Search This Blog

Saturday, April 5, 2014

KUTUHUMU WACHEZAJI KULA RUSHWA HUWAONDOA MCHEZONI, MASHABIKI YANGA WAWE WATULIVU KUTETEA UBINGWA WAO!!


Na Baraka Mpenja, Dar es salaam


KIPIGO walichokipata Yanga sc kutoka kwa Mgambo JKT machi 30 mwaka huu kwenye uwanja wa CCM Mkwakwani, jijini Tanga kimezidi kuwavuruga zaidi viongozi, makocha, na mashabiki wa klabu hiyo.
Imeonekana kuwa ajabu kwa Mgambo JKT kuwafunga Yanga, wakati mpira wa miguu huwa una matokeo ya aina hiyo.
Katika mechi, wachezaji 22 wanapambana kwa maana ya wachezaji 11 kwa kila timu.
Kama wachezaji wanakuwa sawa kwa timu zote kwa mujibu wa sheria, basi kushinda ni haki kwa timu yoyote.
Lakini kuna wakati timu moja inaweza kujipa matumaini zaidi ya kushinda mechi na kusahau kuwa inaenda kucheza na watu waliojiandaa kama wao.
Hakuna ubishi, kupata matokeo kunatokana na mipango mizuri ya uwanjani na nje ya uwanja.
Viongozi wa timu wana wajibu mkubwa kwa nafasi yao kuhakikisha kila kitu kinaenda sawa, mfano; kuhudumia kambi ya wachezaji.
Inapofika muda wa uwanjani, makocha pekee na wachezaji ndio wenye wajibu wa kulipa fadhili za viongozi wao na mashabiki waliopo nyuma yao.
Kutokana na ubora wa Yanga katika kikosi chao, mashabiki wake waliamini Mgambo lazima wale kipigo kikali jijini Tanga.
Ikimbukwe kabla ya mechi hiyo, Yanga walitoka kushinda mabao 5-0 dhidi ya Tanzania Prisons.
Kwa tafsiri hiyo, safu ya ushambuliaji ya Yanga ilionekana kuwa na uchu mkubwa wa kufumania nyavu, hivyo watu wengi walitegema kuona karamu nyingine ya mabao dhidi ya timu ya Mgambo inayoonekana kuwa dhaifu msimu huu.
Kwa watu wanaojua mpira, kama hawakuthubutu kusema Yanga wana asilimia zote kushinda mechi ile, bali waliwapa asilimia nyingi ya kupata matokeo mazuri zaidi ya Mgambo.
Kuipa timu asilimia kubwa ya ushindi kwasababu ya ubora wa kikosi, ni suala la kawaida sana hata huko duniani.
Ndio maana Manchester United walitaniwa kuwa wanaenda kupambana na Bayern Munich yenye kazi nyepesi ya kuvuna ushindi.
Wengine walisema ni vita ya Daudi na Goliathi, lakini wakasahau kuwa mpira wa miguu una matokeo ya aina yake.
Man United walikuwa na haki ya kupata matokeo yale, hata kama Bayern ni bora zaidi yao kwa sasa.
Haimaanishi timu fulani kuwa na kikosi dhaifu, basi haina haki ya kushinda. Soka la uwanjani linahitaji mipango. Ukipata nafasi tumia.
Mgambo JKT walikuwa na haki ya kushinda licha ya kucheza pungufu kwa dakika 60 baada ya mchezaji wao Mohamed  Hussein Neto kuoneshwa kadi nyekundu.
Walionekana kukomaa zaidi na kuwa na mipango mizuri na ndio maana waliweza kuwafunga Yanga.
Kinachoonekana kwa baadhi ya mashabiki wa Yanga ni kuamini timu yao ina haki ya kushinda katika kila mechi kwasababu ya  ubora wa kikosi chao.
Lakini mpira huwa hauendi hivyo, kufungwa kupo hata kama una ubora mkubwa.
Mara ngapi timu ndogo zinapata matokeo mbele ya timu kubwa?. Mpira huwa hauna fomula ya kushinda mechi zote.
Kipigo cha Mgambo kimezidi kuibua mengi. Mojawapo ni tuhuma za baadhi ya wachezaji kula rushwa kupoteza mchezo.
Si rahisi kubaini kama kweli wanaotuhumiwa walikuwa rushwa,  kwasabau jambo hili hufanyika kwa siri na ushahidi unahitajika unapolisema.
Kuna wakati Azam fc walijiingiza mkenge wa kuwatuhumu kula rushwa Erasto Nyoni,  Said Morad na Aggrey Morris na kusababisha timu kufungwa.
Watu wa mpira wanakumbuka  kesi hii ilifikishwa mpaka taasisi ya kuzuia na kupambana na rushwa (TAKUKURU), lakini baadaye ushahidi ulikosekana na kuwaachia huru.
Azam fc walijikuta wakipoteza muda mwingi na kuigharimu timu bila sababu yoyote ya msingi.
Kuwatuhumu wachezaji kula rushwa imekuwa tamaduni ya Simba na Yanga, lakini msimu huu viongozi wa Yanga wameonekana kuwa makini na kukanusha kila inapotokea taarifa kama hizi.
Wengine wamekuwa wakiandika na kusema mitaani kuwa baadhi wa wachezaji wa Yanga ambao ni Athumani Idd `Chuji` , Kelvin Yondani na Juma Kaseja wamesimamishwa kwasababu ya tuhuma za kuhujumu timu kwenye mechi dhidi ya Mgambo.
Duru za habari kutoka Yanga zimesema kuwa uongozi wa klabu hiyo unasikitishwa na taarifa zinazotolewa na baadhi ya vyombo vya Habari tangu siku ya jumatano kwamba wachezaji  Kaseja, Yondani,  na "Chuji" wamefukuzwa kwenye timu na Emmanuel Okwi ameondoka kurejea kwao nchini Uganda.
Yanga wamesema taarifa hizi ni uongo mtupu, na zina lengo la kuwagawa wachezaji.
“Hakuna mchezaji yoyote aliyefukuzwa kwenye timu baada ya kupoteza mchezo dhidi ya Mgambo Shooting mwishoni mwa wiki, taarifa hizo zinasambazwa kwa Propaganda ili kuweza kuvunja umoja uliopo ndani ya timu kwa wachezaji na walimu,  pia kwa Viongozi na wanachama”. Ilisema taarifa ya Yanga.
Taarifa hiyo ilizidi kufafanua kuwa Kelvin Yondani hakuungana na wenzake kambini baada ya kuomba kupumzika na kutatua matatizo yake ya kifamilia.
Benchi la Ufundi lilimpa ruhusa hiyo kwa kuzingatia mchezaji mwenyewe asingeweza kutumika kwa mchezo wa jumapili dhidi ya JKT Ruvu kufuatia kuwa na kadi tatu za njano, lakini ataungana na wenzake mara baada tu ya mchezo huo.
Pia Athumani Idd "Chuji", David Luhende pamoja na kiungo Haruna Niyonzima ni wagonjwa, wanaendelea na matibabu kuhakikisha wanakua `fiti` na kuungana na wachezaji wao mara baada ya mchezo wa siku ya jumapili.
Aidha taarifa hiyo ilisema kuwa Juma Kaseja yupo kambini pamoja na mlinda mlango Deo Munish "Dida" aliyekua majeruhi kwa takribani wiki tatu kufuatia kupata jeraha katika mkono wakati timu ikijiandaa na mchezo dhidi ya Mtibwa Sugar.
Pia Emmauel Okwi yupo jijini Dar es salaam akiendelea na matibabu kufuatia kutonesha goti katika mchezo dhidi ya Mgambo mwishoni mwa wiki, awali Okwi aliiumia katika mchezo dhidi ya Prisons na kutolewa nje na machela.
Kimsingi viongozi wa Yanga wanapokanusha taarifa hizi, unaweza kugundua kuwa wanaelewa kuwa soka huwa lina matokeo kama waliyopata kule Tanga.
Kuwatuhumu wachezaji kunawafanya wawe na msongo wa mawazo na kubeba mzigo mzito kichwani.
Ufanisi wao unapungua wanapokuwa uwanjani, kwasababu wanacheza kuogopa kukosea.
Kama ni mshambuliaji anaweza kuogopa kujaribu kupiga mashuti kwa hofu ya kukosa bao na kutuhumiwa kula rushwa.
Kama ni mlinda mlango anashindwa kujiamini akiwa langoni, na ikitokea akafungwa bao, basi anajivuruga zaidi.
Si wakati muafaka kwa wanayanga kuanza kutuhumiana kwa mambo ya rushwa ikizingatiwa wana kibarua kizito kuteteta ubingwa wao.
Wanapolumbana muda huu na kuwasema vibaya wachezaji wao, wanaingiza balaa katika kikosi chao.
Mbele yao wapo Azam fc waliopo katika hali tulivu zaidi. Kuwang`oa kileleni umakini mkubwa na jitihada  vinahitajika.
Yanga wakubali matokeo ya uwanjani na wajiandae kufungwa kwani mpira ndivyo ulivyo.
Hawana haki ya kushinda tu, hata kupoteza pia.  Hivyo lazima wajifunze kuwa watulivu wanapoharibu ili kujipanga kwa mchezo mwingine.
Kutuhumiana kwa mambo ya rushwa si wakati wake kwasasa.

