Search This Blog

Friday, March 1, 2013

RAGE AMESOMA NA KUELEWA KITABU CHA KROENKE NA HILLWOO





Miaka 12 iliyopita nilikua na umri wa takribani miaka 8, Katika umri huo nilikua na akili ya utambuzi wa mema na mabaya. Darasa langu la tatu lilitosha kujua nini Wazazi wanapenda nifanye na nini hawataki kusikia nafanya. Japo ilikua ngumu kutimiza matakwa yote ya wazazi ila nilijaribu kuwaridhisha. Kati ya mambo ambayo wazazi wangu walichukia ni mchezo wa mpira wa miguu,hapo ndo kulikua na kazi,nilipopenda sana wao ndipo walipochukia sana. Nikakubali kuitwa mtoto msumbufu,mjeuri,mkaidi na majina mengine mengi mabaya kwa ajili ya huu mchezo. Wazazi hawakuishia hapo kila waliposikia nimeenda kucheza mpira jioni yake sebule hujaa fimbo nyingi, ungefikiri sungusungu wanafanya maandalizi kwa ajili ya kwenda kukamata na kupiga waarifu usiku huo, La hasha fimbo zote zilikua zinasubiri mwili wangu mdogo mfano wa fidodido. Nakumbuka nilikua Napata kipigo mithili ya mbwa mwizi. Lakini fimbo hizo hazikunizuia kesho yake kuibuka kwenye kiwanja changu cha koloni kilichopo mpakani mwa Vingunguti na Tabata na kuendelea kula ladha za sembo, nyuzi banana au kipere pasi na kukumbuka kipigo cha jana nillichopewa na bi mkubwa. Kabumbu litasakatwa mpaka mishale ya saa 12 na nusu jioni. Kila mmoja na njia yake kuelekea nyumbani kwake, hapo ndipo mafua ya ghafla yanaponianza sambamba na moyo kudunda mara 180 kwa dakika, huku nikihisi kibofu cha mkojo kinataka kupasuka. Hiyo ilikua ni hofu ya bakora kutoka kwa mama au baba. Nisipowakuta wazee nyumbani hua nafanya kazi nyingi za nyumbani hata zile zisizonihusu ili nifunike kombe mwanaharamu apite. Lakini sikuweza kuwashawishi mahakimu wangu kuwa huru na adhabu ya bakora. Ikafika kipindi ikawa ratiba niliyoizoea, asubuhi naenda shule nikitoka shule naelekea viwanja vya soka nikirudi nyumbani nachezea fimbo kabla ya kwenda kulala.

Nikaendelea kukua kiumri pia kiakili, siku moja nikamuweka mama kitako na kumuuliza “Mama kwanini hutaki na hupendi nicheze mpira?” Mama akanijibu “nakupenda sana mwanangu, sitaki uharibikiwe kama watoto wengine (huku akitoa mifano ya watoto hao kwa majina), wamepoteza muda wao mwingi kwenye michezo, shule imewashinda ona walivyo sasa hawana mbele wala nyuma(mama aliendelea)” Akaniuliza na wewe unataka kuja kua kama wao? Nikajibu kwa haraka “hapana mama” “basi mwanangu soma sana ili uje kua daktari, engeneer, au mwalimu achana na habari za mpira hakuna mtu aliyefanikiwa kwa mpira mpira wa miguu”. Maneno ya mama yaliniingia na kugusa moyo wangu, hasa pale nilipogeuza shingo yangu na kuangalia maisha ya wachezaji soka mashuhuri mtaani kwangu, niliangalia maisha ya Athumani Machepe aliyekua akiichezea Simba, sikuona tofauti yake na kijana asiye na ajira kwa kipindi hicho. Si machepe peke yake bali kuna wachezaji wengi wa miaka ya nyuma walipata kuwa maarufu sana huku mifuko yao ya suruali ikiwa imetoboka. Hao ndo wasakata kabumbu wa zamani, walikua na uzalendo na mapenzi thabiti na soka.

