angalia kwa makini ( jezi nyeupe ni Simba ) wote wanamuangalia Gumbo ( mwenye mpira ) badala ya kumwalia Asamoah ( juu kabisa mwenye jezi ya kijani ) ambaye alikuja kuwafunga..
Simba ni timu ambayo katika hali ya kawaida ina mabeki wenye vimo vifupi, Juma Said Nyoso na Kevin Yondani wote kwa pamoja ni mabeki wa kati wafupi .
Mabeki wa pembeni Juma Jabu,Amir Maftah na Nassor Masoud ‘cholo’ wote ni wafupi pia na mara nyingi ukabaji wao wa mipira ya krosi na ile iliyokufa unatatizwa na ufupi huu .
Kumbuka mchezo wa mwisho baina ya Simba na Yanga kwenye kombe la Kagame , Kevin Yondani aliteleza wakati anaenda kuucheza mpira wa krosi wa Rashid Gumbo na Juma Nyoso pia hakuwa makini wakati wa ‘movement’ nzima ya goli na matokeo yake Kenneth Asamoah alifunga goli rahisi sana la kichwa.
Wakati Gumbo anaambaa na mpira pembeni mwa uwanja walichofanya mabeki wa Simba kina Nyoso na wenzie ni kuelekeza macho yao kwenye mpira na wakasahau kuelekeza macho yao kwa mshambuliaji mmoja aliyekuwa ‘target’ ya kiungo mwenye mpira pembeni mwa uwanjani na wachezaji wengine wa yanga waliokuwa kwenye eneo la hatari ambao kimsingi walikuwa na kazi ya ‘kudraw attention’ ya mabeki wa Simba lakini kutokana na kukosa umakini kwa wachezaji wa Simba wachezaji hao wengine wawili nao wangeweza kufunga kwa wepesi tu na si Asamoah peke yake .
Kwa haraka ukisoma kilichoandikwa hapo juu unaweza kujiuliza jinsi ufupi ulivyokuwa tatizo , ufupi haukasababisha Simba ifungwe kwenye mechi dhidi ya Yanga lakini Simba wamewahi kufungwa mabao ya kizembe kutokana na ufupi wa mabeki wa kati ambao wakati mwingine wanashindwa kucheza mipira ya juu inayotoka pembeni mwa uwanja .
Kilichosababisha Simba ifungwe na Yanga ni umakini mdogo wa mstari wote wa mabeki wa Simba ambao walikuwa wanamtazama mpiga krosi huku wanamsahau anayepelekewa krosi. Kwa beki mrefu ni rahisi
kumbugudhi mshambuliaji na kuondoa uwezekano wa kufunga bao kwa kichwa na hivyo kupunguza uwezekano wa kufungwa kutokana na ‘move inayoanza pembeni mwa uwanja .
Suluhisho-Kujaribu ‘ZONAL MARKING’
Moja ya vitu ambavyo mabeki waliokosa kimo huvifanya ili kuondoa uwezekano wa kufungwa kwenye krosi au mipira iliyokufa kama ya kona ni kukaba kwa mfumo wa ‘zones’ yaani kukaba eneo au nafasi .
Mfano Beki anaweza kujua kuwa hana nafasi ya kugombania mpira wa juu na mshambuliaji mrefu hivyo atakachofanya ni kuhakikisha kuwa eneo ambalo mshambuliaji atakayepiga mpira utaelekea lina mtu anayelinda ili mpira utakapopigwa unaokolewa .
Pia beki anaweza kuhakikisha kuwa mshambuliaji anaghasiwa mpaka anaondoka kwenye eneo la hatari au anakuwa kwenye eneo ambalo hata akipiga mpira kwa kichwa basi hautakuwa na madhara lakini si kitu ambacho bei ya simba walikifanya na kosa lingine la jinai ambalo linafanywa na mabeki wa Simba ni kuwapa washambuliaji nafasi kubwa ya kupumua kama ilivyokuwa kwa Asamoah .
Kwanini Yanga hawafungwi mabao kama yale ni kwa sababu mabeki wa kati wa Yanga (canavaro na chacha marwa) hawana shida ya kukaba , wanakaba vizuri mtu na nafasi pia na ndio maana mara nyingi mabao ambayo Yanga hufungwa yanafungwa kwenye eneo la sita kwa kuwa mabeki hawa wa Yanga nao wana ugonjwa wao mkubwa ambao ni kukosa mawasiliano kati yao na mara nyingi hujikuta eidha wanafuata mpira mmoja wote wawili au wanaachiana na kumpa mshambuliaji nafasi nzuri ya kwenda kumuona kipa akiwa peke yake .
Mwisho.
Muhimu kwa mabeki wa Simba ni kuhakikisha kuwa majukumu yanagawanywa miongoni mwa watu wawili wa mwisho ambapo lazima awepo mmoja ambaye ni msahihishaji wa makosa ya mwenzie .
Kati ya Yondani na Nyoso hakuna yoyote ambaye anaweza kuwa ‘defense field marshall’ yaani kamanda wa eneo la hatari ambaye ni mahiri kwenye kuusoma mchezo na kuwaelekeza wenzie cha kufanya . Labda uwepo wa Victor Costa unaweza kusaidia hili .
No comments:
Post a Comment