Search This Blog

Tuesday, April 8, 2014

NIYONZIMA, CHUJI, LUHENDE KUANZA KAZI YANGA, YONDANI AMALIZA ADHABU YAKE!!

Niyonzima amepona na yuko tayari kuanza kazi

Na Baraka Mpenja, Dar E salaam

HABARI njema kwa mashabiki wa Yanga ni kwamba wachezaji wake nyota Haruna Niyonzima `Fabregas`, David Luhende, Athuman Idd `Chuji`, Emmanuel Anord Okwi wanatarajiwa kuungana na wenzao mara baada ya mchezo uliopita dhidi ya JKT Ruvu.

Taarifa ya Yanga inasema kuwa wachezaji hao walikuwa wagonjwa na sasa wanaendelea vizuri tayari kwa kuanza kazi ya kuitumikia klabu hiyo.

Naye mlinzi wa kati, Kelvin Yondani aliyekuwa akitumikia adhabu ya kadi 3 za njano amemaliza adhabu hiyo na atajiunga na wenzake muda wowote kutoka sasa.

Mchezo uliopita ambao Yanga walishinda mabao 5-1 dhidi ya JKT ndani ya dimba la Taifa, huku Mrisho Ngasa akipiga `Hat Trick` , walikosa huduma za wachezaji hao.

Nafasi zao zilizibwa vizuri na wachezaji wengine ambapo nafasi ya Yondani ilichukuliwa na Mbuyu Twite, huku Juma Abdul akicheza nafasi ya beki wa kulia ambayo mara nyingi Twite hucheza.

Nafasi ya Niyonzima kwa mechi kadhaa sasa imekuwa ikishikiliwa na kiungo kinda, Hassan Dilunga.

Uwepo wa Jeryson Tegete, Hussein Javu, Mrisho Ngasa, Didier Kavumbagu ulionesha kuwa hata Okwi akikosekana safu ya ushambuliaji hakuna tatizo katika kufumania nyavu.

Yanga kesho inashuka dimbani kucheza na wakata miwa kutoka mjini Bukoba, Kagera Sugar katika mchezo wa ligi kuu Tanzania bara, raundi ya 24 uwanja wa Taifa.

Kikosi cha kocha mholanzi Hans Van der Pluijm kitaingia uwanjani kikiwa na kumbukumbu ya ushindi mnono wa mabao 5 - 1 mwishoni mwa wiki dhidi ya Maafande wa Jeshi la Kujenga Taifa  kutoka mkoani Pwani, JKT Ruvu na kufikisha pointi 49 ikiwa ni pointi nne nyuma ya vinara  Azam FC.

Baada ya mchezo wa mwishoni mwa wiki dhidi ya JKT Ruvu, kikosi cha Yanga jana jioni kiliingia kambini mjini Bagamoyo na kufanya mazoezi jana na leo asubuhi kwenye Uwanja wa Boko Beach Veteran  uliopo  eneo la Boko.

Kocha mkuu wa klabu hiyo, Mholanzi Hans Van Der Pluijm ameseme vijana wake 20 walioingia kambini wote wapo kwenye hali nzuri, kiafya, kifikra na morali ya kusaka pointi 3 katika harakati zao za kutaka  kutetea ubingwa.

Katika mchezo wa awali uliozikutanisha Kagera Sugar na Young Africans,  uwanja wa Kaitaba mjini Bukoba, Young Africans iliibuka na ushindi wa mabao 2-1,  wafungaji wakiwa ni Mrisho Ngasa na Hamisi Kiza `Diego`.

No comments:

Post a Comment