Search This Blog

Monday, December 30, 2013

2013 - ULIKUWA NI MWAKA WA ATHUMAN IDD ' CHUJI'


Na Baraka Mbolembole 

Athumani Idd ' Chuji' , sahau kuhusu umri wake, kiungo huyu wa ulinzi na mashambulizi wa klabu ya soka ya Yanga, amepitia vipindi vingi vigumu katika maisha yake ya soka. Akianzia soka lake katika timu ya Polisi Dodoma, 2005, Chuji alitokea kuwa mlinzi bora wa kati katika soka la Tanzania, alikuwa akipata nafasi ya kucheza mara kwa mara katika timu ya taifa ya vijana ' Serengeti Boys' mwaka huo, akitokea timu za nje ya Dar es Salaam. Kupata nafasi ya moja kwa moja katika timu ya taifa ukitokea mkoani, bila shaka wewe utakuwa mchezaji ' asiyegusika' popote pale.
Namba tano mwenye sifa za utulivu, mpangaji mzuri wa ngome na kiongozi mwenye kujiamini, ni sifa ambazi zilimfanya Chuji kusajiliwa na Simba, kwa ajili ya msimu wa mwaka 2006. Chuji, 25 kwa sasa ( umri huu ndiyo unaotambulika' aliingia Simba na kukuta wachezaji wengine wazuri kama yeye. Katika nafasi ya ulinzi wa kati ambayo alikuwa akicheza katika timu ya Polisi Dodoma, ndani ya Simba, nafasi hiyo ilikuwa chini ya Victor Costa, na beki Mrundi, Said Koko'o hivyo ilimfanya kukutana na upinzani mkali wa kuwania nafasi.
TUMIA NAFASI YAKO VIZURI...
Chuji, alitumia mwanya wa matatizo ya kinidhamu yaliyopelekea baadhi ya wachezaji muhimu kuwa kando ya timu. Costa, hakuwa na maelewano mazuri na kocha Neidor dos Santos, na ni hapo ndipo ikapatika nafasi ya Chuji, kuonesha kandanda lake la uhakika. Dos Santos, alipendezwa na viwango vya wachezaji vijana wakati huo, Chuji, Henrry Joseph na Kelvin Yondan na akaamua kuwapata nafasi ya wachezaji watovu wa nidhamu.
YANGA WALIMUONEA SIMBA....
Soka la uhakika akicheza katika idara ya kiungo kwa dakika 120 lilimtambulisha kiungo, mwenye mapafu ya ' mbwa' katika soka la Tanzania. Japo alikuja kukosa mkwaju wake wa penati baada ya mchezo huo wa nusu fainali ya michuano ya Tusker dhidi ya mahasimu wao Yanga, kumalizika kwa sare ya bao 1-1.
ATUA RASMI YANGA, AONESHA TABIA MBAYA KWA SIMBA...
Baada ya kumalizika kwa msimu wa mwaka 2006, Chuji alijiunga na Yanga katika kile alichokiita usajili wa maslai zaidi na si mapenzi. Ni wakati huo alikuwa akisema kuwa kurudi Simba ni bora akauze ndimu. Simba walipigania sana haki zao lakini wakaishia kupigwa chenga na kiungo huyo kila walipomuomba wakae naye meza moja kumaliza utata uliokuwa umegubika usajili wake, na kama kwenda Yanga aende kwa amani. Wazee wa Yanga wakamng'ata masikio na kumwambia akifanya hivyo tu amekwisha kisoka. Mifano mingi ikatolewa huku akiambiwa kuwa Mwinyi Rajab ni mfano mzuri kuhusu wasemayo. Baadae akaruhusiwa kuichezea Yanga na shirikisho la soka nchini, TFF. Baadae akafungiwa kwa kosa la kuonesha kidole cha kati katika moja ya michezo yake ya kwanza akiwa mchezaji wa Yanga. Alifungiwa kwa muda wa miezi sita.
CHUJI WA KADI ZA MARA KWA MARA....
Hata aliporudi uwanjani baada ya kumalizika kwa adhabu yake, Chuji alikuwa ni mchezaji wa kiwango kilekile, akizima kila kitu kuhusu tabia yake kucheza soka la ukosefu wa nidhamu kwa kiwango chake na mchezo uliochangamka. Moja kati ya majuto makubwa ya aliyekuwa kocha wa timu ya taifa ya Tanzania, Taifa Stars, Marcio Maximo ni adhabu ya mchezaji huyo. Akiwa mfuasi ya nidhamu ni wazi Maximo alikuwa akitambua mchango wa Chuji katika kati yake. Tabia yake mbaya ilimfanya kuingia katika vifungo vya mara kwa mara, na hivyo kukosa nafasi ya kuichezea timu ya taifa mara kwa mara.
SAHAU YOTE, ALITUPELEKA  CHAN
Kiwango kizuri cha Chuji, kilionesha ni kwa nini kocha Maximo alipinga adhabu yake wakati ule, 2007. Chuji alikuwa sehemu muhimu ya wachezaji wa timu ya taifa waliozisukuma nje, Kenya, Uganda na Sudan kisha kutinga kwa michuano ya CHAN, 2009, nchini Ivory Coast. Alifunga moja ya mabao bora wakati Stars ikiifunga, Sudan katika mchezo wa mwisho wa kufuzu, jijini Dar, kabla ya kwenda kusaidia ushindi wa kukumbukwa ugenini, jijini Khartoun.
CHUJI APOTEZA DIRA....
Wakati kiwango chake kiliposhuka zaidi, 2009. Chuji aliishia kugombana na kocha Maximo katika timu ya taifa. Makocha wa klabu yake, Dusan Kondic, na baadaye, Kostadin Papic bado walikuwa wakisema kuwa hakuna kiungo kama Chuji katika nyakati za sasa nchini. Baadae kiwango kilizidi kuporomoka huku mambo ya nje ya uwanja yakimuathiri kimchezo, akashuka thamani hata kwa mashabiki wake mwenyewe. Alitumia misimu miwili kuanzia 2009- 10, na 2010 - 11 akicheza soka huku akiitwa ' mzee'. Kisha baada ya kumalizika kwa mkataba wake na Yanga, klabu haikumuongeza tena mkataba. Akarudi Simba, na kusajili katika michuano ya Kagame, 2011. Akaishia kucheza dakika zisizozidi kumi wakati timu yake ikicheza michezo sita hadi fainali.
NITAENDELEA KUMUHUSUDU PAPIC KWA HIKI...
   
