Search This Blog

Thursday, June 23, 2011

VIINGILIO KAGAME CASTLE CUP 2011

Michuano ya Kagame Castle Cup 2011 inaanza keshokutwa (Juni 25 mwaka huu) ambapo
viingilio kwa kituo cha Dar es Salaam vitakuwa VIP A sh. 15,000, VIP B sh.
10,000, VIP C sh. 7,000, viti vya rangi ya chungwa sh. 5,000, viti vya bluu sh.
3,000 na sh. 2,000 kwa viti vya kijani. Kwa siku ambazo timu za Yanga au Simba
hazitacheza kiingilio cha chini kitakuwa sh. 1,000.

Kwa kituo cha Morogoro ambapo mechi zitachezwa Uwanja wa Jamhuri kiingilio
kitakuwa sh. 5,000 kwa jukwaa kuu na sh. 1,000 mzunguko.

Pia kumefanyika mabadiliko katika mechi za kwanza za timu za Simba na Yanga.
Mechi ya Simba na Vitalo ya Burundi iliyokuwa ichezwe siku ya ufunguzi Juni 25
mwaka huu sasa itachezwa Juni 26 mwaka huu.


Nayo mechi kati ya Yanga na El Mereikh ya Sudan iliyokuwa ichezwe Juni 26 mwaka
huu sasa itachezwa Juni 25 mwaka huu. Mechi zote hizo zitaanza saa 10 kamili
jioni Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.

Timu ambayo imeshawasili mpaka sasa ni Vitalo wakati Elman ya Somalia, Ocean
View ya Zanzibar na El Merreikh zinatarajiwa kuwasili leo kuanzia mchana.

Vilevile mtihani wa utimamu wa viungo (physical fitness test) kwa waamuzi
watakaochezesha michuano hiyo utafanyika kesho (Juni 24 mwaka huu) Uwanja wa
Taifa, Dar es Salaam.


Waamuzi ni Gebremichael Lulesghed –Eritrea, Dilicho Sherefa- Ethiopia, Sylvester
Kirwa-Kenya, Wiish Yabarow –Somalia, Hussein El Fadil –Sudan, Israel Mujuni –
Tanzania, Ronnie Kalema –Uganda na Ibada Kombo –Zanzibar.

Waamuzi wasaidizi ni Charles Nizigiyimana –Burundi, Egue Yassen Hassan –
Djibouti, Mussie Kinde –Ethiopia, Brasan Mamati –Kenya, Simba Honore –Rwanda,
Ahmed Waleed –Sudan, Samwel Mpenzu –Tanzania na Mark Ssonko –Uganda.

MAFUNZO KWA MAKATIBU WAKUU


Mafunzo kwa ajili ya mfumo wa uhamisho wa wachezaji (Transfer Matching System-
TMS) na usajili wa wachezaji kwa klabu za Ligi Kuu ya Vodacom yatafanyika kwa
siku tatu kuanzia Juni 27 hadi 29 mwaka huu.

Washiriki wa mafunzo hayo yatakayofanyika makao makuu ya Shirikisho la Mpira wa
Miguu Tanzania (TFF) ni makatibu wakuu na mameneja wa TMS (TMS Managers) wa
klabu hizo.

HATUA YA 16 BORA COPA COCA COLA

Hatua ya 16 bora ya michuano ya Copa Coca Cola 2011 itafanyika Juni 24 na 25
mwaka huu kwenye viwanja vya Kumbukumbu ya Karume na Tanganyika Packers ulioko
Kawe.

Mechi hiyo zitachezwa saa 2.30 asubuhi na saa 10 kamili jioni. Juni 24 mwaka huu
itakuwa ni Kinondoni na Pwani (Karume- asubuhi), Kilimanjaro na Rukwa (Kawe-
asubuhi), Temeke na Mara (Karume- jioni), Shinyanga na Arusha (Kawe- jioni).

Juni 25 mwaka huu ni Kigoma na Dodoma (Karume- asubuhi), Tanga na Mbeya (Kawe-
asubuhi), Mjini Magharibi na Ruvuma (Karume- jioni) na Morogoro na Ilala (Kawe-
jioni). Robo fainali itachezwa Juni 26 na 27 mwaka huu Uwanja wa Kumbukumbu ya
Karume.

UCHAGUZI WA COASTAL UNION

Kamati ya Uchaguzi ya TFF katika kikao chake kilichofanyika Juni 22 mwaka huu
kilipitia fomu za wagombea uongozi wa klabu ya Coastal Union ya Tanga. Kamati
ilibaini wagombea Yakubu Nuru Athumani, Titus Munthali Bandawe na Steven Mnguto
kutotimiza masharti ya uombaji wa uongozi wa klabu hiyo, hivyo kuwaondoa katika
orodha ya wagombea.


Uchaguzi wa Coastal Union utafanyika Julai 2 mwaka huu kwa nafasi ya Mwenyekiti
na wajumbe wa Kamati ya Utendaji. Nafasi ya Makamu Mwenyekiti haina mgombea na
itajazwa baadaye kwa mujibu wa Katiba ya Coastal Union Ibara ya 29(3).


Boniface Wambura
Ofisa Habari

No comments:

Post a Comment