Na Baraka Mbolembole
Nani wakala wa Ramadhani Singano?. Kiungo huyu mshambuliaji wa Simba hakika anaweza kutajwa kama mchezaji hatari zaidi wa timu hiyo. Ukimtoa Amis Tambwe, timu pinzani kwa sasa zinapata wakati mgumu kumkabili mchezaji huyo mwenye kasi, akili, kontroo, bahati mbaya hana nguvu ya kutosha ila anajilinda kwa kutotaka kung'ang'ania kupita mahala pasipopitika.
Moja kati ya mambo ambayo Simba wameingia nayo katika duru hili la pili ni kucheza mchezo wa kukimbia uwanjani. Hapo ndipo unaweza kuona pasi za uhakika. Inahitaji wachezaji wenyewe kujituma ili kufanikisha hilo. Kama wachezaji watacheza kwa mwendo wa chini, mpira unapooza na hapo ndipo soka bovu huonekana.
Singano anakimbia, ni kitu kizuri si kwake tu hata kwa timu pia kwa kuwa kasi yake ufanya timu nzima kukimbia. Ni mchezaji ambaye anacheza mpira wa wazi, ni mjanja na mtu ambaye ana uwezo mkubwa wa kufunga na kusaidia upatikanaji wa mabao. Katika mchezo wa siku ya jumapili dhidi ya timu ya Rhino Rangers, mchezaji huyo aliweza kucheza kwa kiwango cha juu. Alifunga bao pekee, alipoteza mkwaju wa penati, ni kawaida sana.
Singano ambaye alianza kuomesha makali yake katika mchezo kati ya Simba na Azam FC msimu uliopita, akifunga mabao mawili katika sare ya mabao 2-2, alikuwa ni mchezaji tishio kwa timu ya Rangers. Akiwa na umbo dogo, hucheza kiungo wa kulia japo hutumia mguu wa kushoto. Alitengeneza nafasi nyingi katika mchezo huo ila si zote ambazo zilizaa matunda.
Simba ilikataliwa mabao yake mawili, yaliyofungwa na Tambwe, ila bao la shuti kali la Singano akimalizia mpira uliokuwa ukizagaa zagaa katika eneo la hatari la Rangers. Japo alicheza sambamba na wachezaji wasio na kasi, Awadh Juma ambaye alicheza kama kiungo wa ulinzi, Amri Kiemba aliyecheza kama kiungo wa mashambulizi, Said Ndemla ambaye alikuwa na jukumu la kusaidia ulinzi na mashambulizi, Singano alioneka kuwaendesha puta walinzi wa Rangers, Julius Masunga, Amani Juma na kuwachezesha washambuliaji Tambwe na Ally Badru.
Kasi ya Singano ilichochea kwa kiasi kikubwa kiungo Awadh kucheza mipira mirefu ya haraka na kuwalazimu Kiemba na Ndemla nao kukimbia. Simba wakaonekana kwenda na kasi, japo suala la mbinu za kufunga mabao zilikuwa si nzuri sana. Kasi ya timu ilisababisha kocha Zdravko Logarusic kumtoa uwanjani mshambuliaji Bertam Mwombeki dakika 20 baada ya kumuingiza uwanjani kuchukua nafasi ya Tambwe. Betram alionekana kushindwa kuendana na kasi ya wenzake ila sikupenda namna kocha alivyomfanyia mabadiliko. Wakiwa ndiyo kwanza wametoka katika mgogoro, kocha atakuwa amemuua kisaikolojia Betram kwa kuona kama hatendewi ipasavyo na mwalimu wake.
Kwa sasa Simba inaweza kunufaika na kiwango cha Singano, ila wachezaji kama Joseph Owino na Betram wana umuhimu mkubwa pia. Mchezaji huyo aliingia uwanjani na kutolewa kwa kuwa alikwenda kinyume na maagizo ya kocha wake. Kama wanahitaji kupigania ubingwa msimu huu ni lazima waongeze stamina na kuzuia mambo yao ya ndani yasitoke nje kwa kuwa yatatangazwa kwa namna mbalimbali na kuivuruga timu yao. Wakati huu mchezaji aliyekuwa akitegemewa kufanya mambo makubwa sana msimu huu, Haruna Chanongo akionekana kushuka kiwango chake cha umakini, na kujituma Singano anachukua nafasi ya kuichezesha Simba.
Unataka kujua namba ambazo hazijapata watu halisi wa Simba?. Jezi namba 11, ilitoka kwa Mussa Mgosi sasa imempata mwenyewe. Ilikuwa jezi ya Steven Mapunda. Uhuru Suleiman ndiye mchezaji anayevaa jezi namba 10. Namba tangu waitumie kina Nteze John, Emmanuel Gabriel na Athuman Machuppa, waliofuatia wengi iliwashinda. Felix Sunzu na sasa Uhuru anakaa nayo benchi. Awadh ndiyo kwanza amecheza mchezo wake wa kwanza akiwa mchezaji wa Simba akiwa na jezi namba 16. Muhasisi wake ni kocha msaidizi wa timu hiyo, Suleimani Matola, ataiweza? Kwa kiwango chake cha jumapili ameonesha dalili njema ila hata Mohammed Banka alishindwa kufikia juu zaidi ya Matola.
No comments:
Post a Comment