4 comments:

  1. Siku chache zilizopita nilisema katika blog hii Yanga wamebakiza mechi ngumu moja tu dhidi ya Mgambo JKT,lakini kama kawaida ya watu wasiojua mpira wakaanza kutoa matusi kwa nini sikuitaja mechi ya Yanga na Simba SC.Nafikiri sasa wameelewa

    ReplyDelete
    Replies
    1. Mi ni moja kati ya waliokupinga ingawa sijatukana na bado nitaendelea kukupinga km bado utaendelea na mcmamo wako huo kua Yanga amemaliza mechi ngumu ama niseme kua mechi ya Yanga dhidi ya Simba uiite nyepec si kweli ingawa naamini kukuambia kwann c nyepec ni kupoteza muda ila tuombe uzima Mungu atufikishe hiyo 19 April uone watu wanavyohangaika nje na ndani us uwanja tena kabla na baada ya mchezo nadhani litakua jibu toshelezi kwako!!@Anonymous 6:00 Am

      Delete
  2. Shafi waambie waandishi uchwara wenzako waliozua huo ujinga. Yanga tumetulia na tunasonga mbele. Mnachanganyana wenyewe waandishi vihio.

    ReplyDelete
  3. kiufundi mechi ya Yanga na Mgambo JKT ilkuwa ngumu.Kishabiki mechi ya Yanga na Simba inaweza kuwa ngumu

    ReplyDelete