Achana na Habari za mwanzoni mwa karne ya21, siku hizi kuna MAONO MAPYA YA DUNIA. Ndani ya maono hayo kuna bosi na kiongozi mmoja tu. Bosi huyo ana majina mengi kwa kila nchi na kwa kila kabila,wengine watamuita maela, faranga,kwacha, yen, dollar, shilingi na kwa majina ya jumla anaitwa money au Pesa. Majina ya bosi huyu ni mengi lakini yana maana, lengo na kazi zinazofanana. Miaka ya nyuma ili uheshimike kwenye jamii ilikua lazima uwe na elimu, hapo utashinda dhidi ya umma. Lakini Maono mapya ya Dunia Hayatambui Elimu juu ya heshima, Maono mapya ya Dunia yanaamini Mtu mwenye busara, Hekima na kustahili kuheshimiwa ni yule mwenye pesa. 


Uingeneer, Udaktari, ualimu wako bila shekeli hakuna atakayetambua, kuthamini wala kuheshimu taaluma yako. Kwenye Dunia yetu mpya kila kitu pesa. Kinachonifurahisha zaidi hata kwenye ulimwengu wetu wa soka pesa ndiyo inacheza mpira, Wazungu wanasema “Money plays Football” Siku hizi Wazazi Wanaupenda na kuheshimu mchezo huu sababu ya pesa. Ni wazazi wachache sana wanawazuia watoto wao kucheza soka. Mbwana Samatta, Mrisho Ngassa na Juma kaseja wamefanya wazazi kuwahamasisha watoto wao kucheza mpira, miaka hii ya mpira pesa ukiomba hela kwa ajili ya njumu itawahi kuliko pesa ya daftari na peni, Sammata na gari lake anatafuta wapi pesa zake atawekeza huku injinia mwenye degree yake kila siku kwenye daladala na vyeti akitafuta ajira. Hiyo ndo Heshima ya soka bwana.

Katika miaka ya karibu tumeona mabilionea kama Moize Katumbi chapwe kutoka kongo, Patrice Thopane Motsepe wa South Afika, Said Salim Bakhresa wa Tanzania na wengine wengi wamewekeza zaidi kwenye soka na kufanya soka letu Afrika liwe la ushindani. Leo hii Teko Modise anaheshimika kuliko viongozi na watu wengi maaarufu wa mjini kwao SOWETO, Tresor Mabi Mputu ndiye mfalme wa KINSHASA, John Boko amekua maarufu kuliko vibopa wa Sinza na Kijitonyama, hiyo ndo heshima ya pesa za Motsepe, Bakhresa na Katumbi.

Lakini kwenye Ulimwengu huu huu wa mpira pesa kuna watu wajanja wajanja, wenye pesa kiasi wanaojua kuwatumia wachezaji kuchota pesa za kina Motsepe, Bakhresa na Katumbi.Wengi wao huwa wenyeviti au viongozi wa ngazi za juu kwenye timu husika. Kule Uingereza utamkuta mwenyekiti wa Arsenal, Bwana Peter Hillwood hakuna Arsenal bila Hillwood, babu yake mzee Samwel Hillwood alikuwa mwenyekiti wa Arsernal mnamo mwaka 1926-1936 na 1946-1949, pia baba yake mzee Dennis Hillwood alipata kuwa mwenyekiti wa Arsenal mnamo mwaka 1962-1982 kabla ya kufariki na mtoto wake Peter Hillwood kushika hatamu mpaka hivi leo. Peter Hillwood, Ivan Gazids na Mjasiliamali wa kimarekani Stan Kroenke hawa ndo wanaounda CC(central comitee) ya Arsenal. Watu hawa wamejaa siasa na roho ya ujasiliamali zaidi, akili yao yote ipo kwenye kutengeneza pesa kuliko kuimarisha na kujenga timu ya upinzani. Mungu awape nini watu hawa? Wamepata na kocha Mchumi anayejua kucheza na akili ya mashabiki. Profesa Wenger miaka 8 bila kombe ameingiza zaidi ya paund 50 million kama mshahara, Huku akina Piers Morgan na washabiki wenzake wa Arsenal wakiumia juu ya mwenendo wa timu wa kutoka kapa kila msimu, sambamba na kuuza wachezaji nguli bila kutafuta mbadala sahihi, CC ya Arsenal na Wenger wao hutazama kwenye zizi na kutafuta kondoo aliyenona kwa ajili ya kuuza na mwisho wa mwaka kugawana marupurupu kutokana na faida ya kondoo huyo. Hawa kwa kiasi wameifanya Man City iitwe Man city,wamejua jinsi ya kufyonza pesa za Sheikh Mansor, huku wakiumiza mioyo ya mashabiki wa arsenal

