Na Andrew Chale
MIONGONI mwa majina yanayoanza kuvuma kwa kasi hivi sasa kwenye medani ya soka hapa nchini, hutokosa kusikia jina la Shomari Kapombe.
Nyota chipukizi wa Klabu ya Simba ‘Wekundu wa Msimbazi’, Timu ya Taifa ya Vijana chini ya miaka 23 na hivi sasa Taifa Stars.
Shomari Kapombe baada ya kufanya kweli hivi karibuni U-23 iliyokuwa ikiwania kufuzu michuano ya Olimpiki na Mataifa ya Afrika, na kwenye mechi kadhaa za mzunguko wa kwanza wa Ligi Kuu bara iliyomalizika Novemba 3, akiwa na vinara wa ligi hiyo, Simba, Kocha Jan Borge Poulsen, hatimaye kamuona.
Kapombe, amebahatika kuitwa kwa mara ya kwanza katika historia yake ya soka, baada ya kubahatika kuitwa kikosi cha Stars, chini ya Kocha Mkuu, Jan Poulsen, ambacho kiko kambini kikijiwinda na mechi ya kuwania kupangwa kwenye makundi ya kufuzu Fainali za Kombe la Dunia, dhidi ya Chad, itakayopigwa jijini Nd’jamena, Novemba 11, kabla ya kurejeana siku nne baadaye jijini Dar es Salaam.
Katika mahojiano maalumu na Tanzania Daima, Kapombe mwenye historia ndefu katika medani ya soka, licha ya kuwa na umri mdogo, baada ya kutua Simba msimu huu, amefanikiwa kupigana vilivyo na kula sahani moja na nyota kadhaa wakongwe na wa kimataifa na kufanikiwa kucheza mechi karibu zote za mzunguko wa kwanza.
Kocha wa Stars, Poulsen alimwelezea, Kapombe kama mchezaji wa kipekee ambaye ana uwezo mkubwa, hivyo kumuita katika kikosi chake akiwa ana matumaini kuwa atafanya vema kwa kusaidiana na chipukizi wenzake Thomas Ulimwengu na Mbwana Samata ambao aliwahi kucheza nao U-23.
Mbali na Poulsen kukubali uwezo wa chipukizi huyo, mashabiki wengi bila unazi, pia wameonekana kukubaliana na kiwango chake huku wakimtabiria kufanya vema.
DOGO HUYU KATOKA WAPI?
Kapombe anasema soka iko katika damu, kwani alianza kuupenda tangu akiwa na miaka mitano mkoani Morogoro, alikokuwa akicheza ‘chandimu’ katika timu yao ya mtaani kwao Mafiga.
Anasema umri ulivyoongezeka alijiunga na timu ya Santos Fc, ambayo alifanikiwa kuichezea michuano mbalimbali akiwa bado kinda.
Anaitaja baadhi ya michuano hiyo kuwa ni ‘Serve Access Game’ iliyokuwa ikiandaliwa na taasisi ya kuendeleza vipaji vya soka ya Morogoro Youth Academy.
KUOKOTA MIPIRA UWANJANI
Kapombe anabainisha kuwa mbali ya kuchezea Santos, awali aliichezea timu ya watoto wanaookota mipira kwenye uwanja wa Jamhuri mjini Morogoro, ‘Jamhuri Ball Boys’.
“Nilipitia timu mbalimbali wakati nakua, ikiwemo ya Mafiga Kids, Santos Fc, Jamhuri Ball Boys mpaka nilipokuja kuonekana na kituo cha Moro Youth Academy,” anasema Kapombe.
Wakati akicheza katika timu zote hizo, alikuwa na shauku ya kufika mbali, huku kubwa zaidi ilikuwa ni ndoto ya kuchezea timu bora Tanzania, ama duniani.
“Nilipokuwa Ball Boys pale uwanja wa Jamhuri, Morogoro, nilikuwa na shauku kubwa na mimi kucheza timu kubwa kama Mtibwa, Simba, Yanga na nyingine nyingi ambazo nilikuwa nikivutiwa nazo wakati zikija kucheza Jamhuri … nilijipa moyo, kwani nilikuwa nikiongeza juhudi zangu katika mazoezi, ili kutimiza ndoto na kweli imetimia,” anasema Kapombe.
Akiwa na kikosi hicho cha Jamhuri Ball Boys, U-14, aliweza kukiongoza akiwa kama nahodha katika michuano ya WINOME Cup na michuano ya Serve Access Games, alikong’ara, ndipo kituo hicho cha Moro Youth kilivutiwa naye na kumchukua.
Kapombe anampongeza kocha wake, Yahaya Belin, aliyekuwa akimnoa Jamhuri Ball Boys, kwa kumsaidia mbinu mbalimbali za uchezaji, ikiwemo kujituma kucheza namba mbalimbali uwanjani.
