Search This Blog

Saturday, July 9, 2011

COUNTDOWN KAGAME CASTLE CUP FINAL: SIMBA vs YANGA.


Pazia la michuano ya 37 ya kombe la Kagame kwa ngazi ya vilabu vya ukanda wa Afrika ya mashariki na kati, linafungwa hapo kesho kwenye uwanja mkuu wa taifa jijini Dar es salaam, kwa mchezo wa fainali utakaowakutanisha mafahari wawili wa soka la Bongo.

Ni Simba na Young Africans, pambano ambalo linajulikana kama Dar es salaam Derby, linalowakutanisha mahasimu wa kandanda wan chi ya Tanzania, kwa miaka dahar sasa.

Hii ni fainali yao ya tatu, kukutana kwenye michuano mikubwa katika ngazi ya vilabu vya ukanda huu wa Cecafa, baada ya kuwa zimlikwishafanya hivyo katika miaka ya 1975 na 1992 pale visiwani Zanzibar kwenye uwanja wa Aman.

Mwaka 1975, fainali hiyo ilizikutanisha timu hizo, na Young Africans ikaibuka mbabe kwa kuibwaga Simba mabao mawili kwa sifuri, katika fainali ya kusisimua ya michuano iliyokuwa ya pili.

Simba, mabingwa wa kihistoria wa michuano hiyo, wakalipa kisasi kwenye uwanja huo huo wa Aman mnamo mwaka 1992, kwa ushindi wa changamoto ya mapigo ya penati, mitano kwa minne, kufuatia sare ya bao moja kwa moja mnamo dakika mia moja na ishirini za mchezo.

Katika ardhi ya Tanzania bara, bado wana wa Jangwani hawajaonja ladha ya kutwaa uchampioni huo, na hii ni mara ya kwanza kwa timu hizo kukipiga kwenye mchezo wa fainali katika ardhi hii ya Tanzania bara, japo mara mbili zimekutana kwenye ardhi ya upande wa pili, wa Serikali ya Jamhuri ya muungano wa Tanzania.

Ni mchezo ambao unazikutanisha timu mbili zilizo na sura nyingi mpya, tofauti na ilivyozoeleka, kwani takriban nusu ya kila kikosi, kina wanandinga wapya waliosajiliwa kwa ajili ya msimu ujao wa ligi ya Premier ya Tanzania bara, na mashindano ya kimataifa.

Simba, bingwa wa kihistoria wa michuano hii, inaingia uwanja mkuu wa taifa hapo kesho ikisaka heshima zaidi kwenye michuano hii, kwani itakuwa inasaka ubingwa wake wa saba, baada ya kuwa ilikwishafanya hivyo mara sita.

Ina historia nzuri pale michuano hii inapofanyika kwenye uwanja wa nyumbani, na haijawahi kushindwa katika mchezo wa fainali ya michuano hii kwenye ardhi ya Tanzania bara.





Mara ya mwisho kufanya hivyo ilikuwa ni mnamo mwaka 2002 pale kwenye uwanja wa Aman visiwani Zanzibar, ikiondosha St Louis ya Bujumbura Burundi kwa kuilaza bao moja kwa sifuri, hivyo ina kiu ya ubingwa huo kwa kipindi cha miaka nane.

Kwa upande wa mahasimu wao Dar es salaam Young Africans wameshindwa kuupata ubingwa huo tangia walipofanya hivyo mnamo mwaka 1999 kule mjini Kampala nchini Uganda, kwa kuilaza sports club Villa ya Uganda kwa changamoto ya mapigo ya penati, minne kwa mmoja.

Miamba hawa wa bara wamekuwa na historia nzuri ya kutwaa ubingwa huu nje ya ardhi ya Tanzania, kwani kabla ya mwaka huo wa 1999, ilifanya vivyo hivyo kwenye uwanja wa Nkivubo mjini Kampala kwa kuilaza pia Villa mabao mawili kwa moja.

Katika fainali kumi ilizocheza za michuano hiyo, Simba ilipoteza kwenye fainali dhidi ya Young Africans mnamo mwaka 1975 kule visiwani ZANZIBAR, ikapoteza kwa changamoto ya mikwaju ya penati dhidi ya Kampala City Council mitatu kwa miwili mnamo mwaka 1978, kisha ikapoteza mnamo mwaka 1981 kule jijini Nairobi nchini Kenya mbele ya Gor Mahia ikilala bao moja kwa sifuri na dhidi ya Villa mjini Kampala kwa kulala pia bao moja kwa sifuri lililowekwa kimiani na mshambuliaji Vincent Tendwa.

Young Africans imecheza fainali sita za michuano hii, ambapo ilipoteza kwenye fainali tatu, ikiwamo dhidi ya Luo Union ya Kenya mnamo mwaka 1976 kwa kulala mabao mawili kwa moja, kisha mnamo mwaka 1986 dhidi ya El Mereikh kwenye uwanja wa taifa wa zamani jijini Dar es salaam kwa changamoto ya mikwaju ya penati, minne kwa miwili baada ya sare ya mabao mawili kwa mawili kwenye dakika 120.

Kisha ikipoteza dhidi ya hasimu wake Simba kwa changamoto ya mikwaju ya penati mitano kwa minne kwenye uwanja wa Aman visiwani Zanzibar, mnamo mwaka 1992, baada ya sare ya bao moja kwa moja kwenye dakika 120 za mchezo.

No comments:

Post a Comment