Search This Blog
Tuesday, March 12, 2013
KALI YA LEO: RAFU ACHEZA CHOLLO KADI APEWA AMRI KIEMBA
KIUNGO wa Simba, Amri Kiemba amemlaumu mwamuzi, Martine Saanya wa Morogoro kwa kumwonyesha kadi ya njano kwenye mchezo wa Coastal Union pasipo kuwa kosa lolote.
Katika mchezo huo, uliopigwa Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam jana Jumapili, Simba iliibuka na ushindi wa mabao 2-1 na kujiweka katika nafasi ya tatu na pointi 34.
Kiemba mwenye mabao saba kwenye ligi alisema; "Kadi ile alistahili kupewa Chollo aliyechezea rafu mchezaji wa Coastal. Lakini nashangaa ananionyesha mimi pasipo kosa lolote. Nilimweleza kuwa aliyecheza rafu ile ni sio mimi bali ni Chollo. Lakini hakutaka kunielewa."
Kiungo huyo wa Simba na Taifa Stars alisema, Shirikisho la soka Tanzania (TFF) linatakiwa kuwa makini na waamuzi kwani kuna wakati wamekuwa wakitumiwa na watu fulani kupindisha kanuni na sheria 17 za soka.
Beki wa Simba, Nassoro Chollo ndiye aliyemchezea rafu Twaha Hussein wa Coastal Union na mwamuzi kutoa faulo lakini alikosea kumwonyesha Kiemba kadi hiyo, badala yake alitakiwa
kumpa Chollo aliyecheza rafu.
__
PAMOJA na Simba kuilaza Coastal Union mabao 2-1, ililifikia lango la wapinzani hao mara 17 na kupiga mashuti manane yaliyozaa kona sita tasa na mabao mawili.
Katika mchezo huo, uliopigwa Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam jana Jumapili, kocha wa Simba, Mfaransa Patrick Liewig aliwatumia wachezaji watano vijana kwenye kikosi cha kwanza.
Hali hiyo iliwashtua kidogo mashabiki wa Simba, lakini kadri muda ulivyosonga mbele walianza kufurahi kutokana na vijana hao kucheza soka la kasi na utulivu mwingi.
Mfungaji wa bao la kwanza la Simba, Mrisho Ngassa aliongoza kupiga mashuti langoni mwa Coastal Union. Bao la ushindi kwa Simba, lilifungwa na Haroun Athuman 'Chanongo' dakika mbili kabla ya mapumziko.
Kati ya mashuti manane yalipigwa na timu hiyo, Ngassa ambaye ni mshambuliaji wa Simba na Taifa Stars alipiga manne, matatu yakienda fyongo na moja kutikisa nyavu za Coastal.
Kwa upande wa Coastal, ilibisha hodi kwenye lango la Simba mara 11 na kufumua mashuti tisa ambayo yalizaa kona mbili tasa na bao moja lililofungwa na kiungo Razack Khalfan ambaye ni mdogo wake Nizar Khalfan wa Yanga.
Pia, Coastal iliibuka vinara wa kutoa mipira nje ya Uwanja kwa lengo la kutibua mashambulizi ya Simba. Ilitoa mipira 23 wakati wenyeji wao Simba wakitoa mara 16.
Katika hatua nyingi, Simba ilicheza rafu saba dhidi ya 10 za wageni Coastal Union ya Tanga. Rafu hizo zilimfanya mwamuzi Martin Saanya wa Morogoro kuwalima kadi za njano Amri Kiemba na Haroun Athuman 'Chanongo' wa Simba, Hamis Mbwana na Soud Mohamed wa Coastal.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment