Search This Blog

Saturday, March 22, 2014

TABORA KWAWAKA MOTO, YANGA WATAMBA KUWAZIMA RHINO, MINZIRO AWAHOFIA MBEYA CITY LEO CHAMAZI!!


Na Baraka Mpenja , Dar es salaam


MABINGWA watetezi wa ligi kuu soka Tanzania bara, Young African  kwa mara nyingine leo jioni wanachanga karata zao katika uwanja wa Ally Hassan Mwinyi, Mjini Tabora dhidi ya wenyeji wao Rhino Rangers.
Viingilio katika mechi hiyo muhimu kwa timu zote mbili ni sh. 5,000 kwa jukwaa kuu na sh. 3,000 mzunguko.
Afisa habari wa Yanga, Baraka Kizuguto amezungumza kwa njia ya simu na mtandao huu kutoka Tabora na kueleza kuwa kikosi kipo salama na jana jioni kilifanya mazoezi tayari kwa kuwavaa Rhino  leo hii.
“Hakuna majeruhi mpaka sasa. Wachezaji wote wapo katika morali nzuri. Kwetu sisi michezo yote ni muhimu, tunajitahidi kufanya vizuri ili tuweze kutetea ubingwa wetu”. Alisema Kizuguto kutoka Tabora.
Kizuguto aliwataka mashabiki wa klabu hiyo kujitokeza katika mchezo wa leo kuiangalia timu yao katika mchezo wa tatu tangu watolewe katika michuano ya ligi ya mabingwa barani Afrika.
Yanga wanahitaji pointi tatu ili kurudisha hadhi yao ya kutetea ubingwa wao kwasababu si kazi nyepesi kuwachomoa Azam fc waliopo kileleni.
Mpaka sasa Yanga wamejikusanyia pointi 40 baada ya kushuka dimbani mara 19, wakati Azam fc wamecheza mechi 20 wakijikusanyia pointi 44 kileleni.
Mpaka sasa Azam fc wanabakia kuwa timu bora kwasababu hawajapoteza mchezo wowote ligi kuu.
Yanga walitolewa ligi ya mabingwa na Al Ahly kwa penati 4-3 jijini Alexndria nchini Misri machi 9 mwaka huu, na baada ya kurejea ligi kuu hawajashinda mchezo hata mmoja.
Walitoka suluhu na Mtibwa Sugar uwanja wa Jamhuri mjini Morogoro, na katikati ya wiki walitoka sare ya 1-1 dhidi ya Azam fc.
Kwa vyovyote vile hawana cha kupoteza leo hii zaidi ya kutafuta ushindi ili kurudisha imani yao kwa mashabiki.
Itakuwa kazi kwa kocha mkuu, Mholanzi Hans Van Der Pluijm kutuliza akili yake kuwapanga vijana wake ili kuwalowesha Rhino nyumbani kwao.
Rhino kwa upande wao wanaonekana kukata tamaa kubaki ligi kuu kwasababu mpaka sasa wamebakiwa na mechi 5 tu ikiwemo ya leo.
Katika mechi 21 walizocheza, wameambulia pointi 13 tu na wanaburuza mkia mpaka sasa.
Kocha mkuu wa klabu hiyo, Jumanne Chale alisema wanajipanga kuibuka na ushindi katika mechi zote zilizosalia wakianzia na Yanga.
“Tumefanya vibaya na kujichimbia kaburi. Lakini mpira una matokeo ya ajabu. Tunaweza kushinda mechi zote na kujinusuru”. Alisema Chale.
Hata hivyo alionesha kuzungumza hayo akiwa hana matumaini kwasababu mechi alizosaliwa nazo ni ngumu zaidi kuanzia ya leo dhidi ya Yanga. 
Mbali na mchezo huo wa Tabora, nayo JKT Ruvu itakuwa mwenyeji wa Mbeya City katika mechi itakayochezwa leo, Uwanja wa Azam Complex uliopo Chamazi, Dar es Salaam kuanzia saa 10 kamili jioni.
Kocha msaidizi wa Mbeya City, Maka Mwalwisyi ameuambia mtandao huu kuwa kikosi chao kipo salama isipokuwa mchezaji Richard Peter aliyepata majeruhi katika mchezo uliopita dhidi ya Rhino Rangers uwanja wa sokoine jijini Mbeya.
“Timu zote zinacheza kwa mitazamo miwili. Kuna timu zinahitaji ubingwa, kuna timu zinataka kukwepa kushuka daraja. Kwasababu hizi ushindani umekuwa mkubwa. Sisi tunafurahi kuona ushindani mkubwa ili bingwa apatikane kwa halali”.
“Tunawaheshimu JKT Ruvu, wapo katika wakati mgumu kwasasa. Tumejipanga kushindana na kuvuna pointi tatu muhimu”. Alisema Maka.
Maka aliwataka mashabiki wao kujitokeza kwa wingi Chamazi kwani kushinda leo kutawapa nguvu zaidi ya kujikita nafasi za juu.
Naye kocha wa JKT Ruvu, Fredy Felix Minziro alisema Mbeya City ni wazuri zaidi, hivyo wanakabiliwa na mechi ngumu zaidi.
“sisi tunahitaji pointi tatu, Mbeya City wanahitaji pointi tatu. Tunajua wazi kuwa wapinzani wetu ni wazuri, lakini kikosi chetu kipo katika hali nzuri na tunajipanga kuibuka na ushindi”. Alisema Minziro.
Ligi hiyo itaendelea keshokutwa (Jumapili) kwa mechi nne ambapo Simba itacheza na Coastal Union katika Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam. Azam itaoneshana kazi na Oljoro JKT kwenye Uwanja wa Azam Complex. Mechi hizo mbili zitakuwa ‘live’ kupitia Azam Tv.
 Mechi nyingine za Jumapili ni Mgambo Shooting dhidi ya Mtibwa Sugar kwenye Uwanja wa Mkwakwani jijini Tanga, wakati Ruvu Shooting na Ashanti United zitapimana ubavu kwenye Uwanja wa Mabatini, Mlandizi mkoani Pwani.

No comments:

Post a Comment