Hata wakati, Chuji akiitwa 'mzee' katika utawala wake Yanga, kocha Papic bado aliendelea kusema kauli yake ile ile kuwa Chuji ni kiungo wa aina yake. Baada ya kumalizika kwa michuano ya Kagame, Simba iliamua kumtema Chuji, na hivyo akajikuta nje ya soka kwa muda wa miezi sita. Kila mtu alikuwa akisema lake, wapo waliokuwa wakisema kuwa mwisho wake umefika na kuna wakati akakanusha taarifa za yeye kutumia madawa ya kulevya ndiyo sababu ya kutemwa kwake Simba. Baada ya Sam Timbe kufukuzwa kazi ya ukocha, Yanga ilimrejesha Papic na kocha huyo akaamua kumpatia mkataba wa miezi sita ndani ya Yanga.
Akafanya vizuri na kupewa mkataba wa miaka miwili zaidi, na mapema mwezi uliopita alirefusha kwa miaka miwili zaidi ya kuendelea kuichezea Yanga. Kwa sasa, amepevuka zaidi na amekomaa kimaamuzi. Si mkorofi akiwa uwanjani, ana jiheshimu na kuheshimu mchezo wenyewe. Amekuwa kiongozi, na mchapakazi mzuri kwa timu. Kama ni safari, Chuji amepitia safari ndefu, ila kwangu nampa tuzo ya mchezaji mwenye nidhamu kwa kipindi cha mwaka mzima, 2013. Amefanya kazi yake vizuri. Ningemrudisha Chuji katika nafasi ya ulinzi wa kati ili anisaidie katika timu yangu. Nafasi hii inahitaji busara zaidi, na pengine hata Dos Santos angemrudisha katika nafasi aliyomtoa. Beki tano.

1 comment:

  1. wachezaji wengi wa Tanzania wanashuka viwago kwa sababu ya ulimbukeni wa anaza pamoja na utovu wa nidhamu.Chuji ni mmojawapo.leo kiwango kesho balaa! wengi wanategemea na kiwango cha bangi walichovuta !

    ReplyDelete