Search This Blog

Wednesday, March 5, 2014

NIONAVYO MIMI: KUNA MUDA TUNAMUONEA BURE JAMAL MALINZI


Na Oscar Oscar Jr.
0789-784858

Utani wa mashabiki wa Simba na Yanga kwenye mechi za wao kwa wao au mmoja dhidi ya timu nyingine kutoka nje ya nchi kuna muda naupenda na naona faida yake ingawa,kuna muda unakosa maana. Ukiona mashabiki wa Simba wanaiponda Yanga,maana yake ni kwamba,wanawafanya Yanga waendelee kufanya vizuri kwa kukwepa kuzongwa na mashabiki hao wa Msimbazi na kinyume chake, ushabiki wa namna hii, binafsi naupenda. Sina tatizo kabisa siku nitakapokutana na habari kuwa mwenyekiti Ismail Aden Rage ameamua kuwauzia Yanga mshambuliaji wake Amis Tambwe huku, Yussuph Manji naye akiwauzia watani zake hao kiungo, Haruna Niyonzima. 

Kitendo cha kung'oa viti kilichotokea uwanja wa Taifa kwenye mchezo wa timu ya Yanga dhidi ya mabingwa watetezi wa kombe la klabu bingwa Afrika timu ya National Al Ahly toka nchini Misri si cha kiungwana na wala si cha kistaarabu kabisa. Tukio hilo sio mara ya kwanza kutokea, iliwahi pia kutokea kwenye mchezo wa ligi kuu kati ya timu ya simba dhidi ya Kagera Sugar mzunguko wa kwanza msimu huu baada ya mashabiki wa simba kuonekana kutoridhika na maamuzi ya mwamuzi wa mchezo huo. Mashabiki hao walionyesha hasira zao kwa kung'oa viti na kuvitupa chini! Nadhani kuna haja ya kulitazama swala hili upya huku kipaumbele kikiwa ni kupeana elimu na kuepuka kunyoosheana vidole.

Tutakuwa tunamuonea bure Rais wa TFF Jamal Malinzi kama hadi suala la ulinzi wa viti uwanjani tunahitaji yeye ndiye asimamie. Ni muda muafaka sasa kwa viongozi wa klabu zetu zote nchini kukaa chini na mashabiki na wanachama wao na kuwaelimisha juu ya umuhimu wa kutunza miundombinu ya viwanja vyetu hasa, ule wa taifa uliopo jijini Dar es salaam. Tukiendelea kunyoosheana vidole huku hawa wakisema wanaong'oa viti ni mashabiki wa Simba na wale, wakisema ni mashabiki wa Yanga, tutajikuta uwanja wote hauna kiti hata kimoja na hakuna wakumuuliza!

Lakini pia, mashabiki wa Simba na Yanga ni lazima watambue kwamba pamoja na kuwa uwanja huo wa Taifa umejengwa jijini Dar es salaam haina maana kuwa wananchi wanaoishi katika jiji hilo ndiyo wamiliki wa uwanja huo. Mashabiki wachache wanaoharibu miundombinu ya uwanja huo ni lazima watambue kuwa hawawatendei haki wananchi waishio Mwanza, Tabora, Singida, Kigoma, Songea na sehemu mbalimbali za Jamhuri ya muungano wa Tanzania kwa sababu na wao wamechangia kupatikana kwa uwanja huo kupitia kodi mbalimbali wanazolipa serikalini.

Kwenda kuangalia mpira uwanjani ni mtoko kama wanavyotoka watu na familia zao kwenda kwenye majumba ya sinema,kwenda Bar, kuna watu wanakwenda kutembelea mbuga za wanyama na kwenye vivutio mbalimbali. Mashabiki wa klabu ya Arsenal wa jijini London Uingereza huwa wanafurika kuanzia asubuhi maeneo ya starehe yanayozunguka uwanja wao wa Emirates kila siku timu hiyo inapokuwa na mechi hata kama mchezo huo utafanyika saa 1 jioni, wanashinda nje ya uwanja huo wakistarehe na familia zao mpaka muda wa mechi unapofika.

Uwanja wa Ali Hassan Mwinyi-Tabora, Kumbukumbu ya Sokoine-Mbeya na Jamhuri-Dodoma ni baadhi ya viwanja ambavyo nimewahi kuvitembelea na kuangalia mechi mbalimbali lakini kwa utafiti wangu mdogo, nimegundua wanaume ndiyo wengi wanaokwenda kutazama mpira uwanjani. Ukijiuliza kwa nini wanawake,watoto na wazee hawaendi viwanjani,jibu ni rahisi tu. Hivi ni nani atakwenda na mwanae uwanjani wakati timu moja ikifungwa, mashabiki wa timu pinzani wanarusha mawe na makopo ya haja ndogo? Ni nani atakwenda uwanjani na bibi yake wakati kuna muda mabomu ya machozi yanatumika kuwatuliza mashabiki wang'oa viti?

Moja kati ya sababu zinazotajwa kusababisha vurugu viwanjani ni pamoja na watu kutumia pombe hasa aina ya Viroba ambapo mashabiki wa timu kama Mbeya City wa jijini Mbeya wamegueza kama ndiyo utamaduni wao. Lakini najiuliza tena,mbona watu wengi wanakwenda na familia zao Bar kila mwisho wa wiki sehemu ambayo Viroba na vileo vingine viko "Full charge" na wanarudi nyumbani salama? au Viroba vya uwanjani ndiyo vikali zaidi? au kuna kaushamba fulani? au hatujui maana halisi ya mchezo wa soka? au tunamuhitaji Jamal Malinzi atuelekeze na hili?