Hapa kwetu Bongo yupo fundi aliyepata mafunzo kama ya CC ya Arsenal japo kwenye vyuo tofauti. Si mwingine yeye anaitwa Mh. Aden Rage, mtu huyu amejaaliwa fitina ya soka, siasa pamoja na ujasiriamali. Mashabiki wa msimbazi nikiwauliza mbadala wa Samatta ni nani hawatanipa jibu, ila Rage kawapa kibuli cha kujisifu kwa kumuuza Samatta kwa mamilioni ya pesa. Hayo mamilioni ya Samatta yameenda wapi? au yameifanyia nini Simba hilo ndo swali la kujiuliza kama mshabiki wa Simba,vipi kuhusu  Okwi? Kama mmeshindwa kuhoji pesa zilipoenda hojini hata mbadala wa wachezaji hao. Simba ya sasa ina baadhi wachezaji wa kawaida na wasio na hadhi ya kuchezea Simba si kwenye mashindano ya kimataifa pekee bali hata ligi ya ndani. Sina uhakika kama Rage alikua anamtaka Yondani au pesa za usajili za Yondani? Si vibaya Simba kuuza wachezaji nje ya nchi, ni vizuri sana hasa kwa maendeleo ya soka letu kwa ujumla, tatizo lipo kwenye mbadala wa wachezajiwaliouzwa. Leo hii Haruna Chanogo, Singano na Chris Edward wanapewa majukumu makubwa kuzidi umri wao.

Si lazima uwe mshabiki maarufu wa Simba kama Mzee Magoma moto au Mshabiki Nguli wa Arsenal kama Piers Morgan ili uwe na machungu juu ya kupotea kwa ladha kutoka kwenye timu hizi zinazoongozwa na wajasiliamali waliojaa siasa za soka

By kaijage jr

middle ya juu

15 comments:

  1. Umetoa maoni na maono ya hali ya juu sana ila kwenye tamat hujatuonesha ufumbuzi,unajua na upo makini na kazi yako but hii inatakiwa iwe na part 2 kaka

    ReplyDelete
  2. Yani hapa Rage ndio kabolonga kuliko wote ni bora ya Wenger ye timu yake ina uwezo kifedha ila kwa Rage mmh.

    ReplyDelete
  3. Umetisha ile mbaya bonge la makala upo sahihi kwa kila ulichokiandika hongera sana.

    ReplyDelete
  4. GOD is say in the Holly Qur an: Qulil Hakk Wa-inkana Murrah (Sema Kweli hata Chungu). Ulichoandika hapa Kaijage Jr aka Middle ya Juu ni kweli inayoweza kuumiza na kuchoma mioyo ya wasiokubali/wasiotaka kuambiwa ukweli.

    Nakutakia kila la kheri katika kusema ukweli ambao kwa mujibu wa Qur an ni Ibada. Kinachojiri Gunners na hapa kwa Wekundu wa Msimbazi, hasa kutoka kwa viongozi wa aina hiyo kinakera na kurudisha nyuma maendeleo ya timu ikiwamo ustawi wa soka la wachezaji wengine klabuni ambao wangejifunza kupitia kwa wakali wanaouzwa bila nafasi zao kujazwa. Keep it tight Chief.

