Search This Blog

Thursday, October 24, 2013

NURDIN BAKARI: TULIKOSA UMAKINI WA ‘MARKING’ TUKAFUNGWA NA YANGA



KIUNGO wa zamani wa Yanga anayechezea Rhino Rangers ya Tabora, Nurdin Bakari amesema kosa kubwa walilofanya katika mchezo wa jana na kufungwa mabao 3-0 na Yanga ni wachezaji wenzake kushindwa kuwakaba vyema wachezaji wa Yanga.
Nurdin amesema hata ukitazama mabao ya Yanga yalifungwa kutokana na uzembe wa mabeki wa timu yake kushindwa kuwakaba viungo na washambuliaji wa Yanga ambao kuna wakati walicheza wanavyotaka.

“Tumefungwa kutokana na poor marking (umakini mdogo wa kukaba), muda mwingi Yanga walikuwa wakicheza wanavyotaka na kupenya ngome yetu kirahisi. Lakini hili ni jambo la kawaida kwa timu hizi zinazokuwa zimepanda daraja kwa mara ya kwanza, nadhani baadaye mambo yanaweza kuwa mazuri na tutafanya vizuri zaidi,” alisema Nurdin.

Bao la kwanza la Yanga lilifungwa na Hamisi Kiiza dakika ya 12 akiunganisha vyema krosi ya Simon Msuva kutoka wingi ya kulia. Kiiza alifunga bao hilo akiwa katikati ya mabeki wa Rhino ambao ni Julius Masonga na Laslaus Mbogo ambaye amewahi kuichezea Yanga pia.

Bao la pili la Yanga lilifungwa na Frank Domayo dakika ya 72 akimalizia pasi nzuri ya Mrisho Ngassa akiwa ndani ya eneo la hatari la Rhino lakini mabeki hawakuweza kumkaba kiufasaha na kuweza kufunga kirahisi.
Yanga ilipata bao la tatu kupitia kwa Kiiza ambaye alimalizia vyema pasi ya Ngassa ambaye aliichambua safu ya ulinzi ya Rhino kutoka wingi ya kulia na kumpasia Kiiza aliyefunga kirahisi. 

Nurdin alienda mbali kwa kusema kuwa, kitu kingine kilichosababisha kipigo kwao ni kutokana kuwa na wachezaji wengi ambao hawana uzoefu wa kucheza Ligi Kuu ya Bara.
“Wachezaji wengi katika kikosi chetu hawana uzoefu wa kucheza ligi kuu, nadhani hilo nalo lilikuwa tatizo kwetu kuweza kuifunga na kuizuia Yanga kufunga nadhani tukikaa muda mrefu tunaweza kufanya vizuri zaidi,” alisema Nurdin.

No comments:

Post a Comment