“Kocha Belin, alikuwa akinisihi kucheza namba tofauti tofauti uwanjani, ili kuweza kuikoa timu pindi inapokuwa imezidiwa kimchezo...kwa hali hiyo, nilikuwa nakumbuka mawazo yake na mimi nilikuwa nikifuata mawazo yake mpaka leo matunda yake nayaona,” anasema Kapombe.
Akiwa katika kituo hicho cha Moro Youth, baadaye alipanda hadi kikosi cha U-17 cha kituo hicho, ambako aliweza kuchaguliwa kuwa nahodha wa timu ya mkoa wa Morogoro iliyoshiriki michuano ya Copa Coca-Cola 2008, wakati huo akiwa na miaka 16.
Anasema katika mashindano hayo walitolewa hatua ya robo fainali na Kigoma ambayo ilikuja kuwa mabingwa.
Kapombe anasema baada ya mashindano hayo ya Copa Coca-Cola 2008, walichaguliwa wachezaji wengi nyota, akiwemo Zahoro Zeiran waliyetoka naye mkoa wa Morogoro ambapo baadaye walikwenda nchini Brazil. “Baada ya michuano ile, nilirudi katika kituo huku nikiendelea na shule na baadaye timu ya Polisi Morogoro walinichukua,” anasema.
Anaongeza kuwa alichukuliwa yeye na wachezaji wenzake 6, kwenda Polisi Morogoro wakiwa kikosi B ambako walishiriki michuano ya timu za vijana za Ligi Kuu ‘Uhai Cup 2009’, kabla ya kupandishwa kikosi cha kwanza na kucheza Ligi Daraja la Kwanza kituo cha Tanga, akiwa na timu hiyo mwaka jana.
“Nakumbuka kulikuwa na mechi kati yetu na timu moja ya Arusha ambapo katika mchezo huo, kulikuwapo na kocha Jamhuri Kihwelu ‘Julio’ ambaye aliridhishwa na uwezo wangu na kunieleza kuwa ningekuwemo katika kikosi cha timu ya taifa ya vijana chini ya miaka 23 na kuanzia hapo nilijiunga na kikosi hicho,” anasema.
Akiwa na U-23, Kapombe anasema aliweza kuonesha uwezo mkubwa, ikiwemo kwenye hatua za kufuzu michuano ya kimataifa kama vile All African Games na Olimpiki ambapo aliweza kucheza mechi zote, nyumbani na ugenini, ikiwemo na timu za Cameroon, Nigeria na Uganda, jambo lililomuongezea uwezo wake kutoka ule wa awali.
KUIBUKIA SIMBA SC
Kapombe anasema kuwa ndoto yake ilikuwa ni kuona anasonga mbele, ikiwemo kucheza kwenye klabu kubwa nchini na nje ya nchi.
“Naikumbuka mechi baina ya U-23 dhidi ya Cameroon, mchezo uliochezwa kwenye dimba la Taifa, siku hiyo viongozi wa Simba walinifuata na kunieleza nia ya kujiunga na Wekundu hao wa Msimbazi.
Kwangu niliona ni bahati ya pekee, kwani kikosi kizima kilikuwa na wachezaji mahiri, lakini kwa kuwa Simba walinifuata mimi sikuwa na hiyana na nikamshukuru Mungu kuwa ndoto zangu zilikuwa zimeanza kutimia,” anasema Kapombe.
Anasema, baada ya kujiunga na Wekundu hao, furaha yake ilizidi pale alipokabidhiwa jezi namba 15 na kuwa miongoni mwa wachezaji 18 wa kikosi cha kwanza cha kutumainiwa cha Kocha Mganda, Moses Basena.
“Baada ya kumaliza sherehe za Simba Day, Arusha, nilijisikia furaha na sikuamini machoni mwangu kama nimechaguliwa kuwa kikosi cha kwanza cha Simba cha wachezaji 18, huku nikikabidhiwa jezi yangu namba 15,” anasema Kapombe.
Anasema kuwa kwa kuwa Basena alimfundisha kujiamini, aliweza kucheza mechi dhidi ya Yanga kwenye Ngao ya Hisani, ambayo ilikuwa na uangalizi mkubwa ambapo aliingia kipindi cha pili na aliweza kucheza vema bila woga, huku akitumia zaidi uwezo na maarifa ya soka.
Kapombe anasema, katika mzunguko wa kwanza wa Ligi Kuu bara, ameweza kucheza mechi zote 13, huku kati ya hizo tisa akicheza dakika zote 90.
“Ni hakika nimeonyesha uwezo katika mzunguko wa kwanza, hivyo mzunguko wa pili mashabiki wa Simba na wapenda soka wataona vitu vyangu zaidi ya nilivyoonyesha mzunguko wa kwanza...,” anasema.