    ReplyDelete
  5. Duuuuu unatisha kaka..umemsahau kaburu pacha wakeee....

    ReplyDelete
  6. Duuuh gud analysis.. Safi saana umetoa picha ya mbali sana kwa kina. Mwenye akili atakuelewa kaka. Gday.

    ReplyDelete
  7. Wajanjawajanja kama Rage hawatufai kwenye soka wanachojua ni kucheza na mind za watu.

    ReplyDelete
  8. Habari Nzuri Saana Ila Mie Ningetaka Kujua Huyo Ambae Unamsema Alikuwa Anachapwa Kwa kwenda Kucheza Koloni ni Nani ...?? Maana Story Zipo Mbili Ingawa Kichwa cha Habari ni Kimoja ...Then Kinachoniuma Kingine Hizi Timu Zote ni Zangu Yaani Na Maumivu Nje na Ndani .... Lkn Hatuwezi Fanya Lolote juu Ya Malalamiko Yetu Kuwekea Ukuta Wa zege Na Hawawezi Hata Kutusikiliza Ju Ya yote .... ...

    Antary wa Sweden

    ReplyDelete
    Replies
    1. kaka story moja jaribu kutengeneza link,hapo nilikua naonyesha jinsi gani soka lilivokua linadharauliwa miaka ya nyuma tofauti na siku hizi,ila kuna watu wameelewa vibaya kama si kuelewa sana somo la mpira pesa kwa kujali matumbo yao.

      Delete
  9. umetisha kaka rage na kaburu wasome nyakati

    ReplyDelete
  10. Hakika wewe na mwanazuoni mahiri na makini katika tasnia ya habari na mawasiliano kwa umma katika divisheni ya soka.Asante sana kwa uchambuzi wako.

    ReplyDelete
  11. zakayo mwalongo benitezMarch 2, 2013 at 12:54 PM

    what an article sikutegemea kama Allen ungeandika something sincerely kihivi maana ninavyokujua! ha ha ha ha, all the way good Analysis, nasubiri article inayohusu my team @KaijageJr

    ReplyDelete
  12. Wazo zuri Sana kwa Watanzania! Dunia imebadilika,tusikalili Kazi, tuangali riziki inapoweza kupatikana kutokana na rasilimali ulizonazo.

    Pengine kuna ukweli kuwa Rage anacheza na Akili za mashabiki, Lakini siafiki kama tunamsikiliza wote hawafahamu. Simba na Yanga ni timu ambazo zina Ujinga sawa, labda Yanga,wanaweza wakawa sasa wameelewa Baada ya kupitia mikasa kadhaa tokea Mpondela aonekane hafai. Simba pia, sio kuwa washbaiki wa Simba hawaoni,bali wengi wenye kuona hayo, sio eneo lao la chakula.

    Washabiki wengi wa timu hizi wenye upeo wa kuweza kufanya mabadiliko ni watu ambao mpira ni burudani,na sio sehemu ambayo imeshikilia maisha yao na ndio maana hata wakati wa uchaguzi wengi wao huwaoni. Ukiangalia wakati Rage na Kaburu wanachaguliwa unaweza kuona, jinsi mgombea anavyoweza kuongea na ukakadiria ni asilimia ngapi ya wanachama wanaweza kuchanganua yanayosemwa. Wajinga ndio Waliwao. Siku za nyuma kidogo tu, mtu aliweza kuchaguliwa kwa sababu tu ameahidi kuwafunga Yanga,na watu wanaamini ana mbinu fulani za kukamilisha hilo. Kwa hiyo, mashabiki wa Simba wenye upeo huo, hawana nguvu hiyo,wamezidiwa na wale wanaofanya pale shamba la bibi,wakati uwezo wa kuchanganua na kupanga kwa ajili ya timu ni mdogo. Anapotokea mtu mwenye lengo zuri, na uono mkubwa, maana yake timu itatengamaa, hawa walaji watakosa pa kulia. Hivyo,lazima atashambuliwa mpaka aondoke. Na ukiona, kuna utulivu,ujue kundi hilo linalochuma pale linapata kinachokihitaji! Pale itakapotokea tu kuwa CHAKULA itaondoka,moto lazima uwake. Naamini haya yaliwakuta wafadhili Kama Mohammed Dewji. laipotaka tu kuweka utaratibu ambao hela yake iwe effective kwenye timu na sio kwa wapambe,mambo yakaharibika. Japo,utaambiwa mambo mengi! Yanga,nawasihi wasifanye kosa kama sisi tena!

