Search This Blog

Tuesday, February 19, 2013

DIRA YA HAMASA YA KANDANDA NCHINI
Na Gwandumi Gwappo Atufwene Mwakatobe
(Mratibu wa Kujitolea wa Kuibua na Kufufua Vipaji – Mwakaleli, Busokelo)
Februari 2013

1.    Utangulizi

Tukiwa katika mchakato wa kupata viongozi wapya wa Shirikisho la Kandanda Tanzania (TFF) ambao awali ulipangwa kuhitimishwa Februari 24, 2013, nimeona nichukue fursa hii kuainisha nini kifanyike na kubainisha masuala ya msingi ya kuleta hamasa mpya ya kandanda nchini. Aidha, rais anayemaliza mihula miwili ya jumla ya miaka nane Leodgar C. Tenga alisema tunaorodhesha matatizo bila kuyapatia ufumbuzi na akasema ameacha utawala (taasisi) inayofanya kazi kwa uhuru. Haijaniingia akilini hata kidogo, kuwa tunaorodhesha matatizo lakini tuna rais aliyekaa miaka nane hakutupatia ufumbuzi wa matatizo hayo! Je, alitaka tuorodheshe matatizo na tuyapatie ufumbuzi sisi wenyewe? Sawa, lakini kazi ya kiongozi ni kuonesha njia pale ambapo wengine hawaoni na kutoa ufumbuzi wa matatizo yetu.

Ieleweke kwamba kandanda si fani au tasnia ya kukaa ofisini na mafaili kibao ya kiutawala na kusuluhisha migogoro kwa kuunda idara mbalimbli na kamati lukuki. Kama ni kupanga safu ya uongozi isingeweza kuchukua miaka nane, naamini hata mwaka mmoja tu ingewezekana. Hata hivyo, haya ni maelekezo na ufadhili wa FIFA duniani kote na si mipango ya mtu fulani TFF. Kukua kwa kandanda ni kufuzu michuano ya kimataifa, kutwaa mataji, kuzalisha wachezaji wa viwango vya kimataifa na kuwa katika viwango vya juu vya FIFA katika ubora wa timu za kitaifa duniani. Takribani miaka 33 hatujafuzu michuano mikubwa barani Afrika na duniani. Libya walishiriki kombe la mataifa ya Afrika wakiwa vitani; Afrika Magharibi au Kaskazini hawakosi AFCON japo hawana michuano ya kila mwaka kama CECAFA ilikofuzu timu moja tu ya Ethiopia. Mataifa 8 ya Afrika Magharibi yalifuzu AFCON 2013 Afrika Kusini (Cape Verde, Kodivaa, Mali, Burkina Faso, Nigeria, Ghana, Togo na Niger), na saba yaliingia robo fainali. Hawana utawala bora, ila wana shauku ya mafanikio kimpira.

Tuna amani na watu wapenda kandanda, lakini kasumba ya watendaji wa TFF ni kukaa ofisini wakidai kazi si yao kwenda chini kuibua vipaji na kuamsha hamasa ya mafanikio kimpira. Hawajui kuwa wanaongoza kandanda ya nchi nzima na si kwenye majengo yaliyoko uwanja wa Karume. Miaka nane ya Tenga imepata ufadhili mkubwa wa makampuni binafsi na serikali yetu, lakini hatuna cha kujivunia kimpira. Kalusha Bwalya atasema alipokuwa rais wa FAZ (Zambia) walitwaa kombe la mataifa ya Afrika nchini Gabon; Ledgar Tenga anaondoka madarakani hata kushiriki tu mashindano hayo imebakia ndoto. Atataja tu mafanikio yake binafsi na kujulikana FIFA na CECAFA huku nchi ikiambulia patupu! Hatutaki hayo kwa viongozi wapya. Hapa chini naainisha njia sita za kuamsha upya hamasa ya kandanda nchini na kuwika kimataifa.
2.    Dira ya Kuleta Hamasa Mpya ya Kandanda Nchini Katika Maeneo Sita

