Search This Blog

Wednesday, November 23, 2011

BOBAN NA MKWASA WAKAMILISHA KAMBI YA KILI STARS


Kambi ya timu ya soka ya Taifa ya Tanzania Bara ‘Kilimanjaro Stars’, imekamilika baada ya
mchezaji Haruna Moshi ‘Boban’ na Kocha Mkuu wa timu hiyo, Charles Boniface Mkwasa nao kuripoti kambini.

Boban alishindwa kuripoti kambini mapema kutokana na matatizo ya kifamilia, lakini juzi Kocha Msaidizi wa timu hiyo, Jamhuri Kihwelo ‘Julio’ alitishia kumtema kama asingejiunga
hadi kufikia jioni juzi, wakati Mkwasa alikuwa Afrika Kusini kuendesha mafunzo ya ukocha.

Akizungumza kwenye mazoezi ya timu hiyo jana, Julio alisema Boban aliripoti kambini juzi jioni. “Wakati nazungumza na waandishi mapema juzi alikuwa hajaripoti, lakini jioni tulipomaliza mazoezi tuliporudi hotelini tukamkuta tayari amefika,” alisema Kihwelo.

Kihwelo alisema ana furaha sasa idadi ya wachezaji 28 aliyowateua kwa ajili ya mashindano ya Kombe la Chalenji, sasa imekamilika na kikosi chake kiko kamili kwa ajili ya mashindano hayo.

Kihwelo alisema ataandaa ripoti ya timu hiyo na kumpa Mkwasa ambaye alirejea juzi kutoka nchini Afrika Kusini alipokwenda kama mkufunzi wa Shirikisho la Soka Afrika (CAF) ili
kuijadili na kupata majina ya wachezaji 22 wanaotakiwa kwa michuano ya Chalenji ambao atawatangaza leo.

Alisema nidhamu, kujituma mazoezini na uwezo binafsi ndio vitu vya msingi atakavyoangalia kabla hawajateua majina hayo ya mwisho kwa ajili ya mashindano hayo.

Katika mashindano ya mwaka huu, Kilimanjaro Stars ambayo iko Kundi A na nchi za Nambia, Djibout na Rwanda, itaanza kampeni za kutetea kombe lake kwa kupambana na Rwanda ‘Amavubi’ Jumamosi hii Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.

No comments:

Post a Comment