Search This Blog

Friday, April 11, 2014

UCHAMBUZI LIGI KUU: SIMBA SC VS ASHANTI UNITED JUMAPILI, PRISONS VS RHINO, COASTAL UNION VS JKT RUVU KESHO!!


Na Baraka Mpenja, Dar  Es Salaam

0712461976

Michuano ya Ligi Kuu ya Vodacom (VPL) kuwania ubingwa wa Tanzania Bara inaendelea kesho katika raundi ya 25 ambapoTanzania Prisons na Rhino Rangers wataumana Uwanja wa Kumbukumbu ya Sokoine, jijini Mbeya) wakati Coastal Union watakuwa mwenyeji wa JKT Ruvu kwenye Uwanja wa Mkwakwani jijini Tanga.

Ligi hiyo itaendelea Keshokutwa (Aprili 13 mwaka huu) kwa mechi nyingine tano za kukamilisha raundi hiyo.

Simba watavaana na  Ashanti United Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam kuanzia saa 10 kamili jioni. 
Uwanja wa Sheikh Kaluta Amri Abeid jijini Arusha utakuwa mwenyeji wa mechi kati ya wenyeji Oljoro JKT na Yanga.
 Mtibwa Sugar itacheza na Ruvu Shooting (Uwanja wa Manungu, Morogoro), Mgambo Shooting na Kagera Sugar zitaoneshana kazi kwenye Uwanja wa Mkwakwani jijini Tanga huku Mbeya City ikiumana na Azam kwenye Uwanja wa Kumbukumbu ya Sokoine jijini Mbeya.
Kesho mtandao huu utakupatia uchambuzi mwingine kuelekea mechi hizo za keshokutwa ili kubashiri ni timu gani inaweza kushinda.

SIMBA VS ASHANT UNITED 

Hii ni mechi yenye mvuto kwa kuangalia umuhimu wa matokeo kwa Ashanti United waliopo katika hatari kubwa ya kushuka daraja.
Ashanti wamecheza mechi 24 na kufanikiwa kushinda mechi 5, sare 7 na kupoteza mechi 12, hivyo kujikusanyia pointi 22 katika nafasi ya 12.
Mbele ya Ashanti United wapo Tanzania Prisons waliocheza mechi 24 ambapo wameshinda mechi 4, sare 10 na kufungwa mechi 10.
Kinachowafanya Prisons wawe juu ya Ashanti ni wastani mzuri wa mabao ya kufunga na kufungwa.
Prisons wamefunga mabao 21 na kufungwa mabao 30. Ukitoa mabao ya kufunga na kufunga unapata ­hasi tisa (-9).
Ashanti wamefunga mabao 19 na kufungwa mabao 38, hivyo ukitoa mabao ya kufunga na kufungwa unapata hasi kumi na tisa (-19).
Kwa hesabu hizo, Prisons wanakuwa juu ya Ashanti hata kama wote wana pointi 22 katika michezo yao 24 waliyoshuka dimbani.
Kwa mazingira haya ya Ashanti United, mechi ya keshokutwa ni muhimu sana, tena wanahitaji kushinda mabao mengi zaidi kwasababu hata Prisons watakuwa na mchezo dhidi ya vibonde Rhino Rangers kutoka mjini Tabora katika uwanja wao wa Sokoine jiji Mbeya.
Simba sc hawana cha kupoteza mpaka sasa, hawawezi kutwaa ubingwa wala kushika nafasi tatu za juu kwa pointi zao 37, huku wakibakiza mechi mbili tu.
Endapo Simba sc watashinda mechi zote watafikisha pointi 43 ambazo zilishavukwa na Mbeya City walioopo nafasi ya tatu.
Hivyo Simba baishara yao ni nafasi ya nne ambayo wanapambana na Kagera Sugar wenye pointi 34 katika nafasi ya tano, huku wakibakiza mechi mbili.
Kama Kagera Sugar watashinda mechi zote watafikisha pointi 40, na ili kuipata nafasi ya nne watatakiwa kuwaombea Simba wapoteze mechi zote mbili.
Simba sc kwasasa wanahitaji heshima tu kwa kushinda mechi zao zilizobaki.
Kwa mazingira hayo bila shaka wamejiandaa vizuri kuwafunga Ashanti United keshokutwa katika dimba la Taifa.
Kocha Mkuu wa Simba sc, Mcroatia Dravko Logarusic ataingia uwanjani kwa kusaka ushindi mbele ya kocha wa Ashanti Abadallal Kibadeni “King Mputa”.
Huu utakuwa mchezo mgumu zaidi kwa Kibadeni kwasababu matokeo yanayomfaa kwakwe ni ushindi tu.
Kama atashinda mechi ya keshokutwa itakuwa faida kubwa kwake. Kwa mana hiyo kesho ataingia kwa nia ya kushambulia na kulinda lango lake kwa muda wote.
Simba na Ashanti wana malengo tafauti kabisa kwasababu Simba wanahitaji kulinda heshima, wakati Ashanti wanataka kukwepa kushuka daraja.
Mtumwa zaidi katika mechi hiyo ni Ashanti kwasababu pointi tatu zitaamua hatima yao,  wakati Simba kwao hata kama wakizikosa hakuna madhara ya kushuka daraja.
Hii itakuwa mechi nzuri ya kuifuatilia kwani soka la ushindani na maarifa linaweza kuonekana hasa kutoka kwa Kibadeni ambaye mzunguko wa kwanza alikuwa kocha mkuu wa Simba.
Kwa kiasi fulani Kibadeni anawafahamu wachezaji wa Simba na utamaduni wao, hivyo inaweza kuwa faida kwake.
Inadhihirika wazi kuwa kucheza na timu inayokwepa kushuka daraja, mechi inakuwa ngumu zaidi, kwasababu hiyo, Loga wa Simba sc lazima awe na mipango mizuri na asipoangalia anaweza kupoteza mechi hiyo.

