Search This Blog

Friday, May 31, 2013

TAIFA STARS WATAKIWA KUJITUMA KUHAKIKISHIA WANARUDI NA USHINDI NA KUFUZU KOMBE LA DUNIA

Balozi wa Tanzania nchini Ethiopia, Joram Biswaro amewataka wachezaji wa Taifa Stars kuhakikisha wanaipeleka timu hiyo kwenye fainali za Kombe la Dunia zitakazofanyika mwakani nchini Brazil.

Ametoa changamoto hiyo wakati alipotembelea mazoezi ya timu hiyo jana (Mei 29 mwaka huu).

Taifa Stars inayodhaminiwa na Kilimanjaro Premium Lager imepiga kambi nchini Ethiopia na inafanya mazoezi kwenye Uwanja wa Addis Ababa.

“Watanzania tunafurahi kutokana na uwezo mnaouonyesha, hasa baada ya kuifunga Morocco mabao 3-1. Kama mliwafunga nyumbani hata kwao mnaweza kuwafunga. Tunataka kuwaona Maracana (Brazil) mwakani, mimi tayari ninayo tiketi mtanikuta kule,” amesema Balozi Biswaro ambaye enzi zake aliwahi kuichezea timu ya Yanga.

Taifa Stars ambayo iko Addis Ababa tangu Jumatatu (Mei 27 mwaka huu) imeweka kambi katika hoteli ya Hilton ambapo Jumapili (Juni 2 mwaka huu) itacheza mechi ya kirafiki na Sudan (Nile Crocodile) kwenye Uwanja wa Addis Ababa.

Balozi Biswaro ameikaribisha Taifa Stars ubalozini Addis Ababa mara baada ya mechi dhidi ya Sudan ambapo itakutana na baadhi ya Watanzania wanaoishi Ethiopia kabla ya kuondoka alfajiri kwenda Marrakech, Morocco kwa kupitia Cairo, Misri.

Kocha Kim Poulsen amesema kikosi chake kinaendelea na mazoezi vizuri na kitaimarika zaidi baada ya wachezaji Mbwana Samata na Thomas Ulimwengu wanaochezea timu ya TP Mazembe ya Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo (DRC) kujiunga nacho Juni 3 mwaka huu jijini Marrakech kwa ajili ya mechi dhidi ya Morocco itakayochezwa Juni 8 mwaka huu.

Naye Meneja wa Bia ya Kilimanjaro Premium Lager, George Kavishe, akizungumza kutoka Dar es Salaam, alisema wao kama wadhamini wamefarajika kuona timu inaendelea vizuri Mjini Addis na  inaleta matumaini kuwa watacheza vizuri katika mechi dhidi ya Morocco Juni 8.
 “Tuna imani sana na Taifa Stars kwani wameshatuonesha yote yanawezekana…watanzania waiombee timu yetu ili na sisi tupate nafasi ya kucheza Brazil mwakani,” alisema.

Wachezaji walioko katika kikosi cha Stars jijini Addis Ababa ni Juma Kaseja, Aggrey Morris, Mwadini Ally, Ally Mustafa, Shomari Kapombe, Kevin Yondani, Erasto Nyoni, Haroub Nadir, Mwinyi Kazimoto, Frank Domayo, Mrisho Ngasa, Khamis Mchana, Amri Kiemba, Salum Abubakar, Simon Msuva, John Bocco, Vicent Barnabas, Mudathiri Yahya, Athuman Idd, Haruni Chanongo na Zahoro Pazi.

No comments:

Post a Comment