Alex Song akiwania mpira na Gabriel Obertan
Huku wakiwa na mengi ya kuyafanyia kazi ili kufikia pale ambapo mashabiki wao wanatamani kuona timu yao ikifika, Arsenal walijikuta wakianza kwa kasi ndogo baada ya kulazimishwa sare ya bila kufungana na Newcastle United .
Siyo vigumu kuona Arsenal walipojikwaa na kushindwa kupata ushindi mbele ya Newcastle Utd.Moja kwa moja mzigo wa lawama hauna budi kubebwa na Arsene Wenger.
Kitu kimoja kilichomfanya Wenger asipate mafanikio makubwa akiwa na Arsenal ni uwezo wake mdogo wa kutulia hasa pale ambapo timu inapokuwa kwenye mvurugiko na pia siku zote ameshindwa kufanya maamuzi yenye msimamo kwenye timu yake huku akichanganyikiwa mara kwa mara akiwaacha wachezaji wake watoto wasiwe na la kufanya .
Kwa hakika kikosi cha Arsenal kwa mchezo wa kwanza wa ligi kuna aina ya maandalizi ambayo kilikuwa kinapaswa kuwa nayo ili kiweze kuanza ligi kwa ‘statement’ ya nguvu , badala yake Arsenal ilijikuta iki-approach pambano la kwanza huku ikiwa kwenye dimbwi la ‘sintofahamu’ inayowahusu wachezaji wake mahili Samir Nasri na nahodha Francesc Fabregas .
Wachezaji hawa kwa vipindi tofauti kumekuwepo na tetesi za kutaka kuihama timu hiyo,kipindi cha miezi miwili hivi taarifa za Nasri kutaka kuihama timu hiyo zimekuwa zikiongoza kutajwa kwenye vyombo mbali mbali vya habari na kwa upande wa Fabregas ni takribani miaka mitatu sasa amekuwa akieleza wazi wazi hisia zake za kujiunga na klabu yake ya utotoni,Fc Barcelona .
Arsene Wenger alipaswa kuhakikisha kabla ya msimu huu kuanza awe ameshawauza wachezaji hawa na kuitengeza Arsenal mpya pasipokuwa na Nasri na Fabregas.
Siku ya ijumaa zikazuka taarifa kuwa majina ya Nasri na Fabregas yameondolewa kwenye kikosi kitakachoivaa Newcastle Utd .
Moja kwa moja mapungufu yalionekana pale ambapo walikosekana wachezaji wa kuziba nafasi zao na hasa ukizingatia kuwa hakuwepo majeruhi Jack Wilshere.
Badala yake Arsenal ililazimika kuwatumia wachezaji ambao hawakuwepo kwenye mipango ya Arsene Wenger mfano ni Andrey Arsharvin , kiukweli mchezaji huyu hakupaswa kuwemo kwenye kikosi cha Arsenal cha msimu huu ila kutokana na kushindwa kutokea klabu ya kumnunua amelazimika kuendelea kubaki.
Kiujumla Arsenal ilikuwa haina ‘squad depth’ na hilo liliwaathiri sana . Pia Arsenal walikosa kiongozi uwanjani , hapo ndipo linapoonekana pengo la bwana mdogo Jack Wilshere ambaye ametokea kuwa kiongozi wa chini chini kwa wenzake .
Kwa jinsi walivyocheza hawakukosa vitu vingi sana lakini vichache walivyovikosa vilikuwa muhimu . Kwa mfano hakukuwa na pasi yoyote inayoongea yaani ‘ telling pass’ ambayo mshambuliaji Robin Van Persie aliipata, jambo ambalo lilichangia Arsenal kumaliza mchezo huo bila kufunga.
Kwa upande wa safu ya ulizni Thomas Vermalen alicheza vizuri kwa kushirikiana na Laureant Koscielny huku kipa Wojschec Scezny akicheza kwa umahiri mkubwa.
Kwa upande wa pili Newcastle Utd si timu ya kubeza na kama Arsenal watakumbuka ni Newcastle hii hii ambayo ilichukua pointi 4 mikononi mwao msimu uliopita.
Kama Arsenal wangekuwa na mpango thabiti wa kuchukua pointi tatu wangefanikiwa, badala yake Arsene Wenger ni kama aliingia kwenye mchezo huu akiamini kuwa Newcastle walibahatisha kwa sare ya 4-4- na ushindi wa 0-1 waliopata msimu uliopita na alijua kuwa Arsenal wangeenda uwanjani na kushinda kirahisi kwa bao 3-0 na maisha yakaendelea lakini haikuwa hivyo.
Newcastle waliingia uwanjani wakijua fika kuwa wanacheza na timu ngumu na waliipa mechi umuhimu iliohitaji kupewa na pointi waliyopata walistahili kuipata .
Kingine kwa wachezaji wa Arsenal ni utoto . Kulikuwa na haja gani kwa Alexander Song na Gervinho kufanya yale waliyoyafanya ? Ndiyo hapo unapoweza kuona kufeli kwa Arsene Wenger kama baba kwa wachezaji wake.
Ameshindwa kuwajenga kisaikolojia na matokeo yake ni utoto mwingi ambao kwa hakika umekuwa ukiigharimu Arsenal kwa misimu sita iliyopita na utaendelea kuigharimu kwa misimu mingine sita au zaidi endapo Wenger ataendelea na falsafa zake.
Kwa jumla Arsenal wanahitaji kufanyia kazi maeneo makubwa ya matatizo yao iwapo wanataka kutoa changamoto ya ukweli kwa timu nyingine za top –four la sivyo haitakuwa kazi nyepesi kuwatoa kimasomaso mashabiki wake wenye hamu na mataji.
No comments:
Post a Comment