v  Viongozi wa TFF wawe mstari wa mbele na kushiriki kikamilifu kutambua, kuibua, kuamsha hamasa na kuwaendeleza vijana wanaoonesha vipaji, shauku na uwezo wa kusakata kandanda popote walipo nchini. Waache kukaa ofisini kula posho za FIFA na vikao visivyoisha. Waende kuwatia moyo vijana walioko Nanyamba Mtwara, Kamachumu Muleba, llagala Kigoma, Kaliua Tabora, Mwakaleli Mbeya na kwingineko nchini. Inatia shaka na aibu kwa TFF kuona kijana kama Juma Omar toka Mpanda, mkoani Katavi, aliyeonesha shauku na jitihada za kipekee za kutembea kwa miguu toka Morogoro hadi Dar es Salaam kutimiza ndoto yake, lakini hakuna kiongozi yeyote wa TFF aliyejali na kutambua kipaji cha kijana huyu! Je, ni nani awe wa kwanza kama si TFF, kuwajali na kuwaendeleza vijana waliokwenda Brazil na kutuletea ushindi? Nauliza, nani awaendeleze vijana wanaoshiriki michuano ya cocacola kila mwaka?

Ili kijana yeyote mwenye kipaji cha kusakata kandanda awike lazima awe na sifa kuu tatu: Umri, uwezo na umbile stahiki; na pia anahitaji vitu vitatu: uwezeshaji (facilitation), kujulikana (exposure) na mafunzo (training). Mahitaji hayo sita (umri, uwezo, umbile stahiki, uwezeshaji, kujulikana na mafunzo) ndio nguzo au mihimili mikuu sita inayotengeneza magwiji wa kusakata kandanda (The six pillars for soccer legends in the making). Vijana wenye uwezo na maumbile stahiki tunao, hususan kwenye maeneo yenye chakula kingi na hali ya hewa nzuri. Ni kazi ya TFF, na si kila wakati vilabu, kuwawezesha vijana hawa na kuwatangaza ili wajulikane kitaifa na kimataifa, na kuwapa au kuwaelekeza mahali pa kupata mafunzo na/au kulelewa.

v  Pawepo na mashindano mengine ambayo yawe ya mtoano mbali na Ligi Kuu ya Vodacom. Yahusishe timu zinazoshiriki ligi kuu na timu za madaraja mengine mikoani na wilayani ilimradi tu ziwe zimesajiliwa rasmi na kumudu baadhi ya gharama za ushiriki. Kombe litakaloshindaniwa ndilo liitwe Taifa Cup au Nyerere Cup kumuenzi Mwalimu Julius Nyerere ambaye akiwa madarakani tulishiriki kwa mara ya kwanza kombe la mataifa huru ya Afrika mwaka 1980. Washindi wa Taifa Cup washiriki mashindano ya kimataifa barani Afrika yaani kombe la CAF, badala ya mshindi wa pili wa ligi kuu ambapo kwa sasa wanashiriki Azam. Timu inayotwaa ubingwa wa ligi kuu ibakie kushiriki klabu bingwa Afrika ambapo sasa wanashiriki Simba. Endapo timu moja itashinda ligi kuu na Taifa Cup, basi ya pili Taifa Cup ituwakilishe CAF.

Mantiki ya kuwa na mashindano mengine inatokana na ligi kuu kuwa na timu chache na mzunguko mfupi unaowafanya wachezaji kukaa bila kucheza wakisubiri mzunguko mwingine. Ari ya mashabiki na viwango vya wachezaji hushuka kwa kukosa mazoezi na michuano mingi. Wachezaji wetu wanaishia tu kucheza ndondo au kombe la mbuzi ambalo haliwapeleki popote. Aidha, mashindano mengine yatatoa fursa ya vijana wengine kuonesha uwezo na vipaji vyao pasipo kutegemea ligi kuu pekee yenye timu chache na mizengwe mingi. Nchi nyingi zina ligi kuu na michuano mingine inayoshirikisha timu za ligi kuu na za madaraja ya chini. Timu za Uingereza zinashiriki Ligi Kuu, Capital One, Kombe la FA, na zingine hushiriki michuano ya ulaya. Timu moja inaweza kuwa na mashindano ya makombe manne kwa mwaka!

