Search This Blog

Thursday, November 7, 2013

TAMBWE AFIKISHA MABAO 10, SMG HATARI, AMANI SIMBA APIGWA RED CARD

 Picha na Rahel Pallangyo.



STRAIKA wa Simba, Amisi Tambwe leo amefunga bao lake la kumi katika Ligi Kuu ya Bara, lakini mkongwe Saidi Maulid ‘SMG’ amedhihirisha kwamba bado ni moto wa kuotea mbali huku kipa Amani Simba akilimwa ‘red card’ iliyowaacha wengi midomo wazi.
Simba ilikuwa ikicheza kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam dhidi ya Ashanti na kuibuka na ushindi wa mabao 4-2 lakini mchezaji wake Tambwe raia wa Burundi amefikisha idadi ya mabao 10 na kuongoza katika orodha ya wafungaji wa ligi hiyo.
Kabla ya mchezo huo, Tambwe alikuwa ameshafunga mabao tisa akifuatiwa na Hamisi Kiiza wa Yanga mwenye mabao manane. Wengine wanaofuatia ni Elius Maguri wa Ruvu Shooting, Juma Liuzio wa Mtibwa Sugar na Kipre Tchetche wa Azam wenye mabao saba kila mmoja.
Tambwe alifunga bao lake dakika ya 46 akiunganisha pasi safi ya Ramadhan Singano ‘Messi’ ambaye aliwanyanyasa mabeki wa Ashanti upande wa kushoto kisha kutoa pasi safi kwa mfungaji aliyefunga kirahisi.
Akizungumza na mtandao huu mara baada ya mchezo huo, Tambwe alisema anashukuru kufunga mabao 10 hadi sasa na anawashukuru wachezaji wenzake ndani ya Simba na benchi la ufundi kwa ushirikiano waliompa hadi akafiksiha idadi hiyo ya mabao.
“Kazi yangu siku zote ni kufunga, nadhani kama mchezaji natumia vyema nafasi ninazopata kuweza kufunga na kufanya mambo kuwa mazuri kwa watu wote. Nafanya haya (kufunga) kwa faida ya Simba na watu wote wanaoipenda klabu hii,” anasema Tambwe.



 Picha na Rahel Pallangyo.


SMG HATARI…
Winga Said Maulid ‘SMG’ wa Ashanti United leo amedhihirisha kwamba bado yupo katika kiwango chake baada ya kucheza vyema nafasi hiyo dhidi ya Simba na kufanya vizuri.
SMG aliweza kucheza vyema mbele ya beki Issa Rashid maarufu kama Baba Ubaya na kuonyesha bado yumo kiasi ambacho alikuwa akishangiliwa mara kwa mara na mashabiki waliokuwepo uwanjani hapo.
“Nadhani nalinda kiwango changu kwa kufanya mazoezi mara kwa mara tofauti na wachezaji wengine ambao wakiona umri umeenda anajibweteka na kuachana na soka,mimi sipo hivyo ndiyo maana leo umeniona nacheza vile,” anasema SMG aliyewahi kuzichezea Simba na Yanga kwa nyakati tofauti miaka ya mwanzoni ya 2000.
Katika mchezo huo, SMG aliifungia Ashanti bao la pili dakika ya 52 akiunganisha vyema krosi kutoka wingi ya kulia na kuamsha shamra shamra miongoni mwa mashabiki wa Ashanti licha ya timu yao kuwa nyuma kwa mabao 3-2 kabla ya Betram Mombeki hajaifungia Simba bao la nne.
AMANI SIMBA APIGWA RED CARD…
Kipa wa zamani wa Simba, Amani Simba ambaye leo aliichezea Ashanti United, alionyeshwa kadi nyekundu dakika ya 89 baada ya kuudaka mpira akiwa nje ya eneo lake analoruhusiwa.
Mwamuzi Andrew Shamba wa Pwani alimwonyesha Amani kadi hiyo baada ya kuudaka mpira uliopigwa na Ramadhan Singano ‘Messi’ wa Simba baada ya Simba kucheza shambulizi la ghafla huku mabeki wa Ashanti wakiwa wamepandisha timu.
Messi aliiwahi pasi ya kutoka kwa mabeki wa timu yake na kumiliki mpira kisha akawa anamfuata Amani langoni kwake, lakini kwa kutambua hatari inayomfuata kipa huyo akaliacha lango lake na kumfuata Messi ambaye aliunyanyua mpira lakini ghafla Amani akanyoosha mikono yake na kujikuta ameudaka.
Baada ya kuudaka mpira huo, Amani aliduwaa kwa sekunde kama mbili hivi kisha akauachia na moja kwa moja akaanza kuvua grovu zake huku akijua lazima ataonyeshwa kadi nyekundu kutokana kitendo chake hicho.
Mara baada ya mchezo huo, Amani aliuambia mtandao huu kwamba, hakudhamili kuudaka mpira ule lakini pia hakujua kama Messi angepiga juu kidogo na yeye kumfikia mikononi.
“Mimi nilijua atapiga chini halafu nilale ili nimzuie sasa wakati najipanga kufanya hivyo yeye akapiga na mpira ukaja mikononi mwangu, sikuwa na jinsi n ndipo nikaudaka na moja kwa moja nikavua glovu kwani nilijua lazima nionyeshwe kadi nyekundu,” anasema Amani.  

No comments:

Post a Comment