KUITWA TAIFA STARS
Anasema kuwa aliposikia kwenye vyombo vya habari juu ya kuteuliwa jina lake, hakuamini na hata ndugu na jamaa walipomwambia kuchaguliwa kwake huko, bado hakuamini hadi alipohakikisha mwenyewe siku ya pili yake.
“Sikuamini kwa mara ya kwanza kama nimebahatika kuchaguliwa kikosi cha timu ya taifa, siku ya pili niliposoma magazeti na kupigiwa simu na uongozi juu ya kuchaguliwa kwangu, kwanza nilimshukuru Mungu kwa kuniwezesha kwake,” anasema Kapombe.
Anasema uwepo wake ndani ya kikosi hicho cha Stars ni kielelezo tosha cha vijana kuisaidia timu ya taifa, ili iweze kufanya vema na kupata mafanikio ya soka hapa nchini.
“Poulsen ameona mbali, hasa kwa kujaribu kutumia damu changa... uwepo wangu ndani ya kikosi cha Taifa Stars ni changamoto tosha na nawaomba Watanzania wazidi kutuombea, nasi tutajitahidi na tutasonga mbele,” anasema Kapombe.
HISTORIA KWA UFUPI
Shomari Kapombe ni kitinda mimba katika familia ya watoto watatu wa Mzee Salum Kapombe wa mjini Morogoro.
Alizaliwa Januari 28, 1992 katika hospitali ya mkoa wa Morogoro ambapo elimu ya msingi aliipata shule ya Mwale, mwaka 2000 hadi 2006, huku akiwa anajihusisha na soka.
Aliendelea na soka alipojiunga na Shule ya Sekondari ya Lupanga iliyo jirani na Chuo cha Ualimu Kigurunyembe, mwaka 2007 hadi 2010.
SIFA ZA ZIADA
Shomari Kapombe, anasema binafsi amejaliwa kipaji cha kutumia miguu yote miwili na pia awapo uwanjani, hategemei kucheza namba moja.
“Katika kikosi cha U-23, nacheza pembeni kama beki tatu... hivyo hivyo na kwenye klabu yangu ya Simba, ambayo pia wakati mwingine huwa nabadilisha namba,” anasema.
Kapombe anasema siku zote amekuwa akitamani sana uchezaji wa Haruna Moshi ‘Boban’ kwani ndiyo unaomvutia kwa hapa nchini na awapo uwanjani hufuata nyayo zake na anaamini iko siku naye atafika mbali ikiwemo kucheza soka la kulipwa Ulaya.
Kwa upande wa kimataifa, anakunwa na Tom Cleverley wa Mashetani Wekundu na pia ni shabiki mkubwa wa Manchester United ya England.
SHUKRANI
Nyota huyo anasema, katika maisha yake hatoweza kuwasahau walimu pamoja na wazazi wake, kwa kumtia moyo hadi hapa alipofikia.
Anawataja makocha wake hao kuwa ni Yahaya Belin, Allan Sigo pamoja na Rajabu Kindagule wa Moro Youth, John Tamba Polisi Morogoro, Jamhuri Kiwelu ‘Julio’, Moses Basena Simba pamoja na Jan Poulsen wa Taifa Stars.
ASICHOKISAHAU
Kapombe anasema kuwa katika maisha yake hatosahu walipokuwa safarini kuelekea mjini Younde, Cameroon, mwanzoni mwa mwaka huu, hali ya hewa ilikuwa mbaya angani, hivyo kusababisha ndege waliyokuwa wamepanda kuyumba sana ikiwa angani.
“Nilikuwa na hofu kubwa sana, kwani hali ile ilinifanya nibadilike sana kwa hofu, hali ilikuwa mbaya sana na tukio lile sitolisahau kamwe, lakini Mungu alitusaidia na tulifika salama,” anasema.
DONDOO
JINA KAMILI: Shomari Salum Kapombe.
KUZALIWA: Januari 28, 1992.
MAHALI: Morogoro.
TIMU YA MTAANI: Santos Fc, Mafiga Kids na Jamhuri Ball Boys.
KITUO CHA SOKA: Moro Youth Academy
TIMU YA AWALI: Polisi Morogoro
TIMU YA SASA: Simba Sports Club
TIMU ZA TAIFA: Taifa Stars/ U23
NAFASI UWANJANI: Kiraka/Kiungo
NAMBA YA JEZI: Klabu 15, U-23 namba 13, Taifa Stars ?
IDADI MECHI ZA KIMATAIFA: 10.
LIGI KUU: Mzunguko wa kwanza-13.
IDADI YA KADI: Njano moja, U-23 vs Nigeria.
UTAIFA: Tanzania
ELIMU: Kidato cha nne
No comments:
Post a Comment