v  Tuamue sasa na kuchagua timu moja ya vijana (The dream team) itakayoshiriki mashindano yote ya kimataifa, yaani mashindano ya kufuzu fainali za kombe la vijana la Afrika, mashindano ya kufuzu fainali za kombe la mataifa ya Afrika 2015, mashindano ya Olimpiki, mashindano ya kufuzu fainali za kombe la vijana duniani na mashindano ya kufuzu fainali za kombe la dunia mwaka 2018 nchini Urusi. Tuache kasumba ya kila siku kubadili wachezaji wa timu ya taifa na tuhakikishe tunaibua vijana kutoka kila kona ya nchi badala ya kutegemea tu wale wanaocheza ligi kuu na hasa kuangalia tu walioko Simba na Yanga. Nimeona vijana walioko Lwangwa (Busokelo) wanaoweza kushiriki michuano ya kimataifa kuliko walioko Simba na Yanga. Nimewahi kuona vijana walioko Mwandiga Kigoma, Pawaga Iringa, Mwaya Morogoro, Chiola Rwanga (Lindi), Maramba Tanga na Kisesa Mwanza; ni wazuri mno kuliko walioko Simba na Yanga. TFF itoke nje ya Karume, ione vipaji pande zote za nchi na si kukomalia tu Dar es Salaam. Na kwa dira hii, mwalimu wa timu ya taifa awezeshwe kuzunguka nchi nzima kuona na kuibua maajabu ya vipaji vya akina Pele wa karne ya 21 wanaoozea vijijini.

Lazima tuwe na mahali pa kuanzia. Nchi zote zinazopata mafanikio makubwa ya kandanda kimataifa zinaanza na kizazi fulani cha wachezaji na kuendelea nao haohao pasi na kubadili kila mara. Sambamba na kizazi hicho, tutakuwa tunaandaa kizazi kingine (succession dream team or generational backup dream team), kitachobadili kizazi kinachotangulia. Nigeria walianza na kizazi cha akina Stephen Keshi kilichokuja kutwaa kombe la mataifa ya Afrika mwaka 1994, wakati huohuo waliwaandaa akina Nwanko Kanu waliokuja kuwarithi akina Stephen Keshi. Senegal walianza kuandaa kizazi cha timu ya vijana mwaka 1992, miaka kumi baadaye wakashiriki fainali za kombe la dunia nchini Korea Kusini na Japan mwaka 2002 na kuwatandika mabingwa wa dunia Ufaransa. Mifano ni mingi, itoshe tu kusema bila kuwa na pa kuanzia na kupaendeleza pasipo kubadilibadili (consistently), tutaendelea kutapatapa tu na kufumua timu ya taifa kila siku.

v  Tuanze mwaka huu kuwa na utaratibu wa kuwaenzi wachezaji wastaafu waliolitumikia taifa kwa uzalendo wa hali ya juu na kutufikisha mbali kimataifa. Kipimo iwe ni kushiriki fainali za kombe la mataifa ya Afrika na/au fainali za kombe la dunia. Napendekeza kikosi chochote kitakachoshiriki fainali kama hizi, TFF kwa kushirikiana na serikali na wadau wa kandanda nchini, watuongoze kuwajengea nyumba za kisasa badala ya kuwapa fedha taslimu. Na kwa maono haya, kikosi cha taifa kilichotupeleka kwa mara ya kwanza fainali za mataifa huru ya Afrika Nigeria mwaka 1980 kijengewe nyumba ya kisasa kwa kila mchezaji. Kwa waliokufa kama Juma Mkambi (Jenerali), nyumba yake ikabidhiwe familia ya marehemu. Na wote wawe na bima ya afya ya kudumu. Pia nashauri Peter Tino, ambaye goli lake lilitupeleka Nigeria, ajengewe sanamu akiwa katika jezi na akipiga danadana. Sanamu yake isimamishwe kwenye malango ya kuingilia Uwanja wa Taifa.

Wachezaji wote wanaotufikisha ngazi ya kimataifa waenziwe daima popote walipo na iwe marufuku kuwadai kiingilio wanapohudhuria mashindano yoyote nchini. Aidha, waunde umoja wao wa kutatua matatizo yao ma kutoa nasaha kwa vijana, na pia, kila mwaka TFF ikutane nao kupata ushauri wao. Utaratibu huu utawafanya  wanaochipukia watamani kulitumikia taifa waonapo mafanikio ya kaka zao. Tunaweza kuifanyia marekebisho SPUTANZA ijumuishe wachezaji wastaafu na wanaoendelea kucheza kama ilivyo PFA.