TANZANIA PRISONS VS RHINO RANGERS

Wakati Ashanti wakiumiza kichwa kupata matokeo katika mechi hiyonya jumapili, nao Tanzania Prisons ambao ni washindani wao kukwepa kushuka daraja watakuwa na vibonde wa ligi hiyo, Rhino Rangers kutoka mkoani Tabora katika uwanja wa Sokoine jijini Mbeya siku ya kesho.
Pengine mechi hii itakuwa na unafuu kwa Prisons wanye machungu ya kufungwa mechi mbili zilizopita.
Walifungwa mabao 5-0 dhidi ya Yanga na wakafungwa mabao 21 na JKT Oljoro mjini Arusha. Sasa kesho wapo nyumbani kucheza na timu dhaifu ya Rhino Rangers.
Udhaifu unaosemwa hapa ni matokeo wayapatayo Rhino msimu huu, lakini si jinsi wanavyocheza.
Wanajeshi hawa JWTZ  wanacheza mpira mzuri, lakini katika mpira mshindi na mshindwa lazima atokee.
Kwa maana hiyo, Prisons wana kazi kubwa ya kuwafunga vibonde hawa walipo mkiani kwa pointi 16 baada ya kucheza mechi 24.
Mechi hii haina mvuto hata kwa mashabiki wa soka jijini Mbeya kutokana na matokeo waliyonayo Prisons na Rhino, lakini kwa watu wa mpira, hii ni mechi ambayo burudani kubwa inaweza kuonekana.
Prisons watashinikiza kushinda, wakati Rhino ambao wameshashuka daraja kwa asilimia zote watakuwa wanapambana angalau kushuka daraja na ushindi.

COASTAL UNION VS JKT RUVU

Mechi nyingine nzuri ya kesho ni baina ya Coastal Union dhidi ya JKT Ruvu katika uwanja wa CCM Mkwakwani jijini Tanga.
Coastal walipoteza mechi iliyopita kwa mabao 2-1 dhidi ya Mgambo katika uwanja wa Mkwakwani, wakati JKT Ruvu walipoteza kwa mabao 5-1 kutoka kwa mabingwa watetezi Yanga ndani ya uwanja wa Taifa.
Mtazamo wa mechi hii kwa timu zote mbili unatofautina kabisa.
JKT Ruvu wenye pointi 28 katika nafasi ya 9 baada ya kucheza mechi 24 watakuwa wanahitaji ushindi  ili kufikisha pointi 31 ambazo zitaweza kuwaokoa kushuka daraja.
Hata sare itakuwa na faida kubwa zaidi kwao, kwasababu watafikisha pointi 29 ambazo hazitaweza kufikiwa na Ashanti United na Prisons isipokuwa Mgambo waliopo nafasi ya 10 kwa pointi 25 huku wakiwa na michezo miwili mkononi.
Coastal Union wapo nafasi ya 8 kwa pointi 29 baada ya kucheza mechi 24. Nafasi hii si nzuri kwao kwasababu ya kikosi chao kuwa na wachezaji wa gharama.
Kikosi cha wagosi wa Kaya kilitabiriwa kufanya vizuri sana msimu huu, lakini wamegeuka kuwa `mbogo` kwani wanapoteza mechi mara kwa mara.
Kwahiyo mechi ya Mkwakwani itakuwa nzuri kwasababu timu zote zinahitaji ushindi ili kuendelea kujiweka mazingira mazuri zaidi katika msimamo.

Tafadhali endelea kuwa nasi na usisite kutoa maoni yako.


No comments:

Post a Comment