Search This Blog

Saturday, March 22, 2014

PRISONS YATEMA MKWARA KWA YANGA, WADAI MOTO WAO HAUZIMWI KWA PETROLI!!


Na Baraka Mpenja , Dar es salaam


MAAFANDE wa Jeshi la Magereza, Tanzania Prisons Maarufu  kwa jina la `Wajelajela` wamejichimbia mjini Morogoro kujiandaa na mechi yao ya  machi 26 mwaka huu katika dimba la Taifa jijini Dar es salaam dhidi ya mabingwa watetezi wa ligi kuu soka Tanzania bara, Young African.
Katibu mkuu wa Prisons, Inspekta Sadick Jumbe amesema kuwa sababu ya kukaa Morogoro  kwa muda mrefu ni kutafuta mbinu mpya za kuwafunga Yanga wanaosifika kuwa na kikosi bora zaidi msimu huu.
“Jumatatu tunaondoka Morogoro kuja Dar es salaam, jumatano tunacheza na Yanga. Maandalizi yapo vizuri kabisa na tunakuja kufanya maajabu”. Alisema Jumbe.
Aidha aliongeza kuwa mechi iliyopita dhidi ya Kagera Sugar katika dimba la Kaitaba, mwamuzi aliwapendelea zaidi wenyeji wao.
“Tulifungwa 2-1. Lakini hatukufungwa na Kagera sugar. Tulifungwa na mwamuzi. Nawaomba TFF wawe makini katika upangaji wa marefa na kufuatilia maamuzi yao”. Alisema Jumbe.
Kueleka katika mchezo huo, Jumbe alisema Yanga ni wagumu zaidi wanapokuwa uwanja wa Taifa, lakini mzunguko huu wa pili Prisons wamekuwa bora zaidi.
“David Mwamwaja ni kocha mwenye historia nzuri. Baada ya kuchukua kikosi chetu kimekuwa bora zaidi. Sema kuna wakati waamuzi wanatuangusha kabisa. Kaitaba tulinyongwa sana”. Alisisitiza Jumbe.
Katibu huyo alisema moto wao ni mkali na kamwe hauzimwi kwa petrol, hivyo Yanga hata kama watakuwa uwanja wa Taifa, watahenyeshwa mwanzo hadi mwisho wa mechi.
“Tupo nafasi ya 10 kwa pointi 22 na tuna mchezo mkononi. Tunazitaka sana pointi tatu kutoka kwa Yanga. Hakika hatoki mtu na kipigo Taifa. Lazima kieleweke tu”. Alitamba Jumbe.
Mzunguko huu wa pili Prisons wameonekana kudhamiria kubakia ligi kuu kwani wamekuwa wakifanya vizuri zaidi.
Katika mechi ya mzunguko wa kwanza na Yanga uwanja wa Sokoine jijini Mbeya, timu hizo zilitoka suluhu ya bila kufungana,
Yanga wapo katika harakati za kutetea ubingwa wao msimu huu, wakati Prisons wanahitaji pointi ili kujinusuru kushuka daraja.
Kutokana na mazingira hayo, mechi hiyo ya jumatano wiki ijayo, itakuwa na changamoto kubwa kwa timu zote.
Matokeo ya ushindi yatakuwa na faida kubwa kwa Yanga, wakati huo huo kama Prisons watashinda, watazidi kujisafishia njia ya kubakika ligi kuu.

No comments:

Post a Comment