Search This Blog

Friday, June 3, 2011

EXCLUSIVE INTERVIEW NA MACDONALD MARIGA

SHAFFIH DAUDA AKIMKABIDHI NAKALA YA JARIDA LA NUMBER 10,
KIUNGO WA INTER MILAN MCDONALD MARIGA MARA TU BAADA
MAHOJIANO.


Hivi karibuni kiungo wa kimataifa wa Kenya na klabu ya Inter Milan ya Italia McDonald Mariga alikutana uso kwa uso na Shaffih Dauda na kufanya mahojiano na Jarida la NUMBER 10,
Number 10: McDonald unaweza kuelezea kwa ufupi safari yako ya soka mpaka hapa ulipofikia.
Mariga: Nilianza kucheza timu ya Ulinzi, Kenya, baada ya kutoka shuleni na baada ya hapo nikajiunga na Pipeline FC na baadaye nikaenda Tusker; na hapo ndio nikavuka mpaka Sweden kujiunga na timu ya Enkopings SK. iliyokuwa inacheza ligi daraja la tatu, halafu nikahamia Helsinborg ya daraja la kwanza na ndio nikaenda Parma kabla ya kusajiliwa na Inter Milan mwaka huu.
Namber 10: Safari yako unaionaje, je ilikuwa ngumu au nyepesi?
Mariga: Hapana, unajua kila kitu kina ugumu wake.
Number 10: Ni nini siri ya mafanikio yako?
Mariga: Kwangu siri ya mafanikio ni bidii na juhudi katika kazi yangu na baada ya hivyo mengine yanafuatia.
Number 10: Wakati unajiunga na Inter Milan, Rais Massimo Moratti alikupa maneno gani wakati mlipoongea kwa mara ya kwanza?
Mariga: Nilizungumza na wakala wangu kwanza ambaye alizungumza na Moratti kabla yangu; lakini Moratti aliniambia kuwa timu yake inanihitaji na hilo lilinifurahisha kwani Inter ni timu kubwa.
Number 10: Na vipi kuhusu Jose Mourinho, alikueleza nini mlipoongea mara ya kwanza?
Mariga: Mourinho nilimuona mara ya kwanza nikiwa Parma na nilipokuja Inter nilifurahi kuwa naye na kucheza chini yake, kwani Jose ni kocha mkubwa sana hapa duniani.
Number 10: Utotoni ni mtu gani alikuwa shujaa wako?
Mariga: Kwa wachezaji ni Patrick Vierra ndio aliyenivutia, lakini shujaa wangu halisi alikuwa ni baba yangu mzazi Noah Wanyama ambaye aliwahi kuwa mchezaji na kocha akiwa na AFC Leopards na klabu za Uganda pia.
Number 10: Unaizungumziaje nafasi yako kwenye klabu kama Inter Milan ambayo ina wachezaji wengi nyota?
Mariga: Nafasi yangu pale Inter Milan ipo kama mchezaji na nafurahi kuichezea Inter na pia namwomba Mungu anijalie ili nifike mbali zaidi ya hapa.
Number 10: Unaelezeaje kuondoka kwa Jose Mourinho kocha ambaye alikuleta Inter Milan?
Mariga: Ni kweli Mourinho ndiye aliyenileta Inter, lakini unajua makocha wakati mwingine ni wapita njia kwenye timu; wanakuja na kuondoka kwa hiyo nafurahi kuwahi kucheza chini yake na pia namtakia mema huko aendako.
Number 10: Na ikitokea Jose Mourinho akikuhitaji ujiunge naye Madrid itakuwaje?
Mariga: Akinihitaji siwezi kusita kwani Madrid ni klabu kubwa, lakini kwa sasa sijui itakavyokuwa kwani mimi ni mchezaji wa Inter.
Number 10: Kama ungekuwa ‘Tour Guide’ ungempeleka mgeni sehemu gani ya Tanzania.
Mariga: Nafikiri Dar es Salaam ni sehemu nzuri lakini Zanzibar pia ni sehemu nzuri kwenda.
Number 10: Ipi timu bora kwako AFC Leopards au Gor Mahia?
Mariga: Zote ni timu nzuri na zilikuwa kubwa enzi zake, lakini naisapoti AFC.
Number 10: Unaweza kutuambia nini kuhusu rasimu ya katiba mpya iliyopigiwa kura hivi karibuni nchini kenya?
Mariga: Sikuwapo wakati wa kupiga kura kwa hivyo siwezi kujua; labda ningeisoma kwa makini ndio nichague upande upi uko sahihi.
Number 10: Ukiwa kama kijana unawashauri nini vijana wenzio kuhusiana na matatizo kama dawa za kulevya na Ukimwi?
Mariga: Ningewashauri waachane na mambo kama hayo na wazingatie yale ambayo yanaweza kuwasaidia maishani.
Number 10: Unatumiaje nafasi yako kama mchezaji wa kimataifa kusaidia soka la Kenya?

Mariga: Labda naweza kusema kwa vijana wadogo wanaochipukia, kuwafanyisha mazoezi na vitu kama hivyo.
Number 10: Mafanikio yako Inter Milan yana maana gani kwako na kwa taifa lako kwa ujumla?
Mariga: Kwangu ni kitu kikubwa kwa kuwa sikuwahi kutarajia kama ningeweza kufika hapa nilipo kwa hiyo namshukuru Mungu na nadhani hii pia itakuwa nafasi kwa wachezaji wengine toka Afrika Mashariki.
Number 10: Kwa wachezaji wengi ndoto kubwa ni kucheza vilabu vikubwa kama Barcelona na Real Madrid, vipi kwa upande wako?
Mariga: Kwangu hata hapa nilipo Imter Milan ni klabu kubwa kwani tumechukua Kombe la Klabu Bingwa Ulaya na ni timu kubwa Italia pia, kwa hiyo niko sawa hata hapa tu.

Maisha binafsi
. Baba yake Noah Wanyama, alichezea AFC Leopards nafasi ya winga ya kushoto, pia alichezea timu ya Taifa ya Kenya.
. Victor Wanyama ni mdogo wake kwasasa anacheza soka la kulipwa nchini Ubelgiji kunako klabu cha K.F.C. Germinal Beerschot.
. Ndugu yake mwingine Thomas Wanyama anachezea Mabingwa wa ligi kuu ya kenya Sofapaka.
. Mdogo wao wa kike Mercy Wanyama ni mwananfunzi wa shule ya Lang’ata High School pia ni nahodha wa timu ya shule ya mpira wa kikapu
. Mariga alifuga bao lake la kwanza akiwa amevaa uzi wa Inter Milan mnamo mwezi April 24, 2010 dhidi ya Atalanta akiunganisha kimiani pasi ya Samuel Eto’o ,Inter ilishinda mabao 3–1


Source: NUMBER10 FOOTBALL MAGAZINE

No comments:

Post a Comment