Search This Blog

Thursday, November 7, 2013

SIMBA YAIFANYIA MAUAJI ASHANTI, MOMBEKI APIGA MBILI TAIFA


    Picha kwa hisani ya Rahel Pallangyo.

LICHA ya kubaki katika nafasi ya nne kwenye msimamo wa Ligi Kuu ya Bara, mashabiki wa klabu ya soka ya Simba leo jioni walitoka kifua mbele kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam baada ya timu yao kuibuka na ushindi wa mabao 4-2 dhidi ya Ashanti United.

Matokeo hayo yanaifanya Simba kubaki katika nafasi ya nne ikiwa na pointi 24 baada ya kucheza mechi 13, huku iksihinda mechi sita, kutoka sare sita na kufungwa moja. Ashanti yenyewe imebaki na pointi zake 10 baada ya kucheza mechi 13 pia.

Ashanti iliyoanza ligi kwa kusuasua, imeshinda mbili, imetoka sare nne na kufungwa mechi saba. Imefunga mabao 12 na kufungwa 24.

Simba iliingia uwanjani na kumbukumbu ya sare ya bao 1-1 dhidi ya Kagera Sugar, lakini iliwachukua dakika nane tu kupata bao la kwanza lililofungwa na Ramadhan Singano maarufu kama Messi akimalizia mpira wa pasi ndefu kutoka katikati ya uwanja.

Baada ya kuingia kwa bao hilo, Ashanti walikuja juu na kutaka kusawazisha lakini ukuta wa Simba ulioongozwa na Gilbert Kaze ulikuwa makini kuondosha hatari zote zilizoelekezwa kwao.

Wakati mashabiki wakidhani timu hizo zitaenda kupumzika huku Simba ikiongoza kwa bao moja, dakika ya 45 Ashanti ilipata bao la kusawazisha lililofungwa na Hussein Sued aliyemalizia krosi safi ya Joseph Malunda.

Hadi mwamuzi Andrew Shamba kutoka Pwani anapuliza filimbi ya mapumziko, timu hizo zilikuwa sawa kwa bao 1-1.

Kipindi cha pili kilianza kwa kasi lakini walikuwa Simba waliotumia vyema mabadiliko yaliyofanywa na kocha Abdallah Kibadeni baada ya kuwatoa Henry Joseph na Amri Kiemba na nafasi zao kuchukuliwa na Said Ndemla na William Lucian kwani dakika ya 46, Amis Tambwe aliipatia Simba bao la pili akimalizia kazi nzuri ya Messi.

Dakika tatu baadaye, mshambuliaji Betram Mombeki aliipatia Simba bao la tatu akimalizia pasi safi ya beki Haruna Shamte, hata hivyo dakika ya 52 Said Maulidi ‘SMG’ aliipatia Ashanti bao la pili akimalizia krosi safi kutoka wingi ya kulia.

Simba ilipata bao la nne dakika ya 60 mfungaji akiwa Mombeki baada ya mabeki wa Ashanti kushindwa kumzuia Messi aliyewalamba chenga na kuwazidi nguvu mara kadhaa mabeki wa timu hiyo.

Katika hali ya kushangaza kila Simba ilipokuwa ikipata bao wachezaji wake walikuwa wakishangilia kwa mtindo wa kuomba msamaha kwa mashabiki wa timu hiyo ambao leo walikuwa chini ya ulinzi mkali wa polisi baada ya mchezo uliopita dhidi ya Kagera kuvunja baadhi ya viti vya uwanja huo.


Matokeo mengine ya ligi kuu ya Vodacom

JKT RUVU 1:0 COASTAL UNION

RUVU SHOOTING 2:2 MTIBWA SUGAR

KAGERA SUGAR 2:0 MGAMBO SHOOTING

No comments:

Post a Comment