Search This Blog

Friday, April 11, 2014

TIMU YA WATOTO WA MITAANI YATAMBULISHWA BUNGENI, NAYE CHACHA KUCHEZESHA MICHUANO YA AYG!!

Timu ya Watoto wa Mitaani ya Tanzania iliyotwaa ubingwa wa Dunia wa Watoto wa Mitaani nchini Brazil baada ya kuifunga Burundi mabao 3-1 kwenye fainali imetambulishwa leo (Aprili 11 mwaka huu) katika Bunge Maalumu la Katiba mjini Dodoma.

Baadaye timu hiyo leo itapata chakula cha mchana na Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mizengo Pinda. Saa 10 jioni itatembeza kombe hilo katika maeneo mbalimbali ya Manispaa ya Dodoma katika gari za wazi.

Jioni imeandaliwa hafla maalumu ya chakula pamoja na burudani hapo hapo mjini Dodoma ambapo mgeni rasmi atakuwa Waziri wa Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo, Dk. Fenella Mukangara.

MWENYEKITI WA CECAFA KUZUNGUMZA NA WAANDISHI
Mwenyekiti wa Baraza la Vyama vya Mpira wa Miguu Afrika Mashariki na Kati (CECAFA), Leodegar Tenga atakuwa na mkutano na waandishi wa habari Jumatatu (Aprili 14 mwaka huu).

Mkutano huo utafanyika kwenye ofisi za Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) zilizopo Ghorofa ya 3, Jengo la PPF Tower mtaa wa Ohio/Garden Avenue kuanzia saa 5 kamili asubuhi.

CHACHA KUCHEZESHA MICHUANO YA AYG
Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika (CAF) limeteua mwamuzi msaidizi wa Tanzania anayetambuliwa na Shirikisho la Kimataifa la Mpira wa Miguu (FIFA), Ferdinand Chacha ameteuliwa kuchezesha michezo ya Vijana ya Afrika (AYG- African Youth Games).

Michezo hiyo ya kwanza ya Afrika itachezesha jijini Gaborone, Botswana kuanzia Mei 22-31 mwaka huu. Tanzania pia itashiriki katika mashindano hayo ya vijana wenye umri chini ya miaka 15.

BONIFACE WAMBURA
OFISA HABARI NA MAWASILIANO

SHIRIKISHO LA MPIRA WA MIGUU TANZANIA (TFF)

1 comment:

  1. wakati hao madogo wanaungaunga kwenda kwenye michuano TFF ilikuwa na mchango gani kwao!!??..waache kujitia viherehere... UNAFKI ULIOPITILIZA

    ReplyDelete