Search This Blog

Friday, April 11, 2014

MBEYA CITY MSIKUBALI KUPOTEZA MABOYA KWA MANENO YA MTAANI, ENDELEENI NA MAMBO YENU KUWAWINDA AZAM FC!!

Na Baraka Mpenja, Dar Es Salaam

0712461976

HAKUNA uchawi katika mpira wa miguu zaidi ya maandalizi ya timu na soka ni mchezo unaochezwa hadharani na matokoe hupatikana kutokana na ubora wa timu moja dhidi ya timu nyingine.
Ubora ninaousemea hapa ni kuwa na uwezo wa kutumia kila nafasi unayoipata ndani ya uwanjani na kuibadili kuwa goli.
Kuna wakati timu  bora inaweza kupoteza mechi mbele ya timu yenye udhaifu mkubwa katika kikosi chake.
Kuna maneno mengi yanayoendelea kwa wadau wa soa kuwa zipo timu ambazo hucheza mechi mara mbili, kwa maana ya nje ya uwanja na ndani ya uwanja.
Binafsi imani yangu imejengwa katika soka la ndani ya uwanja. Hii michezo michafu ya nje ya  uwanja, naamini ni kuua soka la nchi.
Mshindi wa mechi lazima apatikane hadharani kwa kuonesha kiwango bora na mipango mizuri ya uwanjani.
Makocha wanafanya kazi muda mwingi kuwafua vijana wao. Huwa wanawapa mbinu mbalimbali za kuwafunga wapinzani..
Kwa maana hiyo, kama Simba wanajiandaa kucheza na Yanga, nao Yanga wanajiandaa kucheza na Simba.
Kama Yanga wanamuomba Mungu wawafunge Simba, nao wekundu wa Msimbazi wanamuomba Mungu wawafunge Yanga.
Nasikia kuna watu wanapiga dua za kusaidia timu zipate matokeo mazuri. Ni ngumu kujua hizo dua zinaelekezwa kwa Mungu yupi, kwasababu kuna Mungu na Miungu.
Kama wanapiga dua kwa miungu au waganga wa kienyeji, ni juu yao kwani hiyo ni sayansi inayoaminiwa na baadhi ya watu, lakini huwezi kuiona kwa macho ya kawaida.
Endapo mpira ni uchawi na maombi, basi watu wanaosifika kwa uchawi na maombi wangekuwa na timu nzuri kuliko zote duniani.
Kuna maeneo hapa nchini yanasifiwa kwa uchawi, lakini hakuna soka hata kidogo na kuna timu za kubabaisha tu.
Kwasababu hiyo, nashindwa kuamini sayansi hii ya uchawi katika soka.
Lakini suala la michezo michafu ya nje ya uwanja,  kwa maana ya kuhonga wachezaji, makocha na viongozi wa timu pinzani, naweza kuamini kuwa kuna baadhi ya watu wanafanya biashara hiyo.
Imani yangu inajengwa kulingana na mazingira ya soka letu kwasababu zipo changamoto nyingi kuanzia uendeshaji wa ligi na klabu kwa ujumla.
Viongozi wa soka si wepesi wa kufanya tafiti pale `figisu figisu` za rushwa zinaposemwa na watu.
Nilishawahi kuandika na kulaani vikali tabia ya kula hongo ili kupanga matokeo.
Sababu yangu ilikuwa moja tu, ambayo ni kurudisha maendeleao ya soka letu kitaifa na kimataifa.
Hakuna maana ya kupeleka timu katika mashindano makubwa wakati ubingwa wake imeupata kwa kuhonga timu pinzani.
Hapa katika rushwa,  wanahusishwa watu wengi sana, hata waamuzi ni watuhumiwa wakubwa wa suala hili.
Lakini nasisitiza kuwa suala la rushwa ni gumu kulijua katika hali ya kawaida kwasababu huwa linafanyika kwa siri kubwa mno.
Labda wahusika wenyewe wavujishe taarifa hizo, au wawepo watu makini wa kufuatilia suala hilo.
Watu wanawasiliana kwa mawasiliano yao binafsi na hawakutani ana kwa ana. Labda ugague mawasiliano yao kwa kushirikisha mitandao wanayotumia ili uwabaini.
Ili kuyafanya haya, lazima uwe umejipanga na kuwa na nia ya dhati.
Kwa utaratibu  wetu wa kupotezea mambo muhimu kama haya, kila mtu anasikia na kuliacha kama lilivyo kwa kutumia maneno mepesi kuwa ni uvumi tu.
Uvumi ni msimgi wa kufuatilia ukweli. Unaposikia watu wanasema jambo fulani baya, kama ni mtu mwenye dhamana jipange kufuatilia.
Nimesikitishwa sana na taarifa ya Jana ya Mbeya City kwa vyombo vya habari ambayo ilikuwa inahusu kukanusha kwa tuhuma nzito juu yao kwamba wamehongwa na Azam fc  ili wafungwe mchezo wa jumapili na kuwapa ubingwa wana Lambalamba hao.
Tuhuma hizi zinahusu mambo makubwa matatu ambayo ni kuahidiwa kununuliwa basin a klabu na Azam fc, kocha Juma Mwambusi kujengewa nyumba chamazi na wachezaji wa Mbeya City kuhongwa pesa ili wacheze chini ya kiwango.
Kila mtu anafahamu kuwa Mbeya City wameleta changamoto kubwa katika soka la Tanzania kwasasa.
Mipango yao, juhudi zao zimewafikisha hatua waliyopo sasa tofauti na timu nyingine walizopanda nazo ligi kuu.
