Search This Blog

Tuesday, April 8, 2014

KAMWAGA: SIMBA HAKUNA MGOGORO, TUNAJIPANGA MECHI YA YANGA!!

Kikosi cha Simba sc chini ya kocha mkuu, Mcroatia, Dravko Logarusic kimeshindwa kabisa kuonesha makali msimu huu.
......................................................................................
Na Baraka Mpenja, Dar Es salaam

BAADA ya kuwa na mwendo wa kusuasua katika ligi kuu Tanzania bara,  uongozi wa klabu ya Simba SC umewatoa hofu wanachama na mashabiki wake kwamba hakuna mgogoro wowote ndani ya klabu hiyo bali kufanya vibaya huko kumetokana na hali ya kimchezo.
Katibu mkuu wa Simba Ezekiel Kamwaga amewataka wanachama na mashabiki wa Simba kuendelea kuunga mkono jitihada za uongozi na benchi la ufundi ili kuhakikisha timu hiyo inafanya vyema katika mechi zilizosalia.
“Kwenye mpira kuna wakati upepo unavuma vibaya. Simba msimu huu hatujawa na matokeo mazuri. Lakini haimaanishi tumeshuka morali”.
“Man United hawawezi kushuka morali eti kwasababu wako nafasi ya saba. Kuna wakati Barcelona walimaliza watatu katika Ligi. Timu kubwa kama Liverpool imekaa miaka 24 bila ubingwa, sisi ni nani mpaka tukate tamaa”. Alisema Kamwaga.
Aidha Kamwaga alisema hali ya kikosi chao kwasasa ni nzuri na kimerejea jana jijini Dar es salaam kutoka kanda ya ziwa ambako waliambulia pointi moja dhidi ya Kagera Sugar na kuanza mazoezi leo kujiandaa na mchezo wa jumamosi dhidi ya Ashanti United.
“Tunahakikisha tunashinda mechi zote zilizosalia tukianza na ya Ashanti. Baada ya hapo tutaanza rasmi maandalizi ya mechi ya aprili 19 dhidi ya watani zetu wa jadi Yanga. Siku hiyo tutajidhatiti kuibuka na pointi tatu ili kulinda heshima yetu”. Alisema Kamwaga.


Katibu huyo wa Simba sc aliongeza kuwa bado wana imani kubwa na benchi la ufundi, hivyo baada ya ligi kuisha watakaa chini na kutathimini mwenendo wa timu yao msimu huu.

“Tutapitia ripoti ya benchi la ufundi ili kujua wapi tulikosea na kurekebisha. Nitumie chombo chako kueleza kuwa Simba ya msimu ujao itakuwa tofauti na Simba ya mwaka huu”. Aliongeza Kamwaga.


Simba yenye pointi 37 iko nafasi ya nne huku ikiwa nyuma ya Mbeya City
46, Yanga 49  na vinara Azam yenye pointi 53 huku ligi hiyo ikielekea
ukingoni.

Huu ni msimu wa pili kwa Simba sc kukosa tiketi ya kuiwakilisha nchi katika mashindano ya kimataifa.
Mwaka huu Yanga waliiwakilisha Tanzania katika michuano ya ligi ya mabingwa barani Afrika na Azam fc walicheza kombe la shirikisho.
Msimu ujao kati ya Yanga na Azam zinaonekana kuwa na asilimia kubwa ya kuiwakilisha nchi katika michuano ya kimataifa, huku Mnyama Simba akikosa hata nafasi ya tatu.
Simba na Kagera zinachuana kusaka nafasi ya nne katika msimamo wa ligi kuu soka Tanzania bara.
Kagera Sugar wapo nafasi ya 5 kwa pointi 34 baada ya kushuka dimbani mara 23.


No comments:

Post a Comment