Search This Blog

Thursday, January 2, 2014

MAKALA: AZAM FC WAONDOE KASORO HIZI WATWAE UBINGWA


Na Baraka Mbolembole

AZAM FC, kwa sasa ni moja ya timu mashuhuri katika ukanda wa Afrika Mashariki na Kati. Umaarufu wa timu hiyo hautokani na mafanikio ya soka katika michuano ya ukanda huu. Ni timu changa katika soka la Tanzania, haijawahi kutwaa ubingwa wa ligi kuu, ila katika misimu miwili ya mwisho wameweza kumaliza katika nafasi ya pili ya ligi kuu ya Vodacom Tanzania Bara. Na hadi wakati huu wa mapumziko kupisha michuano ya Challenge, Azam inashikilia nafasi ya pili katika ligi, nyuma ya Yanga SC kwa tofauti ya pointi moja.

WAPO KATIKA MWENDO MZURI KUELEKEA UBINGWA...
Ukitazama mafanikio yao ya kumaliza katika nafasi ya pili katika misimu ya 2011/ 12, na 2012/ 13, Azam ilikuwa katika mbio za ubingwa kwa misimu minne mfululizo ya mwisho. Katika msimu wa 2009/ 10 ambao timu ya Simba walitwaa ubingwa pasipo kupoteza mchezo wowote, Azam ilikuwa ni timu tishio katika ligi, walikuja kuangushwa kutoka nafasi ya kwanza hadi ya tatu mwishoni mwa msimu. Ni wakati huo kocha Itamor Amourin alikuwa amewekeza nguvu zake kwa wachezaji vijana, huku wakiongozwa na kundi la wachezaji bora wa ndani, na baadhi wa kigeni.

Ni wakati huo timu ilipokuwa imeanza uwekezaji wa uhakika wa kusajili wachezaji nyota kutoka ndani na nje ya nchi. Aggrey Morris, Ramadhani Chombo, Jabir Aziz, Mrisho Ngassa, Mwadini Ally, Kipre Tcheche, Ibrahim Shikanda, Kally Ongalla, marehemu Patrick Mafisango, Joseph Owino walitua hapo mara baada ya msimu kumalizika. Kocha, Itamor alikuja kuondolewa na nafasi yake kuchukuliwa na aliyekuwa mkurugenzi wa ufundi wa timu ya taifa ya Zanzibar, Stewart Hall. Kocha huyo alianza duu la pili la msimu wa 2010/ 11 kwa kutoa vichapo kwa timu mbalimbali ikiwemo mechi ya kukumbwa wakati walipoizamisha Simba kwa mabao 3-1, na kuonesha dalili za kutwaa taji.

Yanga waliokuwa taabani katika ligi walianza kunyanyuka taratibu kimchezo, Simba ikawa inashuka kutoka juu kwenda chini, huku Azam wakipanda hadi juu ya msimamo kwa tofauti ya pointi zaidi ya tatu kuelekea michezo minne ya mwisho. WAkaenda kucheza na Yanga katika mchezo ambao ulikuwa ni muhimu kwa kila timu, kwa Azam ilimaanisha kuwaondoa Yanga katika mbio za ubingwa, huku Yanga wakipigania kuingia katika nafasi ya pili. Azam ilipoteza mchezo huo kwa mabao mawili ya Jerry Tegete, akifuta lile la uongozi lililokuwa limefungwa na John Bocco. Siku chache baadae, kocha Hall alimtimua kipa Vladimir Niyonkuru kwa madai kuwa ' alitumika'. Azam ikashuka hadi nafasi ya tau mwishoni mwa msimu, Yanga waliokuwa watatu wakatwaa taji kwa stahili ya aina yake, baada ya kuwazidi bao moja timu ya Simba. ILikuwa ni nafasi ya Azam. Kwa nini walikosa, ni kupoteza mchezo dhidi ya Yanga, na mbuzi wa kafara akawa, Niyonkuru.

Katika kilichotajwa kama msimu mbaya wa ligi kuu katika miaka ya karibuni, ni upendeleo wa waamuzi kwa baadhi ya timu katika msimu wa 2011/ 12. Moja ya timu zilizokuwa zikilalamikiwa sana ni Azam, timu nyingi zilidai kuwa timu hiyo ilikuwa inabebwa na waamuzi, kitu ambacho hakikuwa na maana yoyote. Kwani ni msimu ambao Azam walikuwasanya pointi 12 kutoka kwa Simba na Yanga. Kwa nini hawakutwaa taji. Kama wangeshinda mchezo wao dhidi ya Mtibwa Sugar, Mei, 2012 katika uwanja wa Chamanzi walikuwa na nafasi ya kutwaa taji siku ya mwisho ya msimu. Said Bahanunzi wakati akiwa Mtibwa alifunga bao la kuongoza, likakataliwa na mwamuzi, baadae wakati akigombea mpira na mlinzi wa Azam akaoneshwa kadi nyekundu. Hadi dakika za mwisho matokeo yalikuwa 1-1, ambayo yalikuwa yanaipandisha Simba hadi kileleni na kwenda kuisubiri Yanga siku ya mwisho ya msimu.

