Search This Blog

Friday, June 3, 2011

Serengeti Fiesta Soccer Bonanza ni somo kwa soka letu


sehemu ya mashabiki waliojitokeza kushuhudia Serengeti Fiesta Soccer
Bonanza mwaka 2011.


Na Ibrahim Masoud 'Maestro'
YAWEZEKANA hakuna ambaye alifikiri nini kitatokea pale matangazo ya kufanyika kwa Bonanza la Serengeti Fiesta katika mikoa mbalimbali nchini yalipoanza kusikika, lakini hali ilikuwa kinyume, mwitikio ulikisa katika mikoa yote lilikofanyika Bonanza hilo, ambalo lilizihusu timu nane kubwa za Bara la Ulaya.

Ukitaka kutambua tofauti ya mapenzi ya dhati waliyokuwanayo wapenzi wa soka nchini Tanzania kwa klabu za soka za barani Ulaya, na hata ukitaka kuvuta taswira ya kujua ukweli, hebu kumbuka wakati Bonanza hilo lilipoanzia jijini Dar es Salaam.

Hakukuwepo na mchezo rahisi, hasa baada ya wale waliokuwa wakizitetea timu zao wanazopenda wakiwa ndani ya uwanja.

Soka lilipigwa kwa kiwango cha juu kabisa, hakuna aliyekubali kushindwa kirahisi kwani wachezaji walitumia mbinu zote zinazotumiwa na wachezaji kote duniani wa klabu hizi ndani ya uwanja.

Kwa hakika, endapo hata wachezaji wetu wa klavu za nyumbani wangekuwa na ari ile basi tungekuwa na timu ambazo si rahisi kushindwa, na uwakilishi wa mashindano ya kimataifa ungekuwa wa kuvutia.

Ndani ya uwanja, kama nilivyosema, soka lilipigwa sana, lakini kila mkoa kulikuwa na tofauti, wakati ambapo mikoa ya Dar es salaam, Mwanza, Dodoma, na Mbeya vita ilikuwa kubwa sana, mjini Zanzibar ufundi ulikuwa mkubwa sana na pia waliocheza wakiwa ni vijana zaidi tofauti na miji mingine.

Hakika vijana wa Zanzibar walicheza soka la ufundi wa hali ya juu na pengine kivutio kingine kikiwa ni binti mdogo Sabaha Hashim Yusuph ambaye anafahamika kama Messi kutokana na kupigia mguu wa shoto, na kipaji cha hali ya juu mno alichonacho, wakati akiichezea timu ya mashabiki wa FC Barcelona, huko Visiwani.

Hata jijini Mwanza, alionekana binti mdogo aliyecheza kwa mashabiki wa timu ya Liverpool, Hamisa Athumani, ambaye anatoka kwenye kituo cha kufundisha soka kwa vijana cha TSC, naye alionyesha kipaji cha hali ya juu mno.

Haikushangaza hata pale vijana wawili wa umri wa chini ya miaka 19 waliocheza katika timu za mashabiki wa Barcelona na Real Madrid kule visiwani Zanzibar kuchukuliwa na timu ya Simba ya kikosi cha pili, kutokana na vipaji vikubwa walivyokuwa navyo.

Wakati Bonanza hilo likitoka jijini Tanga, tayari matayarisho yamekwishaanza kule Arusha, ambapo Jumamosi ya Juni 4, litakuwa likifanyika katika mji ambao unasadikiwa kuwa na viunga vingi vya ving�amuzi kwa ajili ya kushuhudia soka la Ulaya, maarufu kama 'Vibanda Umiza'.

Sasa kutokana na sifa ya mashabiki wa jiji la Arusha ya kuthamini sana soka la Ulaya mpaka kuamua kuondoka kwenye Uwanja wa Sheikh Amri Abeid wakati soka letu la ridhaa likiendelea kwa ajili ya kwenda kushuhudia lile la Ulaya linaloitwa la ukweli, basi yawezekana kabisa mji huo ukafunika kwenye Bonanza hilo kwa idadi ya watu watakaojitokeza, kwani hawa ni wadau halisi wa soka hili.

Kimsingi, Bonanza hili limekuwa fundisho kubwa kwa Watanzania na hasa wadau wa soka, kwa namna ambavyo kumeonaka kuwa na tofauti baina ya soka letu la lile la Ulaya.

Ingawa mechi zinazochezwa si za ushindani wa taji lolote, lakini kwa hakika ushindani huu ni somo kubwa kwa wadau kwamba tukiwa na mikakati mizuri na kuwa na ari ya kuzitetea timu zetu tunazozichezea, hasa wachezaji husika, kama tulivyoona walivyokuwa wakizitetea zile wanazozishabikia za Ulaya, tunaweza tukapiga hatua katika maendeleo ya mchezo huo katika ngazi ya kimataifa.

Kama mashabiki tu wanaojifanya kuzipenda Arsenal na Manchester United wanapambana ka jitahidi uwanjani kila mmoja akitaka kulinda heshima yake, si zaidi basi kwa wachezaji walioajiriwa na timu za Yanga, Simba, Azam na Kagera kucheza kwa ari kubwa kuzipatia ushindi timu zao?

Soka letu litakapopiga hatua kuanzia kwenye ligi ya ndani kwa kuonyesha ushindani halisi, ni dhahiri kabisa kwamba linaweza kutangazika kimataifa, na hiyo itakuwa fursa nyingine kwa klabu zetu kuuza jezi zao na pengine mashabiki wanaweza walau kubadilika kwa kuvaa jezi za timu za ndani badala ya 'kushaini' jezi za Man United, Real Madrid au Barcelona.
Bonanza hili liwe somo kwetu sote.

No comments:

Post a Comment