Search This Blog

Friday, May 18, 2012

JEZI YA MAFISANGO KUTOTUMIKA TENA SIMBA SC



JEZI namba 30, aliyokuwa anavaa kiungo wa kimataifa wa Rwanda, mwenye asili ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC), katika klabu ya Simba, Patrick Mutesa Mafisango kuanzi sasa haitakuwa ikitumika tena kwa heshima ya mchezaji huyo aliyefariki Dunia usiku wa kuamkia jana, jijini Dar es Salaam.
Hayo yalisemwa jana Mwenyekiti wa Simba SC, Alhaj Ismail Aden Rage alipokuwa akihutubia mamia ya wadau wa soka waliohudhuria zoezi la kuuaga mwili wa marehemu Mafisango kwenye viwanja vya Sigara Chang’ombe, Dar es Salaam, kabla ya kupelekwa Uwanja wa ndege wa kimataifa wa Mwalimu Julius Nyerere, tayari kwa safari ya kwenda kwao, DRC kwa ajili ya mazishi kesho.
Heshima kama hiyo alipewa kiungo wa zamani wa kimataifa wa Cameroon, Marc Vivien Foe na klabu yake, Manchester City ya England alipofariki Dunia Juni mwaka 2003, ambapo jezi namba 23 ilitunzwa moja kwa moja.
Aidha Rage alisema msiba huu ni mkubwa kwa Simba kwa kuwa mchezaji huyo alikuwa ni muhimili mkubwa kwa timu hiyo akiwashauri wachezaji na kuwa nao karibu ndani na nje ya uwanja.
“Mafisango alikuwa na mchango mkubwa kwa Simba na mara ya mwisho klabu kukumbumbwa na msiba mzito namna hii ilikuwa ni mwaka 1978 ambapo Simba ilimpoteza mchezaji wake mahiri Hussein Tidwa na ukweli ni kwamba wachezaji hawa tutawaenzi miaka yote na ndio sababu ya kutotumia tena jezi namba 30 kwa kuvaliwa na mchezaji yoyote,” alisema Rage.
Rage alisema licha ya umahiri wa Mafisango Dimbani pia alikuwa mchezaji ambaye alitoa mchango mkubwa na hasa wachezaji wawapo nje ya nchi kutokana na umahiri wake wa kujua lugha mbalimbali ambapo alikuwa akiwasaidia wachezaji wenzake.
“Ni pengo kubwa kwa kuwa mchezaji huyo alikuwa akijua lugha nyingi ikiwemo Kiswahili, Kingereza na Kifaransa  na kuwasaidia wachezaji walipokuwa nje ya nchi tutamkubuka sana Mafisango,” aliongeza.
Kutokana na machungu ya msiba huo Rage alishindwa kumaliza kusoma risala fupi ya marehemu mara baada ya kuishiwa nguvu na kumwaga machozi na kupelekea Makamu Mwenyekiti wa klabu hiyo Godfrey Nyange ‘Kaburu’ kumsaidia kusoma risala hiyo.
“Mfisango ni mchezaji ambaye alikuwa akijituma nje na ndani ya uwanja na kabla ya kutua Simba Marehemu aliwahi kucheza soka katika timu mbalimbali ikiwemo Tp Mazembe ya DRC, APR ya Rwanda , Azam na Simba za Tanzania na pia alikuwa Nahodha wa timu ya Taifa ya Rwanda ‘Amavubi’ alisema Kaburu.
Wakati wa kutoa heshima za mwisho katika uwanja wa Sigara maelfu ya watu walijitokeza uwanjani hapo wakiongozwa na mchungaji Tito Kihame ambaye aliongoza ibada ya kuuga mwili wa marehemu, Waziri wa Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo, Fenella Mukangara na viongozi mbalimbali wa serikali na viongozi kutoka klabu mbalimbali za hapa nchini.
Mukangara aliwataka wachezaji wa Tanzania kujituma na kuwa na moyo kama ambao alikuwa nao Marehemu Mafisango kwa kujituma na kuwa na jitihada za zaidi nje na ndani ya uwanja kama ambavyo marehemu alivyokuwa akifanya.
“Kifo chake ni pigo kubwa kwa Simba na Watanzania kwa ujumla na tunamshukuru kwa kuvuka mipaka na kuona umuhimu wa kuja na kucheza Tanzania na pia wachezaji wa Simba wasikate tamaa cha muhimu waendeleze kile ambacho alikiacha marehemu,” alisema Mukangara.
“Ukweli ni kwamba katika familia ya soka hapa nchini tumepoteza mtu muhimu sana na tunamuombea kwa Mwenyezi Mungu ampumzishe kwa amani,” alisema Katibu Mkuu wa Shirikisho la Soka Tanzania TFF Angetile Osiah.
“Sisi Simba ni watani zetu na tunakuwa pamoja katika shida na hivyo basi mimi kama kiongozi wa Yanga nimeiwakilisha klabu nzima na tutaendelea kuwa bega kwa bega na watani zetu katika kipindi hiki kigumu ila mchezaji Mafisango alikuwa ni mchezaji hodari uwanjani hivyo basi anastaili kuigwa na wachezaji wengine,” alisema Selestine Mwesigwa katibu Mkuu wa Yanga.
Nao wachezaji mbalimbali kutoka timu ya Taifa Taifa Stars walijitokeza na kubeba jeneza la mchezaji mwenzao na kuliingiza katika viwanja vya Sigara wachezaji hao Juma Kaseja, Jonh Bocco, Mwinyi Kazimoto, Shabani Nditi, Amiry Maftah, Nurdin Bakari, Agrey Moris na Juma Nyoso.
Profesa Philemon Sarungi akimsaidia Rage
Mara baada ya nyota hao kuufikisha mwili wa marehemu katika sehemu husika ambayo ilipangwa Kazimoto na Kaseja iliwalazimu watu wa ziada kujitokeza na kuwapa sapoti mara baada ya kushindwa kutembea na kuwapeleka katika eneo husika ambalo walikuwa wamepangiwa kukaa.
Katika hatua nyingine Ofisa habari wa wekundu hao wa Msimbazi Ezekiel Kamwaga ‘Mr Liverpool’ alisema kuwa katika msafara wa leo kuondoka kwenda Kongo kuusafirisha mwili wa marehemu kwa niaba ya wachezaji atawawakilisha Haruna Moshi ‘Boban’ ambaye alikuwa karibu na marehemu pamoja na mjumbe wa kamati ya utendaji ya klabu hiyo Joseph Itang’are.
“Mwili wa marehemu utaondoka mapema alfajili ya kesho (leo) kwenda kwao Kongo ila pia leo mtoto wa marehemu Chris Paul, mwenye umri wa miaka mitano ameondoka na mchezaji wa Yanga Haruna Niyonzima ambaye pia ni mchezaji wa timu ya Taifa ya Rwanda,” alisema Kamwaga.

Picha na habari kwa hisani ya http://bongostaz.blogspot.com/

1 comment:

  1. Oh my goodness! Incredible article dude! Thanks, However I am going through issues with
    your RSS. I don't know the reason why I cannot subscribe to it.
    Is there anybody getting similar RSS problems? Anybody who knows the answer can
    you kindly respond? Thanks!!|

    Look into my web blog :: pit 37 pdf [contentoanimation.com]

    ReplyDelete