BEKI wa Simba, Juma Jabu amesema yuko tayari kwenda Yanga au klabu nyingine yoyote itakayoonyesha nia ya kumtaka kwa sababu anajali maslahi yake.
Kauli hiyo ya Jabu imekuja siku moja baada ya kuzagaa tetesi kwamba anataka kujiunga na Yanga pamoja na wenzake Juma Nyoso na Uhuru Selemani waliomaliza mikataba yao ya kuitumikia klabu bingwa ya Tanzania, Simba.
Akizungumza jana na gazeti la mwananchi, Jabu alisema mkataba wake na Simba umekwisha na haoni dalili yoyote ya kuendelea kucheza hapo msimu ujao, hivyo yupo tayari kwenda timu yoyote itakayojali maslahi yake na kiwango chake uwanjani.
"Ni kweli nimemaliza mkataba na Simba na hivi sasa nipo huru kucheza timu yoyote itakayoridhika na mimi, lakini jambo la msingi ni kuangalia maslahi yangu kwanza.
"Sijaona dalili yoyote ya uongozi Simba kutaka niendelee nao kwani wamekaa kimya huku wengine wakisainishwa mikataba mipya,"alisema Jabu.
"Nataka timu itakayonihakikishia namba iwe Yanga au yoyote ile inayoshiriki Ligi Kuu msimu huu," alisema Jabu.
Hata hivyo uongozi wa Simba ulipoulizwa kuhusu suala la kuachana na nyota huyo walidai kwa sasa hawapo tayari kusema lolote hadi muda utakapowadia.
Mwishoni mwa usajili wa msimu uliopita Simba iliingia kwenye mgongano na Jabu pamoja na Meshack Abel baada ya kuamua kuwatoa kwa mkopo katika klabu za African Lyon na Moro United.
Uamuzi huo wa Simba ulipingwa na wachezaji hao na baadaye uongozi wa mabingwa hao ulikubali Jabu kurudi kikosini huku Abel akivunja mkataba na kukaa nje ya uwanja kwa miezi sita.
No comments:
Post a Comment