Search This Blog

Friday, January 10, 2014

UHAMISHO WA SUNZU,SINKALA NA MPUTU NA MILANGO YA KUSONGA MBELE KWA SAMATTA NA ULIMWENGU




Licha ya mmiliki wake, Moise Chapwe Katumbi kusisitiza kuwa TP Mazembe itarudi kwa nguvu Zaidi na kucheza fainali za klabu bingwa duniani mwaka huu, bado ni dhahiri kuwa vigogo hao wakongo wana kazi ya kujenga upya kikosi chao.

Inawezekana TP Mazembe wakaja na nguvu Zaidi kama mmiliki wake anavyodai hasa ukizingatia kuwa fungu la kufanya usajili wa nguvu kuziba mapengo si shida. Pesa za kufanya usajili wa nguvu wanazo, lakini je wataweza kujenga timu yenye umoja kwa haraka haraka kiasi cha kunyakua ubingwa wa Afrika na kukata tiketi ya kufuzu klabu bibgwa duniani ndani ya mwaka mmoja?

Kinara wa ulinzi Stophila Sunzu pamoja na Mzambia mwenzake, Nathan Sinkala wamekwisha ondoka. Sunzu na Sinkala wamefanikiwa kujiunga na klabu ya Sochaux ya Ufaransa. Wanaungana na kocha wao kipenzi, mfaransa Herve Renard.

Kuondoka kwa Sunzu na Sinkala kunaacha pengo kubwa. Mwaka jana, safu ya ulinzi ya Mazembe iliyumba sana kwa kumkosa Stophila Sunzu. Ikumbukwe Mazembe walikuwa wanasifika kwa kutoruhusu mabao, iwe nyumbani au ugeni. Bila ya Sunzu, ukuta wa Mazembe ulijikuta ukiruhusu mabao matatu dhidi ya Orlando Pirates katika mechi ya raundi ya pili ya ligi ya mabingwa Afrika. Safari yao ya kwenye ligi ya mabingwa Afrika ikawa imeishia hapo baada ya kuambulia ushindi mwembamba wa 1-0 kwenye mechi ya marudiano.

Licha ya mabao ya Mbwana Samatta kuwasukuma hadi fainali ya kombe la shirikisho, bado ukuta wao ulionekana kuwaangusha. Tisa kumi, sakata la uhamisho wa nahodha wao tegemeo, Tressor Mputu bado halijafika mwisho. Unapotaja mpira wa Kongo, ni sharti utaje TP Mazembe, na unapoitaja Mazembe ni sharti jina la Mputu liongelewe. Mputu ni kama taasisi, ni kiongozi, ni mhamasishaji na silaha ya ushindi katrika klabu ya Mazembe.
Naijaribu kutafuta picha ya TP Mazembe bila ya Sunzu, Sinkala na Mputu. Napata shida kuona Katumbi akiwaruhusu nyota wake Zaidi waondoke huku akiwa na ndoto za kuwa klabu ya kwanza Afrika kutwaa ubingwa wa dunia.

Bila shaka uhamisho wa Sunzu na Sinkala utakuwa umewaongezea kiu ya kucheza Ulaya Samatta na Ulimwengu. Kuondoka kwa Sunzu na Sinkala kunaweza kuwa kumewafungulia milango au kumewafungia dirisha.

Iwapo Sunzu na Sinkala watang’aa na kuiokoa Sochaux kutoka kwenye dimbwi la kushuka daraja basi mawakala wan je wanaweza kuongeza kasi ya kuimulika TP Mazembe ili kuangalia ‘madini’ mengine. Hii inaweza kuwa bahati ya kina Samatta na Ulimwengu.
Kwa upande mwingine, fungu walilopata TP Mazembe kutokana na uhamisho wa kudumu wa Sunzu linalokadiriwa kufikia bilioni 2 linaweza kutumika kumshawishi Samatta kuongeza Mkataba. Inasemekana mkataba wake unaisha mwakani mwezi wa sita. Katumbi anaweza kutumia noti alizovuna kwa Sunzu kumuongezea Samatta mkataba wenye maslahi makubwa Zaidi.

Samatta anaweza kujikuta anapata maslahi makubwa Zaidi ya yale ambayo anaweza kuyapata kwenye nchi ambazo washambuliaji wengi wa Kiafrika wanaanzia safari zao za kuelekea ligi kubwa. Itakuwa ngumu kwa Samatta na Ulimwengu kuacha mamilioni ya Katumbi kwa ajili ya bahati nasibu ya Ulaya kwa kuanzia ligi ndogo.

Pia kwa upande mwingine, uhamisho wa Sunzu na mkopo wa Sinkala unaweza kufungua ukurasa mpya kwa Katumbi na kuamua kulegeza kamba ya kuuza wachezaji wake. Licha ya mapenzi yake makubwa na msimamo wake, mwisho wa siku Katumbi ni mfanyabiashara. Pesa alizovuna kwa Sunzu pamoja na zile anazotarajia kuvuna kwa Mputu zinaweza kuufungua moyo wake na kuona anaweza kufanya biashara ya kuuza wachezaji huku akiendelea kubeba mataji.

Imeandaliwa na: Michael Mwebe.

1 comment:

  1. jamani MPUTU bado yupo tpmazembe na jana ameripoti klabuni na amekuwa mchezaji wa kwanza kuripoti klabuni baada ya likizo za wachezaji kuisha, tuwe tunajaribu kujirdhishwa kwanza kabla ya kutoa habari

    ReplyDelete