Search This Blog

Monday, March 11, 2013

TFF YASEMA BADO TANZANIA HAIJAFUNGIWA ILA SERIKALI IKIENDELEA KUINGILIA SHUGHULI ZAO FIFA KUIFUNGIA TANZANIA

Shirikisho la Kimataifa la Vyama vya Mpira wa Miguu (FIFA) limesema litaifungia Tanzania iwapo itabainika kuwa Serikali imekuwa ikiingilia shughuli za Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF).

FIFA imesema kumekuwa na shutuma kupitia taarifa mbalimbali za vyombo vya habari nchini kuwa Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo imeonesha nia ya kuingilia uendeshaji wa TFF.

Kwa mujibu wa barua ya jana (Machi 10 mwaka huu) ya FIFA kwenda kwa Rais wa TFF, Leodegar Tenga, vyombo vya habari vimemkariri Waziri (Dk. Fenella Mukangara) kuwa Serikali imeiagiza TFF kutumia Katiba ya mwaka 2006 katika uchaguzi wakati tayari imeshafanyiwa marekebisho.

“Pia imeelezwa kuwa TFF imetakiwa kufanya Mkutano Mkuu pamoja na ule wa uchaguzi kwa tarehe ambazo zimepangwa na Serikali. Vilevile imeelezwa kuwa Serikali inakusudia kuunda Kamati ya Muda iwapo TFF haitatekeleza maagizo yake,” imesema sehemu ya barua hiyo iliyosainiwa na Katibu Mkuu wa FIFA, Jerome Valke.

FIFA imesema iwapo yaliyoripotiwa na vyombo vya habari yatathibitika kuwa kweli, maana yake huo ni uingiliaji wa wazi wa Serikali kwa shughuli za TFF.

“Tunapenda kuwakumbusha kuwa wanachama wote wa FIFA wanatakiwa kuendesha shughuli zao kwa uhuru bila kuingiliwa na mtu mwingine kama ilivyoelezwa katika ibara za 13 na 17 za Katiba ya FIFA.

“Hivyo kama maagizo hayo yanayodaiwa kutolewa na Serikali yatatekelezwa, suala hili litapelekwa katika mamlaka za juu za FIFA kwa hatua zaidi ikiwemo kuisimamisha Tanzania kama ambavyo inakuwa pale panapokuwa na uingiliaji wa Serikali,” imesema barua hiyo.

Barua hiyo ambayo nakala yake pia imetumwa Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika (CAF) imeelezea baadhi ya athari ambazo Tanzania itakumbana nazo endapo itasimamishwa ni timu za taifa pamoja na klabu kutoshiriki mechi za kimataifa kwa mujibu wa Ibara ya 14 ya Katiba ya FIFA.

Vilevile si TFF au wanachama wake na maofisa wengine watakaoweza kunufaika na programu za maendeleo, kozi au mafunzo yanayotolewa na FIFA na CAF.

“Madai ya uamuzi uliofanywa na Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo ni ya kusikitisha kutokana na ukweli kuwa FIFA ilishatangaza itatuma ujumbe wake kuchunguza jinsi hali ilivyo kwa sasa na kutoa mapendekezo yake. Kutokana na hali hii, ujumbe wa FIFA uliokuwa uje kuchunguza (suala la uchaguzi) itabidi usubiri kwa vile ni muhimu kushughulikia tatizo hili kwanza.

“Katika mazingira haya tunaomba ueleze msimamo huu wa FIFA kwa mamlaka zinazohusika (Serikali) na athari ambazo mpira wa miguu wa Tanzania utakumbana nazo. Tunakushuru na tunatarajia utatufahamisha kila hatua inayoendelea katika suala hili,” imesema barua hiyo.

Boniface Wambura

6 comments:

  1. Hivi Tenga na wenzako mna nini humo TFF?mbona mtaka kuendesha chombo cha uumma kama vile NGO?Hamuoni hata aibu mbele ya macho ya Watanzania mmetanguliza uchu wenu badala ya maendeleo ya mpira?

    ReplyDelete
  2. na tunakoelekea ni kufungiwa tu. tumekuwa tukishabikia sana porojo za akina maiko wambura na wapambe wao na kupelekea serikali kukurupuka kwa kufanya maamuzi ambayo tayari TFF, FIFA , na vyombo vyake vilishaanza kuyafuatilia

    ReplyDelete
  3. sometimes FIFA is like a criminal hiding place

    ReplyDelete
  4. binafsi naamini FIFA wamepewa taarifa isiyo sahihi na yawezekana na baadhi ya watendaji ndani ya TFF, ingelifaa huo ujumbe wa FIFA uje upate taarifa zote toka pande zote kisha ujiridhishe nani ni mkweli

    ReplyDelete
  5. bora tufungiwe kuliko kushiriki miaka yote bila mafanikio

    ReplyDelete
  6. Hayo ndio tunayoyataka kwani hatuoni faida ya kuwa na TFF wababaishajI,Wapindishaji wa sheria na wapenda pesa.Nadhani kwa nasfi yangu bila kumung,unya ni afadhali kufungiwa na FIFA ili turekebishe makosa yetu kuliko kuburuzwa na wanaojiita viongozi wa TFF.Ni wanafiki wakubwa wanatupandikizia viongozi wasio na mwelekeo.Mbona serikali ilipoleta kocha toka Brazil hamkusema serikali inawaingilia.Yaani muachiwe mpindishe sheria kwa mapenzi yenu serikali iwaangalie tu.Big up mama endelea kuwakaba mpaka kieleweke sio kupandikiza macollege met katika uongozi

    ReplyDelete