaweka Yanga katika mazingira ya utumwa zaidi ili kutetea ubingwa wao.
Azam fc wao wamebakiza mechi dhidi ya Ruvu shooting, Mbeya City na JKT Ruvu.
Ruvu Shooting hawapo nafasi ya hatari katika msimamo, lakini wataingia kwa lengo la kulinda heshima na pengine kuhitaji kuwa timu pekee kuanza kuvuruga rekodi ya Azam ya kutofungwa msimu huu.
Timu ya kuharibu rekodi ya Azam fc haijapatikana, na kinachosubiriwa ni klabu hizi tatu zilizobakiza mechi nao.
Kocha wa Azam fc, Joseph Marius Omog anahitaji kujiandaa vyema  kwenda kuvuna pointi tatu kwa Ruvu Shooting kule Mabatini, Mlandizi mkoani Pwani.
Atahitaji kuwa na tahadhari kubwa kama kweli anataka  kutwaa ubingwa.
Pia mechi ya Azam fc na  Mbeya City itakuwa na kimuhemuhe zaidi kwasababu City nao wanauwinda ubingwa msimu huu.
Mpaka sasa City wameshashuka dimbani mara 23 na kujikusanyia pointi 45 pointi moja nyuma ya Yanga.
Katika uwanja wa sokoine, Wagonga nyundo hawa wa Mbeya, hawajawahi kufungwa, hivyo Azam fc watahitaji kujipanga kuvunja rekodi yao.
Mechi ya mwisho kwa Azam fc itakuwa dhidi ya JKT Ruvu ,na  uzito wa mechi hiyo utategemeana na matokeo ya timu zote katika michezo miwili ijayo.
Kama JKT Ruvu watakuwa wamefikia hatua nzuri kabla ya mechi ya mwisho, basi inaweza kuwa msaada kwa Azam fc.
 Lakini kama bado watakuwa kwenye mstari mwekundu wa kushuka daraja, basi itakuwa kibarua kizito zaidi.
Hakika utumwa wa Yanga katika dakika 360 za michezo minne iliyosalia ni mkubwa sana na wanahitaji kufuta pengo la pointi 7 dhidi ya Azam fc.
Hakuna jinsi, Yanga lazima washinde mechi zote zilizosalia, huku wakiomba dua mbaya kwa Azam fc  wapoteze angalau michezo miwili.
Azam fc wametangulia mbele kwa pointi, Yanga ni watumwa wa kusawazisha hali hiyo, hivyo wanatakiwa kuwa na mipango mizito zaidi.

No comments:

Post a Comment