Search This Blog

Thursday, November 7, 2013

YANGA YAJIPIGIA JKT OLJORO, YAONGOZA LIGI,



USHINDI wa mabao 3-0 dhidi ya JKT Oljoro na sare ya mabao 3-3 kati ya Azam FC na Mbeya City, kwa pamoja vimeifanya klabu ya soka ya Yanga kujikita kileleni mwa Ligi Kuu ya Bara hadi mwakani mzunguko wa pili utakapoanza.

Yanga ilikuwa ikicheza na Oljoro kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam imeweza kusogea kutoka nafasi ya tatu iliyokuwa inashika awali hadi nafasi ya kwanza baada ya kufikisha pointi 28, huku sare ya mabao 3-3 ya Azam na Mbeya City ikizifanya timu hizo kufikisha pointi 27 kila moja. Timu zote zimecheza mechi 13.
Kwenye Uwanja wa Taifa, Yanga iliuanza mchezo kwa kasi na kufanikiwa kupata bao la kuongoza dakika ya 23 mfungaji akiwa Simon Msuva aliyeunganisha vyema krosi safi ya Haruna Niyonzima kutoka wingi ya kulia.

Baada ya kuingia kwa bao hilo, Oljoro walikuja juu lakini kitendo chao cha kucheza huku wakitumia nguvu nyingi kutaka kusawazisha kiliwasababishia wachezaji wao kadhaa kuumia kila mara huku Yanga wakiendelea kushambulia kwa kasi.
Mrisho Ngassa aliipatia Yanga bao la pili dakika ya 30 kwa shuti kali akiwa nje ya eneo la 18 la Oljoro ambalo kipa Damas Kugesha hakuweza kulizuia na kuamsha shangwe kwa mashabiki wa Yanga. Awali Kugesha alidhani Ngassa angetoa pasi mara baada ya kupokea pasi ya Frank Domayo kutoka katikati ya uwanja.

Mabao hayo ya Yanga yalidumu hadi mwamuzi Simon Mbelwa wa Pwani anapuliza filimbi ya kuashiria timu hizo ziende kupumzika. Kabla ya timu hizo kwenda mapumziko, Oljoro ilifanya mabadiliko kwa wachezaji Yusuph Mchogote na Babu Ally na nafasi zao kuchukuliwa na Deogratius Peter na Hamisi Saleh.
Kipindi cha pili kilianza kwa Yanga kufanya mabadiliko baada ya kumtoa Hamisi Kiiza na nafasi yake ikachukuliwa na Jerry Tegete na mabadiliko hayo yaliongeza uhai kwa Yanga kwani dakika ya 53, Tegete aliipatia Yanga bao la tatu baada ya kupokea pasi nzuri ya Ngassa.

Ndani ya kipindi cha pili Oljoro ilifanya badiliko moja kwa kumtoa Sanu Mwaseba na nafasi yake kuchukuliwa na Amir Omar wakati Yanga waliwatoa Frank Domayo na Haruna Niyonzima na nafasi zao kuchukuliwa na Reliants Lusajo na Said Bahanuzi.
Mabadiliko hayo yaliongeza uhai kwa timu zote mbili lakini hadi dakika 90 zinamalizika hakuna timu iliyoweza kupata bao baada ya mabadiliko hayo kufanywa licha ya Yanga kukosa mabao kadhaa ya wazi huku Oljoro nao wakifika langoni kwa Yanga mara chache.

No comments:

Post a Comment