Search This Blog

Friday, September 23, 2011

BASENA KUWAPIGA BENCHI SUNZU NA MAFTAH DHIDI YA MORO


Kocha wa Simba, Moses Basena amesema atampumzisha mshambuliaji wake tegemeo Felix Sunzu katika mchezo wa kesho dhidi ya Moro United baada ya kuumia wakati wa mechi kati yao na Toto African.

Sunzu aliyekwamisha mabao mawili kati ya matatu yaliyosababisha Simba kupata sare ya mabao 3-3 dhidi ya Toto African katika mchezo uliofanyika juzi kwenye Uwanja wa CCM Kirumba jijini Mwanza, aliumia dakika ya 42 ya pambano hilo na kutolewa nje kisha kukimbizwa hospitali kwa kwa ajili ya matibabu zaidi.

Akizungumza kwa simu akiwa jijini Mwanza jana, Basena alisema hali ya afya ya Sunzu inaendelea vizuri, lakini anakusudia kumpumzisha katika mechi hiyo dhidi ya Moro United ili aweze kupona kabisa.

"Kimsingi Sunzu anaendelea vizuri, leo alienda tena hospitali kwa ajili ya uchunguzi wa mwisho kwa kuwa aliumia sana.

"Ni kwamba alipasuka sehemu ya kichwa, hivyo pamoja na hali yake kuendelea vizuri sifikirii kumtumia katika mechi ya Jumamosi dhidi ya Moro United,"alisema Basena.

Aliongeza kuwa mbali ya Sunzu, pia beki wake tegemeo Amir Maftah ambaye hakucheza katika mechi dhidi ya Toto African ataukosa pia mchezo huo na anaweza hata kukosa mechi ya timu ya taifa,'Taifa Stars' dhidi ya Morocco.

"Kwa kweli nina majeruhi wengi sio Sunzu tu, hata Maftah atakosekana kwani bado hajarejea katika hali yake ya kawaida na inawezekana hata timu ya taifa ikamkosa, tuna wakati mgumu, tunafurahia kurudi kwa Mwinyi wengine wanatoka, lakini hakuna jinsi tutapigana na kuhakikisha hatupotezi mchezo,"alisema Basena.

Wakati huo huo, Basena alizungumzia sare yao ya mabao 3-3 na Toto African kwa kusema walicheza vizuri licha ya kwamba wachezaji wake walifikiri zaidi katika kushambulia na kusahau kujilinda ambapo aliahidi kurekebisha hali hiyo.

Katika hatua nyingine Basena alitoa wito wa askari wanaosimamia usalama kwenye viwanja vya soka kuwajibika kila mmoja kwa nafasi yake ili kuepusha hatari kama iliyojitokeza katika mechi kati yao na Toto African ambapo mbwa alimponyoka askari na kuingia uwanjani na kuwafukuza wachezaji wake akiwamo Haruna Moshi 'Boban' na Sunzu.

No comments:

Post a Comment