SUALA LA AKINA MORRIS, CANNAVARO KWENDA KAMATI YA NIDHAMU
Shirikisho
la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) limepokea barua ya Chama cha Mpira wa
Miguu Zanzibar (ZFA) ikieleza kuwafungia wachezaji kadhaa Wazanzibari
wanaochezea klabu mbalimbali za timu za Tanzania Bara na timu ya Taifa
ya Tanzania (Taifa Stars).
Suala
hilo limepelekwa kwa Kamati ya Nidhamu na Usuluhishi ya TFF kwa hatua
zaidi, hivyo kwa sasa Shirikisho litasubiri uamuzi wa kamati hiyo.
Baadhi ya wachezaji hao ni nahodha msaidizi wa Taifa Stars, Aggrey
Morris, Nadir Haroub ‘Cannavaro’, Nassoro Masoud Cholo, Mcha Khamis,
Seif Abdallah na Selemani Kassim Selembe.
MTIBWA YAINGIA NUSU FAINALI KOMBE LA UHAI
Mtibwa
Sugar imekata tiketi ya kucheza nusu fainali ya michuano ya Kombe la
Uhai inayoshirikisha timu za vijana wenye umri chini ya miaka 20 za
klabu za Ligi Kuu ya Vodacom baada ya leo asubuhi (Desemba 19 mwaka huu)
kuzamisha African Lyon mabao 3-1.
Katika mchezo huo uliofanyika Uwanja wa Kumbukumbu ya Karume, Dar es Salaam, hadi
mapumziko Mtibwa Sugar ilikuwa mbele kwa bao 1-0 lililofungwa dakika ya
22 na Hillary Kasela. Hassan Kabunda aliisawazishia African Lyon katika
dakika ya 53.
Mabao
mengine ya washindi yalifungwa na Godfrey Mohamed dakika ya 64 na Juma
Lazio akapachika la mwisho dakika ya 87. Kwa ushindi huo, Mtibwa Sugar
sasa itacheza mechi ya kwanza ya nusu fainali dhidi ya Azam ambayo nayo
leo asubuhi (Desemba 19 mwaka huu) iliilaza JKT Ruvu bao 1-0 katika
mchezo uliofanyika Uwanja wa Chamazi. Bao la Azam lilifungwa dakika ya
46 na Mudathiri Yahya.
Mechi
hiyo ya kwanza ya nusu fainali itachezwa Ijumaa (Desemba 21 mwaka huu)
saa 8 kamili mchana kwenye Uwanja wa Kumbukumbu ya Karume, Dar es
Salaam. Nusu fainali ya pili nayo itachezwa kwenye uwanja huo huo
kuanzia saa 10 kamili jioni.
Robo
fainali ya tatu kati ya Oljoro JKT na Simba, na robo fainali ya nne
zinachezwa leo saa 10 kamili jioni (Desemba 19 mwaka huu) kwenye viwanja
vya Karume na Chamazi, Dar es Salaam.
Mechi
ya fainali na ile ya kutafuta mshindi wa tatu zitachezwa Jumapili
(Desemba 23 mwaka huu) kwenye Uwanja wa Kumbukumbu ya Karume, Dar es
Salaam.
No comments:
Post a Comment