Search This Blog

Thursday, October 24, 2013

BRANDTS AWAPOZA KAVUMBAGU, CANNAVARO, CHUJI NA BARTHEZBAADA ya kutowatumia wachezaji wake wanne wa kikosi cha kwanza katika mchezo wa jana dhidi ya Rhino Rangers, Kocha wa Yanga, Ernie Brandts amesema amelazimika kuwapumzisha wachezaji wanne wa kikosi cha kwanza kutokana na uchovu.
Katika mchezo dhidi ya Rhino Rangers Jumatano iliyopita, Brandts hakuwatumia wachezaji Didier Kavumbagu, Athuman Idd ‘Chuji’, Nadir Haroub ‘Cannavaro’ na Ali Mustapha ‘Barthez’, lakini kikosi kilichoanza kiliweza kuibuka na ushindi wa mabao 3-0.
Tofauti ya Cannavaro na Barthez, Chuji na Kavumbagu wenyewe waliwekwa benchi lakini hawakuweza kupewa nafasi ya kucheza katika mchezo huo ulionekana kikosi cha Yanga kilichoanza kinaweza kuhimili vishindo vya Rhino.

Mara baada ya mchezo huo, Brandts aliuambia mtandao huu kwamba, hakuwachezesha wachezaji hao kutokana na kutumika katika mechi nyingi za Yanga hivyo aliamua kuwapumzisha ili watumike katika mechi zinazofuata.
“Ni kweli sikuwapanga Chuji, Cannavaro na wengine ambao mmezoea kuwaona kikosi cha kwanza kutokana na kuwa wametumika sana hivyo niliamua kuwapumzisha ili niweze kuwatumia katika michezo ijayo na sikuwa na maana nyingine nje ya hiyo.

“Yanga imesajili zaidi ya wachezaji 25, hivyo kutowatumia wachezaji fulani wa kikosi cha kwanza, haina maana kwamba wapo katika adhabu au kuna jambo tofauti lililotokea naomba nieleweke hivyo, mtawaona katika mechi zijazo hao wachezaji wala msiwe na shaka,” alisema Brandts.

Kikosi cha jana cha Yanga kiliwakilishwa na Deogratius Munishi ‘Dida’, Juma Abdul, David Luhende, Mbuyu Twite, Kelvin Yondani, Rajab Zahir, Simon Msuva, Frank Domayo, Hamisi Kiiza, Mrisho Ngassa na Haruna Niyonzima.
Katika kikosi hicho, Brandts aliwafanyia mabadiliko Msuva na Luhende ambao nafasi zao zilichukuliwa na Oscar Joshua na Nizar Khalfan.  

Yanga ambayo sasa ina pointi 19 katika mechi 10 ilizocheza, Jumanne ijayo inatarajiwa kucheza na Mgambo JKT katika muendelezo wa ligi hiyo kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam. Yanga inashika nafasi ya nne katika msimamo wa ligi hiyo yenye timu 14.

1 comment:

  1. shafii blog yako siku hizi ina boa inatia hata uvivu kuingia kila ukiingia habari ni zile zile tuu! kaa vipi bora radio mpya kila siku kuliko huku

    ReplyDelete