Search This Blog

Thursday, November 7, 2013

ABDI BANDA- COASTAL UNION NI TIMU NZURI TU




Na BARAKA MBOLEMBOLE
  Kiungo- mlinzi wa timu ya soka ya Coastal Union, Abdi Banda, amesema kuwa timu yao ni nzuri kila idara, lakini wamekosa bahati tu katika ufungaji wa mabao. Banda aliyasema hayo kabla ya mchezo wa mwisho wa mzunguko wa kwanza wa ligi kuu Tanzania Bara, ambao klabu yake ilipoteza katika uwanja wa Chamanzi, dhidi ya timu ya JKT Ruvu.
Coastali ilifungwa bao 1-0, huku kwa mata nyingine wakionesha kiwango cha chini katika ufungaji. Wakiwa wamefunga mabao 10 tu katika michezo 13, Coastal imeonekana kuwa na safu ngangari ya ulinzi katika mzunguko wa kwanza kuliko timu nyingine zote, wameruhusu mabao saba tu hivyo kuwa na wastani wa mabao matatu katika michezo yote ya mzunguko wa kwanza.
" Coastal ni timu nzuri tu. Tumejipanga kuanzia idara ya linzi, kiungo na ushambuliaji ila kwa safu ya mashambulizi kwa sasa tumekosa bahati ya kufunga. Tutakaa sawa tu" anasema mlinzi huyo wa kushoto, na mtoto wa mchezaji wa zamani wa timu za Africans Sports ya Tanga, Simba, Malindi ya Zanzibar, TPC Moshi, na timu ya Taifa ya Tanzania, Hassan Banda ambaye alikuwa mlinzi mahiri wa kati hasa katika nafasi za namba nne, na tano.
Wakati akifanya mahojiano na tovuti hii, Banda ambaye ameweza kucheza michezo 11 kati ya 13 ya klabu yake msimu huu, na kutengeneza mabao zaidi ya matao huku akifunga bao moja. Mlinzi huyo wa kushoto anaseme kuwa siri kubwa ya mafanikio yake ni kufuata maelekezo ya walimu wake, huku akitumia muda mwingi kuchunguza wachezaji wa timu nyingine kabla ya kukutana nao uwanjani na anakumbushia namna alivyokuwa makini na kiungo mashambuliaji wa pembeni wa timu ya Yanga, Saimon Msuva na kusema kuwa alimchunguza mara tu alipojua kuwa atakabiliana naye.
"  Mimi napojua tu kuwa tunacheza na timu fulani, basi huwa napendelea kujua mawinga wao ni hatari katika kipi. Ndiyo maana hata nilipokutana na Msuva naamini hakujua kama  tayari nilikuwa nimemfuatilia muda mrefu. Nilipunguza  kupanda mbele sababu ukimuacha kidogo tu ni hatari, ana spidi na ujanja mwingi. Napendelea kupanda mbele na kuongeza mashambulizi kama naona kuna udhaifu kwa timu pinzani, naweza kufunga mwenyewe au kutoa pasi ya mwisho napofanya jaribio la kusonga mbele. Kama uliona gemu yetu na Yanga sikupanda  sana kwa kuwa nilikuwa nikifahamu madhara ya kumuacha Msuva kuwa huru"
Banda alianza kuupenda mchezo huu akiwa na umri wa miaka 14, na hapo akatumia nafasi ya kuwa katika familia ya soka kuuprnda zaidi mchezo huu. Mtoto wa Nyoka ni Nyoka tu. Aliibukia timu ya Vijana ya Kombozi na baadae akapata nafasi ya kuichezea Sports timu hasimu na Coastal na aliyowahi kuichezea baba yake mzazi, Hassan miaka ya nyuma na hapo ndiyo akasajiliwa na timu ya Coastal kama mchezaji wa timu ya vijana U20.
" Nilianzia soka langu katika timu ya Vijana, nikachezea Africans Sports kwa nusu msimu ndipo nikasajiliwa na Coastal. Sikuwa na jinsi mimi kucheza Coastal ( akikumbushia uhasimu wao na Sports), nahitaji kusonga mbele zaidi katika mchezo wangu. Na hii ilikuwa ni nafasi maalumu kwangu. Kutoka ligi daraja la chini hadi kusajiliwa na timu ya ligi kuu ni bahati kubwa sana kwangu, namshukuru Mungu."
