TANZANIA
Bara imefanikiwa kuwa timu ya kwanza kuingia Nusu Fainali ya Kombe la Mataifa
ya Afrika Mashariki na kati, CECAFA Challenge Cup baada ya kuilaza Rwanda mabao
2-0 kwenye Uwanja wa Lugogo mjini hapa mchana huu.
Hadi
mapumziko, Stars inayodhaminiwa na Bia ya Kilimanjaro Premium Lager, walikuwa
mbele kwa bao 1-0 lililotiwa kimiani na kiungo Amri Kiemba, dakika mya 33
akiunganisha pasi ya Mwinyi Kazimoto aliyewapunguza wachezaji wawili wa Rwanda
kabla ya kutoa pasi maridadi.
Katika mechi
hiyo iliyochezeshwa na refa Mohamed El Fadil kutoka Sudan, mshambuliaji John
Raphael Bocco ‘Adebayor’ alikuwa mwiba mchungu kwa safu ya ulinzi ya Rwanda na
aliwafanya waende kwenye vyumba vya kupumzikia wakiwa hoi.
Katika hicho
kipindi cha kwanza, Rwanda walikosa bao la wazi dakika ya 12 baada ya krosi ya
Jean Claude Iranzi kuokolewa na beki Kevin Yondan kwa kichwa na dakika ya 19
Jean Baptiste Mugiraneza alipiga juu akiwa nje kidogo ya eneo la hatari.
Stars pamoja
na kufunga bao hilo kipindi hicho cha kwanza, katika dakika ya 30 krosi nzuri
ya Salum Abubakar ‘Sure Boy’, Mrisho Ngassa na Bocco walishindwa kuiunganisha
na ikawapita wote.
Ngassa tena,
katika dakika ya 38 alipiga shuti kali kutoka wingi ya kushoto, lakini likaenda
nje sentimita chache.
Kipindi cha
pili Stars walirudi vizuri tena na kuendelea kucheza kwa kuonana, ingawa na
Rwanda nao waliendelea kucheza kwa bidii kutafuta bao la kusawazisha.
Hata hivyo,
walikuwa ni Stars tena waliofanikiwa kupata bao la pili 53 baada ya John Bocco
kuuwahi mpira uliotemwa na kipa Jean Claude Ndoli kufuatia shuti kali la Mwinyi
Kazimoto kutoka nje ya eneo la hatari.
Baada ya bao
hilo, Rwanda walionekana kupagawa, lakini hawakusahau kushambulia lango la
Stars na dakika ya 86 Dadi Birori hakujali ameotea akasukuma mpira nyavuni,
lakini refa akakataa bao hilo.
Kwa ushindi
huo, Stars sasa inasubiri mshindi kati ya Uganda na Ethiopia kesho kukutana
naye kwenye Nusu Fainali.
Kocha wa
Taifa Stars, Kim Poulsen alisema baada ya mcezo kuwa wachezaji wake walijituma
wakati wote uwanjani na ikazaa matunda. “Vijana walikuwa na ari ya kufunga,
wakatengeneza nafasi na wakapata magoli mawili ya muhimu,” alisema.
Alisema timu
yake ina vijana wengi na mashindano haya yamewapa uzoefu mkubwa kwani
wamepambana na timu kubwa na kuzipa wakati mgumu.
Naye Meneja
wa Bia ya Kilimanjaro Premium Lager, George Kavishe, alituma salamu za pongezi
kwa Stars huku akisema walistahili kushinda na kuna dalili zote kuwa watacheza
fainali JUmamosi Disemba 8.
“Sisi kama
wadhamini tunafarajika sana kuona timu inafanya vizuri..tunawatakia kila la
heri waendelee hivi hivi na kwenye mashindano mengine ili wazidi kuipeperusha
bendera ya Tanzania,” alisema.
Watanzania
waishio Kampala na wengine kutoka mkoa wa Kagera walijitokeza kwa wingi na
kuishangilia Stars kwa nguvu zote. Balozi wa Tanzania nchini Uganda, Lodslaus
Komba naye alihudhuria mechi hiyo.
Stars; Juma
Kaseja, Erasto Nyoni, Amir Maftah, Shomary Kapombe, Kevin Yondan, Amri Kiemba,
Salum Abubakar/Athumani Iddi dk51, Frank Domayo, Mwinyi Kazimoto, Mrisho Ngassa
na John Bocco/Shaaban Nditi dk 85.
Rwanda; Jean
Claude Ndoli, Emery Basiyenge, Ismail Nshutimayamangara/Fabrice Twagizimana
dk19, Jimmy Mbaraga/Imran Nshiyimana dk67, Charles Tibingana/Barnabe Mbuyumbyi
dk61, Michel Rusheshangoga, Jean Baptiste Mugiraneza, Haruna Niyonzima, Jean
Claude Iranzi, Dadi Birori na Tumaine Ntamuhanga.
No comments:
Post a Comment