Mwamuzi akatoa mkwaju wa penati wakati mlinzi Juma Abdul ( wakati yupo Mtibwa) alipozuia kiki kwa kifua na kusema kuwa aliushika mpira huo. Wachezaji wa Mtibwa waligomea penati hiyo na kupekea mwamuzi kuvunja pambano. Haki na kanuni zikapindishwa, mechi hiyo ikapigwa tena katika uwanja wa taifa siku mbili kabla ya kumalizika kwa ligi na Azam wakalala kwa bao 1-0 ambalo lilifungwa na Juma Abdul. Kwa nini walikosa ubingwa? Walifanya kazi kubwa sana kwa msimu mzima kuzima marudio ya kumaliza nafasi ya tatu kwa msimu wa tatu mfululizo. Hapa mchawi hakupatikana.

Kuanzia msimu huu timu hiyo imejihimarisha zaidi kiuchezaji na kiufundi. Ikiwa ni timu iliyocheza michezo mingi ya ugenini katika duru la kwanza, Azam wanakabiliwa na changamoto ya kuzishinda kwa wakati mmoja Simba na Yanga. Ni kazi sana, ila kuna mahali tayari wameonesha ubabe dhidi ya vigogo hao wa soka nchini. Katika uwekezaji Azam huwezi kuilinganisha na Simba na Yanga, wapo juu katika hilo. Je hiyo ndiyo inaweza kuwa sababu ya kumaliza juu ya Simba na Yanga kwa wakati mmoja? Wanaweza ila ni lazima mambo haya ya ndani kabisa wayatambue.

Binadamu tunasema kuwa wivu ni sehemu ya maendeleo, au pengine tunakuwa tunasema kuwa Majungu ni sumu ya maendeleo. AZam kwa sasa wana wivu na matamanio ya kutaka ubingwa wa ndani ili wapate kucheza michuano ya klabu bingwa Afrika. NI jambo zuri kwa kuwa mtazamo wao hauishii tu katika kucheza michuano ya ndani kila mwaka. Ila wakati Jockins Atudo alipokuwa anaondoka katika timu hiyo mwezi ulipita aliwahi zungumza mahali kuwa kuna matatizo fulani ndani ya timu hiyo ambayo yanatakiwa kutazamwa na kuondolewa kama kweli wanahitaji kuwa timu imara ndani ya uwanja.

Yeye alisema kuwa kuna majungu sana ndani ya timu hiyo, huku vinara wakiwa ni makocha wasaidizi wawili wa timu hiyo. Alisema makocha hao wamekuwa wakiwapiga majungu wachezaji kwa viongozi wao wa juu, huku akisikitika pia mtu anayetoka naye nchi moja kuwafanyia wenzake hivyo. Moja ya sababu za wachezaji wa Kenya kushindwa kudumu hapo ni mmoja kati ya makocha hao wasaidizi.

Pia, inakuwaje kila mchezaji akawa na mawasiliano ya moja kwa moja na bosi wa timu. Jambo hili pia limekuwa likirahisha mawasiliano mabaya kati ya wachezaji na mmiliki wa timu. Wakati fulani Salum Abubakary aliposimamishwa na uongozi ni kutokana na ' unoko' wa uliofanywa na mmoja wa wachezaji kwenda moja kwa moja kwa bosi wa timu, na kumopigia simu akimueleza mambo ya uongo.

Jambo lingine ambalo linatakiwa kuachwa kwa sasa ni kuwatumia wachezaji kama sehemu ya kisasi kwa mtu fulani jambo ambalo limemwondoa Hall, ukiacha propaganda zote zilizokuwa zinasemwa ni kocha huyo kujisifia mara kwa mara kuwa ndiye msimu wa soka la Azam. Baadhi ya viongozi wakawa ni watu wa kukasirika, kwa kuwa wao ndiyo walitaka kuwa msingi wa historia ya timu kimafaniko. Hall alijiamini kuja kutwaa ubingwa siku moja kwa kuwa tayari alikuwa anajua namna ya kuziadhibu Simba na Yanga.

Kuwa sehemu ya historia nzuri ni jambo la kupendeza sana, lakini ni wakati wa Azam kutambua kuwa Jose Mourihno ndiye aliywekata ukame wa miaka 50 wa Chelsea kutwaa ubingwa wa ligi kuu, ila huwezi kuzungumzia uwekezaji wa Roma Abramovich kuwa ndiyo sababu ya mafanikio yote hao. Jose atabaki ni ' mtu maalumu' na Roman atabaki mtu wa aina yake katika historia ya Chelsea. Mafaniko ni ya wote. Azam wanaweza kutwaa ubingwa, ila wakumbuke kuwa wachezaji wao ni walevi sana. Au, ndiyo, fanya kazi, upate pesa, ufanye matanuzi?

No comments:

Post a Comment