Kadri siku zinavyozidi kwenda hapa nchini Tanzania ndivyo ambavyo soka la nyumbani linavyozidi kupoteza mvuto kwa mashabiki ambao wanazidi kutekwa na ushabiki wa soka la kimataifa hasa la barani ulaya.
Kwa takribani siku nne nilizokuwepo hapa Musoma kwa ajili ya tamasha la Fiesta 2012, nimekuwa nikishuhudia namna soka la nje ya nchi lilivyokuwa na kwa mashabiki wa soka katika mkoa huu uliopo kanda ya ziwa.
Katika tembea tembea yangu nimekuwa nikikutana na madaladala mengi sana yakiwa yamebandikwa picha na kuchorwa majina ya wachezaji wa timu za ulaya, kuanzia Barcelona, Chelsea, Man United, Real Madrid mpaka Arsenal na vilabu vingine vikubwa vya ulaya.
Ukiachana na madaladala pia kwenye maduka na salooni za kiume hapa Mara karibia zote zimepewa majina ya wachezaji au timu kubwa za Ulaya.
Nilipojaribu kufanya utafiti ili kujua kwanini mashabiki wa hapa wana mapenzi makubwa na vilabu vya nje kuliko vya ndani ndipo waliponipa sababu zao.
"Kwanza ningependa kuweka wazi kwamba sio kweli watu hapa hawana mapenzi na soka la nyumbani. Watu tunapenda sana mpira hapa Tanzania na tunaushabikia ndio maana naona umekutana na watu kadhaa wenye kuvaa jezi za timu kubwa kama Simba na Yanga japo sio kwa wingi mkubwa," anasema Msafiri Kisase ambaye ni shabiki mkubwa soka la kimataifa.
"Kiukweli hapa Musoma watu wamechoka na ubabaishaji wa viongozi wa soka la Tanzania kuanzia chama mama TFF mpaka vyama mikoa na wilaya. Mambo yanaendeshwa kienyeji sana, hakuna usawa kwenye michezo, hali inayopelekea mkoa huu kukosa hata timu moja kwenye ligi kuu kwa miaka kibao sasa.
"Kwa hali hii unadhani nani atakuwa na mshawasha wa kushabikia soka la ndani kwa nguvu, wakati mkoa hauna timu za kwenye mashindano makubwa kwa miaka kibao sasa, hata hizo Simba na Yanga ambazo zina mashabiki nchi nzima kuna watu wengine wanazisikia tu kama timu za nchi ya nchi. Zitakuja huku kutoka Dar kwa minajili gani wakati hakuna timu ya kushindana nayo? Viongozi wa mkoa wamelala na TFF nayo imeshindwa kuutawanya mpira katika mkoa, wamebaki kwenye eneo moja tu. Soka litaendeleaje kwa hali hii? Matokeo yake watu wanakuwa wanatekwa zaidi na kushabikia timu za nje ya nchi kwa sababu hakuna timu za ndani za kuwashawishi wawe na mapenzi na soka la hapa." - aliongea Msafiri Kisase
No comments:
Post a Comment