Ni moja ya timu inayosifiwa kucheza kitimu na ukiwa uwanjani utagundua kirahisi kuwa timu hii inacheza kwa kuhitaji kitu fulani.
Wachezaji ni wapambanaji ndani ya dakika zote na yanapotokea matokeo mengine mabaya kwao ni suala la kimpira.
Ukija upande wa Azam fc ni dhahiri kuwa wamekuwa bora zaidi msimu huu kwasababu wamecheza mechi 24 bila kufungwa.
Si kazi nyepesi kufikia mafanikio hayo, lakini kwanini mechi na Mbeya City watuhumiwe kucheza mchezo mchafu?.
Kama ndio njia yao ya kupata matokeo, je, wamefanya hivyo kwa mechi zote 24 ambazo hawajafungwa?.
Kwa akili ya kawaida, si rahisi kuhonga katika mechi 24, bali ni mipango mizuri na maandalizi yao.
Hivi soka la Azam fc katika mechi hizo 24 ni baya?. Hapana!, wamecheza vizuri sana na kuwa makini na nafasi wanazopata.
Kwa aina ya wachezaji walionao, nadhani wanastahili kuwa hapo walipo na si haya yanayosemwa.
Sikatai kama hawawezi kufanya hivyo, lakini sidhani kama kuna mtu yeyote anayeweza kutoa ushahidi wa moja kwa moja kama kweli Azam fc wanahonga.
Kama yupo atufahamishe na wengine tusiojua jambo hilo na pengine inaweza ikawa msingi mzuri wa kulitatua suala hili.
Ukifautilia kwa makini maneno ya Mbeya City, utagundua kuwa wamejenga hoja zao kwa kusikia maneno ya watu na mitandao ya kijamii.
Maneno wasemayo watu si sababu ya kuamini kama jambo fulani lipo, cha msingi uyatumie kutafuta ukweli hata kwa kutafiti kwa muda mfupi.
Mitandao ya kijamii ndio chanzo kibovu zaidi kwasababu waliowengi wanaandika na kuchapisha habari kwa wafikiriavyo  bila kujali kama kuna ukweli au la.
Hakuna wahiriri mbali na mwenye mtandao au akaunti yake. Sasa unajengaje hoja yako  kwa kusoma maneno ya facebook, Twita na mtandano mingine?.
Lakini usinielewe vibaya, ipo mitandao ambayo inafanya kazi nzuri ya kuwahabarisha watu taarifa za ukweli.
Cha msingi , lazima uwe makini kuangalia kwa kina ili ujue ukweli wa taarifa na chanzo chake.
Kwa mtazamo wangu, ni kweli mechi ya jumapili ni ngumu kwa timu zote mbili.
Azam fc wanahitaji matokeo ambayo yanaweza kuamua ubingwa mwaka huu.
Wanaweza kupata matokeo ya ushindi kama watakuwa na mipango mizuri ya uwanjani.
Wana wachezaji ambao wanaweza kuwapata matokeo mazuri ndani ya dakika 90.
Watu kama Aishi Manula, Erasto Nyoni, Gadiel Michael, Agrey Moris, David Mwantika, Michael Bolou, Himid Mao,Salum Abubakar `Sure Boy` Guadence Mwaikimba, John Bocco, Kipre Tchetche na wengineo, wanashindwaje kuwapa matokeo bila hata kuhonga?.
Nadhani wana kikosi kizuri ambacho kinaweza kiifunga Mbeya City yenye watu muhimu kama Hassan Mwasapili, Deogratius Julias, Yohana Moris, Steven Mazanda, Paul Nonga, Mwegane Yeya na wengine wengi wanye vipaji vya juu.
Timu zote mbili zina wachezaji wazuri, hivyo kila klabu inaweza kushinda mchezo huo ndani ya uwanja.
Mbeya City kushinda ni haki yao na Azam fc wana haki kama hiyo hata bila kuhonga.
Cha kuwashauri Mbeya City, waachane na maneno ya mitaani kwani hayana msingi wowote.
Bila shaka hata mtu aliyeanzisha propaganda hizo hawamjui pamoja na malengo yake.
Inawezekana ni kutaka kuwatoa mchezoni  ili waingie kwa presha kubwa kuhofia kupoteza mechi.
Manake wakifungwa watawafanya watu waamini kuwa kweli wamehongwa.
 Ili kucheza mechi hiyo kwa ufanisi wanatakiwa kuendelea na mambo yao.
Azam fc wanaendelea na mambo yao ya maandalizi, nao Mbeya City waendelee na maandilizi yao.
Waachane na maneno haya yasiyo na kichwa wala miguu.
 Lakini kama wana ushahidi wa hayo na mtu aliyesema wafike katika vyombo husika.
Hakuna sheria inayosema lazima Yanga, Simba lazima wachukue ubingwa. Na ndio maana timu kama Coastal Union, Tukuyu Stars, Mtibwa Sugar ziliwahi kutwaa ubingwa mbele ya Simba na Yanga.
Kwanini Azam fc wasemwe  kuwa wanahonga, kwani hawana haki ya kuchukua ubingwa?.
Tupunguzeni maneno yasiyokuwa na msingi katika soka.
Kila la kheri Azam fc na Mbeya City katika mchezo wenu wa jumapili uwanja wa Sokoine jijini Mbeya.

1 comment:

  1. wanaovumisha ni watu wa yanga wao wakishinda saba tano uwezo wakifungwa wamehujumiwa tubadilike

    ReplyDelete