v  Kuanzia sasa TFF iwe na vitega uchumi badala ya kutegemea jasho la wachezaji viwanjani na fadhila za FIFA, serikali na/au makampuni binafsi. Inatia aibu kubwa kwa TFF kushindwa kulipa kodi kwa serikali inayoisaidia kulipa gharama za mwalimu wa timu ya taifa. Na ni aibu kubwa zaidi TFF kushindwa kufanya mkutano wa marekebisho ya katiba, na badala yake kuamua kufanya mkutano kwa kutumiana waraka kinyume na katiba na kanuni. Hakuna mkutano wowote halali unaoweza kufanywa kwa kutumiana waraka. Wajumbe wa mkutano ni watu (in person) na si makaratasi. Je, makaratasi yatajadiliana nini? Je, ni mahali gani katika katiba au kanuni za TTF ambapo panaainisha bayana kufanya mkutano kwa kutumiana nyaraka (au teleconference) bila wajumbe kuwepo? Ubabaishaji kama huu kamwe hauwezi kuitwa utawala bora. Ni bora utawala!

Pembeni mwa uwanja wa Karume, mkabala na Kawawa Road, pajengwe jengo la maofisi (Kandanda House) pamoja na maduka ya kisasa kuzunguka uwanja mzima. Fedha za pango la maofisi na maduka zije kutumika kuanzisha kituo cha kisasa cha kuendeleza kandanda nchini (Tanzania Football Academy – TAFOA) nje ya Dar es Salaam kwa ajili ya kuibua vipaji, kuvilea na kuviendeleza. Kituo hicho pia kitatumika kuwaunganisha vijana na taasisi za mpira wa miguu duniani na wachezaji nguli kimataifa. Eneo la Karume linafaa sana kwa uwekezaji kibiashara kwa kuwa lipo eneo la gulio kubwa la biashara Kariakoo. Uwekezaji kama huu unawezekana sana kwa kuwa zipo taasisi nyingi na mifuko mingi ya fedha inayoweza kujenga kwa muda mfupi. Tusiwe na TFF ombaomba!

v  Na mwishowe, njia ya sita napendekeza tuwe na muundo mpya wa TFF kuanzia ngazi ya chini ya vijiji na mitaa. Tushirikiane na serikali bega kwa bega kuhakikisha kuwa kila kijiji au kila mtaa unakuwa na timu inayoweza kulelewa kwa pamoja na serikali za mitaa, TFF na wadau wengine wa mpira. Vijiji au mitaa kadhaa iunde timu ya kata. Na idadi fulani ya kata ziunde timu ya mseto ya eneo kubwa zaidi. Mathalani, eneo la Mwakaleli linaloundwa kwa sasa na kata nne za Luteba, Kandete, Isange na Mpombo liko mbioni kuunda timu ya mseto iitwayo Mwakaleli Palimyee Football Club almaarufu Banyafyale. Eneo la Vituka laweza kuwa na timu ya mseto ya kata kadhaa. Vivyo hivyo eneo la Kyabakari au Butiama Musoma laweza kuwa na timu ya mseto inayoweza kushiriki ligi kuu au kuwa kitalu cha kuzalisha wachezaji wa kitaifa na kimataifa. Mifano ipo - eneo la Sinza lina timu ya Abajalo iliyowahi kuwika kwa miaka mingi na kuzalisha magwiji.

Vikombe vya kushindania mbuzi au ng’ombe vinawasaidia vijana kwa kiasi fulani, lakini haviwapeleki popote. Muundo wa kuwa na timu za wananchi vijijini utawasaidia kujisikia fahari ya kuwa na timu yao kuliko hivi sasa ambapo watu binafsi wanawatumia vijana kujenga majina yao kisiasa ili waje wapate vyeo badala ya kujenga timu za wananchi. Mamlaka za serikali za mitaa zihakikishe kuwa kila kijiji au mtaa unakuwa na timu katika mipango yake ya huduma za maendeleo ya kijamii kama ilivyo kwa elimu, afya, miundombinu, maji, biashara na huduma zinginezo.

Nihitimishe kwa kumshukuru kipekee Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Abbas Kandoro na Mkuu wa Wilaya ya Rungwe Crispin Meela, kwa kuitikia muundo kama huu na kuwa tayari kuufanyia kazi ili vijana wetu waepukane na kuozea vijiweni na kwenye ulevi na uasherati.

No comments:

Post a Comment