    Kwa hiyo,mambo ya kusema hiki ni kipindi cha mpito,kama vingine ni sawa, lakini dunia imebadilika, na tanzania imebadilika, na watu pia wamebadilika,tuniona AZAM na kujifunza mengi juu ya ujinga wetu.Na nahisi,huwa hizi timu zina kauhusiona na dola yetu,na kwa kutambua umuhimu wake viongozi kwenye dola yetu huwa baadae wanatoa mashinikizo yao ili kuziokoa,ndio maana hujitokeza tena watu kama MOH, na kutoa pesa zao nyingi kwa kuamini baadae timu zikiwa safi,wanaweza kuinvest! Na kwa kweli,panavutia sana,na pana pesa nyingi saaana!

    Mimi naamini, wakati wa uchaguzi, washabiki wa Simba walifanya uamuzi sahihi kutokana na wagombea waliokuwepo na sera zao. Tunachagua kulingana na vigezo tulivyojiwekea, kama viongozi wanakuwa wabovu,tubadili vigezo,ili tupate viongozi wazuri. Na Simba kama Tanzania tu, matatizo ni mengi kuliko kipato,na kama wanaokuzunguka hawakupendi kwa kuamini unafaidi,hata ukiwa na nia nzuri huwezi kufanya kitu mpaka uwe na pesa, Mpira Pesa.

    Suluhisho: 1. Serikali ya Tanzania itambua waziwazi kuwa Mpira ni ajira kubwa na hivyo kudhoofisha mpira ni kupoteza mapato na ajira , ni hasara kwa Taifa,hivyo mtu anayeonekana kwa namna moja au nyingine anaweza kuwa anadhoofisha timu, imchukie kama mhalifu wa uchumi mwingine,kwa kupitia mikono yake iangalie itafanyaje kuwaokoa wananchi wake,ambao wakati fulani huwa wanaibiwa kwa waziwazi ila tu hawajui wafanye nini,wasisubiri moto uwake.

    2. Kuchukia uongozi, sio suluhisho,uongozi utafika mwisho wake tu. kikubwa ni Mashabiki,kupitia katiba,kudai yaliyo ya msingi na hasa yaliyoahidiwa. Mfano: Uwanja

    3. Vyombo, vya habari,ndio vinaongoza kusifia hata uozo,ili mradi kufanya biashara,washabiki wenye maono mazuri tuvifokee,kupitia vyombo vya habari vinavyosema ukweli.

    4. Mashabiki tuache ushabiki wa kizamani, tupende ubora na tudai haki zaidi ya kufurahi, kama vile umiliki,sio kuwa nakadi za kujitambia mitaani.

    5. Mwisho, Pesa iwepo kwenye vigezo cha kupewa uongozi!

    SIMBA INAPOVURUNDA NDIO NAIPENDA SAAANA!

    ReplyDelete
  13. kiukweli sasahivi shaffih hauna kitu kabisa katika hii blog yako kiufupi you are lazy maana hau badiliki kabisa mpaka ujisikie kuweka news update ndo unafanya unahabari za toka juzi yani haufai kabisa tena kabisa mpaka naona uvivu sikuizi kukufubngua thats why huna jipya so badilika uturudishie imani

    ReplyDelete
  14. mambo shwari kaka umetisha

    ReplyDelete