Mechi ya Senegal dhidi ya Ivory Coast ambayo ilichezwa mwaka 2012 mjini Dakar kuwania kufuzu fainali za AFCON 2013 ililazimika kusitishwa kipindi cha pili baada ya mashabiki wa Senegal kuanza kung'oa viti na kutupa mawe uwanjani kufuatia Ivory Coast kuwa mbele kwa mbao 2-0.Matukio kama haya yaliyowahi kutokea kwa wenzetu ni lazima tujifunze na kuchukuwa hatua mapema za kuyadhibiti.Kazi ya kuwadhibiti hawa "mashabiki maandazi" sio ya Jamal Malinzi,ni jukumu la kila mdau wa soka bila kujali timu unayoshabikia.

Tukiamua,hatumuhitaji Malinzi wala askari polisi kutusaidia kuwadhibiti watu wachache wanaotaka kutufanya watanzania wote tuonekane hatuna maana.Kila mmoja akiwa mlinzi wa mwenzake ninaamini,huo utakuwa ulinzi wenye tija kuliko kitu chochote kile.Kama walevi wanaweza kuwadhibiti watu wachache ambao huwa wanawaletea vurugu wakati wao wakistarehe na wanafanikiwa,iweje sisi tunawachekea hawa wasio litakia mema soka la nchi yetu?

Ushabiki sugu kuna muda unakuwa kama ujinga.Mara kadhaa tumekuwa tukisikia kwenye vyombo vya habari mashabiki wameuwawa au wamejiuwa baada ya timu wanazoshabikia kutopata matokeo mazuri,huu ni upuuzi.Wakati wewe umejidhuru au kutuharibia miundombinu ya uwanja wetu,wachezaji walioshiriki kwenye mchezo huo baada ya dakika 90,wanabadilishana jezi na kukumbatiana! Hivi unadhani Yussuph Manji na Ismail Aden Rage hawasemeshani? hahahaa...utakuwa bado unaishi zama za mawe!

Rais wa TFF bado anakazi kubwa sana ya kuufikisha mpira wa Tanzania mahali ambapo watu wengi wanatamani tufikie.Watanzania wanatamani kuona klabu zetu zikifika mbali na kupata mafanikio kwenye michuano ya CECAFA na ile ya CAF ili tuweze kutengeneza timu bora ya taifa na yenye ushindani kwenye michuano mbalimbali kama vile ile ya kufuzu CHAN,AFCON na ikiwezekana,hata kombe la dunia pia tunalitaka lakini,kama hadi ulinzi wa viti uwanjani tunamtaka Jamal Malinzi asimamie,atamaliza muda wake hajafanya lolote na tusimlaumu kabisa.

2 comments:

  1. Malinzi anahusika moja kwa moja na kushindwa kudhibiti vurugu za mashabiki kwa kushirikiana na jeshila polisi.Polisi wanatakiwa kuangalia wanaofanya fujo jukwaani na sio kuwa watazamaji mpira waliolipa viingilio.Mimi nilifikiri kazi ya polisi ilikuwa ni kwenda jukwaani kuwakamata washabiki waliokuwa wanang'oa viti kwani iljulikana walikuwa wamekaa upande gani lakini badala kwenda upande ambao washabiki walikuwa wanarusha viti wao wakaenda upande wa washabiki waliokuwa wanarushiwa viti ili kuwadhibiti na kuwafukuza.Wakati wa vurugu hizi sikuona hata kiongozi mmoja waTFF akihangaika kutuliza washabiki badala yake ni viongozi wa Yanga na Jeshila polisi ndio waliokuwa wanahangaika kuwatuliza washabiki hao.Malinzi aliahidi kuleta mabadiliko kwenye uendeshaji wa soka lakini hakuna jipya analofanya zaidi ya ubabaishaji.Namshauri aunde Kamati ya Usalama viwanjani na aweke watu makini wa kumshauri badala ya hawa makomandoo wa Simba na Yanga anaowakumbatia bila sababu za wazi

    ReplyDelete
  2. Siku moja kabla ya mechi hii nilimsikia Malinzi akiongea kwenye kituo kimoja cha redio akiwataka Yanga wawe makini katika mchezo wa marudiano Cairo kutokana na fitna za wamisri wakiwa nyumbani kwao.Malinzi alidai kwamba alikuwepo uwanjani Cairo kwenye mechi ya Super cup baina ya Ahly na Sfaxien ya Tunisia na kwamba washabiki wa Ahly walifanya fujo za kurusha fataki,kuwasha moto na kupiga filimbi pale mchezaji wa timu pinzani alipokuwa anaelekea\ kufunga.Haya yalikuwa maneno ya uchochezi kwa washabiki tulio nao ambao niliwasikia wakiihamasishana kuwarushia chupa za maji benchi la ufundi la Ahly kwa kisingizio kuwa Malinzi amesema Yanga ikienda Cairo itafanyiwa fujo.Kiongozi wa hadhi ya Malinzi hakupaswa kuongea maneno kama hayo hadharani kwani aliangalia zaidi kujijengea umaarufu wake yeye binafsi kwa washabiki wa Yanga bila kuangalia athari za maneno hayo kwa kuzingatia upeo wa asilimia kubwa ya mashabaki wa soka wa Tz. Kama lengo lilikuwa ni kuwatahadharisha Yanga alipaswa kuwasiliana na viongozi wa Yanga kwa njia za kiutawala na sio hii aliyotumia.Pengine suluhisho la vurugu hizi ni Yanga na Simba kujenga viwanja vyao ili wadhibitiane wenyewe kwa wenyewe kwani watakapong'oa viti hasara zitakuwa kwa klabu zao

    ReplyDelete