Anasema mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 18 kwa sasa ambaye tayari amecheza michezo 21 ya ligi kuu, katika muda wa miezi isiyozidi 12.
" Nilijiunga na Coastali msimu uliopota, wakati huo kama mchezaji wa timu ya U20. Nilifanikiwa kucheza michezo 10 msimu uliopita, na hadi sasa msimu huu nimecheza michezo 11. Na tayari nimechukua namba ya kudumu katika kikosi cha kwanza"
Wakati kocha wa timu ya Taifa, Kim Poulsen akitangaza orodha ya wachezaji wa vikosi vya Future Taifa Stars na kile cha timu ya Taifa Stars, makipa wawili wa timu ya Azam, Aishi Munula na Mwadini Ally wameitwa, huku kipa aliyepoteza umakini na kujiamini Ally Mustafa wa klabu ya Yanga pia ameitwa. Zaidi ni pale ambapo katika orodha ya makipa zaidi ya watani jina la kipa Shaaban Kado halipo katika orodha hiyo. Kado amekuwa ni sababu ya Coastal kuwepo hapo ilipo kwa sasa kutokana na uhodari wake wa kuzumia mashambulizi ya timu pinzani.
Pia wakati beki majeruhi wa Simba, Miraji Adam akiitwa katika moja ya vikosi hivyo, jina la Banda halipo katika orodha hiyo. Banda anasemaje kuhusu hilo.
" Kado ni kipa mzuri sana, anajua sana kutupanga mabeki wake. Kitu ambacho kinaniumiza kichwa ni kwa nini sipati nafasi ya kuchaguliwa timu ya taifa. Ila naamini wamenishikia nafasi yangu tu. Mimi ndiyo namba tatu wa timu ya taifa. Muda ukifika nitaitwa tu si shaka yoyote" anasema na kuongeza kuwa yeye ni mchezaji hatari.
" Mimi ni mchezaji ambaye nina uwezo wa kupiga pasi za mwisho nikiwa nyuma kabisa, kufunga mabao na kusaidia wenzangu kufunga. Ninauwezo wa kupiga mashuti ya umbali mrefu, mipira ya faulo na kuisadia timu katika mashambulizi na kujilinda pia"
Simba na Yanga zipo katika fikra za wachezaji wengi nchini na pengine wa Afrika ya Mashariki yote kutokana na historia ya klabu hizo. Ni kama tu kwa wachezaji nyota duniani wanapokuwa na ndoto za kuichezea klabu kama Real Madrid ya Hispania, na hata hapa kwetu wachezaji wengi wana ndoto hiyo vipi kwa Banda?
" Mimi nataka kusonga mbele na pengine kucheza ng'ambo,. Nina miaka mitatu katika mkataba wangu na Coastal ila kuna kipengele ambacho kinaruhusu mimi kuhama endapo kuna timu itakuwa imenivutia na yenyewe kunipatia dau kubwa na kuhitaji huduma yanga. Simba na Yanga? Siwezi kusema, ila Azam na hata Mtibwa popote naweza kucheza kama watafikia makubaliano na meneja wangu, Abdul  Bosnia"
Huyu, Bosnia ni nani hasa.... " Ni meneja wangu. Amewahi kucheza na baba yangu katika timu ya Sports. Amekuwa akinisapoti muda mrefu ni mtu muhimu sana kwa maendeleo yangu
"
Anawazungumziaje, Juma Nyosso, Jerry Santo na Haruna Moshi?
"  Kucheza na wachezaji hao katika timu moja kumenifanya nijiami zaidi. Wamekuwa wanikiambia nifanye mambo yenye malengo kwa ajili ya mpira wangu katika siku za usoni. Wametokea kuniamini sana na kila mchezaji kijana kama mimi katika timu anajivuania kucheza kando yao. Ukitazama ushindani uliopo msimu huu utaona umuhimu wao kwetu ni wachezaji ambao wametufanya kuweza kuhimili vishindo vya ligi kuu msimu huu"
Pia mlinzi huyo anamtupia sifa nyingi kocha aliyemaliza muda wake, Hemed Morocco na kumuita kama mtu wa muhimu sana kwake. " Nawashukuru wazazi wangu kwa kunisapoti hadi hapa nilipo sasa, meneja wangu na kocha Hemed Morocco, aliniamini sana sitamsahau"

No comments:

Post a Comment